SoC02 Shairi la Mwarubaini wa Haki

SoC02 Shairi la Mwarubaini wa Haki

Stories of Change - 2022 Competition

Anna Meleiya Mbise

New Member
Joined
Sep 7, 2022
Posts
3
Reaction score
0


Mtunzi wa Shairi- Anna Meleiya Mbise (annambise2015@gmail.com)

Jina la Shairi – Mwarubaini wa Haki


Mwarubaini wa Haki


1. Amani tunda la haki, kukua lataka wote,
Wenye viti nazo dhiki, pamoja tunda liote,
Na lenyewe si kisiki, halipendi hali tete,
Lashamiri lanawiri, penye uongozi makini.


2.Uongozi kubwa kazi, sisi sote twatambua,
Tusidhani usingizi, kulala bila fumbua,
Yahitaji usikizi, busara za kupembua,
Madhali mmeamua, fanyeni yote kwa haki.

3.Nisemapo uongozi, sisi sote twahusika,
Kwa ya familia ngazi, na ya taifa kufika,
Kila kona uongozi, wote tunawajibika,
Tusichukulie poa, tuna vyeo na wajibu.

4. Japo wote viongozi, wajibu haufanani,
Wa ile ya juu ngazi, ni wabeba tumaini,
La kuongoza jahazi, kufikia kusudini,
Mkanda wakilegeza, kwa raia ni hujuma.

5. Wale wangazi ya chini, ni pevu zao shughuli,
Watapita mitaani, kujua kero kamili,
Na wanayo kiganjani, mipango nazo kauli,
Pote wawe shirikishi, na wongoze kwa haki.

6. Wana mchango muhimu, wa jamii viongozi,
Wa dini ndio walimu, wa kimila ni wenezi,
Wa sera zetu adhimu, tena ni wasimamizi,
Wasijepewa shutuma, siasa ipende haki.

7. Nililete kwenu kundi, la mahiri viongozi,
Ndio kundi la mafundi, wenye nchi kila ngazi,
Linanenepesha hundi, kwa kodi na zao kazi,
Mlio kwenye hatamu, heshimuni wenye nchi.

8. Kiongozi alo bora, kwa sifa utamjua,
Husimama kama dira, huangaza kama jua,
Kutwa asaka busara, wala haleti kujua,
Mwarubaini wa haki, ni uongozi makini.

9. Apaswa kuwa mfano, kwa kazi kujisumbua,
Tena aunge mkono, mema mabaya chambua,
Yasiwe mengi maneno, yataja kumuumbua,
Asijione wa juu, awe na umma kazini.

10.Sheria azitumie, jamii kuikwamua,
Si wengine waumie, na kushindwa kupumua,
Hisia azipimie, na busara kuamua,
Mwarubaini wa haki, ni uongozi makini.

11. Atambue tamaduni, na ujuzi wa wazawa,
Avipende vya nyumbani, vina tija maridhawa,
Ataepuka uduni, na kuvikuza vipawa,
Awe chachu ya usawa, kwa uongozi makini.

12. Jamii yetu hakika, inayo makundi mengi,
Nyie mtaaminika, mkishirikisha wengi,
Watoto, mama na kaka, dada, wazee kwa wingi,
Watu wenye ulemavu wote wataka usawa.

13.Mazuri twayataraji, kwenu tulo wachagua,
Wageni hata wenyeji, si vema kutubagua,
Sisi tulo vijijini, kero zinatukwangua,
Tunafaidi kejeli, japo tumewaajiri.

14. Mashambani na mijini, tuna mazito mawazo,
Twaona ni uhaini, hasa huko kwenye tozo,
Twashindwa kutadhimini, ni uwezo ama uozo,
Zibeni ubadhirifu, iko wapi haki tozo?

15. Amani ya Tanzania, ni jukumu letu sote,
Uongozi dhahania, huita karaha zote,
Ni budi kukazania, haki sawa watu wote,
Mwarubaini wa haki, ni uongozi makini.

Haya ni maoni yangu ukiongeza na yako tunapata mawazo bora zaidi.

Unalipa maksi ngapi shairi hili?
 
Upvote 0
Back
Top Bottom