MUDA umewadia kutafakari, kama nchi, kuwa na muundo wa Muungano wa Serikali Tatu. Inawezekana tusikubaliane au tukakubaliana kuwa na muundo huu katika kipindi hiki cha kuandika Katiba Mpya. Lakini, si dhambi kutafakari kwa mapana.
Muundo tulionao, ambao bila shaka umetulea kwa miaka takribani 50, haujaleta tija yenye mashiko na ndiyo chanzo cha matatizo ambayo yamekuwa yakibadilishwa maneno kwa takribani miaka 50 ya Muungano huu. Yameitwa matatizo na baadaye changamoto, na sasa kero.
Suala la Serikali Tatu siyo jipya. Kuna taarifa lukuki za Tume na Kamati mbalimbali zilizopendekeza hili katika miongo kadhaa iliyopita. Kati ya kamati na Tume hizi, zipo zilizoongozwa na watu wenye heshima kubwa na iliyotukuka nchini. Kati ya Kamati na Tume hizo, zipo za Tume ya Jaji Mkuu Mstaafu Francis Nyalali ya mwaka 1991; ipo ya Jaji Robert Kisanga ya mwaka 1998; ipo ya Jaji Mark Bomani na nyingine nyingi. Zipo pia zile zilizojikita katika kero mahususi kama ile Kamati ya William Kusila; Kamati ya Mzee Edwin Mtei na nyingine nyingi.
Mbali ya hizi, wapo wanasiasa na wasomi wengi waliopendekeza, kupitia maandiko na hotuba mbalimbali, kuridhiwa kwa muundo wa Serikali Tatu. Hawa ni pamoja na Mzee Pius Msekwa, Spika Mstaafu na Kiongozi wa Chama cha Mapinduzi wa muda mrefu, akiwahi pia kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa chama hicho kikongwe. Humu pia pia yumo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif na wengineo wengi, ambaye ameenda mbali zaidi na kutaka Muungano wa mkataba.
Muundo wa Serikali Mbili una matatizo gani?
Kuna mambo mawili yanayoweza kuzungumzwa kuhusu muundo wa sasa. Mosi ni migogoro, ambayo nina diriki kuiita mikubwa, ya kikatiba na kisiasa ambayo yumkini imesababishwa na muundo huu. Hii ni pamoja na kuondoka madarakani kwa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Mzee Aboud Jumbe mwaka 1984 na pia kuundwa kwa kundi la wabunge 55, maarufu kama G55, lililodai na kuwasilisha bungeni hoja ya kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika mwaka 1993. Katika matukio yote haya mawili, malalamiko (kutoka pande zote) yalikuwa kuwa muundo wa serikali mbili una upungufu na hivyo na kutaka mabadiliko kuiongezea Zanzibar madaraka kuhusu mambo yake na kuunda Serikali ya Tanganyika.
Jambo jingine, la pili, mbali na migogoro ya kikatiba na kisiasa, ni hizi ambazo leo tunaziita kero za Muungano. Kimsingi, kero hizi zimekuwa zikiongezeka katika kipindi chote cha uhai wa muungano wetu wakati, katika hali ya kawaida, zilitakiwa kupungua na hatimaye kumalizika kabisa na hivyo kutufanya tuishi kama ndugu. Ukichambua kwa makini, kama ambavyo Tume na Kamati mbalimbali zimewahi kufanya, kero zote zinazotajwa ni matokeo ya mfumo au muundo wa Muungano wetu.
Kero zenyewe, ingawa zinaorodheshwa kuwa ni nyingi, lakini ukweli zinagusa maeneo makubwa mawili ulinzi wa utambulisho wa Zanzibar na hata iliyokuwa Tanganyika katika Muungano; na pili mamlaka ya Zanzibar na hata iliyokuwa Tanganyika katika kuamua mambo yake hasa yale yanayogusa haki za Zanzibar kiuchumi, kijamii na kisiasa. Kila upande unaona utambulisho wake, iliyokuwa nao kabla ya kuungana, umepotea au unapotea kila uchao.
Binafsi, hili ni jambo jema na nawashangaa wale wanaoona eti utambulisho wao unapotea. Mnapoungana, kama vile ndoa, haitegemewi mmoja wenu aendelee na mambo yote ailiyokuwa nayo awali. Hii ndio ile kwa kimombo inaitwa the spirit of give and take. Lakini, nchi yetu ni ya kidemokrasia, na kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni.
Historia ya Muungano wetu
Labda turudi kwenye hoja yetu ya leo kuhusu muundo wa Serikali mbili. Tunaambiwa na kusoma kuwa Muungano wetu ulioundwa mwaka 1964 ni matokeo ya Hati ya Muungano (Articles of the Union). Hati hii iliridhiwa na sheria mbili, Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964 (kwa Tanzania Bara) na kwa Zanzibar sheria yake nayo iliitwa Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964.
Lakini nini kipo au tuseme kilikuwa katika hii Hati ya Muungano? Tunasoma na kufundishwa kuwa, kimsingi, ibara ya nne ya hati hii ilikuwa na mambo 11 tu ya Muungano, na kuongezwaongezwa hadi kufikia 22 leo hii. Tume ya Mzee Warioba inapendekeza yawe saba tu ambayo ni Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Uraia na Uhamiaji; Sarafu na Benki Kuu; Mambo ya Nje (sio ushirikiano wa kimataifa); Usajili wa Vyama vya Siasa; na mwisho ni Ushuru wa bidhaa na mapato ya maduhuli yatokanayo na mambo ya Muungano.
