Sheria ya Mabadiliko ya Katiba: Kuna Mgongano wa Kimaslahi ama ni Maslahi ya Umma Yanalindwa?

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba: Kuna Mgongano wa Kimaslahi ama ni Maslahi ya Umma Yanalindwa?

HKigwangalla

JF-Expert Member
Joined
Feb 6, 2008
Posts
722
Reaction score
971
Wiki iliyopita niliandika makala iliyokuwa inachambua ni nini iwe njia ya kupita kufikia kukamilisha mchakato wa kukamilisha ‘sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013' kwa muafaka wa kitaifa. Kufuatia nia safi ya Mhe. Rais Jakaya Kikwete, kupitia hotuba yake adhimu kwa Taifa ya mwezi uliopita, wengi tulibaki tukijiuliza ni nini kifuate?

Mhe. Rais anataka muafaka wa kitaifa na anataka kutuunganisha watanzania wote ili tufike salama kwenye kukamilisha mchakato wa kuandika katiba mpya. Hili, narudia tena, kwa yeyote yule mwenye akili timamu na mwenye kulitakia mema Taifa letu atalikubali, na kwenye hili asirudi nyuma kamwe. Akijaribu kurudi nyuma kwa hakika nafsi yake itamsuta na kwa Mungu atapaswa kujibu. Mzigo wa Taifa hili uko mikononi mwake. Hautui mpaka dhamana tuliyompa imuondoke.

Sisi kazi yetu ni kumshauri na kuonesha tunachokitamani, na yeye atapima na kuamua.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 62 na 63, Bunge lina sehemu mbili, Rais wa Jamhuri na wabunge, na kwa maana hiyo sheria ama jambo lolote lile haliwezi kuwa limekamilishwa bila kupitia moja ya sehemu hizi. Sheria tunayoizungumzia hapa imepitia hatua ya kwanza ya kupitishwa na wabunge, inasubiri uamuzi wa sehemu ya pili sasa, Rais wa Jamhuri. Anaweza kuamua lolote kwa mamlaka aliyopewa na Katiba ya Jamhuri wa muungano, kusaini ama kutokusaini.

Katika makala ile nilijaribu kuchambua kwa ufupi sana, nini kitatokea kama angechukua njia ipi. Binafsi, nilijitahidi sana kuepuka kuonesha msimamo wangu mkali kwenye jambo hili, kwa kuheshimu mamlaka ya Rais na kuepuka kuonekana najaribu ‘kumteka nyara' fikra zake.

Ukweli utabaki kuwa ukweli tu kwamba, niliegemea zaidi kwenye njia ya muafaka wa kitaifa na ambayo itatuacha wabunge wote na watanzania ‘washindi'. Staili hii ni ya kimarekani. Inaitwa ‘win – win situation'. Sikuweka msimamo wa chama changu ila nilisema ukweli tupu.

Nimepata maoni na maswali mengi sana kutoka kwa wasomaji, nikaamua nijibu baadhi ya hoja hapa. Kwanza, nisisitize kuwa mchakato wa kupitishwa kwa sheria ile bungeni ulikamilika ipasavyo na hakukuwa na mapungufu yoyote yale kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni na tamaduni zilizopo. Wengi wanataka kuaminishwa ama wanajilazimisha kuamini kuwa sheria haiwezi kutungwa na kupitishwa na Bunge bila kupelekwa kwa ‘wadau'. Si kweli, maana si lazima. Hili ni jambo la busara tu ndani ya kamati husika kuamua kukusanya ‘maoni' na ‘ushauri' wa watu ambao wanaaminika kuwa ni ‘wadau' ama walengwa wa sheria inayotungwa. Napigia mstari tena, kuwa ni ‘busara' tu na hivyo si hitaji la lazima la Katiba, Sheria ama Kanuni.

Vyombo vyenye kazi ya kutunga sheria ni Rais kwa upande mmoja na Wabunge kwa upande wa pili. Wabunge walikwishamaliza kazi yao, bado tunasubiria Rais naye afanye ya kwake.

