Shajara ya mwanamzizima: ''mjue mama kizimkazi na kwao'' sehemu ya kwanza

Shajara ya mwanamzizima: ''mjue mama kizimkazi na kwao'' sehemu ya kwanza

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
SHAJARA YA MWANAMZIZIMA:

MJUE ‘MAMA KIZIMKAZI’ NA KWAO!—1

Na Alhaji Abdallah Tambaza

1727693611219.png

ILIKUWA ni Jumapili angavu yenye nuru tokea kulipopambazuka asubuhi, Agosti 21, mwaka huu, mbele ya jumba jeupe (Ikulu) la Makao Makao ya Serikali, kijijini Chamwino, yapata kilometa 35 kutoka Dodoma, mjini.

Mahala hapo asubuhi hiyo, kulikuwa na shamrashamra, pirikapirika, vifijo na nderemo zisizokuwa na kifani; kukiwa kumetapakaa maturubai na mahema meupe ya kupendeza kuashiria kwamba kuna tukio kubwa tarajiwa siku hiyo.

‘Brass Band’ ya Jeshi la Polisi ilikuwapo; wasanii wakongwe wa ngonjera akina Mpoto na wengineo walikuwepo; vikundi vya ngoma za kiasili za kina Mwinamila wa Unyanyembe vilikuwapo; na kundi la Burudani la Toti la CCM nalo hali kadhalika lilikuwepo.

Siku ile, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT), Dk Samia Suluhu Hassan; ukipenda mwite ‘Mama Kizimkazi’, ama ‘Chifu Hangaya’, alikuwa na jambo lake yeye na viongozi wenzake wa kichifu, kijadi, kimila na kitamaduni mahala hapo.

Alikuwa ameandaa hafla maalumu ya chakula cha mchana pale mjengoni kwa heshima ya waheshimiwa wale.

Picha mbalimbali zikimwonyesha Rais Samia akiwa amevalia mavazi rasmi ya kichifu ya Usukumani – Chifu Hangaya— zilikuwa zikionyeshwa kwenye ‘maskrini’ makubwa ya runinga yaliyokuwa yamelipamba eneo hilo.

Wahudumu wa kiserikali, hususan kutoka Jumba Kuu— wake kwa waume— wakiwa wamevalia maridadi kabisa, walipita huku na kule kuwasalimia waalikwa waliokuwa wameketi kwenye ‘mameza makubwa meupe’ yaliyosheheni vilaji, vinywaji na vitafunwa pia.

Wapiga picha za TV na kamera zao; waandishi wa habari na ‘vinoti buku’ vyao, walikuwa wakiandika hiki na kile kilichokuwa kikiendelea mahala pale.

Shughuli ile, kwa kiasi kikubwa, ilikuwa imeandaliwa na kuratibiwa na waziri, mwenye dhamana ya ‘Mila na Utamaduni’, Dk Damas Ndumbaro na katibu mkuu wake Greyson Msigwa, ambao walishirikiana na Ofisi ya Rais pale Chamwino.

Ghafla, kupitia kipaza sauti, ikasikika sauti ya Mshereheshaji wa shughuli ikisema,

“Mabibi na Mabwana, tafadhali nisikilizeni… Chifu Hangaya karibu ataingia mahala hapa… tunaomba akifanya hivyo wote tusimame na kumshangilia kwa nguvu zote rais wetu huyu tunayempenda sote,” MC wa shughuli ile aliiambia hadhira iliyokuwa imetulia kama maji ya mtungini.

Kwa kishindo kikubwa, huku akisindikizwa na wapambe wake wa karibu na vifijo vikihanikiza mahala hapo, Chifu Hangaya aliingia na kuanza kusalimia watu wote, akiwafuata mlemle mezani, mmoja baada ya mwengine; akiwatania na kuangua vicheko pamoja nao pale ilipobidi!

Kwa mbali na kwa sauti za upendo, hadhira ile ikawa inaimba kwa pamoja, wimbo mashuhuri wa ngonjera za siasa:

‘Tunaimani na Samia! Oya Oya Oya! ‘

‘Tunaimani na Hangaya! Oya Oya Oya!’

‘Samia Oya, Oya! Hangaya Oya Oya!’