Labda tukumbushane hayo mambo 11 yaliyokuwemo katika Hati ya Muungano Katiba na Serikali ya Jamhuri Muungano; Mambo ya Nje; Ulinzi; Polisi; Mamlaka ya kutangaza hali ya hatari; Uraia; Uhamiaji; Biashara ya Nje na Mikopo; Utumishi katika Serikali ya Muungano; Kodi ya mapato, makampuni na ushuru wa forodha; na mwisho ilikuwa ni bandari, usafiri wa anga, posta na simu.
Ukiangalia orodha ya mwaka 1964 na ukiilinganisha na hii iliyotolewa juzi na Mzee Warioba, utagundua kuwa angalau zinakaribiana. Kwa lugha nyingine, orodha zote mbili zimejikita katika mambo ya kidola na kinchi tofauti ambayo kimantiki ndiyo yanapaswa kuwa ya Muungano. Haya mambo ya afya, elimu, maji, nishati, mali asili waachiwe washirika. Tukifanya hivi, tutakuwa tumemaliza mambo mawili, kila mshirika atahangaika na mambo yake ya kiuchumi na kijamii lakini pia ule utambulisho ambao wote wamekuwa wakiona unapotea, wataona wamerudishiwa. Tutakuwa na Tanganyika na Zanzibar na muungano wetu wambao wote wanaukubali.
Hata sasa tuna Serikali tatu
Pamoja na mambo mengine, Hati ya Muungano inataja mfumo wa Serikali mbili yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Lakini tukiangalia historia na hata hali ya sasa ya mfumo huu, tunaona mamlaka tatu za utawala. Mamlaka ya Muungano; Mamlaka ya Tanzania Bara; na Mamlaka ya Zanzibar. Kwa lugha nyepesi kueleweka, na kwa minajili ya makala hii tuzibatize hizi mamlaka jina la Serikali kwa hiyo, tuna Serikali Tatu ingawa hii ya tatu haionekani wazi, yaani maruhani.
Tutakumbuka kuwa wakati fulani, kabla ya mwaka 1994, kiongozi wa mamlaka ya Muungano alikuwa akiitwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akisaidiwa na makamu wa Rais wawili mmoja akiwakilisha Mamlaka ya Zanzibar (ambaye pia alikuwa Rais za Zanzibar) na mwingine mamlaka ya Tanzania Bara. Hata baada ya mabadiliko ya mwaka 1994, mamlaka hizi hazikuondoka na kilichobadilika ni majina ya wawakilishi wa mamlaka hizo tu Rais wa Zanzibar; Rais wa Muungano; na Makamu wa Rais.
Ni vema kukumbuka kuwa ibara ya 47(3) ya Katiba yetu ya Muungano ya sasa imefafanua zaidi kuhusu mamlaka hizi tatu. Kwa mujibu wa ibara hiyo, iwapo Rais atatoka upande mmoja wa Muungano, basi Makamu wa Rais atatoka upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano na hivyo kila mamlaka, kati ya zile tatu, bado ipo ingawa kwa sasa, Rais Kikwete amevaa mamlaka ya Muungano na Tanzania Bara. Kwa hakika, maelezo haya yangeeleweka zaidi na labda mamlaka hizi zingeonekana vizuri zaidi, iwapo Rais wa sasa wa Muungano angetoka Zanzibar.
Nini kimezuia Muungano kuvunjika?
Muundo wa sasa wa Serikali mbili lakini wenye mamlaka tatu umedumu kwa miaka takribani 50 sasa. Ni wazi kumekuwa na kero nyingi na jitihada za kuziondoa kero hizi pia zimekuwa nyingi. Pamoja na jitihada hizi, bado kuna malalamiko, manunguniko na ubishani baina ya wananchi na wakati mwingine viongozi wa pande mbili za Muungano.
Kwa kweli, ukisoma na kupata simulizi za kweli, unaona kuna wakati Muungano ulitaka au unataka kuvunjika. Lakini nini kilichozuia kuvunjika kwa Muungano kwa miaka takribani 50 ya uhai wake? Kwa maoni yangu, tukiangalia historia, jibu la swali hili ni Chama cha Mapinduzi (CCM) na aina yake mfumo wa uongozi na kufanya maamuzi uliowekwa kwenye Kamati Kuu ya chama. Kwa hakika, kama kuna chama chenye heshima ya kuwekana sawa pale mmoja wao anapokiuka makubaliano ya chama basi ni CCM. Na hili limekisaidia chama na, kwa hili la Muungano, pia taifa.
Lakini wakati tukiliangalia mfumo huu wa CCM, ni vema pia tukakumbuka kuwa hali ya kisiasa kwa sasa imebadilika sana na hata CCM yenyewe nayo inabadilisha mifumo yake na kupeleka mamlaka kwa wanachama na wananchi ili kufanya maamuzi mbalimbali. Aidha, tuna vyama vingi na baadhi yao vinaongeza wafuasi na mashabiki kila kukicha. Vyama hivi pia vina mifumo na sera tofauti hata kuhusu Muungano wenyewe na namna ya kuondokana na kero zenyewe za Muungano.
Kwa kumalizia, sote tunakubaliana kuwa Muungano wetu una kero ambazo tunapaswa kuondokana nazo. Ukiondoa chache, nyingi ya kero tunazozisikia zinatokana na kile ambacho wengi wetu tunaona kama kunyimwa fursa za kiuchumi, kisiasa na kijamii kutokana na mfumo uliopo wa Muungano. Kama hivi ndivyo, basi ni ushauri wangu kuwa tutafakari kwa kina huku tukiweka misimamo yetu kando. Binafsi, naamini wakati umefika kufikiria kuwa na muundo wa shirikisho wenye serikali tatu. Kama nilivyosema hapo awali, kwanza tayari tuna serikali tatu, ingawa moja haionekani, ni maruh
Source: http://mzalendo.net