SoC02 Siku rahisi ni jana tu (the only easy day was yesterday)

SoC02 Siku rahisi ni jana tu (the only easy day was yesterday)

Stories of Change - 2022 Competition

Mr Antidote

JF-Expert Member
Joined
Jan 11, 2015
Posts
953
Reaction score
1,304
Kwa Majina wananiita bwana Kupata Majaliwa, mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto wanne inayoongozwa na mama pekee. Familia yetu haikuwa familia yenye uwezo wa kifedha lakini pamoja na hayo mama yetu alijitahidi kila mwanafamilia anapata mahitaji ya kimsingi hasa elimu.

Pamoja na yote hayo Watangulizi wangu (yani kaka (wa kwanza kuzaliwa) na dada wa pili kuzaliwa) hawakufanikiwa kumaliza kidato cha nne kutokana na sababu mbali mbali. Kutokana na makundi mabaya ya marafiki kaka mkubwa aliishia kidato cha tatu na kukataa shule na kisha kuondoka nyumbani na kuanzisha maisha ya ghetto na vijana wengine wa mtaani. Dada nae alipata ujauzito kidato cha pili na safari yake ya kielimu ikaishia hapo.

Hali hiyo ilipelekea Mama kupata shinikizo la moyo na kuanza kuyumba kiafya. Kwakua mama yetu hakupata elimu Zaidi ya msingi tu; hivyo kiu yake kubwa ilikua kuona watoto wake wanafika pale yeye ambapo hakufika, alitamani siku moja kuona kwamba watoto wake wanafanikiwa hasa kupitia elimu kwani aliamini kwamba elimu ndio ufunguo wa maisha na si vinginevyo.

Baada ya kupitia hayo yote mama alikua ni kama alieumwa na nyoka hivyo kwa sisi watoto wake wawili ambao tumebaki tulipata tabu. Kwanza tulipata changamoto ya maisha kuwa magumu kutokana na kuyumba kwa afya yake hivyo hata kidogo alichokipata kilipungua kutokana na muda mwingi kuwepo nyumbani kujiuguza badala ya kwenda kutafuta. Hii ilisababisha hali ya maisha kuwa ngumu zaidi ilifikia muda hata mlo mmoja wenyewe ukawa unapatikana kwa shida sana au usipatikane kabisa.

Pili kila tulilokua tukifanya hata kwa makosa ya utoto alifanya marejeo kwa watangulizi wetu hivyo tulipata viboko vya kutosha.

Pamoja nilikua najitahidi sana darasani lakini matokeo ya darasa la saba yalipotoka sikuchaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza kwa shule za serikali (Ikumbukwe pia watangulizi wangu hawakuchaguliwa walipohitimu shule ya msingi hivyo sekondari walipelekwa shule binafsi). Mama yangu alisononeka sana akiamini kwamba matarajio yake ya kuona watoto wake wanafanikiwa kupitia elimu yanafifia hii ilisababisha hali yake ikazidi kuwa mbaya siku hadi siku. Sikufanikiwa kwenda shuleni kwa mwaka huo kutokana na mama kutokua na uwezo hivyo nikakaa nyumbani. Tumaini pekee lilobakia kwake (mama) ilikua kumlilia Mungu katika roho na kweli.

Mama aliamua kujiunga na kikundi cha Kalistimatiki kanisani (hiki ni kikundi kama cha walokole ndani ya kanisa katoliki) katika kikundi hiki aliweza kupata rafiki (wa kike) ambae siku moja alifika nae nyumbani na kunikuta naendelea na shughuli za nyumbani. Baada ya kusalimiana nae alitaka kufahamu kama nasoma swali hili lilimuumiza sana mama ni kama lilimkumbusha yaliyomtokea hapo awali. Nilipata tabu kumjibu yule mama mgeni ila kwa ufupi nilimjibu sisomi, yule mama alitaka kujua kwanini sisomi wakati nipo katika umri wa kwenda shule ikabidi kumueleza ukweli kwamba sikufanikiwa kuchaguliwa baada ya kuhitimu darasa la saba. Basi yule mama akanitia moyo akasema Mungu atafanya njia na utasoma tu, na mimi nikajibu AMINA.

Urafiki ule ulidumu sana kati ya mama yangu na mama yule hadi akawa na mimi ni mama yangu, alitusaidia sana haswa suala la mahitaji ya chakula pale nyumbani. Mama huyu alikua ni muajiliwa katika wizara fulani.

Ilipofika mwezi wa kumi na moja mwaka ule ambao sikufanikiwa kwenda shule, siku moja kama ilivyokawaida yake alifika nyumbani kutusalimia akiwa anatoka kazini, siku hiyo mama hakuwepo nyumbani alinikuta peke yangu nyumbani tulikaa tukaanza kupiga stori mbili tatu. Alikaa pale kwa dakika zisizopungua 20, lakini kabla hajaondoka alifungua mkoba wake akatoa karatasi akanipatia kuzisoma, zile karatasi zilikua ni fomu za kujiunga na shule kwa masomo ya sekondari katika moja ya shule maarufu sana hapo mjini. Akaniambia jiandae ukafanye mitihani ya usaili kama unavyoona katika fomu hiyo.

