Nawashukuru wote kwa tungo hizi kali sana! Thanks you have brightened my day!!!!
WOSIA NIMEUPATA
kweli nazidi shukuru, mengi wanisaidia
wanipa mwanga na nuru, kwa yale nisojulia
Nisingependa kufuru, na mola takujalia
Wosia nimeupata, nasema tazingatia
.........................................
Mchina ajulikana, popote hakosekani
Iweje twaambiana, vya bara hapatikani
si kama twachunguzana, niondoe mashakani
Wosia nimeupata, nasema tazingatia
SMG
Tungo zimeenda shule na ujumbe umefika
ZAFANANA
Mimi mchimba mahiri, kazi yangu naijua
Nimetafiti dhahiri, yote nimeyajua
Nimekula vya hariri, hakuna asiyejua
Zimefanana kwa hila, tabia na maumbile
Visima si tofauti, maumbile nagusia
Utakunywa kwa nyakati, hilo nakumbia
Fanya zako harakati, kiasi utajutia
Zimefanana kwa hila, tabia na maumbile
Kisima wakiingia, mbizi wajipigia
Hazina wakimwagia, maradhi cha kupatia
Kauli yakuishia, vilinge wavikimbia
Zimefanana kwa hila, tabia na maumbile
Sadiki yangu maneno, visima vyote ni sawa
usije jitoa meno, utamu wako maridhawa
Umejikunya kiuno, akili za kupagawa
Zimefanana kwa hila, tabia na maumbile
Usijitie kisoi , utamu wako mwenyewe
Kamuulize mtoi, mrukaji kama mwewe
Hata lile goigoi, lawa tamu kama wewe
Zimefanana kwa hila, tabia na maumbile
Chama
Gongo la Mboto DSM
Kubwa kubwa ndogo ndogo iweje kubwa iwe ndogo na ndogo iwe kubwa!!!! Hata siwezi mwaya
Haijalishi ni wapi;
Nimefurahi mtani, kisima watafutia
Mradi ni kisimani, ambapo waelekea
Iwe bara au pwani, kikubwa ni kutunzia
Kisima bora kutunza, mengine ni majaliwa
Wa bara wamenitonya, mchina awakwepea
Wasema wanawamanya, kuweza watapelia
Wanakukwepa Makanya, Malinyi pia Songea
Kisima bora kutunza, mengine ni majaliwa
Mradi kipenda roho, majiyo ukajinywea
Hata uitwe mroho, wakati wafaidia
Yawe kule Peramiho, ama Pwani asilia
Kisima bora kutunza, mengine ni majaliwa
Haijalishi mchina, na siri hiyo sikia
Mradi unajichana, kwa maji hayo sawia
Ni siri yako kijana, kwa nini kutangazia?
Kisima bora kutunza, mengine ni majaliwa
Nimefurahi mtani, na hapa nakomelea
Haijalishi ni nani, ama wapi chatokea
Si chupa ni kisimani, majiyo kujipatia
Kisima bora kutunza, mengine ni majaliwa
KUBWA NI SAWA NA NDOGO?
Kwanza acha majisifu, eti mchimba mahiri
Yaonyesha hu nadhifu, kazi kikiri kikiri
una mengi mapungufu, chunguza na tafakari
Naomba hebu nijibu, kubwa ni sawa na ndogo?
Wajidai mtafiti, kumbe wewe kimeo
koti si sawa na shati, u wapi wako upeo
Acha kujipa na chati, umeshapiga kileo?
Naomba hebu nijibu, kubwa ni sawa na ndogo?
Maumbile si yasawa, ni nyingi zimepishana
Na ile ya Havijawa, si kama eti ya Ana
Kata haiwi upawa, iweje zitafanana
Naomba hebu nijibu, kubwa ni sawa na ndogo?
Vyote vyabeba maji, kwa hili nalikubali
Tofauti ni mtaji, ladha na kwenye shughuli
Na pia kuna vipaji, mwali hamuwezi nguli
Naomba hebu nijibu, kubwa ni sawa na ndogo ?
Na ndefu nayo si fupi, jaribu kulinganisha
ureshe wako mshipi, halafu tofautisha
Hoja yako hailipi, mtani wabahatisha
Naomba hebu nijibu, kubwa ni sawa na ndogo
SMG
AKILI
Kipimo gani watumia, tueleze tupatejua
Kisima wakizamia, kiza chakusumbua
Usije angamia, kwa uroho wa kutumbua
Akili ya juu hulala, ya chini ikiamka
Macho yapo kizani, huna ukionacho
Wageuka hayawani, kwa utamu ukilacho
Mayowe ya punguani, fahamu zaruka macho
Akili ya juu hulala, ya chini ikiamka
Utakipima kwa kipi, akili zimekuruka
Umeyashika makapi, kwa akili ya mzuka
Ndefu imekuwa fupi, pasina kuna kuwa dhihaka
Akili ya juu hulala, ya chini ikiamka
Kama maji huyawezi, waachie majirani
Watakunywa kama wakwezi, warukiapo mnazini
Una papara za panzi, kisima kimekuzini
Akili ya juu hulala, ya chini ikiamka
Usijitie uchimvi, usiozaliwa nao
Kula kwangu chumvi, ujuzi nimekua nao
Usilikimbie jamvi, kwa udaku ulionao
Akili ya juu hulala, ya chini ikiamka
Chama
Gongo la Mboto DSM
Nimekumbuka zamaaaaaani enzi za Sungura sizitaki mbichi hizi
BASI UJUVI HUNAO
Chama punguza papara, mtani fanya tulia
Uache ya masighara, au umeshafulia?