Lakini nikiri pia kuwa kuna vipengele vya sheria ile iliyopitishwa na Bunge vinaweza kuwa na mapungufu; hili si kitu sana, kwa maana hakuna sheria iliyowahi kutungwa na ikategemewa kuwa kamili ("perfect") kama msahafu wa quran ama biblia. Na ndiyo maana ikawepo fursa ya kufanya marekebisho kwenye sheria. Na labda niseme tu hapa kwamba, huu ni moja ya msingi wa ushauri wangu kwa Mhe. Rais kwenye makala yangu iliyopita. Kwamba akikamilisha mchakato wa kutungwa na kupitishwa kwa sheria hii kwa kusaini na kisha kuelekeza serikali kupeleka bungeni mapendekezo ya marekebisho kwa njia ya ‘hati ya dharura' atakuwa ameliokoa Taifa na kila kitu kitaenda kwa ratiba kama ilivyo.

Kilichotokea Bungeni ni kwamba, wapinzani walisusia mchakato wa kutunga sheria ile ilhali wakijua fika kuwa hakuna kilichoenda mrama zaidi ya kuwa na mapendekezo yao ambayo walishindwa kuyapenyeza kwa njia ya ‘ushauri na ushawishi' (Consultation and consensus building) katika hatua za awali na walijua kuwa kwa kuwa wao ni wachache wasingefanikiwa kuyapitisha bungeni. Wakaamua kutengeneza hoja za maksudi za kususia mchakato ili hapo baadaye wapewe fursa ya kusikilizwa na Rais ili washinikize yapite ama sivyo ‘wataliteka nyara' Taifa kwa vitisho vya kuhamasisha uasi wa wananchi dhidi ya serikali.

Kuna wasomaji waliniandikia wakisema kuwa ni heri ya wale wabunge waliotoka nje ya bunge kuliko ya wale waliobaki ndani ya bunge ‘wakitukana!' Kutukana ndani ya bunge ni jambo linalokatazwa. Hivyo hakuna aliyebaki na kuanza kutukana.

Lakini, tabia ya kususia kikao cha bunge si ya kiuongozi na ni kosa la kikatiba. Kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, wabunge ni wawakilishi wa wananchi kwenye kuisimamia na kuishauri serikali, na kwenye kutunga sheria. Kuwepo ndani ya Bunge ni kutekeleza jukumu la kwanza la msingi la Mbunge yeyote yule la kikatiba la ‘uwakilishi'. Kusema lolote ama kutosema ni mambo ya upili. Kuwa na hoja ya msingi ama ‘pumba' ni mambo ya nafasi ya tatu kabisa kwa umuhimu, ukizungumzia demokrasia ya uwakilishi bungeni.

Kwa maoni yangu, mchakato wa mashauriano na maridhiano ungepaswa uwe unafanyika mwanzoni kabla hatujaingia bungeni kujadili sheria na hatimaye kuingia kwenye tofauti kubwa namna hii. Niwashauri wenzetu wa upinzani na hata wa CCM bungeni kuitumia vizuri nafasi ya Waziri Mkuu pale Bungeni, maana yeye ni msimamizi mkuu wa shughuli za serikali Bungeni. Mashauriano, maridhiano na mapatano yataleta utangamano na mshikamano wa kitaifa, tuyakumbatie. Hili Taifa ni letu sote, hatuna sababu ya kuhitilafiana kiasi hiki kama kweli kuna hoja za msingi.

Kwa namna mchakato ulivyoenda na kwa kuzingatia hapa tulipofikia, njia pekee iliyopo si ya kuonesha namna gani wabunge walio wengi waliupitisha muswada huu bungeni bila umakini. Siwaoni wabunge wa CCM wakifurahishwa na wakiridhia mtazamo ama uamuzi wenye msingi huu.

