Sheikh Yahya amtabiria JK
Imeandikwa na Maulid Ahmed; Tarehe: 9th April 2009 @ 22:01 Imesomwa na watu: 299;
Mtabiri maarufu wa Afrika Mashariki na Kati, Sheikh Yahya Hussein, aliyekuwa nchini India kwa matibabu amerejea nchini na kutabiri kuwa Rais Jakaya Kikwete ndiye atakayeshinda tena katika uchaguzi mkuu mwakani.
Mbali na hilo, ametabiri kuwa uchaguzi huo utagubikwa na wazee na viongozi kupigwa makofi na kuzomewa na kuongeza: "Kati ya Aprili na Oktoba ni kipindi cha aibu kubwa kwa watu kuwasukuma wazee na kibaya zaidi ni kwa sababu ni karibu na uchaguzi".
Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliochukua takribani saa mbili baada ya kuwasili nchini, Sheikh Yahya alisema mtu atakayeshinda urais mwakani ni ambaye amewahi kuchaguliwa na kushinda mara 10 matukio mbalimbali ambapo alisisitiza:
"Mimi namwona ni Kikwete amepata hadhi zaidi ya mara 10 ikiwamo kuunganisha Comoro na hiyo ni tiketi yake". Alitaja mengine kuwa ni pamoja na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) na kuteuliwa kwa Dk. Asha-Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Hata hiyo, alisema hampendelei Rais Kikwete na kama yupo mtu mwingine aliyewahi kushinda matukio 10 mbalimbali na atawania uongozi mwakani basi ataweza kushinda katika uchaguzi huo. Kuhusu utabiri kwa wazee kupigwa, alisema mikosi na mabalaa yataanzia kwa wazee na kutolea mfano Rais mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi na kuongeza:
"Hilo ni kofi baya na litarudiwarudiwa na hata Alhaji Mwinyi nilishamwonya, hapa nchini kutakuwa na matukio mengi ya viongozi kupigana na kusukumana". Kuhusu safari yake ya matibabu ambayo alizushiwa amefariki dunia, Sheikh Yahya alisema amegundulika kuwa moyo wake ni mkubwa hali iliyokuwa ikimsababishia kuvimba miguu na amepewa dawa za kutumia kwa miezi mitatu.
"Nilikuwa na ugonjwa ninaoudharau na Rais Kikwete akasikia na kunieleza amesikia naumwa lakini nilimwambia siumwi basi akaniambia kama siumwi niende India nikaangaliwe afya yangu na akatupatia tiketi mimi, mke wangu(anaitwa Ketty) na binti yangu na huko madaktari 12 walinizunguka kunipatia matibabu," alisimulia.
Alisema alipokuwa India aligundulika kuwa moyo wake ni mkubwa, umechoka na unashindwa kusukuma damu vizuri na katika matibabu hayo, alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi mara tatu na kutolewa. Sheikh ambaye alipelekwa India wiki mbili zilizopita, alisema ilikuwa afanyiwe upasuaji mdogo kusaidia moyo kufanya kazi vizuri, lakini waliacha na kumpa tiba ya sindano na dawa na kuongeza: "Niliingizwa kwenye kitu kama kaburi la vioo na watu wamevaa nguo nyeusi walinizunguka nilishituka kumbe lile ni kwa ajili ya kunichunguza