Hukumu katika kesi ya mhubiri tata Paul Mackenzie imeendelea kufichua maelezo mazito kuhusu mafundisho ya kanisa lake la Good News International, huku Jaji Diana Kavedza-Mochache akieleza jinsi wafuasi walivyoaminishwa kuikataa mifumo ya kawaida ya maisha.
Katika usomaji wa hukumu hiyo yenye kurasa zaidi ya 1000 katika Mahakama Kuu ya Mombasa leo, Oktoba 19, jaji alisema Mackenzie alizipinga taasisi za Serikali na kuzihusisha na Shetani, huku akipinga pia Demokrasia na elimu rasmi.
Mahakama ilisikia kuwa kadri mahubiri kuhusu mwisho wa dunia yalivyozidi, baadhi ya wafuasi waliuza mali zao na kuhamia katika eneo la msitu wa Shakahola, wakiamini kuwa walikuwa wakijiandaa kwa siku za mwisho.
Kwa mujibu wa maelezo ya Jaji, kuhamia msituni kulilenga kuwatenga wafuasi na ulimwengu wa nje, ambao Mackenzie aliuwasilisha kama sehemu ya dunia iliyopotoka. Mafundisho hayo pia yalihusishwa na kuwazuia watoto kwenda shule na wafuasi kutafuta matibabu hospitalini.
Mackenzie na washirika wake wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya watu 191( watoto 190 na mtu mzima mmoja) katika kesi inayohusishwa na mkasa wa Shakahola.
Hata hivyo, elewa kuwa idadi hiyo ni ya mashtaka katika kesi hii mahususi. Katika uchunguzi mpana wa mkasa huo, zaidi ya miili 400 ilipatikana. Aidha Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu Kenya iliripoti vifo 448 katika ripoti yake ya Machi 2024.