Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni

Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Joined
Nov 22, 2012
Posts
1,985
Reaction score
1,286
SASA HAMSINI RASI, HAMSINI MAJINUNI.
I SAW THEM, THEY ARE REAL!!!!!
The things out there in the shadows, they are real, i can't go against my fate at all, all these i know recently after i wake up from vivid dreams or some sort of vision. Am i dreaming? if so my real life is a part of nightmare. I don't trust her, but something inside me(i don't know what da thing is), tell me that bitch saved my life!!!!!!!

Niko na wino chupani, na ujiti mkononi,
Naandika ya moyoni, yalo nifika jamani,
Sikuwahi kuamini, kuna viumbe majini,
Hadithi za kizamani, ndivyo nilivyodhani.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni

Naanzia mwishoni, nilipokaa jamvini,
Fatma bint Subiani, akipandishwa rasini,
Niliketi kitangani, na chano kiko pembeni,
Lewa iko kilingeni, yanapungwa malohani.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Mloketi upenuni, na wa mbali sogeeni,
Muingie uwanjani, tuyapunge malohani,
Kiti apate amani, imtoke mitihani,
Alisema hadharani, Kachiki bint Ngonyani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Kachiki bint Ngonyani, aso mjua ni nani,
Wanasiasa nchini, na wauzaji sokoni,
Hufika kwake nyumbani, wapate ndele usoni,
Anaishi Magomeni, pale Kilosa Mjini,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Mshike vya mikononi, vilaji vya malohani,
Kitezo na zafarani, na udi wa malohani,
Manenane na ubani, na uvumba wa majini,
Shime viwepo chanoni, ni muhimu si utani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Maji ya zamda chupani, sanamaki ya kusini,
Uzire, giligilani, na vizimba vya barani,
Mafuta ya asumini, na mkongojo wa jini,
Ada za bint Sultani, visikose kitangani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni

Rabi Mola Sultani, Muumba wa mitihani,
Raha, dhiki na huzuni, majaliwa ya Manani,
Ameumba mashetani, kwa siku ya ushetani?
Kaweka mwiba njiani, ili umchome nani?
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Niwe na mbawa tisini, nipae hata mbinguni,
Na nifike arshini, nitabaki kuwa chini,
Kudura haiwi chini, huwa juu tambueni?
Upatalo duniani, limeandikwa zamani.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Fatma mwana wa jini, ndio wangu mtihani.
Kwani niko shubuani, sijui nifanye nini,
Habanduki ubavuni, wala hatoki rasini.
Nifanyeje wenzanguni, initoke mitihani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Nimezama vitabuni, kazi za wanazuoni,
Biblia na furukani, maandishi ya zamani,
Naitafuta yakini, iliyopo vitabuni.
Hukumu yake n’ nini, sijaipata jamani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Fatma wewe ni nani, na hasa wataka nini?
Vilaji vipo chanoni, sema sasa ya moyoni,
Au nichore baoni, nijue ya ghaibuni?
Wewe ni wa baharini, au wale wa barani?
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Haya sasa sogeeni, msikie ya moyoni,
Ninayo mengi mtimani, yalo nifika zamani,
Sitochora ubaoni, kusema ya kifuani,
Haya yangu ya nguoni, wa kuyasema jirani?
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Ninayo mengi mtimani, yalo nifika zamani,
Nilikuwa darasani, mwaka ule wa huzuni,
Nikapigwa kichogoni, kiza nikawa sioni,
Kisunzu tele mwilini, puu nikabwagwa chini.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Kabla sijabwagwa chini, nilimuuliza jirani,
Aliyenipiga nani, cha mno hasa ni nini?
Nimewakera nini, hata nipigwe kichwani.
Wakanicheka jamani, nikaihisi tafrani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Dotto uko na nini? Akanishika begani,
Aliyekupiga nani? amekupiga na nini?
Una mawazo gani? Una wazimu kichwani?
Akaiomba amani, nisiizue tafrani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Nilipoanguka chini, Nikawa niko ndotoni,
Niko mwenyewe njiani, nchi ya ughaibuni,
Nakimbizwa na manyani, wenye mawe mikononi,
Nikasemea moyoni, Lile si Joka jamani?
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Joka hili joka gani? Mwenye kipembe kichwani,
Ana shanga shingoni, pete tano mkiani,
Mwale wa moto machoni, moshi watoka puani,
Akazichochea kuni, kwa kuungana na nyani,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Nilisoma vitabuni, habari ya maluuni,
Mwenye kipembe kichwani, ndiye huyo maluuni?
Aliyezua tafrani, duniani na mbinguni,
Ana matobo kichwani, hana jema asilani.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Mwenye pembe kichwani, alifukuzwa mbinguni,
Akashuka duniani, kama Amiri jeshini,
Watu hawaelewani, kisa huyu punguani,
Nilo soma vitabuni, leo dhahiri machoni,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Mwenye kipembe kichwani, likaungana na nyani,
Loo! niko hatarini, kutolewa duniani.
Na hawa mahayawani, watia ndimi puani,
Nikamuomba Manani, anitoe hatarini.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Jasho likanimwaika, na miguu ikachoka,
Manyani wakanifika, Joka likanizunguka,
Hakika nilitishika, mwili ukatetemeka,
Mama nikamkumbuka, na yowe likanitoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Mkojo ukanitoka, bila mwenyewe kutaka,
Mwili wote ukachoka, nikahisi kuanguka,
Li Joka likajisuka, mwili akauzunguka,
Mwili ukasisimka, na woga ukanishika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Sauti zikasikika, ya mifupa kuvunjika,
Nyani wakaongezeka, sijui walipotoka,
Wakawa wakinicheka, vile ninavyoteseka,
Tena wakirukaruka, duara wakizunguka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Miguu ilinyooka, ulimi ukanitoka,
Shingo ilivutika, koo likakabika,
Mwili ukatetemeka, baridi ikanishika,
Ningeweza kuanguka, ni joka lilonishika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Roho iliangaika, nikahisi yanitoka,
Pumzi ziliathirika, kuruzo lilinitoka,
Mishipa ilipasuka, damu zikachuruzika,
Koo lilinikauka, na kiu ilinishika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Mambo yaso kufika, masikio huyachoka,
Vigumu kuaminika, hadi yata’po kufika,
Kweli nimeona Joka, Baada ya kuzimika,
Hata nilipozinduka, kichwani hakunitoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Ndotoni nikiteseka, Kwa waja nilizimika,
Nyuso zilifadhaika, huku wakiangaika,
Wapo walonishika, wakisema pepo toka,
Visomo vilifanyika, ili nipate zinduka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Waliomba kwa Rabuka, ili nipate ponyeka,
Maneno yakanitoka, sauti ikachujika,
Mimi si mwenye kutoka, hapa ndio nimefika,
Fanyeni mnalotaka, katu si mwenye kutoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Watu waliongezeka, sauti iliwafika,
Dotto nataabika, joka limenizunguka,
Kumbe hovyo naboboka, na sauti zabadilika,
Macho yalinitoka, na shingo ilipindika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Mrembo aloumbika, sijui alipotoka,
Manyani wakatishika, ajabu wakatoweka,
Joka likafokafoka, na ndimi ilimtoka,
Kipembe kikatamka, mambo yasoelezeka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Hatua akairuka, haraka akanifika,
Vitisho vyote vya joka, Mrembo hakutishika,
Machoni alinishika, nikayafumba haraka,
Macho yalipofumbuka, nikawa nimezinduka.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Loo amezinduka, mmoja akasikika,
Damu zinamtoka, ulimi umechanika,
Taratibu kapashika, damu zinaponitoka,
Kumbe hapajachimbika, ni kama amechubuka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Kivivu nikainuka, tayari kwa kuondoka,
Nguo zilivyochafuka, rangi zilibadilika,
Nyumbani nilifika, si kama niloanguka,
Wale walonipeleka, wala hawakusumbuka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Wala sikupumzika, nyumbani nilipofika,
Ndugu walonizunguka, niliwatoa mashaka,
Jinsi nilivyoanguka, kuwaficha sikutaka,
Yale yaliyo nifika, wala sikuyafutika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Wala sikuyafutika, yote yaliyo nifika,
Kisunzu na kuanguka, kiza na kuzimika,
Habari za yule joka, na bint aloumbika,
Wale nyani walozuka, mwisho nilivyozinduka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Wote walifadhaika, huzuni iliwashika,
Hasa walipokumbuka, Bibi alivyoondoka,
Alianza kudondoka, na kisha akazimika,
Naye aliweweseka, na macho yalimtoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Kitu alichotamka, Bibi alipozinduka,
Nilizingirwa na Joka, na nyani walonicheka,
Mwanamke alipozuka, machoni akanishika,
Roho nahisi yatoka, akaaga na kuwatoka,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Bibi aliyependeka, ndivyo alivyowatoka,
Kifo chake cha mashaka, sasa wakakikumbuka,
Wenzangu hawakutaka, yaleyale kunifika.
Hatimaye wakatoka, nami nikapumzika.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Jinsi walivyotishika, wala hapakukalika,
Nyumbani wakaondoka, wote wamehamanika
Hofu iliyowashika, mganga wakamsaka,
Wallahi hawakutaka, yale yale kunifika.
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

