Nimezipata, japo kwa ufupi kutoka kwa mmoja anayeishi hapo.
Kisa chenyewe kimetokea katika parokia ya Kipalapala iliyopo karibu kabisa na seminari. Hapo parokiani alikuwepo padre mpya, siku chache tu toka apadirishwe. Majambazi hao walitaka kupora vijizawadi alivyozawadiwa kijana huyu na waamini katika kumpongeza kwa kuupata upadre. Kwa kweli, kadiri ya mzungumzaji, hapakuwa na vitu vya thamani kiasi cha kuwafanya majambazi wurushiane risasi na walinzi wa seminari! Wanasema majambazi walifaulu kuchukua vitambaa vya kushonea nguo na zawadi nyinginezo na pia kiasi fulani cha pesa.
Padre mhusika hakupigwa kwani alitulia humo ndani mwake, wavamizi hawakumwona. Padre mwingine ndiye aliyeteswa sana na kujeruhiwa, akishurutishwa kutoa chochote hasa hizo zawadi alizopewa padre mpya.
Kilio kiliposikika wanakijiji waliizingira parokia, ndipo wavamizi waliaanza kurusha risasi hewani. Wanakijiji walijitahidi kutumia zana walizokuwanazo kama vile mawe, na wavamizi walianza kutafuta mpenyo kutoroka. Njia waliyopitia ndio hapo seminarini, ambapo walipita huku wakirusha risasi. Walinzi wa seminari walianza kujibu mapigo na wanachuo/waseminari walipasika kujificha kwa muda. Mambo yaya yalidumu kwa muda wa nusu saa hivi, na Polisi walifika eneo la tukio baada ya majambazi kukimbia, bila shaka watawasaka ili sheria ichukue mkondo wake.
Basi hivyo ndivyo nilivyozipata, nimeandika kwa ufupi.
Ninatoa pole nyingi sana kwa wanajumuia wote wa Kipalapala. kwa namna ya pekee, huyo padre majeruhi, na wote walioathirika kwa namna moja au nyingine. Ni kitu cha kushangaza kidogo, zawadi za upadirisho tu ndizo zinasababisha yote haya!