View attachment 736318
Unamfahamu Shariff Abdallah Attas (pichani)? Mzee Attas aliishi mtaa wa Twiga na Sikukuu nyumba yake ikiwa mkabala na Msikiti wa Shadhili, jijini Dar es Salaam.
Katika miaka ya 1950 mzee Attas alikuwa akifanya kazi Soko la Karikaoo kama dalali, wakati huo Meneja wa soko hilo akiwa Abdulwahid Sykes. Sifa kubwa ya Shariff Attas ni ubingwa wake katika hesabu. Alikuwa na uwezo wa kukokotoa hesabu ndefu kichwani bila ya kutumia ‘’calculator.’’
Lakini mzee huyu alikufa na masononeko. Licha ya kuwa rafiki wa chanda na pete wa Nyerere wakati wa kupigania uhuru, lakini alipomfuata ofisini (baada ya uhuru) "alijifanya" kumsahau.
Kisa chake kimeelezwa na Mwandishi nguli wa historia nchini Mohamed Said, katika kitabu ''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924-1968)..'' (Phoenix Publishers, Nairobi, 2002). Mohamed alipata nafasi ya kukaa na mzee Attas miaka ya 1980 akamueleza jinsi alivyoshirikiana na Nyerere wakati wa harakati za kudai uhuru. Japo ushirika wake haukuwa kwenye mambo ya kisiasa, lakini alishirikiana nae kwenye mambo ya kijamii.
Mwaka 1986 Mohamed akiwa na Kleist Sykes, mtoto wa mzee Abdul Sykes (muasisi wa TANU na meneja wa zamani wa soko la Kariakoo) walikaribishwa kula sikukuu ya Eid nyumbani kwa mzee Attas.
Walipofika walikuta veranda imejaa wazee maarufu wa Dar es Salaam wanafuturu. Mzee Attas alipowaona alifurahi na kuwakaribisha nao wakajumuika katika futari.
Katikati ya futari mara Mzee Hamida Tuli akasimama na kuomba ruksa kwa niaba ya wenzake akasema, ‘’Mzee Attas tunaomba ruksa tuondoke kwa kuwa tumealikwa futari Ikulu kwa Rais Ali Hassan Mwinyi.’’
Basi ikapigwa fatha ikaombwa dua wazee wakapeana mikono na Shariff Attas hao wakatimka kwenda Ikulu kula futari na Rais. Ukumbi ukabaki watu watatu tu. Mzee Shariff Attas, Klesit na Mohamed. Kleist akamuuliza mzee Attas "wenzako wote wamealikwa Ikulu kwa Rais, wewe umebaki hapa peke yako, huna akujuaye?’’
Mzee Attas akainamisha kicha chini akazubaa kwa dakika kadhaa akitafakari jambo kisha akajibu "Kama kuingia Ikulu ningeingia enzi za Nyerere sio sasa. Nyerere yeye ndiye alikuwa mwenzangu. Mimi Mwinyi atanijulia wapi?"
Alisema mzee Shariff Attas na kuongeza;
"Miaka ya 1954 na 55 Nyerere alikua anakaa pale Stanley wakati huo ndiyo TANU inapata umaarufu. Nyerere alikuwa amesha acha ualimu, kwahiyo hakuwa na pa kukaa. Mzee Sykes akamsaidia nyumba. Akitoka nyumbani anaenda ofisi za TANU, akirudi anaenda ofisini kwa mzee Sykes pale Kariakoo. Wakati wa mchana mzee Sykes anamnunulia chakula. Siku nyingine ananiita ananiambia nifatane na Nyerere nyumbani kwa ajili ya chakula cha mchana.
Mimi na Nyerere mguu kwa mguu, tunaingia Swahili, Narung’ombe, Gogo, Mchikichi, Sikukuu hadi Stanley. Njia nzima mimi na Nyerere tunazungunza mambo mbalimbali. Wakati ule hakuna anayemjua. Alikuwa kijana wa zaidi ya miaka 30 lakini hakuwa na fedha na kazi aliacha ili akitumikie chama. Hakuwa mashuhuri.
Tunafika nyumbani kwa mzee Sykes tunakuta chakula kipo mezani tunakula tukimaliza tunarudi ofisini pale Kariakoo sokoni. Nyerere alikuwa mwenzangu na mzungumzaji wangu sana wakati ule. Akipata safari ya chama na hana mzee Sykes alikua akiagiza nimpatie. Wakati mwingine namsindikiza hadi stesheni kupanda treni. Namfungashia vyakula vya kula njiani.
Basi miaka ikenda hadi tukapata uhuru na Nyerere akawa Waziri Mkuu kabla ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962 na kuwa Rais.
Siku moja nikaenda ofisi za TANU. Nyerere akaingia. Watu wakasimama, kwa heshima ya Waziri Mkuu. Nyerere akapeana mikono na watu waliokuwa pale. Alipofika kwangu nami nikampa mkono. Akanitazama na kuniuliza "unaitwa nani?" Nikamwambia "Shariff Abdallah Attas". Akaniuliza ‘’Tumepata kuonana?’’ Nikamjibu, ‘’Hapana hatufahamiani.’’
Basi akapita zake kusalimiana na watu wengine. Kuanzia wakati huo hatukuonana tena. Urafiki wetu wa kukatiza mitaa ya Swahili na Sikukuu kwenda kula chakula cha mchana kwa mzee Sykes ukawa umeishia hapo. Yeye mtu mkubwa bwana, ameshanisahau. Waziri mkuu atanikumbukaje mimi dalali wa soko?
Kwahiyo kama ni kualikwa Ikulu ilikuwa nialikwe enzi za rafiki yangu Nyerere lakini bahati mbaya alinisahau.’’