Senegal: Patrick Vieira atangazwa kuwa kocha mpya wa Simba wa Teranga

Senegal: Patrick Vieira atangazwa kuwa kocha mpya wa Simba wa Teranga

Richer

JF-Expert Member
Joined
Jun 9, 2025
Posts
2,318
Reaction score
4,079
Aliyekuwa kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Patrick Vieira, ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Senegal, maafisa wa soka nchini humo wametangaza Jumanne.

Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limetangaza kupitia mtandao wa kijamii wa X, leo Agosti 18, 2026, kwamba, “Patrick Vieira ndiye kocha mpya wa timu ya taifa ya Senegal.”

Shirikisho hilo limeongeza kuwa tarehe ya kumtambulisha rasmi pamoja na maelezo zaidi kuhusu uteuzi huo vitatangazwa baadaye.

Vieira mwenye umri wa miaka 50, ambaye alizaliwa jijini Dakar, Senegal, anachukua nafasi ya Pape Thiaw, ambaye alimaliza muda wake baada ya timu ya Senegal, maarufu kama Simba wa Teranga, kutolewa katika hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia la FIFA msimu huu wa kiangazi.

Soma Senegal yamtimua kocha Pape Thiaw na benchi lake la ufundi

Vieira alianza kazi yake ya ukocha katika ngazi ya juu akiwa na klabu ya New York City FC ya Ligi Kuu ya Soka ya Marekani (MLS), aliyoifundisha kuanzia mwaka 2016 hadi 2018.

Baadaye alifundisha klabu za Ligue 1 nchini Ufaransa, Nice kuanzia 2018 hadi 2020 na Strasbourg kuanzia 2023 hadi 2024. Pia aliwahi kuwa kocha wa Crystal Palace ya Ligi Kuu ya England kuanzia 2021 hadi 2023.

Kazi yake ya mwisho ya ukocha ilikuwa katika klabu ya Genoa ya Serie A nchini Italia, ambako alifundisha kuanzia Novemba 2024 hadi Novemba 2025.

Vieira aliisaidia Genoa kupanda kutoka nafasi ya 17 hadi kumaliza msimu wa 2024-25 ikiwa nafasi ya 13, ikiwa na tofauti ya pointi 12 dhidi ya eneo la kushuka daraja. Aliondoka baada ya timu hiyo kuanza msimu uliofuata bila kupata ushindi.

Akichukuliwa kuwa mmoja wa viungo bora wa kizazi chake, Vieira alikuwa sehemu ya timu ya taifa ya Ufaransa iliyotwaa Kombe la Dunia mwaka 1998 na UEFA Euro 2000.

Katika ngazi ya klabu, Vieira alicheza mechi 406 akiwa na Arsenal, akiisaidia klabu hiyo kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu ya England na FA Cup katika misimu ya 1997-1998 na 2001-2002.

Baadaye akiwa nahodha, aliiongoza Arsenal ya “Invincibles” kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu wa 2003-2004 bila kupoteza mchezo hata mmoja.

1787069087176.png

Patrick Vieira, Kocha mpya wa Simba wa Teranga
​
Historia ya Ukocha
  • Manchester City Academy (2013–2015)
  • New York City FC (2016–2018) — Asilimia ya ushindi: 44%
  • OGC Nice (2018–2020) — Asilimia ya ushindi: 39%
  • Crystal Palace (2021–2023) — Asilimia ya ushindi: 29%
  • Strasbourg (2023–2024) — Asilimia ya ushindi: 34%
  • Genoa (2024–2025) — Asilimia ya ushindi: 27%
 
Atauweza kweli ubabaishaji wa viongozi wa vyama vya soka vya Afrika?
 
Back
Top Bottom