Serikali yaja na mpango wa miaka 10 ujenzi wa bandari kavu mitaani

Elias Msuya

Platinum Member
Joined
Dec 23, 2011
Posts
267
Reaction score
1,014


Kutokana na ongezeko la mizigo katika bandari ya Dar es Salaam, Serikali imekuja na mpango wa miaka 10 kuanzia Julai 2026 kwa ajili ya kupanua maeneo ya kuhifadhi mizigo kwa ujenzi wa bandari kavu (ICD) mitaani.

Hayyo yameelezwa Juni 16, 2026 na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Jomaary Satura akisema mizigo inayopakuliwa bandarini imezidi maradufu.

“Kutokana na ufanisi wa bandari, kuna makontena 160,000 yanayopakuliwa kila mwezi, kiwango ambacho kilikadiriwa kufikiwa mwaka 2030. Kwa kuwa bandari sio sehemu ya kuhifadhi mizigo, ndiyo maana hizo bandari kavu zinajengwa huko mitaani.

“Katika mizigo hiyo, asilimia 90, hubaki Dar es Salaam na asilimia 10 ndio inakwenda mikoani. Kati ya inayobaki Dar es Salaam asilimia 67 inabaki wilayani Temeke ambao ndio kuna viwanda vingi na kwa sababu ndio karibu na soko la Kariakoo.

“Kwa hiyo, Baraza la Madiwani lililoketi hivi karibuni, limeidhinisha kuongezwa kwa kata 10 kwa ajili ya upanuzi wa bandari,” amesema.

Ametaja baadhi ya kata hizo kuwa pamoja na Keko, Chang’ombe, Mtoni, Mbagala na Buza.

Amesema katika mpango huo, kuna uwezekano wa wananchi kuhamishwa kwa sababu haiwezekani kuihamisha bandari.

“Ukiangalia mwanzo wa wilaya ya Temeke ni pale Bendera Tatu inapoanzia reli ya SGR kwenda mpaka Kongowe, hapo katikati huwezi kupata hata nafasi ya mita 20. Hivyo ni lazima tupange upya, ndiyo maana tumekuja na mpango huo,” amesema.

Bandari kavu zaanza kuleta kero mitaani

Miongoni mwa maeneo yanayolalamikiwa ni Wilaya ya Kigamboni, ambapo mkazi mmoja aliyeandika katika Jukwaa la Jamii Forums ameeleza kuwa ni kero.

“Mimi ni mkazi wa Mtaa wa Magogoni Wilaya ya Kigamboni, mtaa wetu umekuwa na changamoto za kuwa na bandari kavu karibu na makazi ya watu katika njia zinazoingia mtaani kwetu.

“Mojawapo imekuwa ikileta changamoto malori yanayosubiri kupakia na kushusha kontena yanapaki barabarani na kutuachia matumizi ya njia moja ambayo inatakiwa kupeleka na kurudisha magari kuelekea Kimbiji.

Soma pia: Bandari kavu kwenye makazi ya watu Mtaa wa Magogoni – Kigamboni ni hatari na kero kwa Wananchi

“Imekuwa ni kero kwa sasa Watumiaji wa njia hiyo wakati mwingine tunapata mpaka kuharibu vifaa, tunavunjiwa side mirror na magari yao yanaegeshwa njiani inakuwa kero sana. Hivi Mamlaka inakuwaje inakubali bandari kavu kama hizi zinakuwa kwenye magazi ya watu, kwanza ni hatari na inaweza kusababisha usumbufu mkubwa,” ameeleza mchangiaji huyo.
barabara ya Kilwa

Eneo lililolalamikiwa jukwaani ni Mbagala Rangitatu wilayani Temeke. Mchangiaji wa Jamii Forums amesema licha ya upanuzi wa barabara hiyo, lakini sasa kumekuwa na msongamano wa magari.

Soma pia: Hivi aliyeruhusu ujenzi wa bandari Kavu Mbagala Rangi tatu anajua changamoto inayotokea?

“Miaka yote Mbagala tumekuwa tunalalamikia juu ya foleni na ufinyu wa barabara, ilipokuja mradi wa mwendokasi tuliona inaweza kuwa utatuzi wa hiyo issue, ingawa ilipunguza kiasi lakini bado haikuondoa tatizo.

“Mwendokasi imejengwa sawa changamoto iliyopo hawakujenga stand za daladala, hii imesababisha foleni. Pale kuna terminal ambayo ni ndogo ukilinganisha na idadi ya daladala zilizopo. kumbuka hiyo Teminal pia inatumiwa na gari zinazokwenda mikoani kwahiyo imepelekea kuzidiwa.”

Mchangiaji huyo ameshauri eneo hilo lingetumika kujenga stendi kubwa ili kuwezesha magari ya mikoani na daladala kupata nafasi ya kutosha kuegeshwa na kupakia abiria, ili kupunguza msongamano wa magari na foleni kwa ujumla na kuiwezesha halmashauri kupata mapato.

Mchangiaji mwingine kwenye jukwaa ametaja maeneo ya Buza pamoja na mji mpya wa Mwanagati akisema kumekuwa na wimbi kubwa la kupachika hizi bandari kavu katika makazi ya watu jambo linaloleta kero kubwa sana ya malori maeneo ya makazi na kuleta foleni kubwa sana.

