SoC04 Siasa na Taaluma

SoC04 Siasa na Taaluma

Tanzania Tuitakayo competition threads
Joined
Sep 22, 2020
Posts
7
Reaction score
1
Nchi yetu Tanzania, ni fahari ya Watanzania,
Lazima tujue mipaka, na tusifanye mzaha,
Siasa iwe njia, njia ya kuleta ufanisi,
Lakini taaluma iheshimike, na isiburuzwe na siasa.

Uongozi bora ni lazima, hili halipingiki,
Lakini nafasi wapewe, walio na taaluma,
Wasiathiriwe na siasa, katika kutenda kazi,
Ni uongozi bora, na si bora uongozi.

Mafuta, joto, oksijeni vyahitajika, ili moto uwake,
Elimu pia afya, vinahitaji wataalamu,
Wale wenye ujuzi, si watoto wa shangazi,
Wasiingiliwe siasa kali, huduma bora watatoa.

Uchumi utaimarika, kama taaluma zitaaminiwa,
Taaluma ni mizizi, ya maendeleo ya taifa,
Siasa ziwekwe mbali, mbali na taaluma,
Taaluma ijengewe sanamu, kwenye kilele cha Afrika.

Siasa iwe kiongozi, kwa watoto wa Butiama,
Na taaluma ishike usukani, kuelekea kanaani,
Tuondoe mgongano, tupate mwafaka,
Maendeleo tutapata, bila kuweka bondi.

Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu,
Tuunge mkono taaluma, bila kuleta uchawa,
Tusiishi tungali wafu, bali wafu walio hai,
Akili tuzitumie, kuyaleta maendeleo.

Siasa zisitawale kila sekta, tuwape wataalamu nafasi,
Wafanye kazi bila ya bughudha, hiyo ndio siasa safi,
Vitendea kazi wapewe, na sio zawadi za vitisho,
Hii ni njia ya mafanikio, iliyojazwa miiba na misumali.

Tumechoka na majungu, siasa za kibinafsi,
Misingi ya utawala bora, imeliwa na siasa,
Maneno mengi mdomoni, yasio kuwa na mpangilio,
Yameharibu taaluma, zilizotengenezwa na serikali.

Viongozi heshimuni taaluma, msiingilie kila jambo,
Taifa litaimarika na kustawi, siasa zikiwa na mipaka,
Hili halihitaji D mbili, bali uzalendo kamili,
Sio ule wa maneno, bali ule wa mwalimu.

Siasa ziwe kwa manufaa ya wananchi, na sio ya familia,
Kila mmoja atunze haki na uhuru, kama isemavyo katiba,
Taaluma iheshimiwe kwa dhati, na kwenye katiba iandikwe,
Tanzania itasimama imara, maendeleo yatamwagika.


Na Adolph Emmanuel
 

Attachments

Upvote 1
Back
Top Bottom