Kuna msemo wa Kichina unaosema Wakubwa walioteketeza nyumba wanapiga marufuku watu wa kawaida kuwasha taa. Maana yake ni kwamba watu wenye nguvu hukiuka sheria na utaratibu kama wanavyotaka, lakini hawaruhusu wengine kutekeleza haki zao halali. Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani na baadhi ya nchi nyingine za Magharibi zimeiwekea China vikwazo vingi visivyo na sababu katika nyanja ya teknolojia ya juu, ikiwa ni pamoja na kuyawekea vikwazo makampuni ya China na kupiga marufuku uuzaji wa vifaa vya kutengeneza chip na bidhaa nyingine za teknolojia ya juu kwa China. Hata hivyo wakati China ilipotangaza kudhibiti mauzo ya bidhaa za kimkakati kama vile Gallium na Germanium, nchi hizo zimekuwa na wasiwasi kwamba China itazilipiza kisasi, na kuishutumu China kwa kuvuruga mnyororo wa uzalishaji na ugavi duniani.
Galliamu na Germanium ni nyenzo za kimkakati katika sekta ya utengenezaji wa semiconductor na vifaa vya anga ya juu. Ni hali ya kawaida kwa nchi mbalimbali duniani kutekeleza udhibiti wa mauzo ya bidhaa husika, na nchi nyingi kubwa duniani zimeshafanya hivyo tayari. Kutokana na hali ya utatanishi duniani, serikali ya China imeamua kudhibiti mauzo ya Galliamu na Germanium ili kuhakikisha kuwa, zinatumika kwa madhumuni halali. Wala China haipigi marufuku mauzo ya bidhaa zinazohusiana na Gallium na Germanium, inachofanya ni usimamizi mzuri wa mauzo hayo. Kulingana na taarifa iliyotolewa na Wizara ya Biashara na Mamlaka ya Forodha nchini China, Kampuni zinazouza bidhaa nje zinapaswa kupitia taratibu za utoaji wa leseni za kuuza Gallium na Germanium kwa nchi za nje, zinatakiwa kuwasilisha ombi kwa serikali kwanza, na kueleza wazi matumizi ya mwisho. Hii inaonyesha kwamba, kama bidhaa hizo hazitatumiwa kwa lengo linaloweza kuhatarisha usalama wa taifa la China, zitapatikana kama zamani.
Kwa upende mwingine, wasiwasi mkubwa wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi kutokana na uamuzi huo wa China unaonyesha kwamba China ina uwezo wa kukabiliana na ukandamizaji wa kibiashara kutoka nje. Galliamu na Germanium ni muhimu katika sekta ya uzalishaji wa teknolojia ya juu duniani, na zimewekwa katika orodha ya nyenzo za kimkakati katika nchi zilizoendelea kama vile nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, Marekani na Japan. China ndio mzalishaji mkubwa zaidi wa Gallium na Germanium, na zaidi ya nusu ya vitu hivyo vinavyotumika katika nchi za Magharibi huagizwa kutoka China. Ukweli unakumbusha Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwamba uchumi wa dunia umeunganishwa kwa kina, na jaribio lolote la kutenganisha China litadhuru mnyororo wa ugavi wa kimataifa, na pia litadhuru maslahi ya nchi hizo zenyewe.