Sioni lenye busara, hutaki kufikiria
Kama huwezi kupima, basi ujuvi hunao
Punguza zako porojo, eti wewe umjuzi
Kwa hoja hizi urojo, wewe ni wajuzi juzi
Muone bwana kitojo, akupe ya utambuzi
kama huwezi kupima, basi ujuvi hunao
Vipi palipo na shimo, eti ushindwe kupima
sisi wajuzi wa vimo, twaingiza yote nzima
sisemi kwa majivuno, 'machoyo' hayatopima
kama huwezi kupima, basi ujuvi hunao
Viungo 'kazie' nini, anza sasa kutumia
Au ndio majirani, wanao kusaidia?
Huu ni uhayawani, watakuja kuibia
kama huwezi kupima, basi ujuvi hunao
Heri ya kufunga mwaka, nayo ninakupatia
Mola akupe baraka, mwaka unaofatia
Aondoe ya mashaka, nilosema zingatia
kama huwezi kupima, basi ujuvi hunao
kheri akujaalie, akhera na duniani
maisha ufurahie, aondoshe mitihani
shari azikimbishie, vya watu usitamani
Kama huwezi kupima, basi ujuvi hunao
SMG
Happy new year to all of you Choveki, Yakuonea & Elli ; 2012 make the best of you. No matter how hard it is God will make the way for and your family
Peace!
Chama
Gongo la Mboto DSM
Nakukumbusha Mtani;
Nakujulisha mtani, ni mengi tumeshanena
Wayataka kisimani, ama zako danadana?
Nahisi mwangu kichwani, Unaikwepa dhamana
Kisima bora kutunza, nakukumbusha mtani
Ni mengi umejulishwa, na Chama shahidi yangu
Na pia ukakumbushwa, vina siri kama chungu
Halafu ukaamshwa, vina ladha na machungu!
Kisima bora kutunza, nakukumbusha mtani
Amani naye akaja, kawacha kula kobisi
Na mengi akayataja, kasema bila tetesi
Uwache wako ujanja, tafuta hata Nkasi
Kisima bora kutunza, nakukumbusha mtani
Kitu kikubwa kupenda, mengine ni siri yako
Visima vipo zote kanda, waweza vifata huko
Ufike hata Mpanda, akili kichwani mwako
Kisima bora kutunza, nakukumbusha mtani
Kwa heri ya kuonana, nina kuaga mtani
Ni mengi tuliyonena, mambo yote kisimani
Usifanye kushindana, ameshasema Amani
Kisima bora kutunza, nakukumbusha mtani
VIPIMO
Kibaranga wakimbia; mjini wakimbilia
Sindano nakumbia, yamjini vumilia
Uhodari wakudandia, utakuja jililia
Umechanganya hisabu, vipimo vyako batili
Mjini kuna hatari, huna ulijualo
Pokea yako habari, wamjini tujualo
Utaja pigwa kabari, na wahuni tololo
Umechanganya hisabu, vipimo vyako batili
Macheni watumbukia, baridi waibugia
Kimwana waibukia, maneno wamgusia
Nyumbani wakimbilia, kimwana wakilalia
Umechanganya hisabu, vipimo vyako batili
Kimwana chacheza shere, uani cha kupeleka
Walia kama tetere, akili yakuchanguka
Uani wala udere, vya mbele hujavishika
Umechanganya hisabu, vipimo vyako batili
Hakika imedhihiri, kula kizani huwezi
Wajitia uhodari, wa kujifanya mkwezi
Utamu wa jodari, hautazidi wa mbuzi
Umechanganya hisabu, vipimo vyako batili
Mwaka mpya waingia, tuliza wako mzuka
Makini ukiingia, mlango wa mbele tumika
Mola atajalia, kuondelea gharika
Umechanganya hisabu, vipimo vyako batili
Chama
Gongo la Mboto DSM
CHAMA HUISHI UTATA
Naja ninarudi tena, kwako kijana mtata
Lengo ni kukumbushana, ni vyema mema kufata
Usione nakuchana, Wosia hebu kamata
Chama huishi utata, hoja unavyopindisha
Na huo sio ujana, chama haujatulia
sasa watafuta lana, mola wamjaribia
kule hakuna maana, madhambi wajichumia
chama huishi utata, hoja unavyopindisha
Siseme ni yamjini, La hasha hilo ni lako
Eti kwenda kwa macheni, wewe waona ujiko
umo wewe hasarani, achana uchafu wako
chama huishi utata, hoja unavyopindisha
Hivi kwa kweli kisima, takipata magomeni?
Yaonyesha humzima, kushindia kwa macheni
wenye nazo tumepima, sioni yako 'visheni'
Chama huishi utata, hoja unavyopindisha
Na chema hutokipata, danguroni nakwambia
wapo washika ukuta, vipi wajisaidia?
Machafu umefumbata, mtani fanya tulia
chama huishi utata, hoja unavyopindisha
sasa picha napata, wewe wanamna gani
uani unavyopata, utakuwa punguwani
vinyezi kuvikamata, wewe kweli hayawani
chama huishi utata, hoja unavyopindisha
SMG