Shairi: Kongole Dayamondi

Shairi: Kongole Dayamondi

JOTO LA MOTO

JF-Expert Member
Joined
Apr 11, 2018
Posts
758
Reaction score
555
KUTOKA KWA:MSANII JOTO LA MOTO

Mondi.jpg

Ninajitokeza mbele,ninalo la kueleza.
Yule Simba wa Tandale, nataka kumpongeza.
Nimpe yake kongole,kwa kazi anavyoweza.
Msanii Dayamondi,hongera kwa hapo upo.

Alianza mwaka ule,jamii tukapokea.
Akakuwa polepole, sasa gwiji katokea.
Ana wafuasi tele,kazi wanasherekea.
Msanii Dayamondi,hongera kwa hapo upo.

Jina limevuka boda,ngazi juu umepanda.
Ulivuka zile shida,kona zote ukapinda.
Wakazuka kina dada, ushawishi wakashinda.
Msanii Dayamondi,hongera kwa hapo upo.

Mali sasa wamiliki,sanaa imezalisha.
Wapuuze wenye chuki,wapangao kukushusha.
Kama mtu hakutaki,ni bure anajichosha.
Msanii Dayamondi,hongera kwa hapo upo.

Tangu nenda kamwambie,tulianza kuelewa,
Leo acha utambie, jasho tele ushatowa,
Wenye chuki wakimbie,relini watakutowa,
Msanii Dayamondi,hongera kwa hapo upo.

Mitandaoni ni shazi, wapo maelfu kule.
Wapenzi wa zako kazi, wapiga vigelegele.
Usiifanye ajizi, uharibu kipengele.
Msanii Dayamondi,hongera kwa hapo upo.

Wenzako waelekeze, nao wafikie kule.
Kona usiwapoteze, TV waweke mbele.
Na ngoma zao ucheze,uhondo wapate tele.
Msanii Dayamondi, hongera kwa hapo upo.

Tahadhari uchukue, sifa usije kulewa.
Adui yako mjue,adhabu usije kupewa.
Mitego uitegue,yote utayotegewa,
Msanii Dayamondi, hongera kwa hapo upo.

Ila nikwambie jambo,wasifu huja na mengi.
Yatakuzingira mambo, utashindana na wengi.
Upunguze majigambo,uvihimili vigingi,
Msanii Dayamondi, hongera kwa hapo upo.

Mgema akisifiwa,tembo maji hulitia.
Usikubali kulewa, hatiani kujitia.
Ni mengi utazushiwa, ili tabu kukutia.
Msanii Dayamondi, hongera kwa hapo upo.

Boli hapa natuliza,machache nimeongea.
Nimejaribu kuwaza,yale nimejionea.
Ongeza buti kukaza,usia nakutolea.
Msanii Dayamondi,hongera kwa hapo upo.
 
Andika na ya Kiba ifunike hiyo ya Mondi.
 
Back
Top Bottom