SIMULIZI: ELECTION SAGA (MONEY IN BLOOD)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
UKURASA WA KUMI NA SABA
“Unajua mimi sikuwa nikiamini kama ni huyu kiongozi ndiye ambaye alikuwa amepigwa risasi mpaka nilipo hakikisha sura yake kabisa ndipo nikaamini kwamba ni yeye mwenyewe. Daah maskini mzee wa watu huyu ndiye aliyekuwa anategemewa kuja kuibadilisha nchi hii lakini wale ambao wanaonekana kwao madaraka ni kila kitu wameamua kumuua”
“Inakuwaje mtu mkubwa kama huyu anatembea bila walinzi?”
“Hata mimi nimeshangaa sana maana kwa tukio ambalo limetokea asubuhi la mtoto wake kuuawa ilitakiwa awe na ulinzi mara mbili zaidi ya hapa hata jeshi la polisi lilitakiwa kuwa naye sambamba. Mimi nilikuwa nimetoka kuchukua chakula pale KFC nikawa namuona mtu kama amelewa maana alikuwa anayumba yumba huku anakimbia lakini ghafala sana nikaiona Noah nyeusi ikiwa nyuma yake, akashuka mwanaume mmoja ambaye amejifunika uso wake akampiga risasi za kutosha kisha akaingia kwenye gari na kutoweka. Ndipo pale nilianza kupiga makelele na watu wakaanza kufika hapa”
“Kwamba hakuwa na mlinzi hata mmoja wakati hayo yote yanatokea?”
“Mimi nimemuona akiwa mwenyewe tu hakuwa na mlinzi yeyote yule mpaka nikawa nashangaa. Nimeogopa sana ndugu yangu, naona tatizo hata kurudi nyumbani mwenyewe maana usije ukakuta na mimi ndiyo siku yangu ya mwisho” yalikuwa ni maongezi ya vijana wawili ambao walikuwa wapo pembezoni mwa kundi kubwa la watu ambalo lilikuwa limeuzunguka mwili wa kiongozi huyo huku wengine wakiwa wanaupiga picha mwili huo kusubiri polisi wafike na kuiondoka nao maana walikuwa wanajua kwamba alikuwa ni mtu mfu tayari.
Wakati wanaendelea na hayo maongezi yao, pembeni alikuwa amesimama Tommy kwenye suti yake baada ya kushuka kwenye gari akiwa anawasikiliza kwa umakini sana, hicho ndicho kilimfanya atulie kwanza ili kuwasikiliza wanaume hao kile ambacho wanakizungumzia hapo. Baada ya kuwasikia kwa umakini alipenya katikati ya watu na kusogea mpaka ulipo mwili huku akishangazwa sana kutowaona polisi mpaka wakati huo kwani kwa muda ambao ulikuwa umepita polisi walikuwa wanatakiwa wawe tayari kuwepo hilo eneo.
Alimgusa baba yake mzazi kabisa shingoni huku watu wakiwa wanamshangaa lakini hata hakujali jambo hilo, baada ya kumgusa alishtuka na kumbeba haraka sana ambapo alikimbia naye mpaka kwenye gari na kuondoka hilo eneo kwa kasi sana watu wakiwa wanamchukua video na kumpiga picha akiwa na mwili wa kiongozi huyo ambao aliondoka nao huku hilo eneo watu wakibaki kwenye sitofahamu maana wao walikuwa wanaogopa hata kuugusa wakiogopa kuingia kwenye adha ya kukutana na polisi.
Mwanaume alinyoosha moja kwa moja mpaka hospitali kuu ya mhimbili ambapo alisistiza sana kwamba mtu huyo alikuwa hai bado hivyo walitakiwa kufanya uataratibu wa kumtoa risasi haraka sana huku akiwapigia simu walinzi wa nyumbani waweze kufika haraka sana ndani ya hilo eneo wengine wakitakiwa kubaki kuwalinda wadogo zake. Akiwa amesimama nje ya hilo wodi ambalo baba yake aliingizwa kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji ili kuona namna ya kusaidia maisdha yake kwa kumtoa risasi polisi walifika hapo ambapo walimkwida na kumkamata Tommy tena kwa dharau sana, walinzi wake walitaka kuingilia aliwapa ishara ya kutulia huku akiwasisitiza wahakikishe baba yake yupo salama yeye angerudi.
Alipelekwa ndani ya kituo kikuu cha Osterbay kutokana na aina ya kesi ambayo alikuwa amejiingiza nayo.
“Wewe ni nani haswa mpaka uende kubeba mwili wa mtu tena kiongozi kama yule bila ya sisi polisi kufika?” ni polisi mmoja kati ya watatu ambao walikuwa wamemuingiza kwenye chumba cha mahojiano mwanaume huyo kwa sababu alifanya kosa kubwa sana la kuhusika na kuushika mwili kabla hata ya polisi kufika lile eneo kitu ambacho kisheria lilikuwa ni kosa. Hata hivyo Tommy hakujibu kitu akabaki anamtazama askari huyo kwa hasira kali sana kitu ambacho kilipelekea askari huyo kumpiga na kitako cha bunduki kwenye pua yake kwa kulidharau swali lake.
Damu ilianza kumtoka kwenye hilo eneo hata hivyo hakuwa na muda nayo, walikuwa wamemfunga vyema wakamvua na viatu kisha wakaanza kumshushia kipigo kwa kushindwa kuwa msikivu huku moja kati ya wale askari watatu akiwa ameganda tu maana ni kama hakuwa anaelewa kwamba ni kipi wenzake walikuwa wanakifanya. Waliacha kumpiga baada ya yule mwenzao kuguna kwa nguvu kitu ambacho kilikuwa ni kama ishara, ni kweli ndani ya dakika moja tu IGP alikuwa ameingia ndani ya hicho kituo na alihitaji kuelekezwa kwa mtu ambaye alikuwa amekamatwa na kuletwa hapo alipo kitu ambacho kilileta taharuki kubwa sana ndani ya kituo hicho kuweza kutembelea na kiongozi huyo mkuu wa jeshi la polisi.
Hapo ndipo alipo elekezwa kwenye hicho chumba ambacho Tommy alihifadhiwa, alikuwa kwenye spidi kubwa sana lakini wakati ule taarifa zilikuwa zinasambazwa kwa njia ya redio kwamba mheshimiwa IGP yupo hapo kituoni na kwa wakati huo alikuwa anaelekea kumuona mtu wake ambaye alikuwa amemfuata hapo. Wakati wale askari wawili wakiwa wanaendelea kumpiga Tommy ndio muda ambao taarifa hiyo ilitoka hivyo hawakusikia ila mwenzao ambaye alisikia aliguna kama kuwashtua kwamba muda wowote mheshimiwa alikuwa anaingia hapo ndani.
Walishtuka kwa huo mguno na jamaa akawapa ishara ya kuacha hicho walichokuwa wanakifanya, wakati bado wanashangaana walishangaa wanatangulia askari wawili ndani humo ambao walikuwa na vyeo zaidi yao, wakati wanatoa saluti za heshima ndipo walipopigwa na bumbuwazi baada ya huyo kiongozi mkuu wa jeshi la polisi alipoweza kuingia ndani ya chumba hicho. Ilikuwa ni ghafala sana hivyo walijikuta wanaanza kutetemeka hawakuutarajia huo ugeni kwa wakati huo kiasi kwamba wakawa wamesahau hata kutoa heshima ambapo walikuja kushtuka baadae baada ya kiongozi huyo kuweza kuwaangalia kwa hasira sana.
“Kwanini mnampiga huyu mtu na kwanini mmemkamata?” lilikuwa swali fupi sana ambalo lilihitaji majibu yenye maelezo ya kutosha ili waweze kwenda sawa kwenye huo uwanja wa kujibu.
