Duru za siasa kutoka mjini Zanzibar na Dodoma kwa nyakati tofauti, zimethibitisha kwamba wapinzani wa Dk. Shein anayepewa nafasi kubwa kutokana na kuungwa mkono na vigogo wa serikali, wamekamia kutumia sheria ya Katiba ya Zanzibar kumuengua kwenye kinyanganyiro hicho.
Vyanzo vyetu vya habari vilisisitiza kuwa Katiba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya mwaka 1984, ndiyo itakayotumika kumbana Makamu huyu wa Rais wa Muungano.
Kwa mujibu wa Katiba hiyo toleo la mwaka 2003, iliyopitishwa Julai 17, sura ya 15, kifungu cha pili kinataja sifa za mtu anayefaa kuwa Rais wa Zanzibar.
Kifungu hicho chenye sehemu (a) hadi (d), kinataja sifa za mtu anayefaa kuwa rais wa Zanziabr kuwa ni pamoja na kuwa Mzanzibari wa kuzaliwa, awe ameshatimiza umri wa miaka 40.
Sifa nyingine ni kwamba awe na sifa za kumuwezesha kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na sifa ya mwisho inamtaka awe mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa kilichosajiliwa rasmi kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa 1992.
Katika kifungu cha 2(C), kinachosema awe na sifa za kumwezesha kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, ndicho kitakachotumika kumbana Dk. Shein maana hana sifa hiyo, alisema mmoja wa makada wa CCM.
Kwa mujibu wa kifungu hicho, sifa za mtu anayefaa kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi ni pamoja na kwamba awe Mzanzibari aliyetimiza umri wa miaka 21.
Sifa nyingine ambayo wapinzani wa Dk. Shein wamejipanga kumnyuka nayo ni ile ya kifungu cha 68(b) ambacho kinasema awe amejiandikisha au ana sifa za kujiandikisha katika jimbo la uchaguzi kama mpiga kura katika uchaguzi wa Baraza la Wawakilishi.
Kifungo hicho kinadaiwa kinaweza kuwa kitanzi kwa Dk. Shein kwani hakujiandikisha katika jimbo lake la uchaguzi kama mpiga kura katika uchaguzi wa Baraza la Wawakilishi.
Kwa hiyo, Dk. Shein ana mtihani mzito wa kuteuliwa maana hakujiandikisha katika jimbo lake kama mpiga kura. Amekiweka chama na yeye mwenyewe kwenye wakati mgumu sana wa kufanya maamuzi, alisema mmoja wa wajumbe wa NEC ya CCM.
source:tzdaima