Nimezipokea habari za kifo cha kada Kipepe kwa mshtuko mkubwa sana.Nilipoamka tu asubuhi majira ya saa 1.30 asubuhi kwa saa za hapa Marekani nikiwa najitayarisha kwenda kibaruani,kuwasha kompyuta na kuingia kwenye JF ghafla,nakutana na kichwa cha habari chenye habari yenye kisikitisha sana.Ukweli ni kwamba kwa kiwango fulani,hii taarifa japo ni vema kuwa nimeipata mapema,lakini imeniharibia siku yangu.Hakika nimeguswa sana!
Marehemu Kipepe tulifahamiana tangu mwaka 1998 wakati sote kwa pamoja tulipoingia kwenye uongozi wa UVCCM,mimi nikiwa Mwenyekiti wa UVCCM wa Wilaya na yeye wakati huo alikuwa ni mchumi wa UVCCM,makao makuu.Tuligombea kwa pamoja ujumbe wa baraza kuu la UVCCM, Taifa katika uchaguzi wa mwaka 1998 mjini Dodoma.Mimi sikufanikiwa kushinda bali comrade Kipepe alishinda nafasi hiyo baada ya kutofanikiwa katika nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM dhidi ya Mh.Dr.Emaanuel Nchimbi(MB).
Tulifanya kazi wote kwa kipindi hicho chote cha miaka 5 ya uongozi wetu,alikuwa ni kijana makini sana mwenye uwezo mkubwa sana wa kujenga hoja na mwenye kujiamini sana.Sifa ambazo ninaamini zilipelekea kupandishwa cheo hadi kuwa Afisa Tawala Mkuu wa UVCCM,Makao Makuu.Mara ya mwisho nilikutana naye mjini Dodoma katika kikao cha baraza kuu la UVCCM mwaka jana nilipokuwa nyumbani Tanzania,kwa likizo fupi ya majira ya kiangazi.Tuliongea masuala mengi sana yahusuyo jumuiya yetu na chama kwa ujumla.
Hakika UVCCM tumempoteza kada mahiri sana hasa katika kipindi hiki muhimu kabisa,ambapo jumuiya inakabiliwa na uchaguzi mkuu.Ni imani yangu kwamba busara,hekima,umakini,na zaidi sana, uzoefu wake mkubwa katika shighuli za UVCCM,vilikuwa bado vinahitajika sana hususani kwa uongozi mpya tunaoutarajia kuupata mwishoni mwa mwaka huu.
Nahitimisha kwa kutoa pole kwa uongozi wote wa UVCCM chini ya Mwenyekiti comrade Nchimbi,Familia,ndugu, jamaa,na marafiki wote walioguswa na msiba wa mpendwa wetu Samson.Mungu awape faraja ya kweli na kuwatia nguvu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi."Ukagone Kikolo,ijo joo njila jitu twesa!!!!".Bwana alitoa na hatimaye Bwana ametwaa,Jina lake Libarikiwe"