Kifo cha dereva wa CCM kilisababishwa na CCM-Dk.Slaa
Na Muhibu Said
24th October 2010
Mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, ameelezea vurugu zilizosababisha kifo cha dereva wa gari la Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Maswa, mkoani Shinyanga na kusema zimetokana na CCM kujitakia maafa.
Aidha, Dk. Slaa anatarajiwa kufanya mikutano mitatu jijini Dar es Salaam leo katika majimbo ya Kawe, Kinondoni, Ilala na Ubungo. Dk. Slaa alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni zake katika uwanja wa Benki, mjino Mombo, wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga jana.
Alisema kinyume na ilivyodaiwa na baadhi ya watu kwamba Chadema imeleta maafa Maswa, dereva huyo alipigwa hadui kufa baada ya wafuasi wa CCM kuvamia mkutano wa kampeni wa Chadema wilayani humo.
Kwa hiyo kusema Chadema imeleta maafa Maswa nasema hapana. CCM imejitakia maafa, alisema Dk. Slaa. Alisema baada ya mkutano wao kuvamiwa na wafuasi wa CCM, Chadema walistahili kujihami na kujitetea.
Hata hivyo, Dk. Slaa alisema kabla ya maafa hayo kutokea, tangu aanze kampeni zake Agosti 29, ameshafanya mikutano 460 ambayo pamoja na mambo mengine aliitumia kuhubiri amani wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Alisema amekuwa pia akikemea vijana wa CCM maarufu kama Green Guard, ambao alisema hupelekwa kwenye makambi kufunzwa ukakamavu lakini baadaye wanaleta vurugu kwenye uchaguzi. Alieleza kushangazwa na kitendo cha polisi kumkamata mgombea ubunge wa jimbo la Maswa Magharibi kupitia Chadema, John Shibuda, kwa sababu ya vurugu hizo.
Alisema kukamatwa kwa Shibuda ni uonevu kwa sababu wakati vurugu zinatokea, alikuwa jukwaani akihutubia mkutano wake wa kampeni.
Akijibu swali la mwananchi katika mkutano wake uliofanyika mjini Muheza, Dk. Slaa alisema akiingia madarakani, atalipokea suala la kurejeshwa kwa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara lilipofikia katika mazungumzo yanayoendelea baina ya kamati ya Waislamu na ile ya serikali na kuliwekea msimamo.
Katika swali lake, mwananchi huyo, Othman Akida, alisema ni muda mrefu sasa Waislamu nchini wamekuwa na tatizo la kutokuwa na mahakama hiyo, hivyo akataka kujua Dk. Slaa akiwa Rais atawasaidiaje waumini wa dini hiyo.
Wakati huo, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alisema maandalizi ya kumpokea Dk. Slaa yamekamilika.
Dk. Slaa atapokelewa kwa msafara wa watu kwa baskeli, pikipiki na magari kuanzia Kiluvya jimboni ubungo, atafanya mkutano Tanganyika Packers Kawe kuanzia saa 6:00 mchana, ataelekea Magomeni shule ya msingi na Mchikichini, alisema.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI