SoC03 Siasa inapoharibu mijadala ya kitaifa

SoC03 Siasa inapoharibu mijadala ya kitaifa

Stories of Change - 2023 Competition
Joined
May 4, 2020
Posts
32
Reaction score
37
SIASA INAPOHARIBU MIJADALA YA KITAIFA

Hivi karibuni kumekuwa na mjadala mpana sana kuhusiana na Bandari, Mjadala huu umeibuka baada ya kupatikana kwa taarifa kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Waziri Prof. Makame Mbarawa kuingia makubaliano/mkataba wa awali wa ushirikiano kwenye nyanja mbalimbali zinazohusu uendelezaji wa Bandari ya Dar Es Salaam, Inaelezwa kuwa mkataba huo unahusisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Kifalme ya Dubai kupitia Kampuni ya Umma ya DP World Logistics company (DP WORLD)

Agenda yangu 'Mama' kwa hapa si kuelezea au kuingia kwa undani kwa kuuchambua mkataba huo, lakini pia siko hapa kueleza mkataba/makubaliano ni halali ama la au mkataba huo una maslahi kwa Taifa au hauna?, lakini pia siko hapa kueleza kuwa mkataba huo unahitaji kuendelea au usitishwe?, Hayo yote si sehemu ya agenda yangu ninayotaka kueleza hapa bali niko hapa kuzungumzia mkanganyiko unaoletwa na Wanasiasa kwenye jambo hili na mambo mengine mengi yanayohusisha mijadala ya kitaifa

Nadiriki kueleza kuwa Wanasiasa wamekuwa sababu ya kupeleka mkanganyiko na sintofahamu kubwa kwenye jamii kuliko kuwa 'mwarobaini' wa jambo lenyewe

Kama inavyofahamika Wanasiasa ni miongoni mwa makundi ambayo yanaaminika sana kwenye jamii na ukweli usiopingika kuwa hawa wana raslimali watu wa kutosha ambao wengi wao wanaamini anachokizungumza Mwanasiasa fulani au tamko lililotolewa na Chama fulani, huyu akishikilia hilo katu huwezi kumbadilisha mawazo yake labda itokee yule anayemuamini yeye au chama anachokiamini kitoe tamko tofauti na lile la awali hapo inawezekana mkaenda sambamba

Kwenye Sakata hili la Bandari na DP World kwa mara ya kwanza kabisa lilianza 'kuchemka' kwenye mitandao ya Kijamii, hii ilikuwa baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchapisha taarifa iliyotaka Wadau/Wananchi wafike Ofisi za Bunge au watumie njia mbadala zilizotolewa na Bunge kuwasilisha maoni yao kuhusiana na jambo hilo (hii ilikuwa kabla Bunge halijaridhia na kutoa baraka zake kwa Serikali kuendelea na hatua zinazofuata) hata hivyo ilitolewa tarehe moja ya kuwasilisha hoja au maoni hayo na hapo ndipo kazi ilianzia.

Nini kilitoa kwenye mitandao ya Kijamii?, Kwanza kabisa wadau wa mitandao 'waliobeba' jambo hilo wengi wao walikuwa ni Wanasiasa hasa wale ambao wana mrengo wa Upinzani na hoja zao nyingi zililenga kukosoa Bunge kwa kuweka muda mchache wa Wadau kutoa maoni, lakini pia walienda mbali na kuhoji kwanini suala hili limekuja kwa dharula na ghafla wakati linahitaji mjadala mpana wa kitaifa kutokana na umuhimu wake, wengine walienda mbali zaidi kwa kutoa wito kwa Wabunge kutopitisha jambo hilo pindi litakapotua mezani kwao kwakuwa halina maslahi kwa Taifa

Kwanini walikuwa wanaeleza kuwa halina maslahi kwa Taifa?, Hoja zao zilijikita kuueleza Umma kuwa kwanza mkataba pendekezwa unabinafsisha Bandari zote za Tanzania Bara (kuanzia zile la Bahari, Maziwa na mito) rasmi na zisizokuwa rasmi sasa zitamilikiwa na Waarabu (DP World), walienda mbali na kueleza kuwa mkataba huo unawamilikisha DP World kwa miaka 100, hayo na mengine mengi yakaanza kuwa agenda mitandaoni hatimaye kwenye jamii kila mtu alibeba hayo (hasa wale wanaoamini kwenye siasa za upinzani) lakini nakumbuka siku kama ya pili au tatu tangu mjadala huo uanze 'kuwaka moto' Tundu Antipus Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa akaleta hoja 'mpya' kuwa yeye hajaona eneo lolote linaloainisha kuwa mkataba huo utadumu kwa miaka 100 bali kwa maelezo yake alisema kuwa hajaona ukomo wa mkataba huo hivyo kutengeneza tafsiri ya kuwa unaweza kuwa ni miaka 10, 20, 50, 100, 200 au hata zaidi ya miaka hiyo na kuanzia hapo mjadala kuhusu miaka 100 'ulikufa kifo cha Mende' na suala la mkataba usio na ukomo likaendelea huku wafuasi wa upande wa kupinga nao wakiendelea na 'mdundo' huo

