Nakukumbusha Mtani;
Nakujulisha mtani, ni mengi tumeshanena
Wayataka kisimani, ama zako danadana?
Nahisi mwangu kichwani, Unaikwepa dhamana
Kisima bora kutunza, nakukumbusha mtani
Ni mengi umejulishwa, na Chama shahidi yangu
Na pia ukakumbushwa, vina siri kama chungu
Halafu ukaamshwa, vina ladha na machungu!
Kisima bora kutunza, nakukumbusha mtani
Amani naye akaja, kawacha kula kobisi
Na mengi akayataja, kasema bila tetesi
Uwache wako ujanja, tafuta hata Nkasi
Kisima bora kutunza, nakukumbusha mtani
Kitu kikubwa kupenda, mengine ni siri yako
Visima vipo zote kanda, waweza vifata huko
Ufike hata Mpanda, akili kichwani mwako
Kisima bora kutunza, nakukumbusha mtani
Kwa heri ya kuonana, nina kuaga mtani
Ni mengi tuliyonena, mambo yote kisimani
Usifanye kushindana, ameshasema Amani
Kisima bora kutunza, nakukumbusha mtani
KUTUNZA HAKUNA SHAKA
kwanza pokea salamu, kheri ya mwaka mpya
mola akupe fahamu, akukinge na mabaya
wasikudhuru dhalimu, watu wenye roho mbaya
Hili ninalitambua, kutunza hakuna shaka
Na sipigi danadana, ni kweli natafutia
Nalia nae rabana, cha kheri kunijalia
meisha wangu ujana, uzee umeingia
Hili ninalitambua, kutunza hakuna shaka
Na mola nipe subira, nimechoka kusubiri
Niongoze kwenye dira, nimeshakata shauri
Ni njema yangu dhamira, naomba kiso na shari
Hili ninalitambua, kutunza hakuna shaka
Nahimiza msimamo, vya ovyo sintodandia
Angalia hilo somo, waweza jifunza pia
kwa haya yangu makamo, nitakacho kutulia
Hili ninalitambua, wajibu wangu kutunza
Amani ameshauri, kwa nini sinywi ya chupa
Si kwamba nina kiburi, siridhiki hata pipa
Naomba nawe fikiri, hivi kweli yanalipa?
Hili ninalitambua, kutunza hakuna shaka
Chama nae kajongea, asema zina fanana
kwa hapa nimegomea, nadai zinapishana
vipi wewe waongea, hebu tupe bayana
Hili ninalitambua, kutunza hakuna shaka
Nasema nikikipata, mengi nitakifanyia
kutwa kucha nakumbata, kisimani naingia
miliki nitakamata, watani nitawambia
Hili ninalitambua, kutunza hakuna shaka
SMG