‘Oya! Oya! Oya!

Sasa, alipofika kwenye meza ya machifu na viongozi wa kijadi wa Mzizima (Mkoa wa Dar es Salaam)—uso wake na wangu uliangaliana— Chifu Hangaya, alitabasamu sana akasema, “Ah! Kumbe, Dar es Salaam nako kuna machifu pia!” akacheka akaenda zake.

Ni kweli, machifu walikuwepo Mzizima; tena siku nyingi nyuma kabla ya nchi haijaitwa nchi ya Tanganyika na wala wale watawala walioleta neno ‘chief’ hawajafika hapa, karne nyingi nyuma.

Walijulikana kama Madiwani, Mamwinyi, Majumbe, Maakida, Wandewa, Makadhi, wakiongoza sehemu zao za kiutawala—Diwanates.

Machifu wa Mzizima, ambao asili yao inatokana na Diwani Mwinyimadi Mwinchuguuni ‘wa Mwambao’ kule Bagamoyo aliyetawala Bandari ile ya kihistoria kwenye karne ya 1600 hivi.

Shujaa huyu, anatajwa kwa kushirikiana na kiongozi mwengine kutoka Ukutu, Dutumi kule Morogoro, Pazi Kibamanduke, ama Pazi Kilama; aliweza kupigana vita na watu wa kabila la Wakamba waliotokea nchi za Sudani na Kenya kunyang’anya, kubaka na kuharibu mali za watu (wanton destruction) kwa sababu za kijahili (ujinga tu)!

Chifu mwengine mashuhuri wa Mzizima na Dar es Salaam yake ni Digalu Kibasila, aliyesumbuana sana na Wajerumani waliovamia nchi yetu kibabe.

Watu wamezowea kumpa sifa hizo Mkwawa Mkwavinyika peke yake na Mbano Songea kwenye Vita vya Majimaji vilivyopoteza maisha ya watu wetu wengi siku hizo akiwamo na Chifu Mkwawa aliyejinyonga na Mbano kunyongwa na Wajerumani wale makatili.

Lakini, mara zote humsahau Digalu Kibasila wa Uzaramuni, ambaye alitengeneza gobole yeye mwenyewe kienyeji na aliweza kuwaua Wajerumani wanne kwa bunduki yake hiyo ya ‘mabua’.

Wajerumani walimsaka kwa udi na uvumba kila kona ya nchi hii bila mafanikio akiwa amewatorosha wakeze na wanawe watorokee sehemu tofauti tofauti nchini.

Mmoja wa watu waliomficha na kumhifadhi Chifu Kibasila asipatikane kirahisi na Wajerumani alikuwa ni Mzee wa Kizaramu kutoka Masaki, Kisarawe Madhehebi Abdallah Tulli.

Madhehebi Abdallah Tulli, ni mjomba wa Mwenyekiti wa Wazee wa Dar es Salaam, ambaye alikuwapo kama kiongozi wa kimila na kijadi akiwakilisha Mkoa wa Dar es Salaam, pale Dodoma kwenye hafla ya Chifu Hangaya.

Mwengine aliyekuwapo siku ile ni Mzee Hamis Bushiri Pazi mwenye nasaba na silsila ya Chifu Pazi Kibamanduke, au Pazi Kilama wa Uzaramuni.

Chifu Digalu Kibasila, ambaye ndiye jina lake limepewa moja ya majengo makuu ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, na ile Shule ya Sekondari ya Kibasila pale Temeke, Dar es Salaam, alipokamatwa alitiwa Gerezani na kunyongwa kikatili juu ya ‘Mwembe Kibasila’ ama ‘Mwembe Kinyonga’ uliopo pale kwenye Stendi ya Mabasi ya Mwendo Kasi Gerezani.

Machifu wengine mashuhuri wa Mzizima, ambao watu kimazoea wanasema Mzizima na Dar es Salaam haina mwenyewe, ili wapate fursa ya kugombea nafasi za udiwani na ubunge walitambulika kama madiwani kiungozi.

Kwa mfano Mzizima ya kale iliongozwa na Diwani Shomvilaali Shomvilahaji, aliyekuja kuzaa watoto waliomrithi kiungozi akina Diwani Kitembe, Tambaza, Uweje, Uzasana, Zarara, Mwenye-Kuuchimba na Gungurugwa.