Wakati upande wa wapingaji wakiendelea na uwasilishaji wa kuilazimisha Serikali kuachana na mpango huo, Upande wa Serikali kupitia Waziri mwenye dhamana husika, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya Bandari Nchini, Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali na Viongozi wengine waandamizi ndani ya Serikali wakajitokeza kujibu 'mashambulizi' kwa kuelezea manufaa ya makubaliano hayo na kueleza wazi kuwa wale wanaopinga mara zote wamekuwa wakipotosha

Wengine wameenda mbali zaidi na kueleza kuwa wapingaji wamekuwa wakitumia hoja ambazo ni kinyume cha mjadala husika ikiwemo Udini, Ukanda, Uzanzibar na Utanganyika nk jambo ambalo wamedai kuwa linaweza kupelekea kuvunjika kwa umoja, amani na muungano wetu

Hoja yangu kama nilivyoeleza hapo awali si kuzungumzia mwenendo wa sakata hili bali kuonesha namna Wanasiasa 'walivyohodhi' agenda

Baada ya upande wa Serikali na Chama Tawala (CCM) wakiongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo ambao kwa nyakati tofauti wamejitokeza kuzungumzia sakata hilo wafuasi wao nao wakaanza kujibu kwa kucheza 'midundo' ya Chama Tawala na Serikali

Hapo ndipo nilipogundua kuwa Wananchi wengi hasa wale wa kawaida hawajuwi wafanye nini maana hata hao walioko 'front' kulizungumzia jambo hili wameonesha dhahiri kujadili kwa taswira ya kisiasa na sio kiuhalisia

Inawezekana mawazo yangu yakawa tofauti lakini ngoja niulize kitu, Hivi inawezekanaje Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu (Makamu Mwenyekiti), John Mnyika (Katibu Mkuu), John Pambalu (Mwenyekiti BAVICHA), Catherine Ruge (Katibu Mkuu BAWACHA) nk wote msimamo wao uwe sawa kuwa wanapinga jambo hili tena kwa sababu zinazofanana?, bila shaka huu sio msimamo wa mtu bali ni msimamo wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwenye Sakata hili kwahiyo hakuna mfuasi wa Chama hicho atakayeenda kinyume na kauli za 'Vigogo' wao

Upande wa pili Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya Bandari na wengineo ndani ya Serikali wamekuwa wakitetea hoja hii kwakuwa imeanzia kwao na Serikali ndio 'inayopigwa mawe' hilo sina shaka nalo

Lakini wasiwasi wa kuwa hata upande huo pia unahodhiwa kisiasa ni pale tuliposhuhudia Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo, Mwenyekiti wa UVCCM Mohamed Ally 'Kawaida', Wabunge wa CCM, na Makada wengi tu wa CCM wamekuwa wakitoa hoja za kupinga hoja za upinzani na kutoa hoja zinazoitetea Serikali na kuilinda CCM kama Chama Tawala, unadhani wafuasi wa CCM watakuwa upande upi? au watasema nini kama sio kukubaliana na hoja za CCM na Serikali?

Nakupa mfano mmoja kuwa hii hoja ni ya kiasa na si maoni ya mtu mmoja mmoja mbunge wa Tarime vijijini mkoani Mara mwita waitara akiwa bungeni akichangia hoja hii ya bandari alisema "mbunge wa CCM ukipinga hoja ya Rais Samia utakuwa hujipendi, ukitaka tafuta chama kingine, hoja ya Samia lazima iungwe mkono'

Nafahamu kuwa wapo baadhi ya Wanataaluma hususani Wanasheria waliojitokeza kuzungumzia jambo hilo lakini ukweli ni kwamba limebebwa na Wanasiasa kwa 'Jicho la Kisiasa' kuliko uhalisia na hivyo kuwaacha wasiokuwa na mrengo wa Siasa kuwa 'mbumbumbu' wasijuwe lipi sahihi na lipi si sahihi kwenye hili

Sie 'Wananzengo' tulitarajia kuwa Wataalamu/Wadau hasa wale wa masuala ya Sheria, Biashara, Uwekezaji kutoka ndio wangekuwa wazungumzaji wakuu wa jambo hili kwa maana ya kulifafanua kisheria na kiuhalisia kutokana na mazingira tuliyonayo hapa Nchini bila 'unazi' wa aina yoyote

Kwa kutumia njia hii pekee ya kutochanganya siasa na maendeleo jambo hili ambalo kila mwananchi,mwanasiasa na kila mpenda maendeleo atapata kujua ni kipi kifanyike kumaliza utata huu
 
Upvote 1
Back
Top Bottom