Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,771
- 41,027
MASKINI AKIKOPA KAPATWA, TAJIRI AKIKOPA KAPATA
Na. M. M. Mwanakijiji
Tuangalie ukweli wa hoja hii na tulinganishe nani yuko karibu zaidi na hili kati ya wanaotetea mikopo isiyoulizwa na wale wanaouliza kuhusu mikopo na misaada ya kigeni. Yanayofuatia siyo maneno yangu nimeyanukuu tu.
Njia moja tunayotumia kujaribu kuepukana na lazima hii ya kukiri kodi zaidi ikiwa twataka fedha zaidi ni kutilia sana mkazo fedha za kutoka nje ya Tanzania. Fedha hizi za kutoka nje ni za aina tatu:-
(a) Zawadi: Yaani Serikali ya nje iipe Serikali yetu fedha za bure tu kama sadaka kwa ajili ya mpango fulani wa maendeleo. Wakati mwingine shirika lo lote la nje liipe Serikali yetu au Shirika jingine katika nchi yetu msaada fulani kwa ajili ya maendeleo.
(b) Mkopo: Sehemu kubwa ya fedha tunazotazamia kupata kutoka nchi za kigeni si zawadi au sadaka, bali ni mkopo. Serikali ya nje au Shirika la nje, kama vile Benki, hukopesha Serikali yetu fedha fulani kwa ajili ya kazi zetu za maendeleo. Mkopo huu huwa una masharti yake ya kulipa, kama vile muda wa kulipa, na kima cha faida.
(c) Raslimali ya Kibiashara: Aina ya tatu ambayo pia ni kubwa kuliko ya kwanza, ni ile ya fedha za watu au makampuni yanayotaka kuja katika nchi yetu kuanzisha shughuli mbali mbali za uchumi kwa manufaa yao wenyewe. Na sharti kubwa walitakalo jamaa hawa wenye fedha zao ni kwamba shughuli yenyewe iwe ni ya faida – kwao – na pia kwamba Serikali iwaruhusu kuondoa faida hiyo Tanzania na kuipeleka kwao. Hupenda pia kwa jumla Serikali iwe na siasa wanayokubaliana nayo au ambayo haihatarishi uchumi wao.
Hizo ndizo njia tatu kubwa za kupata fedha kutoka nje ya nchi yetu. Kuna mazungumzo mengi ajabu juu ya jambo hili la kupata fedha kutoka nchi za kigeni. Serikali yetu na viongozi wetu wa makundi mbalimbali hawaachi kufikiria njia za kupata fedha kutoka nje.
Na tukizipata au japo tukipata ahadi tu ya kuzipata mara magazeti yetu, au radio zetu na viongozi wetu hutangaza jambo hilo ili kila mtu ajue kuwa neema imekuja au iko njiani inakuja. Tukipata msaada hutangaza; tukipata mkopo hutangaza; tukipata kiwanda kipya hutangaza; tukiahidiwa msaada, mkopo au kiwanda kipya hutangaza. Japo tukianza mazungumzo tu na nchi au shirika la kigeni juu ya msaada, mkopo au kiwanda, mara hutangaza japo hatuna hakika ya matokeo ya mazungumzo hayo. Na kisa? Ni kuwajulisha wananchi kwamba, tunaanza mazungumzo ya neema!
TUSITEGEMEE FEDHA KULETA MAENDELEO
Ni jambo la kijinga kuchagua fedha kuwa ndiyo chombo chetu kikubwa cha maendeleo na hali tunajua kuwa nchi yetu ni maskini. Ni ujinga vile vile, kwa kweli ni ujinga zaidi, tukidhani kuwa tunaweza kuondoa hali hii ya unyonge wetu kwa kutegemea fedha za kutoka nje badala ya fedha zetu wenyewe. Ni ujinga kwa sababu mbili. Kwanza, hatuwezi kuzipata. Ni kweli kwamba zipo nchi ambazo zaweza na zapenda kutusaidia.Lakini hakuna nchi moja duniani ambayo iko tayari kutupa misaada au mikopo au kuja kujenga viwanda katika nchi yetu kutimiza shabaha zake zote za maendeleo. Nchi zenye dhiki ni nyingi sana duniani. Na hata kama nchi zote zenye neema zingekubali kuzisaidia nchi zenye dhiki, bado ingekuwa msaada huo hautoshi. Lakini nchi zenye neema hazitakubali. Hata katika nchi ile ile, matajiri huwa hawatoi fedha zao kwa hiari ili zisaidie Serikali kuondoa dhiki. Njia ya kuzipata fedha za matajiri ili zisaidie umma ni kuwatoza kodi wakipenda wasipende. Hata hivyo huwa hazitoshi.
Ndiyo maana japo tungewakamua vipi wnanachi na wakazi wa Tanzania, matajiri na maskini, hatuwezi kupata fedha za kutosha kutimiza mipango yetu ya maendeleo. Wala duniani hakuna Serikali ambayo yaweza kuyatoza kodi mataifa yenye neema, yakipenda yasipende, ili kusaidia mataifa yenye dhiki. Hata hizo zisingelitosha. Hakuna Serikali ya Dunia nzima. Fedha ambazo nchi zenye neema hutoa huwa kwa wema wao, au hiari yao au kwa manufaa yao wenyewe. Haiwezekani basi, tupate fedha za ktuosha kwa njia hiyo.