Namna pekee ya busara itakayotoa ushindi kwa kila kundi ni kutambua kazi ya wabunge walio wengi walioupitisha muswada ule na pia kutambua mapungufu yaliyopo – mfano lile la kuiua tume ya mabadiliko ya katiba kabla ya mchakato kufikia mwisho. Hili kiukweli lina mantiki ndani yake; tukiwa kwenye bunge la katiba hakutokuwa na serikali, sasa ni nani atakayejibu na kuweka sawa hoja za wabunge? Hili kwa kweli wabunge tuliopitisha muswada ule hatukuliona vizuri. Hivyo basi, jambo hili na mengine ya namna hiyo yasipuuzwe, yapelekwe bungeni kama marekebisho.

Kama Rais akiamua kuchukua njia ya kutoisaini sheria hiyo na hivyo kuirudisha bungeni ikiwa na maoni yake itakuwa fedheha kubwa kwa wabunge wa CCM, chama tawala anachotokea, na wale wachache wa upinzani walioshiriki kuupitisha muswada huu. Siwezi kuamini kama anaweza kuwafedhehesha wabunge wake kiasi hicho. Najua kuna wasomaji wataguna kwenye hili, lakini haiondoi ukweli kwamba hili halina sura nzuri kwenye siasa na uongozi wa Taifa letu. Hata kama tunamtaka Rais wetu asimame kitaifa namna gani, lakini si kwa gharama ya kuwafedhehesha wabunge wake. Ni busara kutafuta njia ya kuyaunganisha mapendekezo ya wapinzani kwenye sheria hii kimkakati bila kuleta ‘stalemate'.

Rai yangu kwa watanzania wenzangu ni kuwa, kuweni makini sana na sisi wanasiasa, kuna nyakati baadhi yetu huyageuza maoni na malengo yao ya kisiasa kuwa ya umma. Mitazamo ya kisiasa ya kundi moja la kisiasa si lazima iwe sahihi zaidi ya kundi jingine. Tusishabikie bila kujua ukweli wa mambo maana tutaliangamiza Taifa kisha tuje kujuta wakati maji yalikwisha mwagika. Na sisi wanasiasa tuwajibike ipasavyo (tuwe ‘responsible') kwa Taifa hili maana yakiharibika hapa wanaopoteza zaidi ni wananchi! Hii ni dhamana yetu, tuitendee haki.


Dkt. Hamisi Kigwangalla ni Mbunge wa Jimbo la Nzega na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Anapatikana kwa simu na +255782636963 na Email: hkigwangalla@gmail.com
 
Mheshimiwa, kwanza nikutaarifu kuwa wengi tulishauri mchakato wa katiba ufuate taratibu kwa kuanzia na mkutano wa katiba. Nasikitika umeliona hilo wakati mambo yameshaharibika.

Tulipoonya kuhusu muafaka wa kitaifa tulionekana wazushi, sasa mnarudi na kusema kuna umuhimu wa kuwa na muafaka na kwamba tuwaepuke wanasiasa.


Haya yote yametokea ukiwa bungeni. Tukaonya kuwa katiba si ya chama ni ya taifa, CCM na wewe ukiwemo mkaamua kuweka mpaka na wenzenu wa upinzani kwa kutumia wingi na si umakini au umuhimu wa hoja.
Leo nashangaa unarudi nyuma na kuona kile tulichokiona miezi 12 iliyopita.


Ni makosa kuwalaumu wapinzani kutoka nje ya bunge. Kususia bunge maana yake ni kuonyesha kutoridhishwa na utaratibu uliotumika na kuonyesha kuwa wao si sehemu ya uzembe ambao leo umekiri CCM wameufanya na kupelekea hatima ya taifa mashakani.


Kwa ubabe wa Spika wa CCM hakukuwa na nafasi ya demokrasia, si sahihi kusema eti wapinzani wamekiuka katiba. Unaelewa kuwa Spika Makinda na Nduga ni watu wa kutumwa na makundi ya wanasiasa.
Unaelewa walivyo na viwango vya chini katika utaifa na usimamizi wa mambo ya kitaifa.


Nadhani wewe na wabunge wengine wanaoipenda nchi hii mnapaswa kusimama kidete kuhakikisha hawa hawasimamii masuala muhimu ya kitaifa kwasababu hawana uwezo.
Kama ungeshauri kura ya maoni kuwaondoa ungelitendea haki taifa hili.

