- Feb 10, 2006
- 4,324
- 13,967
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SERIKALI HAIPENDI KUONA WANANCHI WAONEWA PINDA
Ametoa kauli hilo leo asubuhi (Alhamisi, Juni 4, 2009) wakati akijibu maswali yaliyoulizwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwenye ukumbi wa Mikutano wa CCT/CTC mjini Dodoma.
Alikuwa akijibu swali la kwanza lililoulizwa na Askofu wa KKKT - Kaskazini Mashariki, Dk. Steven Munga ambaye alitaka kujua Serikali ina msimamo gani juu ya wananchi wanaonyanyaswa au kuuawa katika maeneo ya migodi au hata kuwekewa sumu katika mito wanayoitumia kwa maji ya kunywa..
Waziri Mkuu alisema licha ya juhudi mbalimbali ambazo Serikali imekuwa ikichukua bado matendo kama hayo yamekuwa yakifanyika iwe katika makampuni, mashamba binafsi au migodini.
Alisema suala la migodoni alilogusia Askofu munga ni nyeti kwa sababu linagusa hisia za watu wengi na ndiyo maana Rais Jakaya Kikwete aliunda Tume ya Bomani na kuitaka ifuatilie mambo mengi ambayo yamekuwa yakinungunikiwa na wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya migodi.
Alisema ripoti hiyo imekwishakabidhiwa Serikalini na pindi utekelezaji wa mapendekezo yake utakapoanza, utapunguza baadhi ya mambo yaliyolalamikiwa kwenye ripoti hiyo.
Akifafanua zaidi Waziri Mkuu aliwataka wamiliki wa migodi hiyo wawe na staha na waijali jamii inayowazunguka. Kuna haja ya Serikali kuipitia upya sekta hii kwa sababu wanaoathirika hapa ni Watanzania, tukiwaacha na kuwapuuza haya uliyoyasema ndiyo yanajitokeza,.
Akijibu swali la pili lililoulizwa na Dk. Mwita Akili ambaye ni Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, aliyetaka kujua ni kwa nini Serikali inaachia wananchi wanajenga katika maeneo yaliyozuiliwa halafu inakuja kuendesha bomoabomoa wakati kuna watendaji hadi katika Serikali za Mitaa, Waziri Mkuu alisema kutokujua sheria siyo utetezi wa kisheria kwani hata kama kuna watendaji hiyo siyo dhamana kwamba watu waendelee kuvunja sheria. Hii siyo dhamana kwamba mtu aendelee kujenga ndani ya eneo la akiba ya barabara eti kwa sababu hajaambiwa na mtendaji wakati akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria , alisema.
Hata ukiangalia ujenzi holela wa nyumba, hakuna mtu anaweza kujenga mahali bila kupangiwa. Hapa Dodoma hatuwezi kuruhusu pawe na squatters hata kidogo, kabla hujajenga nenda kaulize kwenye ofisi ya mtendaji taratibu zikoje ili ujue kama eneo hilo ni halali au la, alisema.
Naye Askofu Jacob Mameho ole Paulo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Morogoro alitaka kujua Serikali imejifunza nini na zoezi la kuhamisha wafugaji maeneo ya Ihefu, Ifakara ya bonde la Rukwa na kwa nini Serikali haiondoi wakulima waliovamia maeneo ya wafugaji.
Akijibu swali hilo Waziri Mkuu alisema katika kikao cha Bunge kilichopita Serikali iliamua kusitisha zoezi la kuhamisha wafugaji kwa sababu kuwepo kwa mapungufu mengi ya kiutendaji katika zoezi hilo. Alisema mkoa wa Morogoro ndiyo unaongoza kwa idadi kubwa ya watu waliokufa kutokana na zoezi hilo.
Baadhi ya watendaji wamekamatwa kwa rushwa, baadhi ya wafugaji wamerudishiwa mifugo yao ukiuliza sababu hupati, baadhi ya watendaji wamenunua mifugo iliyokamtwa kwa sababu ulikuwa inauzwa kwa bei chee na haya ndiyo masuala ya maadili ya viongozi tuliyoongelea leo kama kiongozi, huyu mtu alipaswa asiguse hata ngombe mmoja, alisema.
Akifafanua, Waziri Mkuu alisema bado kuna tatizo ambalo kuhusu migogoro ya wafugaji na wakulima ambalo halijachunguzwa kwa umakini. Bado kuna tatizo ambalo hatujalijibu, nimepanga tukimaliza Bunge la Bajeti niende mikoa ya wafugaji ya Mwanza, Shinyanga, Manyara na sehemu ndogo ya mkoa wa Singida maana huko ndiko kwenye matatizo, alisema huku akishangiliwa.
Kama Serikali bado hatujakaa na wafugaji na kuainisha tatizo ni nini hasa kama tatizo ni maji, malambo, majosho au malisho nini basi dawa yake? Inabidi tuangalie mahitaji halisi na kuamua malambo na majosho mangapi yajengwe, au eneo la malisho litengwe kwa ajili ya idadi kadhaa ya mifugo, mingine iuzwe ili inayobaki itoshe kwenye eneo lilipangwa alisema.
Alisema: Inabidi yajengwe machinjio ya kutosha ili wafugaji wauze nyama kwa faida na si kwa bei ya kutupa na kuwapa hasara kama wakati wa zoezi lililopita changamoto ziko huko na dawa si kusafirisha mifugo hadi Rukwa kwa vile umesikia kuna bonde la malisho.
Akitoa mfano wa mkoa wa Dodoma, Waziri Mkuu alisema kuna machinjio ya kisasa moja tu wakati wafugaji waliopo ni wengi. Hebu jiulize ni kwa nini hali iko hivi? Alisema kuna haja ya kupima maeneo na kuweka mifumo ya miundombinu ambayo itawapa wafugaji uhakika wa masoko.
Alisema katika mkutano uliomalizika jana jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete wa kujadili mbinu za kuinua kilimo Tanzania, washiriki walikubaliana kuweka mifumo ya uwekezaji ya kusaidia wafugaji ili kuboresha sekta hii.
Waziri Mkuu amerejea jijini Dar es Salaam leo mchana ili kuhudhuria kikao cha Kamati Kuu ya CCM.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
DAR ES SALAAM
ALHAMISI, JUNI 4, 2009