Serikali imeombwa kukiongezea nguvu Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi ili uzalishaji wake ufike tani 75,000 kwa mwaka kutoka makadirio ya tani 50,000 za sasa.Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Mkulazi, Dk Hildelitha Msita wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda hicho uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, wilayani Kilosa mkoani Morogoro leo Jumatano Agosti 7, 2024.
“Mheshimiwa Rais kiwanda hiki kimejengwa kwa teknolojia ya hali ya juu kama ulivyoelekezwa na mtendaji mkuu wa kampuni, kiwanda hiki kina uwezo wa kuchakata tani 500,000 (miwa) kwa maana tunaweza tukapata tani 50,000 za sukari kwa mwaka lakini pia, ikiongezwa gharama kidogo tunaweza kufika tani 75,000 za sukari kwa mwaka.
“Pia, mheshimiwa Rais tunaomba uendelee kutoa fedha zaidi kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa barabara kwenye mashamba ya wakulima wadogo wadogo ambayo itaweza kufikisha miwa katika kiwanda chetu,” amesema Dk Msita.