Ninachotaka kusema ni kuwa ulichokiona ni sehemu tu ya tatizo, siku taifa litakapokuwa katika machafuko wewe na wabunge wenzako mtaangalia nyuma na kujuta sana.
Hapa tulipo taifa lipo katika wakati mgumu sana.

Hivyo kama umeona tofauti basi waambie na wenzako kuwa mnachokifanya Dodoma si kujenga taifa ni kuliangamiza nanyi mkiwa sehemu yake. Taifa likitekeketea hakuna miongoni mwenu atakayekuwa salama si Dodoma au nyumbani na chumbani kwake.


 
ninachokiona kwenye bango lako hapo juu ni muendelezo wa siasa za kufuata upepo, siasa zilizokosa uzalendo na umakini. siku chache zilizopita mulikuwa bungeni lakini hukuyaona haya unayoyaita mapungufu muliyoyafanya.
kwa kutumia uwingi wenu(na si umakini) mulipitisha madudu halafu munamshawishi rais aweke saini kwenye hayo madudu mnayoyaita muswaada.

lakini rais naye ni tofauti kidogo na nyie wabunge wake, ameyaona mapungufu yote. mnachofanya ni kumpa wakati mgumu rais kwa kumfanya awaepushe na fedheha ambayo iko mbele yenu. kama rais atakubali kusaini muswada ili kuwaepusha na fedheha inayowakabili, naye ataingia kwenye kundi lenu la watu wasioitakia mema nchi hii.
 
Katiba siyo sheria; katiba ni zaidi ya sheria,ni mama wa sheria. Pote penye demokrasia (rule of the people),katiba inabaki kuwa mali ya umma na lazima iwe na matakwa/maoni ya umma wa tanzania. Na kama ni hivyo kwa nini maoni ya wazanzibar yaachwe nje ya katiba inayoitwa ya watu wa JMT.

Je! Huoni kuwa wewe naye umechoka (pinda:Tumechoka) kiakili kwa kushiriki kuboronga mswada na kisha kuridhia ukasainiwe na rais licha ya kuwa na kasoro nyingi, kubwa na za wazi ambazo mngezirekebisha siku ile ile ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima?.

Je! bado unatuwaaminisha kwamba umma unapoamua kuchukua hatua dhidi ya watawala dhalimu kama nyie mliochoka kifikra watakaoumia ni wao tu peke yao?

Zingatieni kuwa kwa madudu haya umma hautakaa kimya na kuridhika milele na kwamba hali hii ikitokea wewe Kigwangala na sijui mheshimiwa wako huyo unayemtaja kinafiki na kujikomba huku ukiwasaliti wapigakura wako hamtabaki salama.

Tazameni nchi kama Iraq, Libya, Misri, n.k . Je! hazkuwa na waheshimiwa? Wako wapi? HESHIMUNI UMMA.
 
Huyu Kingwangala ni mmoja wa wabunge wa CCM waliopata nafasi ya kuchangia muswada huu wa katiba mpya mara baada ya wabunge wa vyama vya upinzani kutoka nje. Badala ya kuchangia muswada Kingwangala alishia kutukana na hakuna jambo lolote la maana aliloongea bungeni kuhusu muswada wenyewe. Kumbukumbu za bunge zipo, na vizazi na vizazi wataweza kuona mchango (matusi) ya mbunge huyu.

Kama kweli Kingwangala si mnafiki na msaliti wa watanzania ni kwanini hakusema haya anayohubiri hapa jukwaani na siyo kwenye chombo cha kutunga sheria - bunge? Kama mbunge nini wajibu wa mtu kama Kingwangala bungeni?

Nakosa kabisa hamasa ya kundelea kuchangia mjadala wa Kingwangala kuhusu muswada wa katiba mpya kwa sababu hasimamii haya anayoandika hapa hata pale anapopewa nafasi ya kuongea bungeni. Inaudhi!
 
