Sanaa ya jadi ya paka mlinzi wa paa “Wamao” mkoani Yunnan ni lulu inayohifadhiwa ili isipotee

Sanaa ya jadi ya paka mlinzi wa paa “Wamao” mkoani Yunnan ni lulu inayohifadhiwa ili isipotee

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,310
Reaction score
1,265
1779409284293.png



Wakati 2026 ni mwaka wa mawasiliano baina ya watu wa China na Afrika, shughuli nyingi za mawasiliano zinafanyika zikiwemo za kitamaduni. Katika kutimiza azma hii iliyowekwa na viongozi wa pande mbili za China na Afrika, wakati nilipotembelea mkoani Yunnan, nami nikajiunga kwenye shughuli za kuendeleza utamaduni kwa kutaka kujua na kujifunza mambo mbalimbali ya utamaduni wa China hasa wa mkoa wa Yunnan.
Ili kuyapata yote hayo mimi na timu yangu tuliamua kutembelea Kituo cha Urithi wa Utamaduni wa Watu wa Kunming cha Hexu. Na kama wahenga walivyosema kwamba “Mguu wa kwenda Mtume kauombea”, basi nasi tulikuwa watu wenye bahati kubwa sana siku hiyo, kwani kituo hicho kilikuwa kinaadhimisha Siku ya Vitabu Duniani, yaani Aprili 23, ambapo mbali na shughuli nyingi zilizofanywa siku hiyo, mimi pia nilishikiri kucheza ngoma ya jadi nikiwa pamoja na wasanii wa kikundi cha sanaa cha jamii ya huko.
Wakati tunacheza ngoma hiyo kusema kweli tulichangamka kabisa na nyuso zetu zilijaa furaha. Miondoko myepesi ya ngoma hiyo pamoja na vicheko na tabasamu lililojaa kwenye kila uso wa mshiriki vilipamba tukio hilo na kuleta shauku kubwa kwa hadhira nzima huku tukio hili la kitamaduni likigusa moyo wa kila mtu aliyekuwepo hapo.
Baada ya kupata uhondo wa ngoma ya jadi, ukafika wakati wa kuingia darasani kujifunza namna ya kutengeneza sanaa ya jadi ya ufinyanzi “Wamao”. Unapokwenda kwenye vijiji vya zamani Kusini mwa China, juu ya mapaa ya nyumba zao utakutana na mnyama wa ajabu aliyefinyangwa kwa udongo akikutazama. Mnyama huyu anaonekana kama paka, lakini sio paka mpole. Akiwa na mdomo mpana, meno makali, macho mapana, paka huyu mkali anaonekana kama anajaribu kumtisha mvamizi.
Wamao ni paka anayejificha kama mlinzi makini wa mapaa ya makaazi ya jadi ya Yunnan kwa maelfu ya miaka. Mnyama huyu anayepamba mapaa ya nyumba huwa anatengenezwa kwa mfano wa chuimilia, lakini amepewa jina la paka. Akiwa amesimama mdomo wake ukiwa wazi kwenye ukingo wa paa, wenyeji wanaamini kuwa anakinga watu kwa kumeza pepo wabaya, anafukuza mikosi, na kuleta utajiri na bahati nzuri. Hivi sasa urithi huu wa utamaduni umebadilika kutoka kitu cha jadi hadi bidhaa maarufu ya kitamaduni yenye ubunifu, na kuwa alama ya kipekee ya utamaduni wa Yunnan.
Kwa karne nyingi, wanakijiji walifinyanga sanamu hizi kwa udongo, wakazichoma kwenye moto kwa mikono yao, na kuziweka juu ya milango yao bila hata kuiita sanaa, bali ilikuwa ni sehemu ya maisha yao tu. Na ilikuwa ni njia ya watu wa China kuonesha upendo na heshima yao kwa paka, ambao wamelinda familia za Wachina katika historia yote.
Mwalimu Wang Hua wa kituo cha mafunzo alitupatia darasa dogo la kuvutia kuhusu urithi wa utamaduni huu usioshikika, akielezea wazi historia na asili ya paka mlinzi wa paa na sifa za kipekee za kitamaduni za nyumba za watu wa Yunnan. Alituonesha maumbo mbalimbali ya Wamao kama vile chuimilia, simba, na paka, na kuchambua tofauti za kipekee kati ya mitindo mbalimbali ya eneo hilo. Ufundishaji wake ukatufanya sote tulioshiriki kuzama kabisa katika haiba ya urithi wa utamaduni usioshikika wa Yunnan.
Baada ya kupata mafunzo ya nadharia, sasa ukaja wakati wa mafunzo ya vitendo, ambapo mwalimu Wang alitufundisha mbinu moja baada ya nyingine kama vile kuchonga na kuweka maumbo. Nikiwa mtu ninayependa kujaribu mambo, sikurudi nyuma hata kidogo wakati mwalimu aliponitaka nami nifinyange Wamao wangu. Kwanza kabisa kwa mujibu wa mwalimu tulianza kutengeneza umbo la paka, baadaye mkia ulioinuka kisha tukaja eneo la uso ambapo tulitengeneza kinywa kipana, meno, ulimi na sharubu mbili.
Mafunzo haya ya vitendo yalikuwa ya kina, hata kutupa wepesi kwa watu wanaoanza kujifunza kama mimi. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kumfinyanga Wamao lakini kwa mujibu wa mrithi wa sanaa hii Wang Zhongde, Wamao wangu alionekana kama aliyefinyangwa na mtaalamu.
Hivi sasa Wamao imekuwa sanaa nzuri ya kazi ya mkono na zawadi inayopendwa yenye ukubwa na rangi mbalimbali, na kuwa mojawapo ya zawadi maarufu zaidi kwa wageni kutoka kote duniani. Inaweza kutumika kama sumaku ya kupamba kwenye friji, pambo la kauri au kishikio cha ufunguo. Kwa muundo wake mzuri na ishara njema, Wamao sio tu kwamba inawakilisha utamaduni wa wenyeji wa Yunnan bali pia inasimama kama urithi wa utamaduni usioshikika wa Yunnan.
Hivi sasa mapaa haya ya zamani yanatoweka. Kadri ukuaji wa miji unavyobadilisha mandhari ya Kunming, nyumba nyingi za zamani sasa zimetoweka. Warithi wa kazi hii ya sanaa ya jadi ya Wamao wanatarajia kuwa kuendelea kuienzi sanaa hii kutasaidia kuhifadhi kumbukumbu na moyo wake wa kitamaduni.
 
Back
Top Bottom