Madiwani wengine ni wale wa kule Magomeni akina Ndugumbi Kitembe na Mwinyimkuu Mshindo Kitembe, ambako kote huko kuna maeneo mashuhuri ya makaburi ya kuzikia wakazi.

Kule Kinondoni na Mwananyamara ni himaya ya Diwani Mwinjuma Mwinyikambi wa Kitembe, ambaye ametoa mchango mkubwa sana katika harakati za kuikomboa nchi hii kutoka kwenye minyororo ya kutawaliwa na wazungu wakoloni.

Kama ilivyokuwa kwa nduguye Tambaza wa Upanga, Diwani Mwinjuma Mwinyikambi Kitembe alikuwa kwenye Baraza Kuu la chama cha TANU na mjumbe wa kudumu wa Halmashauri Kuu ya chama hicho akiingia humo bila kupigiwa kura.

Uhuru ulipopatikana mnamo mwaka 1961, Diwani Mwinjuma Mwinyikambi, alilitoa bure shamba lake lote lile la Kinondoni (maeneo ya Kambi ya Vijana Hosteli), iwe zawadi kwa chama chake cha ‘TANO’ ili pajengwe makazi mapya ya kisasa waishi Watanganyika wenzake waliokuwa wakibaguliwa na sheria kandamizi za kikoloni zilizotenganisha makazi kwa rangi ya mtu! (Rejea vitabu Shajara ya Mwanamzizima vilivyoandikwa na mwandishi huyu na kupatikana kwenye maduka ya vitabu ya TPH pale Samora Av. Dar es Salaam na Maduka ya IBN HZM Media Center mkabala na Msikiti wa Manyema, jijini Dar es Salaam.

Sasa, wiki hii kule Songea kunaadhimishwa Tamasha kubwa la Kitamaduni ambalo linatarajiwa kufunguliwa na ‘Chifu Hangaya’ mwenyewe, ambaye pamoja na uanamajumui wake alionao, amehiari kuwakilishwa na Waziri Mkuu kwenye kikao cha viongozi wakuu wa Umoja wa Mataifa (UN), ili yeye awepo Songea kwa tukio lile kubwa kitaifa.

Tayari machifu na viongozi wa kijadi wameshamiminika huko Songea kwa ajili ya Tamasha hilo muhimu kiutamaduni kitaifa.

Kwa sababu ambazo hazikuelezwa kisawasawa, machifu wa Mzizima hawatakuwepo kwenye hafla hizo muhimu, pamoja na kwamba, na mialiko ya kuwataka kuwa sehemu ya shughuli hiyo kuwasilishwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Ofisa Utamaduni wa Mkoa, alimwambia mwandishi huyu kwamba ofisi yake haikuwa na bajeti ya kuwahudumia machifu wa Mzizima kuwafikisha huko pamoja na kwamba ni miongoni mwa walengwa wakuu pia.

Alichofanya yeye ni kukodisha basi ndogo na kuambatana na kikundi cha ngoma za kiutamaduni kwenye tukio hilo muhimu kwa machifu pia.

Kitendo hicho kinasikitisha na kufikirisha sana sasa kimezoeleka sana nchini mwetu kwa kutothamini mchango wa watu wa Mzizima kihistoria na kiutamaduni.

Katika hotuba yake ndefu aliyoitoa siku ya kukumbukwa pale kwenye hafla ile kijijini Chamwino ilipo ofisi yake ‘Mama Kizimkazi’ alisema kwamba tayari kiwanja na michoro kwa ajili ya jengo la UTAMADUNi HOUSE limeshatengwa kule Dodoma.

Jengo hilo litakuwa ndio makao makuu ya shughuli za kichifu na uongozi wa kijadi nchini na mchoraji ameambiwa liwe na taaswira ya kiutamaduni wa Mtanzania.

Amewataka viongozi wakuu wenye dhamana ya mila na utamaduni waandae sera mpya ya kiserekali itakayotambua uwepo wa heshima ya viongozi wa kijadi kimaeneo, kikata, kiwilaya na kitaifa kwa kuwatambua uwepo wao kwenye hafla zote zinazofanyika kwenye maeneo husika!