Wabunge wa CCM hamkuwakilisha watanzania Bali Chama chenu pamoja na madai ya taratibu kufuatwa. Hamkuweka Maslahi ya wananchi.:disapointed:
 
....Kama Rais akiamua kuchukua njia ya kutoisaini sheria hiyo na hivyo kuirudisha bungeni ikiwa na maoni yake itakuwa fedheha kubwa kwa wabunge wa CCM, chama tawala anachotokea, na wale wachache wa upinzani walioshiriki kuupitisha muswada huu. Siwezi kuamini kama anaweza kuwafedhehesha wabunge wake kiasi hicho. Najua kuna wasomaji wataguna kwenye hili, lakini haiondoi ukweli kwamba hili halina sura nzuri kwenye siasa na uongozi wa Taifa letu. Hata kama tunamtaka Rais wetu asimame kitaifa namna gani, lakini si kwa gharama ya kuwafedhehesha wabunge wake. Ni busara kutafuta njia ya kuyaunganisha mapendekezo ya wapinzani kwenye sheria hii kimkakati bila kuleta ‘stalemate'.....
Hapo kwenye red,kwa hiyo hata kilicho cha hovyo asaini tu ili kutofedhehesha wabunge wa chama chake!!!! Deo Filikunjombe alikua sahihi kusema "mnautumia wingi wenu vibaya".
 
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba: Kuna Mgongano wa Kimaslahi ama ni Maslahi ya Umma Yanalindwa?

Kwa hiyo Chama chako bado inamsimamo gani!
Kwa hiyo awali hamkuona umuhimu wa Masilahi ya Umma ?
Mnaweza kuaminika vipi kwa sasa kuwa mmeachana na Msimamo wa Chama.

Ukweli utabaki kuwa ukweli tu kwamba, niliegemea zaidi kwenye njia ya muafaka wa kitaifa na ambayo itatuacha wabunge wote na watanzania ‘washindi'. Staili hii ni ya kimarekani. Inaitwa ‘win – win situation'. Sikuweka msimamo wa chama changu ila nilisema ukweli tupu.


Kweli unaweza kusema hakuna kilicho enda Mrama, ebu uwe mkweli mlikuwa na agenda gani ya siri kupitisha madudu kama yale.

Wapinzani walitoa maoni lakini kwa jeuri yenu na masilahi binafsi mkawapuuza!

Nawashauri Wapinzani kuwa makini wasijetumika kama Muhuri Mapendekezo yote mliyoyaweka wazi kama hayatapata nafasi ya kupitishwa na Bunge kwa sababu ya Uwingi wa CCM Bungeni ni heri kuendelea na Msimamo wa Awali wa kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge.


Lakini nikiri pia kuwa kuna vipengele vya sheria ile iliyopitishwa na Bunge vinaweza kuwa na mapungufu; hili si kitu sana, kwa maana hakuna sheria iliyowahi kutungwa na ikategemewa kuwa kamili ("perfect") kama msahafu wa quran ama biblia.

Kilichotokea Bungeni ni kwamba, wapinzani walisusia mchakato wa kutunga sheria ile ilhali wakijua fika kuwa hakuna kilichoenda mrama zaidi ya kuwa na mapendekezo yao ambayo walishindwa kuyapenyeza kwa njia ya ‘ushauri na ushawishi' (Consultation and consensus building) katika hatua za awali na walijua kuwa kwa kuwa wao ni wachache wasingefanikiwa kuyapitisha bungeni. Wakaamua kutengeneza hoja za maksudi za kususia mchakato ili hapo baadaye wapewe fursa ya kusikilizwa na Rais ili washinikize yapite ama sivyo ‘wataliteka nyara' Taifa kwa vitisho vya kuhamasisha uasi wa wananchi dhidi ya serikali.

Kiuhalisia kupitisha pumba zile ni sawa na matusi kwa watanzania, na wewe kama msomi ulitakiwa kulitambua hilo!
 
Huyu Kingwangala ni mmoja wa wabunge wa CCM waliopata nafasi ya kuchangia muswada huu wa katiba mpya mara baada ya wabunge wa vyama vya upinzani kutoka nje. Badala ya kuchangia muswada Kingwangala alishia kutukana na hakuna jambo lolote la maana aliloongea bungeni kuhusu muswada wenyewe. Kumbukumbu za bunge zipo, na vizazi na vizazi wataweza kuona mchango (matusi) ya mbunge huyu.

