SHEWORKS in Tech: Licha ya wengi kutumia mitandao, uelewa wa usalama Mtandaoni bado ni mdogo

SHEWORKS in Tech: Licha ya wengi kutumia mitandao, uelewa wa usalama Mtandaoni bado ni mdogo

informer 06

Senior Member
Joined
May 11, 2024
Posts
184
Reaction score
170
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Shework in Tech, Matilda Moses Mashauri amesema licha ya watu wengi kujua kutumia vifaa na mitandao ya kidijitali, bado kuna pengo katika uelewa wa namna ya kujilinda dhidi ya hatari zinazoweza kujitokeza wanapokuwa mtandaoni.
IMG_3909.jpeg

Akizungumza katika mafunzo ya Binti CyberSafe Day yaliyowakutanisha mabinti kutoka shule mbalimbali za Dar es Salaam, Oktoba 13, 2026 yakiandaliwa na Shework in Tech kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo UN Women na Ubalozi wa Ubelgiji Nchini Tabzania, Mashauri amesema shirika hilo limeamua kuwekeza katika kuwapa mabinti elimu ya usalama wa mtandaoni, hususan katika kipindi cha Oktoba kinachohusishwa na uhamasishaji kuhusu usalama wa mtandao.

“Tumeamua kuwachukua watoto wa kike na kuwafundisha namna ya kuwa salama wanapokuwa mtandaoni. Watu wengi wanajua kutumia mitandao ya kidijitali, lakini hawajui namna ya kuwa salama katika mitandao hiyo,” amesema Matilda

Amesema kupitia kazi wanazofanya kwa karibu na shule na vyuo, wamebaini changamoto za matumizi ya teknolojia zinazoweza kusababisha madhara kwa vijana na wakati mwingine kuathiri masomo yao.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Shirika la Shework in Tech limekuwa likitoa elimu ya matumizi salama ya teknolojia kwa watoto na vijana, likilenga kuwajengea uwezo wa kujilinda wanapotumia mitandao ya kidijitali.
IMG_3912.jpeg

Mtaalamu anaeleza

Wito umetolewa kwa Jamii kutumia vyema mitandao ya kijamii kwa usalama na kujilinda dhidi ya changamoto mbalimbali, zikiwamo vitendo vya udhalilishaji mtandaoni ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.
IMG_3701.webp

Mtaalamu wa Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Kidijitali, Yusuph Kileo, akizungumza Oktoba 13, 2026 katika mafunzo ya Binti CyberSafe Day yaliyoandaliwa na Shirika la Shework in Tech amesema udhalilishaji mtandaoni unaongezeka, huku vitisho vya kusambaziwa picha na video za faragha vikiendelea kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili watumiaji, hususan watoto, vijana na wanawake.

Amesema miongoni mwa changamoto zinazotazamwa kwa uzito ni uonevu mtandaoni (cyberbullying), unaojumuisha kutukanwa, kudhalilishwa na kufanyiwa vitendo vingine vinavyoweza kuathiri heshima na ustawi wa waathirika.
IMG_3910.webp

Kileo amesema matumizi ya akili unde (Artificial Intelligence – AI) na teknolojia ya kutengeneza maudhui bandia yanayofanana na picha, sauti au video halisi (deepfake) yanaweza kutumiwa kumdhalilisha mtu.

“Kwa sasa tumeona kuna matatizo kama uonevu mtandaoni, ambao umekuwa mkubwa. Watu wanafanyiwa mambo mengi sana huko mtandaoni, ikiwa ni pamoja na kutukanwa au kutengenezewa picha za uongo kwa kutumia akili unde na teknolojia ya deepfake. Kwa hiyo, eneo hilo tunaliangalia sana,” amesema Kileo

Ameongeza kuwa changamoto nyingine ni vitisho vinavyohusisha picha au video za faragha, ambapo mtu anaweza kutumiwa vitisho vya kusambaziwa maudhui hayo ili alipe fedha au atekeleze matakwa ya mtishiaji.

“Watu wamekuwa wakiteseka sana katika eneo hilo. Tumeona wanawake wakiteseka, na nimepata ushuhuda wa watu wengi ambao wameripoti matukio ya kutishiwa kusambaziwa picha au video zisizofaa,” amesema Kileo

Kwa mujibu wa Kileo, eneo jingine ambalo amesmea kwamba lanaliangalia kwa kipaumbele matukio ya kurubuniwa kwa watoto mtandaoni na watu wazima, jambo linaloweza kuwafanya watoto kushawishika kufanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama na ustawi wao.

Amesema kwa sasa kuna mjadala unaolenga kuanzisha kadi za laini za simu (SIM cards) mahususi kwa watoto, hatua inayotarajiwa kuchangia kuimarisha usalama wao wanapotumia vifaa vya kielektroniki.

Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa watu wanaokumbana na changamoto hizo kujua mahali pa kupata msaada na kuripoti matukio. Amesema namba 116 inaweza kutumika kwa ajili ya kupata msaada katika changamoto zinazowakabili watoto, ambapo ameongeza kuwa Serikali ipo katika jitihada za kuandaa mfumo maalumu (portal) wa kuripoti matukio ya uonevu wa kimtandao ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wakati.

Elimu ya usalama wa mtandaoni kwa mabinti

IMG_3685.jpeg

Aidha katika hatua nyingine Mashauri amesema shirika hilo limefikia zaidi ya mabinti 300 pamoja na wanawake katika maeneo mbalimbali nchini kupitia juhudi za kutoa elimu ya kidijitali.

“Vijana wengi wana vifaa vya kidijitali na wanatumia mitandao, lakini hawako salama. Hatuhitaji tu wajue kutumia kompyuta na simu, bali pia wajue kuzitumia kwa usahihi na, wanapokumbana na changamoto, wafahamu mahali pa kuripoti,” amesema.

Teknolojia iwe nyenzo ya maendeleo, si chanzo cha madhara

Kwa upande wake, mwanzilishi mwenza Shework in Tech, Annagrace Malamsha amesema elimu ya usalama wa mtandaoni ni muhimu kwa mabinti na jamii kwa ujumla, kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia katika shughuli za kila siku.
IMG_3721.jpeg

Amesema pamoja na fursa zinazotokana na teknolojia, watumiaji wanapaswa kuwa na uwezo wa kutambua taarifa za kweli na zile za uongo, huku wakijua namna ya kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji vinavyofanyika kupitia mitandao.

“Tunatoa elimu hii ya usalama wa mtandaoni kwa mabinti na jamii kwa sababu wakati mwingine mtu anaweza asijue kama taarifa anayoiona ni ya kweli au ya uongo. Vilevile, kuna watu wanaopitia udhalilishaji mtandaoni,” amesema Annagrace

Malamsha amesema teknolojia inapaswa kuwa nyenzo ya kuwawezesha mabinti kujifunza, kujiendeleza na kutumia fursa mbalimbali, lakini hilo linawezekana zaidi iwapo watakuwa na maarifa ya kujilinda dhidi ya hatari za mtandaoni.

Amesisitiza kuwa kushindwa kujilinda katika mazingira ya kidijitali kunaweza kuwa kikwazo kwa mabinti kutumia ipasavyo fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia.

Itakumbukwa waanzilishi wa Shirika la Shework in Tech ni sehemu ya wanufaika wa mafunzo ya UN Woman ambayo yalihitimishwa mwaka 2023 kwa kuwajengea uwezo mabinti katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya teknolojia inayohusisha matumizi ya mitandao na akili mnemba (AI).
 
Back
Top Bottom