Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Maoni ya katuni
Taifa hili limekuwa likijitumbukiza katika mkanganyiko usiolazima kila wakati hata katika vitu ambavyo kimsingi viko wazi, hali ambayo ama imeathiri ufanisi au uelewa wa watu wetu katika nyanja nyingi.
Katika siku za hivi karibuni mjadala wa matumizi ya lugha ya Kiswahili umepamba moto miongoni mwa wadau mbalimbali, hasa baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo kutoa kauli ya serikali bungeni juu ya ulazima wa watumishi wa serikali kuitumia lugha hiyo katika kutekeleza majukumu yao.
Mjadala wa matumizi ya lugha ya Kiswahili pia umekuwapo katika kushawishi itumike kama lugha ya kufundishia katika utoaji wa elimu kuanzia ngazi ya shule za sekondari na elimu ya juu; mjadala huu hata hivyo haujazaa matunda tarajiwa kwa kuwa kuna hoja zinajengwa na wale wanaunga mkono matumizi hayo na wale wanaopinga. Mjadala bado unaendelea.
Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa mijadala ambayo haijakamilika juu ya matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia, kuna utaratibu wa serikali kutumia Kiingereza badala ya Kiswahili katika kutunga sheria. Sheria zote zinazotungwa na Bunge zinakuwa katika lugha ya Kiingereza ingawa wakati wabunge wanajadili muswada wa sheria husika hutumia Kiswahili.
Sheria hizi zikishapitishwa huendelea kubakia kwenye lugha hiyo hiyo, hivyo kuwa vigumu kwa wananchi waliowengi kutambua maana yake kwa kuwa si siri Kiingereza ni lugha ya wachache nchini.
Hali hii ndiyo inakabili sheria nyingi za nchi hii ikiwamo ambayo kwa sasa serikali inakimbizana nayo ya Gharama za Uchaguzi. Sheria hii imeanisha nini kinaruhusiwa na kukatazwa katika kugharimia uchaguzi mkuu, baada ya kusainiwa na Rais mbele ya kadamnasi. Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa katika harakati za kuandaa kanuni za matumizi ya sheria husika.
Hakuna ubishi kwamba sheria hii ndiyo itatumika kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwaka huu, lakini bado iko kwenye lugha ya Kiingereza hali ambayo inakuwa vigumu mno kwa wagombea wengi kuisoma na kuielewa vema ili wasijekutumbukia kwenye vitendo ambavyo kisheria haviruhusiwi katika uchaguzi huo.
Tunatambua kwamba uchaguzi ni mchakato, huhitaji muda na rasilimali nyingine kama fedha, watu, vyombo vya aina mbalimbali vikitambuliwa kama vitendea kazi; hivi vyaweza kuwa vyombo vya usafiri na vitu vingine vyote vinavyorahisisha mawasiliano baina ya mgombea na wapigakura.
Mchakato huanzia mbali, kwanza mtu kujitambua kwamba anasukumwa ndani ya nafsi yake kuomba kuchaguliwa kuongoza kupitia chama cha siasa, kutafuta kuungwa mkono na wanachama wa chama chake na mwisho kujinadi kwa wapigakura; mambo haya yote katika sheria ya Gharama za Uchaguzi yameanishwa na yatafafanuliwa kwenye kanuni zinazosubiriwa kutolewa.
Wakati wagombea wamekwisha kuanza kujipitisha huko na huko kutafuta kuungwa mkono kwa nia zao za kutaka uongozi, wengine hata hawajui sheria hii inasema nini kwa maana ya kuisoma wenyewe na kuielewa bila kutafuta mkalimani kwa kuwa iko katika lugha ambayo ni ngeni kwa wengi. Kwetu tunaona ni udhaifu mkubwa kwa sheria zetu kuwa kwenye lugha ambayo si inayozungumzwa na wananchi waliowengi.
Ndiyo maana tunasema matatizo mengi ambayo yatakuja kugundulika baadaye uchaguzi ukishafanyika, kama vile watu kupinga matokeo ya uchaguzi labda kwa sababu za matumizi ya vitu ambavyo vimeharamishwa kwenye sheria ya Gharama za Uchaguzi, yangeweza kabisa kuepukwa kama sheria hiyo ingekuwa katika lugha ya Kiswahili kuanzia siku ya kwanza kabisa ya kutungwa kwake.
Ni jambo la habati mbaya kwamba hata kwa baadhi ya wabunge sheria hii watakuwa wameipitisha si kwa sababu walijua wanafanya nini, ila kwa sababu tu waliwajibika kufanya hivyo; huu ni udhaifu kwetu kama taifa kwa sababu ni jambo la kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwamba tumejaliwa kuwa na lugha ya moja ya taifa inayozungumzwa na kila mwananchi, msomi na asiyemsomi; wa mijini na wa vijijini sawia.
Kwa hali hii kuendelea na kasumba hii ya ukoloni mamboleo ya kuamini kwamba bila sheria kutungwa kwa Kiingereza haitimizi sifa za kisheria, ni kurudisha nyuma juhudi za kujitegemea za taifa hili, lakini zaidi sana kuzidi kuminya fursa ya watu wetu kupata elimu kwa wepesi na haraka zaidi kama tungeendesha mambo mengi kwa lugha ya Kiswahili; ikiwa ni pamoja na kutunga sheria kwa kutumia lugha ya taifa.
CHANZO: NIPASHE