Kama kweli Kingwangala si mnafiki na msaliti wa watanzania ni kwanini hakusema haya anayohubiri hapa jukwaani na siyo kwenye chombo cha kutunga sheria - bunge? Kama mbunge nini wajibu wa mtu kama Kingwangala bungeni?

Nakosa kabisa hamasa ya kundelea kuchangia mjadala wa Kingwangala kuhusu muswada wa katiba mpya kwa sababu hasimamii haya anayoandika hapa hata pale anapopewa nafasi ya kuongea bungeni. Inaudhi!
Mheshimiwa HKigwangalla ndugu FJM kaja na neno! anasema 'you preach what you don't practice' unasemaje?

Pili, kuna hili suala la hansard za bunge ambako wengi wana mashaka na ule mchango wako. Je, unadhani ukiangalia nyuma na hasa nyuzi hii unaweza kutuambia nini kwa mtazamo wa ulichokisema siku ile.

Tatu,katiba ni mwongozo ambao kila mbunge anaushika kabla ya kuanza kazi. Ni kwanini unadhani sasa hivi umuhimu wake unaonekana kwako na si kuanzia siku uliyoapa.
Ni kwanini unadhani uchama hauna tija leo hii na si wakati mswada umeleta kuandika upya katiba.

Nne,umesema wanasiasa wasiaminiwe lakini ndio hao wanaouendeleza mchakato. Una maana kuwa suala hili hata rais ambaye ni mwanasiasa namba moja naye tumtilie shaka au una watu unaodhani ni muhimu tuwatilie shaka.

Mh, tunakuomba katika mjadala huu ambao wengine tunauona ni changamoto na ushiriki wako ni muhimu sana kama mchokoza mada.
 
Last edited by a moderator:
  • Thanks
Reactions: FJM
Mimi nakuuliza wewe Kigwangalla,mdau mkubwa wa jambo hili kwa maana ya MP kuwa ;

Ni kweli kilichowafanya ninyi wabunge wa ccm kupuuza hoja za Lissu na pia kuwanyima wabunge wengine wa kambi ya upinzani waliokuwa na hoja nzito zilizoainisha mapungufu na kasoro zote za muswada (ambao sasa umekiri kuwa na ulikuwa na kasoro) kilikuwa ni kwa maslahi ya umma uliowachagua au ni kwa maslahi yenu wanasiasa wa sisiemu ambao wengi wenu mmepoteza uwezo wa kiakili ktk kupambanua mambo kwa kina?

Kama umekiri kuwa hakuna hata siku moja mliyowahi kutimiza wajibu wenu: 1) wa kutunga sheria iliyo bora (perfect) na 2)wa kumshauri rais juu ya maswala muhimu yanayolihusu taifa. Je! hauoni kuwa tayari wewe na wabunge wenzako wa ccm mmepoteza sifa ya kuendelea kuwawakilisha vyema wapiga kura wenu na pia kuitwa majina makubwa makubwa ya waheshimiwa wabunge?

Je!Unakubali sasa watanzania wawafute kazi 2015 wabunge wa ccm kwani mmekuwa mzigo kwa rais(kuwaepusha na fedheha)na wananchi wanaogharamia posho za vikao vyenu vya kipuuz?
 
benderaq fuata upepo...Kumbuka utafiti wa REPOA...Wanaoiunga mkono CCM wengi ni watu wasio na Elimu na kwa jinsi ilivyo wanazidi kupungua. Kuanzia 2015 Wabunge hasara kama wewe hamtaonekana bungeni. Hatuwezi kuishi kwa kufuata upepo, leo unasimama bungeni unashusha mipasho weee, kesho unasema Rais asisaini muswada, kesho unasema Rais amefanya jambo la maan kusiani muswada...Hujifunzi kitu kwea Deo Filikunjombe?
 
Back
Top Bottom