Torra Siabba
JF-Expert Member
- Jul 24, 2016
- 243
- 287
Kijiji chetu kipo Kata ya Uyui, Manispaa na Mkoa wa Tabora, kilianzishwa Mwaka 2010 na watu wakaanza kuishi hapa rasmi Mwaka 2015, lakini tangu wakati huo pamoja na kukua kwa kaya za watu kwenye hiki kijiji, hatujawahi kujengewa shule iwe ya sekondari ama ya msingi, badala yake watoto wetu wamekuwa wakisafiri umbali mrefu zaidi ya kilometa 12 kila siku kwenda kuifuata elimu jambo ambalo linasababisha Mdororo wa kielimu kwenye kijiji chetu na ufaulu ukishuka siku hadi siku.
Kwa sasa Watoto wetu wanasoma shule ya msingi iliyopo kwenye kijiji jirani cha Uyui, na hapo ndio kuna umbali wa Kilometa sita wakati wa kwenda, hivyo kwenda na kurudi watoto wetu hawa wanatembea Kilometa 12 kila Uchwao kufuata elimu jambo ambalo sio sawa hata kidogo.
Kwakweli kukosekana kwa shule ya msingi na sekondari iliyopo karibu kwenye hiki kijiji inatupa wakati mgumu.
Maana Mzazi huwezi kuacha kwenda kutafuta ugali wa familia eti kila siku ukamsindikize mwanao kwenda shule, sasa shughuli zingine za maendeleo nitazifanya saa ngapi?
Wakati wa kwenda shule kwa kuwa kuna misitu mikubwa kuna vijana ambao hujificha kwenye hiyo misitu, wale vijana huwakamata watoto wetu wakati mwingine kuwabaka, huwafanyia vitendo vya ukatili au kuwatishia.
Hapa tena tunalazimika kufyeka njia ili watoto waone kwa umbali mrefu wanapoenda hata wakiwa mbali ili wakiwaona hawa vijana wajue namna ya kuwaepuka aidha kwa kurudi nyumbani au kwa kutoa taarifa ili wapate usaidizi.
Sababu ya umbali uliopo baina ya kijiji chetu na shule, kuna watoto zaidi ya asilimia 60 hawaendi kuanza masomo ya awali sababu ya umbali, wengine imefikia hatua wanaanza darasa la kwanza wakiwa na miaka 10 hii yote ni kuogopa kumtembeza mtoto wa miaka mitano hadi saba umbali mrefu kwa kuwa anaweza kudumaa.
Kingine ni kwamba sisi wakazi wa huku wenye muamko na elimu ni wachache sana tena kwa kipindi hiki ambacho shule ziko mbali wazazi wanawatumia watoto wao kwenye shughuli za kilimo na biashara kutokana na shule kuwa mbali, na hapa ndipo tunajenga takwimu za Mkoa wa Tabora kuongoza kwa wasiojua kusoma wala kuandika.
Shule iliyoanza kujengwa imeishia njiani
Kutokana na changamoto hii ya ukosefu wa Shule ya msingi na sekondari kwenye kijiji chetu, tuliamua kukubaliana tujenge shule ya Msingi kwenye kijiji chetu ili watoto hawa wapate eneo la karibu la kusoma, tulijichanga tukajenga msingi na malengo ni kuwa na vyumba viwili vya madarasa pamoja na ofisi moja ya waalimu.
Nguvu yetu imeishia kwenye msingi pekeake na gharama za kumaliza hili jengi ni Sh milioni 46, hivyo tunaendelea kujichanga ili watoto wapate elimu iwasaidie kwenye maisha yao.
Wakati hilo likifanyika iko haja kwa mamlaka za Manispaa ya Tabora kuja na mpango wa kuhakikisha elimu bora kwa wote inatolewa kwa uhakika tofauti na hali ilivyo sasa maana Inafahamika Elimu ni ufunguo wa maisha hivyo kijiji chetu kipewe kipaumbele kwa kutugengea shule ili watoto wetu nao wasome.
Nina mengi ya kusema kwa leo naishia hapa.... Bwana awe nanyi