MAAFISA waliohusika na majadiliano ya kuandaa mkataba kati ya shirika la Umeme nchini (Tanesco) na Kampuni ya Richmond Development Corporation (RDC) wamejulikana, JamboForums.com imeweza kubaini.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari ambavyo mtandao huu limeelezwa na kuona, maofisa wa serikali walioshiriki wanatoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Madini na Nishati, Tanesco, Chama cha Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AGC).
Pia wamo wajumbe kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na Kampuni ya Lahmeyer International, wote hawa walikaa pamoja na wawakilishi wa RDC, ambao walitoka na mkataba ambao ulisainiwa Juni 23, mwaka huu na kutoa muda wa siku 150 kwa umeme wa megawati 100 kupatikana kulingana na siku ambayo hati ya dhamana (letter of credit LC) itakapotolewa na Tanesco.
Vyanzo vya habari vinasema kwamba timu hiyo ya majadiliano ilikaa katika mkutano kwa siku saba, kuanzia Juni 8-15 na ulifanyika katika moja ya kumbi za kituo cha kimataifa cha mikutano cha Dar es Salaam (DICC).
Kulingana na vyanzo vyetu katika orodha ya maofisa wa umma walioshiriki majadiliano na Richmond yumo SIngi R. Madata kutoka Wizara ya Fedha, na anaelezwa kwamba alikuwa mwenyekiti wa Timu ya Serikali iliyoingia katika majadiliano hayo.
Mwakilishi wa Wizara ya Nishati na Madini ni Theophillo Bwakea pamoja na Julius Sarota anayeelezwa kwamba alikuwa kwenye sekretariati.
Wawakilishi wa Tanesco katika mazungumzo hayo ni Stephen Mabada; Mohamed Saleh; Godson Makia; James Mtei na Wangwe Mwita aliyekuwa kwenye sekretariati.
Kampuni ya Lahmeyer International iliwakilishwa na Klaus-Uwe Huhnke na Wolfgang Pauly; mwanasheria Mkuu wa Serikali aliwakilishwa na Donald L. Chidowu na CTI iliwakilishwa na Gideon Nasari.
Kwa upande wa RDC vyanzo vyetu vinasema kwamba kulikuwa na Mohamed Gire na Naeem Gire; Gary Borges na Cuthbert Tenga.
Vyanzo vya habari vinasema kwamba timu ya serikali ilikuwa na udhaifu mkubwa kwani ilijihusisha tu na masuala ya kiufundi ya mtambo wa kuzalisha umeme wa megawati 100.
Uchunguzi wa muda mrefu baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, umethibitisha kwamba udadisi wa kina (due diligence) Juu ya uwezo na nguvu za Richmond haukufanyika.
Hali hii ndiyo imesababishwa matatizo makubwa kuibuka baada ya mkataba kusainiwa kwamba Richmond walishindwa kutimiza wajibu wao wa kuwasilisha nchini mashine za kuzalisha umeme ilipotimu Oktoba 8, mwaka huu.
Kulingana na vyanzo vya habari hata kabla ya Timu ya Serikali ya majadiliano na Richmond kumaliza mazungumzo, Richmond ilithibitisha kwamba tayari ilikuwa imekwisha kupata kampuni ya kuipatia mitambo yote kwa pamoja yenye uwezo wa kuzalisha migawati 100.
Richmond kwa kauli yao wenyewe waliweza kueleza wazi kwamba upatikanaji wa mitambo hiyo, yaani yenye uwezo wa kuzalisha megawati 100 ni wa asilimia 95, jambo ambalo lilikubaliwa na Timu ya mashauriano bila hata Mjumbe mmoja kuonyesha kuhoji uthabiti wa kauli hiyo ama kwa kupata taarifa mbadala juu ya kampuni hiyo iliyoonyesha kila kitu kikiwa rahisi kabisa.
Hata hivyo, baadaye ilikuja kuthibitika kinyume chake kwani hadi sasa Richmond wameweza tu kuwasilisha nchini mashine zenye uwezo wa kuzalisha megawati 20 na hizo nyingine 80 inadaiwa na vyanzo mbalimbali kwamba zinatafutwa nchini Afrika Kusini.
Mashine za awali zilipatikana nchini Marekani ambako Richmond ina makao yake makuu, katika jiji la Houston, jimboni Texas.
Katika mazungumzo ya Richmond na Timu ya serikali iliweza kujenga hoja ambayo ilikubalika kwamba wangeweza kutekeleza kazi hiyo kwa mpango wa kuingiza nchini majenereta yenye uwezo wa kuzalisha megawati 25 kwa mikupuo minne.
Mkupuo wa kwanza kulingana na makubaliano hato, ni kwamba Richmond baada ya kupata LC, ingewasilisha mtambo wa kwanza katika kipindi cha siku 60 kama ingetumia ndege au siku 90 kama ingetumia usafiri wa meli; mejenereta ya awamu ya pili yangeingia katika kipindi hicho hicho cha siku 60 baada ya za kwanza au siku 120 tangu utekelezaji wa mkataba uanze.
Majenererta ya awamu ya tatu na nne yangeingia nchini na kuanza kuzalisha umeme katika kipindi cha siku 30 baada ya awamu ya pili, hivyo kufanya utekelezaji wa mradi wote; yaani kusafirisha, kufunga na kuwasha majenereta hayo yenye uwezo wa kuzalisha megawati 100 kutimia katika kipindi cha siku 150 tangu tarehe ya kupatikana kwa LC.
Vyanzo vyetu vinasema kwamba awali ilikubalika kwamba LC ingetolewa siku saba baada ya mkataba kusainiwa, yaani juni 30, 2006.
Hata hivyo baadaye hisia ziliibuka serikalini kwamba Richmond haikuwa ni kampuni yenye nguvu na uwezo kama ilivyokuwa imejitangaza na kuthibitisha yenyewe katika majadiliano, na hivyo serikali ilivuta sana miguu kuruhusu kutolewa kwa dhamana hiyo, ambayo kimsingi ni mzigo wa serikali kwamba inajitoa kuiwekea kifua kampuni husika ili iweze kupata fedha za kuendesha shughuli zake na ikitokea la kutokea ingeweza kuwajibika kwa benki husika.
Hofu hii ndiyo ilisababisha LC kupigwa danadana kuanzia Juni 30, hadi Oktoba 5, 2006 siku inayodaiwa ndiyo ilipatikana na kukubaliwa na moja ya benki.
Danadana ya LC hiyo ilielezwa kurushwa kutoka Agosti 24, 2006, ikaenda Septemba 9, 2006; ikarushwa tena Septemba 18, 2006; ikafutwa na kutolewa nyingine ya Septemba 25, 2006; nayo ikafutwa ikitolewa nyingine ya Oktoba 3, 2006; ikanyofolewa pia na mwisho ikitolewa ya Oktoba 5, 2006 ambayo ndiyo inafanya kazi.
Kwa maana hiyo utekelezwaji wa mradi wa Richmond unahesabika kuanzia Oktoba 5, mwaka huu