“Tunaomba mamlaka ituangalie Wananchi na kuangalia namna ya kuzisogeza hizi ICD nje ya mji, mfano kwa sasa kuna waarabu wanajenga ICD katikati ya makazi ya watu hapa Mwanagati”

Mchangiaji mwingine ametaja bandari kavu iliyoanzishwa bandari kavu chuoni karibu na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE), jambo analosema limeharibu mwonekano wa eneo hilo.

“Kwa maoni yangu haikuwa sahihi kuweka bandari kavu karibu na chuo kikibwa kama kile muda wote malori ya makontena getini uongozi ungeliangalia upya suala hili,” amesema.

Serikali yakiri ongezeko la bandari kavu

Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Dar es Salaam, Geoffrey Mkinga amekiri kuwepo kwa ongezeko la ujenzi wa bandari kavu, akisema ni kutokana na mafanikio ya utendaji wa banfari ya Dar es Salaam.

“Ni kweli kuna influx ya watu wanaojenga bandari kavu mitaani na hiyo ni kutokana na mafanikio ya bandari ya Dar es Salaam. Sasa hiyo tunafanya kazi kwa kushirikiana na wadau wengine.

“TARURA tunapojenga barabara tunaweka alama, lakini wanaosimamia sharia za usalama barabarani ni Polisi, kuna kitengo cha Wrong Parking ambacho zamani kilikuwa kwetu, lakini kimepelekwa kwenye halmashauri za manispaa na wilaya, hao ndio wanaofuatilia uvunjifu wa sharia,” amesema.

Amesema kutokana na changamoto hiyo, Serikali imeunda kikosi kazi kinachofuatilia uanzishwaji wa bandari hizo.

“Jana (Juni 15) kikosi kazi hizo kimekutana kujadili changamoto ya bandari kavu na kitatoka na mikakati ya pamoja,” amesema.

Tatizo limeanza kushughulikiwa

Meneja wa masoko na uhusiano wa Umma, wa Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC), Saidi Ahmed Mkabakuli amesema wamepokea malalamiko ya wananchi kuhusu ongezeko la bandari kavu mitaani na wameshaanza kuchukua hatua.

“Kwanza waendeshaji wa bandari kavu wanaolalamikiwa wametakiwa kuwasilisha mpango utakaohakikisha wanakuwa na maeneo ya kupaki malori ili yasiendelee kupaki kwenye barabara na kusababisha foleni na kero kwa watumiaji wengine wa barabara.

Pili, katika kipindi cha muda mfupi wametakiwa kusimamia utaratibu wa kutoa vibali vya malori kwenda kwenye yadi zao (booking system) baada ya malori hayo kuwa yamekamilisha taratibu zote za forodha ili kuondoa hali ya malori hayo kufika bandari kavu bila vibali na hivyo kukaa nje yakisubiri taratibu za kiforodha kukamilika na hivyo kusababisha foleni na kero kwa watumiaji wengine wa barabara,” amesema.

Akieleza mikakati ya TASAC katika kukabiliana na changamoto hizo, Mkabakuli amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha waendesahji wa bandari kavu wanakuwa na maeneo ya maegesho na yanatumika ili malori yasipaki barabarani.

“Kufanya na mipango ya pamoja na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mipango miji, TARURA, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kutatua changamoto ambazo ni mtambuka na kufanya marekebisho ya Kanuni za Bandari Kavu kwa lengo la kuboresha masharti ya uanzishwaji wa bandari kavu ikiwemo ukubwa wa eneo na mahitaji ya vitendea kazi ili kupunguza utitiri wa bandari hizo.”

Nyingine ni kusisitiza matumizi ya bandari kavu ya Kwala ambayo ina fursa ya kutumia reli kuhamisha mizigo kutoka bandarini na hivyo kupunguza idadi ya magari barabarani na kukamilisha taratibu za matumizi ya SGR kubeba mizigo kutoka bandarini kuelekea katika maeneo ya Morogoro na Dodoma na hivyo kuchangia kupunguza msongamano barabarani kwa kupunguza mahitaji/idadi ya magari kubeba mizigo.

 
Hizi ICD ni fursa nzuri sana kwa ajira ila ni kero mno kuziweka mjini. Miundombinu ya barabara kuwezesha ufanisi wake ni duni mno. Kero kubwa kwa wananchi ni foleni ya malori ila kuna kero nyingine kubwa zaidi hasa kwa CFA's kama ucheleweshwaji wa kuingia na kutoa mizigo ambao hupelekea ugumu wa utoaji ukizingatia kadri unavyochelewa kutoa mzigo ndivyo gharama zinazidi kuongezeka.

Wenye mamlaka wapo tu na ukifatilia kuomba unafuu unaambulia punguzo la 10% au kukosa kabisa. Ni muhimu sekta husika kujitathmini upya kwenye hili.

Pia kwenye suala la ushushaji wa empty containers ni kero sana. Gari inaweza zunguka na kontena siku 3 na zaidi kwa foleni au kukosa sehemu ya kushushia lakini bado gharama za tozo zipo pale pale kadri unavyozidi kukaa na kasha lao ndio gharama inazidi kuongezeka. Yahitajika mabadiliko.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…