Shiari: Ametoweka!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Joined
Mar 10, 2006
Posts
33,771
Reaction score
41,027
Napiga hodi watani, wa kijiji naingia,
Ngojea niketi chini, swali kuwaulizia,
Nilonalo mtimani, beti ninalitungia,
Ndege niliyemnasa, mtegoni katoweka

Ni ndege niliyemwinda, asubuhi na jioni,
Ndege mwenyewe si kinda, nilipomuona mtini,
Na ndipo nilimpenda, nikatamani moyoni,
Ndege niliyemnasa, mtegoni katoweka

Mtego nikauweka, na punje nikamwagia,
Ndege pweke akaruka, mtegoni kashukia,
Mara puh! Kanasika, Miguu kajifungia,
Ndege niliyemnasa, mtegoni katoweka.

Ndipo nikafanya hima, kukimbilia nyumbani,
Kumtaarifu mama, ndege yuko mtegoni,
Kwamba ninaleta nyama, ya chakula cha jioni,
Ndege niliyemnasa, mtegoni katoweka

Mama kanipa pongezi, mwanangu sasa kakua,
Yakamtoka machozi, na kicheko cha kishua,
Mwenyewe nikala pozi, huku nikijishaua,
Ndege niliyemnasa, mtegoni katoweka.

Baba kaniangalia, kaniona mimi chizi,
Ndipo kaniulizia, huyo ndege wa ulozi,
Mtego nimeachia, ni nani wangu mlinzi,
Ndege niliyemnasa, mtegoni katoweka.

Kwa haraka nikatoka, kumuwahi ndege wangu,
Mara pale nikafika, nikapatwa na uchungu,
Mtego umevunjika, au umepigwa rungu!
Ndege niliyemnasa, mtegoni katoweka.

Mwili ukatetemeka, hasira zikanishika,
Nilidhani nimefika, kumbe nimekamatika,
Na ndipo nikaondoka, na kichwa nimekishika,
Ndege niliyemnasa, mtegoni katoweka.

Nilipokuwa njiani, nikamwona Shaabani,
Ana ndege mkononi, ni yule nilotamani,
Kamkuta kichakani, ndege yuko taabani,
Ndege niliyemnasa, mtegoni katoweka.

Sijui nifanye nini, nimpate ndege wangu,
Shaabani haniamini, huyo ndege ndiye wangu,
Ananicheka kihuni, wa kwake siye wa kwangu,
Ndege niliyemnasa, mtegoni katoweka!


Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Shamba)
 
Ni shole au njiwa, kunguru au mwewe?
asopenda kufungiwa,vya bure aletewe
kakunjua zake mbawa, enda kuishi mwenyewe
Huyo ndege ndege gani, hapa kwetu duniani?

si bata migulu baja,ni kipanga wa angani?
kumjua nina haja,huyu ndege ndege gani?
huyu ni ndege mjanja,vya bure havitamani
Huyo ndege ndege gani, hapa kwetu duniani?
 
Kosa moja ulotenda, kamwe sitokuthamini
Wamkamata halafu wenda,Wamwacha mtegoni
Umeniacha njia panda,ulichofanya kitu gani
Ungemtoa mtegoni na kwenda naye nyumbani

Mtego ukishanasa,wawindaji wafahamu
Hakuna cheza sakasa,Unatoa kwanza damu
Hebu wewe ona sasa,Umepoteza wa hamu
Ungemtoa mtegoni,na kwenda naye nyumbani

Sina shida na Shabani,Silaha zake ni sumu
Kitoweo mtegoni,Hakukilazia damu
Akae subiri nani,ajipate kazi ngumu?
Ungemtoa mtegoni,na kwenda naye nyumbani
 
Pole sana pole tena, Mzee Mwanakijiji,
Usicheze cheze tena, kama mtu wa kijiji,
Bali ujipange tena, kwa kubadili kijiji,
Kupoteza ndege wako, ni pole Mwanakijiji.

Ni pole Mwanakijiji, kupoteza ndege wako,
Tegemeo la vijiji, ni ndege kama wa kwako,
Usiwe kama wa jiji, kutega kivyako vyako.
Kupoteza ndege wako, ni pole Mwanakiji.

Wewe kama muwindaji, ni kama mvuvi kinda,
Tena sio mtegaji, ndo mana wamekukwinda,
Bora uwe mpangaji, wa mambo unapowinda,
Kupoteza ndege wako, ni pole mwanakijiji.

Na hapa ninaishia, ndege mwingine tafuta,
Utamu utaishia, kwa ndege mwenye mafuta,
Nawe usijeishia, tukaja kukutafuta
Kupoteza ndege wako, ni pole Mwanakijiji.
 
Nimeipenda hii wakuu,inafurahisha.Mnanikumbusha malenga wetu kipindi hicho bado nasikiliza RTD.Nitajipanga nami nijitokeze.Asanteni sana hasa mwanakijiji kwani usema wenye kujua tatizo ni kuanza.Ijumaa njema.
 
Ndege huyo ndege gani? mwenye rangi ya kijani?
Anazua tafrani, pindi ajapo nyumbani
Tunahitaji imani,wakwe kumuamini
Huyo ndege kaondoka,Kurudi majaaliwa
 
Dah Hii kiboko wakuu..mbona mmetengeneza sana siku yangu jioni ya Leo... Amani sikujua kama na wewe hauvumi lakini umo...

Tuendeleze hili.
 
.............mmmhhh!!!! mmenikunaa hassaa, baada ya uchovu wa kutwaa nzima yaleo!!ASANTENI SANA!!
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…