“Nimekuiteni hapa tukutane leo ili mje mshuhudie kazi inayofanywa na Serikali yenu nanyi mkawe mabalozi mtokako kwa watu wenu kwamba tunawapenda nyote na tunatimiza ahadi tulizoweka kwa raia waliotuamini…

“Watu wanasema hakuna kinachoendelea Dodoma, hivyo mtapelekwa mkaone kazi ya ujenzi wa majengo ya Serikali kule kwenye kijiji cha Mtumba; Chuo Kikuu cha Udom; na kukamilika kwa Treni ya SGR na nyinyi ndio muwe watu wa mwanzo kuipanda ikianzia safari yake ya mwanzo kesho kuelekea Dar es Salaam,” alisema mama yule!

Kweli tuliiona; kweli tuliipanda treni ile ya kisasa ya SGR kwa mara ya mwanzo tukiwa peke yetu mpaka Dar es Salaam tukiambatana na Mkurugenzi Mkuu wa TLC mwenyewe.

Kama tulivyoona hapo juu; ni mtu ambaye anathamini sana watu wengine hata ikabidi kuandaa hafla hiyo kubwa ya machifu; ili awe amewagusa kupitia wawakilishi hao wa kijadi, watu wote wa taifa hili analoliongoza.

Jina lake halisi ni Samia Suluhu Hassan, ambaye aliuchukua uongozi wa taifa hili baada ya kutokea kifo kisichotarajiwa cha aliyekuwa rais wakati huo hayati John Pombe Magufuli.

Almanusra nchi isambaratike; kwani wale waliokuwa viongozi waandamizi wakati huo ambao walitakiwa kutekeleza matakwa ya katiba kwa kuandaa mazingira ya kumwapisha SSH, aliyekuwa Makamu wa Rais, walijiumauma na kujing’ata ndimi zao wakichagua kumnyima haki hiyo.

Haki ile ilicheleweshwa tu, lakini hatimaye aliapishwa na kuwa rais na hofu ikatanda maradufu kwa wale wababaishaji (demagogoues), kwamba ‘itakuwaje! Itakuwaje!’

Hakuna baya hata moja lilotokea hapa nchini zaidi ya ufanisi wa utendaji kazi na kuongezeka utawala bora uliochochea ukuaji wa uchumi usiomithilika.

Sasa, sijui wewe msomaji lakini kwa kweli wengi wetu tu mashahidi kwamba yule mama ambaye alijitokeza kwenye vikao vya Bunge la Katiba kule Dodoma na kuwa mmoja wa wenyeviti wa Bunge lile, akatia fora kwa umakini na umahiri wake kiungozi, leo ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Nchi hii.

Akiwa mmoja wa wajumbe wa Bunge lile, kijana mdogo Paul Makonda, alishindwa kuiacha fursa ile ipite hivi hivi; bali kwa sauti ya upole aliwaomba— kwa vile ule ulikuwa mwaka wa uchaguzi— wale wagombea urais wamweke SSH kama mgombea mwenza ili hekima na busara zake ziwe endelevu kwa taifa.

Dua ile aliyoiomba kijana Makonda ilifika mbinguni; na wakati ulipofika, MwenyeziMungu, mwingi wa rehema aliijibu na leo ‘Mama Kizimkazi’ ndiye Rais wa SMT.

Tunamwomba Mungu, ampe Mwanamama huyu uwezo zaidi, kwani kwa kila kigezo ana haki ya kuungwa mkono wa kuyaendeleza yale aliyoanzisha kwa maendeleo ya Taifa letu pendwa.

Hii ni sehemu ya kwanza ya makala hizi, lakini katika matoleo yajayo, tutamwangazia zaidi na kumdadavua hasa huyu ‘Mama Kizimkazi’ ni nani na rundo la mafanikio yake kuyaweka hadharani ili kusiwe na chembe ya shaka ya kumfanya akatishwe tamaa na wale aliowaita ‘walioota mikia na wenye vichwa vya samaki’, wanaoutaka uongozi kwa kila hali.

Alamsiki! Tukutane juma lijalo.

atambaza@yahoo.com, 0715808864​
 
Back
Top Bottom