fungafunga,
Jina hili, 'Shamba la Chumvi' linamaanisha, kwa Kiingereza, 'Salt pans', na Wavunaji wa Chumvi huyaita "mabirika ya chumvi".
Uvunaji wa Chumvi unasimamiwa na Wizara ya Madini, ikimaanisha kuwa Chumvi ni moja ya madini yanayovunwa Tanzania.
Pamoja na ukweli kuwa Jukwaa la Kilimo siyo jukwaa sahihi kwa mada hii, ningependa, kwa ufupi kabisa, nielezee kidogo kuhusu Chumvi na Uvunaji wa Chumvi.
Madini ya Chumvi, nchini Tanzania, huvunwa katika mikoa ya Kigoma (Uvinza), Simiyu (Ziwa Natron), Ukanda wa Pwani, (Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara).
Matumizi ya Chumvi nchini Tanzania yanakadiriwa kufikia tani 500,000 kwa mwaka wakati uzalishaji hapa nchini ni tani 150,000 kwa mwaka.
Upungufu wa tani 350,000 kwa mwaka unajazwa na Chumvi toka Kenya.
Chumvi iliyoko madukani yenye nembo ya K-Salt au Malindi Salt inatoka Kenya.
Kenya inatulisha chumvi wakati sisi tuna uwezo wa kuzalisha chumvi MARA TATU zaidi ya Kenya kwa sababu Pwani yetu ya Bahari ya Hindi ni ndefu zaidi ya Pwani ya Kenya.
Pwani yetu, 'shoreline length' ni kilomita1424, wakati 'shoreline' ya Kenya ni kilomita 536 tu. Hapo bado tuna Simiyu na Kigoma.
Chumvi, pamoja na kutumika kama kiungo cha chakula cha binadamu na mifugo, hutumika pia katika viwanda vya minofu ya samaki, usindikaji wa nyama, usafishaji wa maji, utengenezaji wa karatasi, uchimbaji wa visima vya gesi na mafuta, na matumizi mengine mengi sana.
Chumvi inayotumika kama kiungo cha chakula hutakiwa kuwekewa Madini Joto, 'iodine' ambayo ni chanjo muhimu sana dhidi ya mtindio wa ubongo 'mental retardation' kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano.
Kwa kumalizia, Uvunaji wa Chumvi ni FURSA ya kipekee kwa sababu CHUMVI NDIYO MADINI PEKEE DUNIANI, AMBAYO KILA UKIYAVUNA, MWENYEZI MUNGU ANAKULETEA TENA UPYA, ili uendelee kuyavuna.
Kwa lugha ya wachimbaji Madini, "Chumvi ni makinikia pekee duniani, ambayo kila ukiyavuna, Mwenyezi Mungu anajazia upya pale ulipovuna".
Taratibu za "kilimo" hiki cha chumvi zinapatikana katika Ofisi za Madini (Regional Mines Offices- RMO's) katika Mikoa ya Kigoma, Simiyu, Tanga, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.