Majani ya mkirika, mizizi ya msanaka,
Buni zilizokauka, na mafuta ya mbarika,
Ndivyo vilivyotumika, mwili wangu kuzindika,
Lengo nipate epuka, matatizo kunifika,
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni.

View attachment 196951

View attachment 196952

View attachment 196953

Itaendelea.

Njano5.
0784845394
 
Daaaaah! Mkuu, asante kwa vitu adimu hivi humu jamvini. Ngoja wafike vijana wa Kalukuleta na simu a.k.a Viduku. Watatoka kapa na maneno ya kutapatapa.
 
Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni
Hasa makini ya basi, vitu va ughaibuni
Hapa ubini ukwasi, msitu nyingi kanuni
Mwana kuchelea kiza, ni ada si miujiza

Mwana kuchelea kiza, ni ada si miujiza
Hata ende akiza, elimisha kwa himiza
Ende kwa kuapiza, mapiramidi ya Gizah
Udogo wa mafikira, hupandisha taathira

Udogo wa mafikira, hupandisha taathira
Ukaja weka na nira, pa kwenda boya mpira
Hwenda wingi ukiwa, bila hata ya kufiwa
Utakuja kuibiwa, bila hata kuraiwa

Mrembo aloumbika fanya hima umuoe
Tukuweke kwa mkeka, tukuvike Mgolole
Vipi wende ota ndoto, taraji baba watoto?
Na kuwewesekea shoto, kama Mrisho Mpoto?

Umefanya jambo zuri, nduguzo kuwaeleza
Kama marashi uturi, kweli ya kuendeleza
Majinuni na kiburi, yataleta kuteleza
Si hasi wala sifuri, adili kubembeleza

Kaweka mwiba njiani ili umchome nani?
Kiumbe wake manani, mweusi au yunani?
Ukifikiri undani, jibu halipatikani
Ukifikiri mizani, kama tungo za kudhani

Ugoro unaovuta, leo umekuadhiri
Umeuvuta kwa puta, sasa umekuathiri
Umeupiga kwa shuta, naona umekithiri
Jenerali kwa kuruta, hawezi kuwa mahiri

Sasa hamsini rasi, hamsini majinuni
Kaditama sema basi, zaidi vunja galuni
Fanya uondoe ghasi, kwa kulisaka gauni
Wazee wapige pasi, kwa mkaa Kisauni
 
Daaah hilo joka limeniharibia usiku wangu najuta kufungua huu uzi
 
Ni malenga wetu?...tupen tafsiri yake, hii ni fasihi kali sana inahitji IQ ya kutosha
 
Daaaaah! Mkuu, asante kwa vitu adimu hivi humu jamvini. Ngoja wafike vijana wa Kalukuleta na simu a.k.a Viduku. Watatoka kapa na maneno ya kutapatapa.

Acha kujifanya wewe ndiyo unauelewa zaid humu jf.
 
Back
Top Bottom