Shairi: Sauti ya Dahuu

Shairi: Sauti ya Dahuu

JOTO LA MOTO

JF-Expert Member
Joined
Apr 11, 2018
Posts
758
Reaction score
555
KUTOKA KWA:MSANII JOTO LA MOTO.
Husna copy.png


Leo naishika peni,nilo nayo niyatoe.
Msidhani mi mgeni,maoni mnikosoe.
Ni mwenyeji kwenye fani,acheni yangu nitoe,
Sauti yake Dahuu,inanipa burudani.

Bi Husna Abduli, kongole hii pokea.
Ya kweli hii kauli,sisemi nikichekea.
Nimewaza toka mbali,na leo nimetokea.
Sauti yako Dahuu,inanipa burudani.

Moyo wangu umefura, ya ndani acha nitoe,
Wala wasipige kura, mstarini wanitoe,
Na kama nitakukera, povu ruksa ulitoe.
Sauti yake Dahuu, inanipa burudani.

Nisikiapo sauti,redioni natulia.
Walahi sifurukuti,dada nakufagilia.
Kimya tuli kwenye kiti, habari kufatilia.
Sauti yako Dahuu, inanipa burudani.

Kicheko uachiapo, haki nguvu huniisha.
Ukianza na michapo,Dada yangu unatisha.
Natamani nije hapo,nione unavyoshusha,
Sauti yake Dahuu,inanipa burudani.

Awali kukusikia,swali nilijiuliza.
Ni pua unabania, wenzio kutupumbaza.
Au labda watania, fulani wamuigiza.
Sauti yako Dahuu, inanipa burudani.

Ipo siku nitakuja,kazini nikutazame.
Getini nitakungoja, nikusikie useme.
Usije fanya kiroja, mate chini uniteme.
Sauti yake Dahuu,inanipa burudani.

Nimewasikia wengi,kwako sijakurupuka.
Tangu shule ya msingi, kabla hapa sijafika.
Sasa unashinda wengi,namba kwangu unashika.
Sauti yako Dahuu,inanipa burudani.

Ila lipo moja jambo,rekebisha nisikie.
Tena la tangu kitambo,sitaki nikuchukie.
Sema vyombo sio vombo, maana ikabakie.
Sauti yake Dahuu,inanipa burudani.

Ninamaliza kusema, ila pia nikwambie.
Usiwe kama mgema, sifa nikuharibie.
Na ukiona ni vema,na kwetu ukaribie.
Sauti yako Dahuu,inanipa burudani.
 
Da huu ana sauti ya kawaida ila inavutia sana kusikiza,,,
 
Back
Top Bottom