Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,833
- 1,301
NAIBU WAZIRI EXAUD KIGAHE - SERIKALI IMEANZISHA MFUKO & PROGRAM KUWAWEZESHA KIUCHUMI WANAWAKE WASIOJIWEZA
Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda Na Biashara Mhe Exaud Kigahe amesema Serikali imeanzisha mifuko na programu za uwezeshaji kwa lengo la kuwawezesha na kuwainua wananchi kiuchumi wakiwemo wanawake wasiojiweza.
Kigahe amesema hayo Juni 14, 2023 Bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Mwantumu Dau Haji katika swali lake je Serikali ina mpango gani wakuwawezesha na kuwainua kiuchumi wanawake wasiojiweza
Akijibu swali hilo Kigahe amesema Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imeendelea kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini - Awamu ya Pili kwa kuhawilisha ruzuku ili kuwawezesha wananchi wasiojiweza ikiwemo wanawake kupata mahitaji ya msingi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kujiunga kwenye vikundi na kuanzisha shughuli za kiuchumi.
Amesema Serikali imeanzisha mifuko na programu za uwezeshaji kwa lengo la kutatua changamoto zinazozuia wananchi wakiwemo wanawake wasiojiweza kutoa mchango katika kukuza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla. Hadi kufikia machi, 2023 kuna jumla ya mifuko na Programu za Uwezeshaji wananchi kiuchumi 72 ambapo mifuko na programu 63 zinamilikiwa na Serikali na tisa (9) zinamilikiwa na Sekta Binafsi. Mifuko na programu hizo, hutoa huduma za uwezeshaji kwa wananchi wakiwemo wanawake wasiojiweza ambazo ni: mikopo, ruzuku, dhamana ya mikopo na ukuzaji ujuzi kwa wananchi wakiwemo wanawake wasiojiweza.
Kigahe amesema Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Mamlaka za Maeneo ya Utekelezaji wa Mpango 134 imeendelea kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa kuweka akiba na kuwekeza. Jumla ya vikundi vya kuweka na kukopa 43,302 vya walengwa wa Mpango wa TASAF vimeundwa vyenye jumla ya wanachama 578,776. Kati ya wanachama hao, wanawake wasiojiweza ni 492,479 (85.1%) na wanaume wasiojiweza ni 86,297 (14.9%).
Aidha amesema Serikali kupitia mifuko na programu zinazotoa mikopo na dhamana ya mikopo imeendelea kuwawezesha wananchi wakiwemo wanawake wasiojiweza kwa lengo la kuanzisha na kuendeleza biashara. Katika mwaka 2022/23, kiasi cha shilingi bilioni 713,790,924,000.00 kilitolewa kwa wajasiriamali 2,203,838 wakiwemo wanawake 1,234,149 na wanaume 969,689.