“Mkuu huyu amekutwa kwenye eneo la tukio la mauaji na baada ya kufika pale akajichukulia sheria mkononi kwa kuondoka na mwili wa marehemu kabla hata polisi hawajafika. Hivyo tumemkamata ili tuweze kumhoji kwamba yeye ni nani na aliuchukua ule mwili kwa ajili ya kazi gani na alikuwa na maana gani kuweza kuupeleka hospitali asije kuwa ndiye muuaji mwenyewe” lilikuwa jibu jepesi ambalo hata IGP alibaki anajiuliza kijana huyo alifanikiwaje kupata kazi wakati alionekana kabisa kuwa wa hovyo sana.
“Muda wote huo hamkuwa mmefika eneo la tukio mlikuwa wapi?” aliwaongeza swali lingine
“Tulikuwa posta ila tuliambiwa kwamba mapolisi wa kule kule wangelishughulikia hivyo tukawa tumekaa mahali tunasubiri ripoti” alipokea kofi zito sana kutoka kwa huyo kiongozi wao ambaye ndiye aliwauliza wakati huo IGP aliwapaishara askari ambao alikuja nao waweze kumfungulia mtu huyo.
“Hiyo amri ya kuweza kukamatwa kwake na kumleta hapa ni nani amewapa?”
“Mkuu wa kituo”
“Una uhakika?”
“Ndiyo mheshimiw….” yule askari hakumalizia sentensi yake alipigwa risasi ya kichwa pale pale, wakati Tommy anasimama kutoka hiyo sehemu aliyokuwa amefungwa, alichomoa bastola moja kutoka kwenye kiuno cha askari mmoja kwa kasi sana kisha akairuhusu kwenye kuelekea kwenye kichwa cha mmoja wa maaskari ambao walikuwa wanamtesa hapo kisha akampiga na yule mwingine kwenye moyo ambaye naye alikuwa amejumuika na mwenzake kisha akamrudishia askari mwenye bastola yake mkononi huku akiinama na kuanza kuvaa viatu vyake.
Wote walibaki wanamshangaa hata IGP hakuwa akiamini kwamba hilo jambo lilikuwa limetendeka hapo.
“Umefanya nini bwana mdogo? Nmekuja hapa kukutoa kwa sababu baba yako alikuwa mtu mkubwa sana na aliwahi kunisaidia kipindi fulani mpaka mimi nikafanikiwa kuwa kwenye hii nafasi. Nilipopata taarifa kwamba umekamatwa halafu bila hatia maana nadhani hawa hawakujua kama wewe ni mwanae nikaamua kuja kukutoa lakini hasira zako zinakufanya mpaka umeua, huoni kama unaweza kufungwa hata kifungo cha maisha kwa kosa la kuua askari wawili? Kwanza unanipa maswali hata bastola kutumia umejulia wapi?” yalikuwa ni maswali mfululizo kutoa kwa IGP ambaye bado hakuwa na uhakika na kile ambacho alikuwa anakiona mbele yake maana mambo yalikuwa yanaenda kwa kasi sana.
“Mheshimiwa hivi kama ungekuwa wewe watu wa namna hii ungewafanya nini? Wapo sehemu wamejibanza wanamwangalia baba yangu anakufa halafu nayasaidia maisha yake wanakuja kunikamata na kunitesa? Walikuwa wapi kumlinda? Walikuwa wapi kuwahi eneo la tukio mpaka waje kuniwahi mimi? Nadhani umesema kwamba baba yangu aliwahi kukusaidia basi na mimi leo inabidi unisaidie kwenye hili maana ingekuwa ni mbaya sana kama ningeenda kwenye vyombo vya habari na kujitambulisha kama mimi ni mtoto wa Apson Limo kipenzi cha watanzania nilikuwa najaribu kuyasaidia maisha yake halafu nyie mkanikamata na kuanza kunitesa. Unahisi jeshi la polisi mtakuwa mmechafuka kwa kiasi gani? Mimi naenda mzee huenda siku nyingine tutapata wasaa wa kuzungumza vizuri zaidi ya leo” mwanaume alimuacha kwenye mshangao kiongozi huyo kisha akatoweka ndani ya hilo eneo ili kurudi hospitali kujua hali ya baba yake maana aliacha akiwa anafanyiwa oparesheni ya kutolewa risasi ambazo ziliingia kwenye mwili wake.