MISAADA NA MIKOPO VITAHATARISHA UHURU WETU
Pili, japo kama tungeweza kuzipata; hivyo ndivyo tunavyotaka kweli? Kujitawala ni kujitegemea. Kujitawala kwa kweli hakuwezekani ikiwa Taifa moja linategemea misaada na mikopo ya Taifa jingine kwa maendeleo yake. Hata kama pangetokea Taifa au mataifa ambayo yako tayari kutupa fedha zote tunazohitaji kuendesha mipango yetu ya maendeleo isingekuwa sawa kwa nchi yetu kuipokea misaada hiyo bila kujiuliza matokeo yake yatakuwa nini kwa Uhuru wetu na uzima wetu.
Msaada ambao ni kama chombo cha kuongeza juhudi, au nyenzo ya juhudi, ni msaada ambao una manufaa. Lakini msaada unaoweza ukawa sumu ya juhudi si msaada wa kupokea bila kujiuliza maswali. Kadhalika mikopo. Kweli mkopo ni bora kuliko misaada ya “bure”. Mkopo nia yake ni kuongeza jitihada au kuifanya jitihada itoe matunda mengi zaidi. Sharti moja la mkopo huwa ni kuonyesha jinsi utavyoweza kuulipa. Maana yake ni kwamba sharti uonyeshe kuwa unakusudia kuufanyia kazi itakayoleta manufaa ya kukuwezesha kuulipa.
Lakini hata mikopo ina kikomo. Sharti upime uwezo wa kulipa. Tunapokopa fedha kutoka nje mlipaji ni Mtanzania. Na kama tulivyokwisha sema Watanzania ni watu maskini. Kuwabebesha watu maskini mikopo ambayo inawazidi kimo si kuwasaidia bali ni kuwaumiza. Na hasa inapokuwa, mikopo hiyo ambayo wanatakiwa walipe haikuwafaidia wao, bali ilifaidia watu wachache tu.
Na Viwanda vya wenye raslimali zao je? Ni kweli tunavitaka. Hata tumepitisha katika Bunge sheria ya kulinda raslimali ya wageni wanaoanzisha mipango mbali mbali ya uchumi katika nchi yetu. Nia yetu na matumaini yetu ni kuwafanya waone kuwa Tanzania ni nchi inayofaa kuingiza raslimali zao. Kwani raslimali yao itakuwa salama italeta faida. Na faida hiyo wenyewe wataweza kuiondoa bila vipangimizi. Tunayo matumaini ya kupata fedha za maendeleo mbali mbali kwa njia hii. Lakini hatuwezi kupata za kutosha.
Lakini hata kama tungeweza kuwaridhika kabisa Wageni hao na Makampuni hayo mpaka yakubali kuanzisha mipango yote ya uchumi tunayohitaji katika nchi yetu, hivyo ndivyo tunavyotaka kweli? Kama tungeweza kushawishi wenye raslimai wa kutosha kutoka Amerika, na Ulaya kuja kwetu na kuanzisha Viwanda vyote, na mipango mingine yote ya uchumi tunayohitaji katika nchi hii, hivi kweli tungekubali bila kujiuliza maswali? Tungekubali kweli kuacha uchumi wetu wote uwe mikononi mwa wageni kwa ajili ya kupata faida na kuipeleka katika nchi zao?
Hata kama wasingedai kuhamisha faida na kupeleka makwao, bali faida yote watakayopata wataitumia hapa hapa Tanzania kwa maendeleo zaidi. Hivi kweli tungekubali jambo hili bila kujiuliza hasara zake kwa Taifa letu? Huu Ujamaa tunaosema kuwa ndiyo shabaha yetu tungeujengaje? Twawezaje kutegemea nchi za nje na Kampuni za nje kwa misaada na mikopo na raslimali kwa maendeleo yetu bila kuhatarisha uhuru wetu? Waingereza wana methali isimayo “Amlipaye mwimbaji ndiye huchagua wimbo”. Tutawezaje kutegemea nchi za kigeni na Makampuni ya kigeni kwa sehemu kubwa ya maendeleo yetu bila kuzipa nchi hizo na makampuni hayo sehemu kubwa ya uhuru wetu wa kutenda tupendavyo. Ukweli wenyewe ni kwamba hatuwezi.
Tukariri basi. Tumefanya makosa kuchagua fedha, kitu ambacho hatuna, kiwe ndicho chombo kikubwa cha mipango yetu ya maendeleo. Tunafanya makosa kudhani kuwa tutapata fedha kutoka nchi za kigeni. Kwanza, kwa sababu kwa kweli hatuwezi kupata fedha za kutosha kwa maendeleo yetu. Na pili, hata kama tungeweza, huko kutegemea wengine kungehatarisha uhuru wetu na siasa nyingine za nchi yetu.
Julius Nyerere - Azimio la Arusha (1967) Uk. 13 - 19.
Maswali:
a. Msimamo wa Ndugai kuhusu Mikopo unakaribiana na huu wa Azimio la Arusha
b. Msimamo wa Azimio la Arusha ni potofu na hivyo msimamo wa sasa wa kifikra wa serikali ndio sahihi - tutegemee mikopo na misaada kuleta maendeleo?