Kiranga sende mrama, kaditama sio kiama ,
Kienda si mwanae kwenda, kienda rudi tuanze sema ,
Nani matusi kasema, nayasaka nitoe lana ,
Raha ya nyege nyegeni, shairi lake uhuru .
Utusi u kamusini, kwani yalowekwa na nani ?
Ninayo I kamusini , hilo katazo la nini ?
Si wanayo shubakani, hawalioni kwa nini ?
Raha ya nyege nyegeni, shairi lake uhuru .
Tulikwenda na shuleni, tukakariri vichwani ,
Mwanagenzi yu huruni, kukunja viriga tungoni ,
Haya kwetu ni mageni, sizo kunga shairini ,
Raha ya nyege nyegeni, shairi lake uhuru .
Andanenga na Mloka, sifazo kwao hakika ,
Walitunga yakatundika, na Shabani msifika ,
Wote nao na Soyinka, walijua kuandika ,
Raha ya nyege nyegeni , sheria zilianza lini ????
Vitabu viliandika, vuguvugu hatakiwi
Hata peponi kufika, tiketiye hapatiwi
Vipi kufumba hakika, cheusi cheupe Kiwi
Tungo vina na mizani, vingine wenda kizani
Tungo vina na mizani, vingine wenda kizani
Utatupiga tufani, kutufunga gerezani
Tuachia tafrani, tukosekane nyumbani
Ya kivinje hutaghani, kutupaya Mikindani
Chaguzi ni kuchagua, kwa hakika kwa agua
Sifanye kujibutua, kwa tungo zenye kujua
Vipi kwenda kwa kujivua, sanaa kuiumbua?
Kwafagio kubagua, kwa majilisi vumbua
Nyege ni kunyegezana, si tungo ya lelemama
Upitie karakana, si vungo la maulana
Vipi tungo kwama kwama, kwa rula hazilalana?
Tungo za malenga wana, hazikeshi za mchana
Tungo huru nazijua, kiziona natambua
Zenda zarudi bamvua, kwa urefu ka mashua
Haiku nazo chagua, sheria zake pasua
Vipi waruka kagua, upande unapotua?
Kaditama nachutama, kata niletee maji
Shairi mithili kama, la malenga wajuaji
Silete rai za chama, za kwenda kama Bajaji
Tungo tunga za maana, wakusikize wazazi