Kesi Namba Cc 32444/24 inayomkabili Mwalimu Saleh Ayoub (39) mkazi wa Salasala Jijini Dar es Salaam kutoka Shule ya Msingi Green Acres iliyopo Mbezi Africana, anayedaiwa kumlawiti Mwanafunzi wake (11) imeendelea Februari 17, 2025, ambapo shahidi mmoja kati ya sita upande wa Jamhuri amekamilisha kutoa ushahidi.
Shahidi huyo (jina linahifadhiwa) ambaye ni Mama Mzazi wa Mtoto anayedaiwa kufanyiwa tukio hilo, ameiambia Mahakama kwamba alifahamu kwa mara ya kwanza baada ya mtoto wake kumueleza kuwa anapata maumivu wakati wa haja kubwa huku akidai maumivu hayo alianza kuyapata tangu alipoanza kuingiziwa uume kwenye sehemu yake ya haja kubwa.
Shahidi huyo ameendelea kueleza kwamba alipoanza kumdadisi mtoto kutaka kujua nani alikuwa anamfanyia kitendo hicho, amedai mtoto alipata 'kigugumizi' kabla ya kueleza alikuwa akifanyiwa hivyo na Mwalimu Mkuu aliyefahamika kwa jina Saleh Ayoub.
Anaeleza kwamba Mtoto huyo wa kiume (jina linahifadhiwa) alimueleza kwamba Mwalimu Saleh Ayoub akiwa shuleni alikuwa anamtoa darasani na kumpeleka kwenye chumba kisicho na matumizi pamoja na kwenye choo kisha kuanza kumuingizia uume kwa nguvu kwenye sehemu ya haja kubwa na kisha kuutoa kwa nguvu na baada ya hapo kumtaka ajisafishe.
Akiongozwa na Wakili wa Jamhuri, shahidi amedai kwa maelezo ya mtoto wake, alimwambia kwamba amekuwa akimfanyia kitendo hicho mara nyingi na Mwalimu huyo huku akimtisha kwa kumwambia akisema popote atampiga amvunjevunje.
Katika hatua nyingine shahidi adai kwamba majibu ya Daktari kutoka Hospitali ambayo mtoto alipelekwa kwa ajili ya kufanyiwa vipimo mara baada ya kupewa mwongozo na Jeshi la Polisi, yalieza kwamba mtoto alikuwa ameharibika sana sehemu ya haja kubwa.
Akifanyiwa Cross-Examination na Wakili wa utetezi, Faraji Mangula, shahidi ameulizwa kama anafahamu au anahusika na taarifa ambazo zimekuwa zikiripotiwa Mtandaoni kuhusu shauri hilo, pia kama ameona taarifa hizo zinazodaiwa kuripotiwa, akijibu suala hilo shahidi amekana na kusema hafahamu juu ya uwepo wa taarifa hizo kwenye chombo cha habari ambacho hakikutajwa jina lake.
Baada ya shahidi huyo kukamilisha kutoa ushahidi wake, Hakimu Mkazi Mkuu, Hawa Magesa ameahirisha shauri hilo linalosikilizwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni mpaka Februari 26, 2025 huku akisisitiza kuwa mpaka Februari 2025 anataka mashahidi wawili wawe wamemaliza kutoa ushahidi wao ili kuepuka shauri hilo kucheleweshwa.
Itakumbukwa, mshtakiwa huyo alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza siku chache baada ya Mdau wa JamiiForums.com kuhoji sababu za kutofikishwa Mahakamani kwa Watuhumiwa aliodai wanahusika na vitendo vya ukatili katika Shule ya Green Acres iliyopo Mbezi Africana, Jijini Dar es Salaam.
Kusoma taarifa za nyuma za kesi hii, bofya:
~ Walimu wa Shule ya Green Acres (Dar) wanaotuhumiwa kulawiti na kuwadhalilisha Wanafunzi, wanalindwa na nani?
~ Dar: Mwalimu wa Shule ya Green Acres anayedaiwa kumlawiti Mwanafunzi wake afikishwa Mahakamani
~ Watu 6 kutoa ushahidi Kesi ya Mwalimu wa Shule ya Green Acres anayetuhumiwa kumlawiti Mwanafunzi wake
~ Ushahidi wa Kesi ya Mwalimu wa Green Acres, Saleh Ayoub anayetuhumiwa kumlawiti Mwanafunzi wake kuanza kutolewa Februari 6, 2025
~ Kesi ya Mwalimu wa Shule ya Msingi Green Acres anayetuhumiwa kulawiti Mwanafunzi yaahirishwa Mwezi mzima, Hakimu apata hudhuru
~ Dar: Kesi ya Mwalimu Saleh Ayoub anayedaiwa kumlawiti Mwanafunzi yaahirishwa hadi Februari 17, 2025