IGP alikuwa na hasira sana, baada ya kutoka humo ndani aliangalia saa yake na kukuta ni saa tano usiku, alisogea mpaka kwenye ofisi ya mkuu wa kituo ambaye alimkuta anapanga panga vitu vyake akiwa kama mtu anayehitaji kutoka hilo eneo. Alimfuata na kumzaba kibao kikali sana
“Una sababu ya msingi ya kunifanya nisikufukuze kazi usiku huu?” aliuliza kwa hasira akiwa anamwangalia kijana wake wa kazi huyo.
“Ndiyo mheshimiwa ninayo” alijibu haraka sana kwani kauli yake ndiyo ingemhakikishia aendelee kuupata mshahara, hakujibiwa zaidi ya kukaziwa macho hivyo akalazimika kuendelea kwa lazima.
“Nimepokea simu kutoka Ikulu, wameniambia kwamba nijiweke kando na hilo jambo na huyo bwana mdogo nimkamate mpaka kesho ndipo utaratibu uweze kuwa sawa, maana mpango ni kwamba ilitakiwa akamatwe kabla ya kufika hospitali na mgonjwa ila vijana wamechelewa ndiyo maana wamemkamatia hospitali” IGP alichoka mpaka akabaki anatabasamu tu maana hakutegemea jambo kama hilo.
“Umesema umepokea simu kutoka Ikulu?”
“Ndiyo mkuu”
“Kwahiyo lengo lao ni yule mzee asifike hospitali bali afe sio?”
“Hilo sijui mkuu”
“Na ulijua kwamba yule bwana mdogo ni mtoto wa damu wa Apson Limo?”
“Hapana mkuu” IGP hakuwa na neno la kuongeza, nafsi yake ilikuwa inamuuma isivyo kawaida yaani watu wanapambana kuilinda nchi halafu Ikulu ndo inaanza kurudisha mambo nyuma, alisonya na kuondoka hilo eneo kwa ghadhabu mno.
Taarifa zilikuwa zinasambaa kwa kasi sana mitandaoni, kila sehemu, kila chombo cha habari kilikuwa kipo busy sana kuzungumzia habari hizo. Ni kuhusu matatizo ambayo yalikuwa yametokea ndani ya familia ya Apson Limo kuanzia asububi ya siku hiyo ambapo mwanae wa kike alikuwa ameuliwa na watu wasio julikana na cha kushangaza sana kichwa cha mtoto huyo hakikuweza kupatikana hali ambayo ilizua taharuki kubwa sana lakini majira ya jioni ya siku hiyo zilianza kusambaa taarifa kwamba hata mtoto wake mkubwa wa kike alikuwa amepotea kwenye mazingira ambayo yalikuwa ya kutatanisha sana na kuzua taharuki nyingine.
Kabla hata habari hizo zote hazijatoka kwenye maskio ya watu ilikuja nyingine hiyo kubwa ambayo ndiyo iliwacha watu hoi huku wengine wakiwa wanatoa mpaka machozi. Mwanaume ambaye wao waliwekeza imani zao kwake, alidaiwa kuwa amekufa huku watu wengine wakidai kwamba alikuwa kwenye hali mbaya sana akiipambania afya yake kitandani na asingechukua muda mrefu ni lazima angeweza kufariki. Watu walianza kuvilaumu sana vyombo vya ulinzi na usalama kwa huo uzembe mkubwa wa kushindwa kumlinda kiongozi huyo ambaye walitamani kwamba ndiye anaweza akaisaidia nchi kutoka kwenye hali iliyokuwepo kuyafikia yale mafanikio mkubwa sana ambayo waliyatarajia kufanyika nchini mwao.
Naam naweka nukta sehemu ya kumi na saba.
Wasalaam,
Febiani Babuya.
Sent from my SM-A107F using
JamiiForums mobile app