Na: Alex E. Bubelwa.
KUHUSU LILIKO SANDUKU LA AGANO!
Sanduku la Agano lilitengenezwa na fundi aliyeitwa Bezaleli mwana wa Huri kwa maelekezo toka kwa Mungu kama alivyomwagiza Musa, ilikuwa ni kama mwaka mmoja tangu walivyokuwa wametoka Misri. Kuhusu ukubwa wake na jinsi kilichotengenezwa tafadhali soma mwenyewe katika (Kutoka 25:10-22).
Baada ya kutengeneza, vitu vilivyokuwa vimewekwa hapo mwanzo ni kama vilivyoorodheshwa kwenye (Waebrania 9:4)
"..... na sanduku la agano lililofunikwa kwa dhahabu pande zote, mlimokuwa na kopo la dhahabu lenye ile mana, na ile fimbo ya Haruni iliyochipuka, na vile vibao vya agano;.." (soma pia Kutoka 16:33).
Sanduku la Agano lilikuwa ni ishara ya uwepo wa Mungu katikati ya wana wa Israeli. Lilikuwa linahifadhiwa katika hema maalum ilotengenezwa kwa ajili yake, wakati Israeli wakiwa jangwani ni katika hema hiyo Musa alikuwa anakwenda kuongea na Mungu.
Sanduku hili lilikuwa lina utisho mkuu mno, haikuruhusiwa mtu asiyekuwa kuhani kuligusa au kulikaribia, kama angelikaribia angekufa. ( 1Sam 6:19). Waisraeli wakati wanaingia nchi yao ambayo wakati ule iliitwa Kanaani, waliobeba hilo sanduku walipofika mto Yordani maji yalijitenga wakavuka kwa miguu.
Mwaka 967KK Sulemani alipojenga Hekalu, Sanduku la Agano lihamishiwa humo, lakini FIMBO YA MUSA na KOPO LA DHAHABU LENYE MANA (chakula ambacho Mungu aliwalisha Israeli jangwani) havikuwemo, zilikuwemo tu mbao mbili za mawe zilizoandikwa amri kumi. Ona maandiko yanavyoonesha:
(1 Wafalme 8:9)
"Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliziweka ndani huko Horebu, BWANA alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka katika nchi ya Misri."
Hivi kopo lenye mana na fimbo ya Haruni ile ilogeuka nyoka na pia kuchipua vilienda wapi? Katika Biblia haijaelezewa popote, ila inasemekana karibu mwaka 1100KK enzi za kuhani Eli, Israeli walipomtenda Mungu dhambi akawaacha na hilo Sanduku la Agano likaporwa na Wafilisti mpaka Ashdodi, wakakaa nalo kwa muda wa miezi saba, ni kwa wakati huo vitu hivyo viliibiwa na hao Wafilisti! (1Sam 6:1).
Mfalme Yosia alitawala Yudea mwaka 641-609KK, wakati wa utawala wake ikiwa imebaki miaka zaidi ya 40 kabla Nebukadreza kuteketeza Hekalu lililojengwa na Sulemani, nabii Yeremia alitoa unabii kuhusu sanduku la Agano, kwamba utakuja wakati ambapo Wayahudi hawatakuwa nalo sanduku la Agano na wala hwatalitaja! Ona unabii kwa kinywa cha Yeremia :
(Yeremia 3:16)
".... siku zile hawatasema tena, Sanduku la agano la BWANA; wala halitaingia moyoni; wala hawatalikumbuka, wala hawatalizuru, wala hayatafanyika hayo tena."
Mwaka 586KK wababeli walipigana na Yuda, Wayahudi wakashindwa vita, huku wapiganaji na raia wasiopungua laki moja wakauliwa na waliosalia wakachukuliwa hadi Babeli, mali za Hekalu zikaporwa na hekalu lenyewe likateketezwa kwa moto.
Baada ya Hekalu kuteketezwa hatima ya Sanduku la Agano haikujulikana, na wala halikubebwa na Wababeli!
Baada ya miaka 480 kupita tangu Hekalu la Sulemani lilipoharibiwa, mwaka wa 100KK kitabu cha Wamakabayo (kimojawapo kati ya vitabu 7 vya deuterokanoni) kiliandikwa. Katika 2Wamakabayo 2:4-10 inaonesha kabla ya Wababeli kuishambulia Yerusalemu, Mungu alimwamuru nabii Yeremia alichukue Sanduku la Agano aende nalo mpaka mlima Nebo, alifiche kwenye pango.
Mlima Nebo uko katika nchi ambayo kwa sasa inaitwa Jordan, kuna umbali wa maili 29 tokea Mashariki ya mji wa Yerusalemu. Ni katika mlima huo Mungu alimwambia Musa apande aangalie nchi ambayo anawapa wana wa Israeli, na ndiko alikofia na mwili wake kuzikwa na Mungu mwenyewe, haukuonwa tena.
Ilikuwa ni kama mwaka 96BK, kwa mara ya mwisho Sanduku la Agano lilionekana kwa mara ya mwisho, aliyeliona ni Yohana mwana wa Zebedayo, wakati huo alikuwa kisiwani Patmo, miongoni mwa mambo aliyofunuliwa ni pamoja na sanduku la Agano ambalo aliliona likiwa ndani ya Hekalu la Mbinguni (Ufunuo 11:19).