23rd February 2010
B-pepe
Chapa
Maoni
Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhani
Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhani, amewaonya watu wanaotoa msimamo kuhusu mgombea binafsi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Alisema hakuna raia wa kawaida, mwenye dhamana ama mamlaka inayopaswa kutoa msimamo wa suala hilo, isipokuwa mahakama pekee.
Jaji Ramadhani alisema: Hata mimi binafsi ingawa ni Jaji Mkuu, siwezi na sina uwezo wa kulizungumzia suala hilo, sasa sijui hawa watu wanaofanya hivyo wanapata wapi mamlaka hayo.
Wakati Jaji Mkuu akitoa kauli hiyo, tayari mawaziri wawili wamekwisha kutoa misimamo kwa niaba ya serikali, kwamba hakutakuwa na mgombea binafsi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Mawaziri ambao wamezungumzia suala hilo na kutoa misimamo kwa niaba ya serikali ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera na Uratibu wa Bunge), Philip Marmo.
Jaji Mkuu alisisitiza: Hata mimi sina uwezo wa kuzungumzia suala ambalo bado lipo mahakamani kwa mujibu taaluma yangu, lakini hao wengine wanaofanya hivyo
sijui.
Hata hivyo, Jaji Ramadhani hakutaka kuingia kwa undani kuhusu suala hilo na badala yake alisema wananchi wasubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ifikapo Aprili 8 mwaka huu.
Mbali na mawaziri hao, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (Nec), Rajabu Kiravu, alizungumzia suala hilo na kusema mabadiliko yatakayoruhusu mgombea binafsi, lazima yahusishwe mabadiliko ya sheria.
Pia Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila, aliyefungua kesi iliyosababisha kutolewa uamuzi wa kuwepo mgombea binafsi, amekuwa akilizungumzia suala hilo mara kadhaa.
Wiki iliyopita Membe aliwaeleza mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, kuwa suala la mgombea binafsi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu halitawezekana.
Mabalozi hao waliomba kukutana na Waziri Membe ili awaeleleze hali ya kisiasa nchini na maandalizi ya uchaguzi huo.
Membe alisema serikali haipingi suala la mgombea binafsi, lakini kwa kuwa suala hilo linagusa katiba inabidi kwanza mabadiliko ya sheria yafanyike.
Alisema mabadiliko ya katiba ni mchakato unaochukua muda mrefu, hivyo ni dhahiri kwamba mgombea binafsi hawezi kushiriki katika uchaguzi wa mwaka huu.
Mahakama kuu mwaka 2006 iliruhusu kuwepo mgombea binafsi hakumu ambayo haijabadilishwa mpaka sasa.
Wakati huo huo, Jaji Ramadhani jana alifungua mafunzo ya masuala ya takwimu kwa watendaji wa mahakama kutoka mikoa mbalimbali.
Akizungumza na watumishi hao, alisema mahakama hapa nchini inakabiliwa na uhaba wa takwimu hatua inayosababisha kusikiliza tena kimakosa kwa kesi zilizowahi kutolewa uamuzi.
Alisema kutokana na kutokuwepo takwimu za kesi mba limbali kunawafanya majaji kupelekewa kesi zilizotolewa maamuzi bila kujua.
Mafunzo hayo ya watumishi wa mahakama yaliyofunguliwa jana na Jaji Ramadhani yanafanyika chuo cha takwimu kilichopo Changanyikeni jijini Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE