BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,165

SERIKALI imetoa Mwongozo wa Mavazi kwa Watumishi wa Umma, ulioanza kutumika Julai mwaka huu ili kuboresha unadhifu.
Katika mwongozo huo, Serikali imeonya kuhusu mtindo wa sasa kwa baadhi ya watumishi kuwa na kucha ndefu au kukata nywele mtindo wa ‘rafu dread’ zenye rangi. Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa mapema mwezi huu na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, mwongozo huo wa mavazi ni kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Umma Namba 6 wa Mwaka 2020.
Kwa maana hiyo, waraka huo mpya unafuta Waraka Namba 3 wa mwaka 2007 uliokuwa ukitumika. Katika waraka mpya mambo kadhaa yameongezwa, ukiwemo unadhifu wa watumishi, kwa kuzingatia mabadiliko ya wakati na teknolojia.
Kwa kuzingatia mwongozo huo ni marufuku kuwa na kucha ndefu zaidi ya milimita tano za asili au bandia. Kwamba kucha zinatakiwa kuwa fupi, nadhifu na zisiwekwe mchanganyiko wa rangi nyingi.
Mbali na kucha, pia unadhifu wa nywele umezingatiwa, hasa kwa kuwa maisha ya sasa kuna mitindo ya ukataji nywele ama kwa wanaume au wanawake; na pia kuweka nywele bandia za mitindo tofauti.
Katika waraka huo, sasa watumishi wa umma kwa kike, hawaruhusiwi kuweka kali au ‘rafu dread’ zenye rangi. Badala yake, ukataji wa nywele kwa wanaopenda, upande wa wanawake, zinatakiwa ziwe nadhifu na si zenye mchanganyiko wa rangi nyingi. Pia, kwa watumishi wanaopenda kuvaa viatu virefu, kwa waraka huo mpya ni marufuku kuvaa kiatu kirefu zaidi ya inchi tano.
Imeelezwa kuwa madhumuni ya waraka huo, ni kuimarisha heshima ya taifa kwa kuhakikisha watumishi wa umma, wanavaa mavazi ya heshima na nadhifu wanapowahudumia wananchi ofisini. Kwa upande wa wanaume, waraka huo mpya unasisitiza na kuonya kuhusu mambo kadhaa, ikiwemo uvaaji wa viatu vya rangi mchanganyiko na vya wazi, kuvaa mikufu juu ya nguo na kuweka ndevu rangi kali.
Waraka huo umebainisha mavazi katika makundi matatu yanayoruhusiwa na viwango vya unadhifu. Kundi la kwanza ni Kiwango cha Kawaida (Casual) kwa wanawake na wanaume, ambapo mavazi katika kundi hili ni hususan yale yanayovaliwa Siku ya Ijumaa, au Sikukuu, au siku yoyote itakayoamuliwa na Mwajiri , au siku za Maadhimisho.
Mavazi yanayotakiwa kuvaliwa kwenye kundi hilo ni pamoja na blauzi yenye kola yenye maudhui ya kitaasisi na sketi au suruali na au hijabu kwa wanawake. Kwa wanaume wanaopenda kuvaa vazi la kanzu, lazima walivae pamoja na koti na baragashia kwa watumishi wa ngazi zote.
Mavazi ya Kiwango cha Kati ni pamoja na gauni na koti au blauzi yenye mikono mirefu au mifupi au hijabu, sketi, suruali na blauzi, koti, hijabu, vazi la kitenge na au hijabu kwa upande wa wanawake. Upande wa wanaume, mavazi yao katika kiwango hicho ni pamoja na suruali na shati la kitenge au kawaida au kaunda suti, tai au safari suti ya mikono mifupi, sweta, koti bila tai.
Mavazi ya Kiwango cha Juu yanayokubalika kuvaliwa kwa wanawake ni pamoja suti ya sketi/suruali na au hijabu, blauzi na sketi/ suruali na au hijabi na vazi la kitenge . Kwa wanaume ni suti za Kimagharibi, tai, kaunda na safari suti ya mikono mirefu ya kola au isiyo na kola na shati la kitenge.
Waraka huo umeelekeza pia kuwa watumishi wa umma, wanapaswa kuvaa mavazi hayo kulingana na mahali na matumizi. Kwenye mikutano inayohusisha nchi au taasisi na taifa lingine, mavazi ya kiwango cha juu yanapaswa kuvaliwa .