Ulikua ni kama muujiza kwangu japo nilibaki na maswali nani atalipa ada lakini nikasema suala la msingi ni kwenda kufanya usaili. Katika maisha unaweza kupitia changamoto lakini kupitia hiyo changamoto inaweza kukupa nafasi nzuri ya kujitafakari wapi ulipotoka, ulipo na unapotaka kufikia. Katika kipindi hicho cha mwaka mmoja nyumbani pamoja na kuwa na umri mdogo lakini nilipata kutafakari mambo mengi sana na kujiwekea maazimio;

  • Nilitafakari maisha ya nyumbani kwa ujumla yalivyo magumu
  • Nilitafakari maono ya mama na matarajio yake kwa watoto wake
  • Nilitafakari afya ya mama na kuhusanisha na watangulizi wangu
  • Nilifanya tathmini ya maisha ya watangulizi wangu
Baada ya kutafakari hayo yote ikabidi nije na suala moja tu ni kufanikiwa kwa namna yoyote ile na kuweka msawazo wa makosa ambayo walifanya watangulizi wangu na kuhakikisha pia kwamba huyu anaenifuatia nyuma yangu (mdogo wangu) anakwenda katika mstari mnyoofu. Na katika hilo niliona kwamba sijachelewa kabisa. Hivyo baada ya yule mama kunipa ile fomu alamu ikalia kichwani “muda ni huu wa kurejesha tumaini la mama”

Usaili ulifanyika nikawa wa 4 kati ya wote waliofanya usaili hivyo kwa msaada wa yule mama alinisomesha kuanzia kidato cha kwanza hadi nikahitimu kidato cha nne katika shule ambayo wote tulikua tunaonekana wakishua kwa mavazi. Sio tu ada ya shule bali yule mama alienda mbali zaidi hadi nauli ya shule alikuwa akinipatia. Kwa kweli sina maneno yanayojitosheleza kushukuru kwa huyu mama. Maendeleo yangu ya shule kitaaluma yalikua yakuridhisha na sikuwahi kutoka nje ya nafasi tatu za juu shuleni hadi namaliza kidato cha nne. Matokeo yakatoka nikawa nimepata daraja la pili (Div 2 points 19). Mama yangu alifurahi sana kuona mwanae wa kwanza (sio kwa kuzaliwa) nimeweza kuhitimu kidato cha nne na kufaulu hii tafsiri yake ni kwamba nitamaliza kidato cha sita hata kama nisingekua na mfadhili tena ningeweza kuendelea kwenye shule ya serikali na kumaliza elimu yangu ya juu ya sekondari.

Katika watu waliofanikiwa kunipongeza alikuwepo mtu mmoja ambae si ndugu ila tulibahatika kufahamiana kutokana na kuishi mazingira tuliyokuwepo, huyu jamaa nilizoea kumuita Anko. Huyu anko “ali-play” nafasi kubwa sana katika makuzi yangu, ni mtu ambae tulikua tunakaa tunapiga stori nyingi sana za maisha na akinifundisha vitu vingi sana. Itoshe tu kusema ule upande wa pili wa mafundisho ya baba uliokuwa unakosekana hasa kwa mimi mtoto wa kiume niliyapata kwa huyu anko.

Alinijengea ujasiri wa kupambambana na kutokata tamaa kama mtoto wa kiume. Baada ya matokeo kutoka aliniita akanipongeza na akanipa zawadi ya laptop yake ambayo alikua haitumii na kisha akaniambia maneno haya ambayo yanaishi kichwani hadi leo “Hongera kwa kufaulu hiyo ni hatua moja kati ya nyingi zinazokuja mapambano ndio yameanza kumbuka “Over the fence is not always evergreen

Nilichaguliwa kwenda kusoma katika shule moja ya serikali huko kisarawe kwa mchepuo wa PCB. Kwa kuwa nilitoka shule ya binafsi hivyo sikuwa na ufahamu na mazingira ya shule za serikali hivyo term ya kwanza niliyumba kwa kiasi Fulani haswa katika somo la Fizikia ambalo nilitakiwa kujiandaa mapema hata kabla ya kuanza masomo. Hivyo nilipata daraja F ambalo sikuwahi kupata katika maisha yangu ya shule. Niliporudi likizo mama alisononeka sana na ile F, akaanza kuona tena sasa narudi nilipokua alinisema sana.

Basi baada ya kumalizana na mama nilienda kumsalimia anko na kupiga stori kadhaa. Katika stori nilimshirikisha suala langu la masomo na F yangu ya fizikia. Aliniuliza kwanini nimepata F, nikamjibu tu masomo magumu haswa hilo la Fizikia. Katika mtu ambae niliwahi kumuona amechukia zaidi hata ya mama yangu kuhusu mimi ni huyu anko.

Hakuchukia mimi kupata F, alichukia jibu langu la kumwambia masomo magumu, kwa ukali akaniuliza unajua tafsiri ya jibu lako? Hivi ulielewa maana ya ule usemi “Over the fence is not always ever green? Akaniambia tafsiri ya jibu lako ni kwamba umeshashindwa na huwezi kufanikiwa kwakua umeshaona masomo magumu hivyo utafeli tu.

Kama ni hivyo usiendelee kupoteza muda rudi shuleni kabebe sanduku lako urudi nyumbani uachane na shule utafute shughuli nyingine. Kauli yako inaonesha hujui shida yako ni nini na umeshakata tamaa na kukubali masomo ni magumu sioni kama utafanikiwa. Akaenda mbali zaidi akasema wewe ni mkristo na kwenye biblia wameandika Mwanaume atakula kwa jasho je unadhani Mungu ni mjinga kusema hivyo? hebu ngoja nikupe maana ya ule usemi (Over the fence is not always evergreen) labda hukuelewa tafsiri yake labda haukunielewa (hapa akatumia lugha ya picha kunielezea)

“Hebu jenga picha umekutana na mbwa mkali njiani na wewe baada ya kumuona ukashtuka na kujihami kwa kukimbia yule mbwa akaanza kukufukuza, lakini kule ambako unakimbilia ukafika mwisho ukaona ukuta na ukapata wazo la haraka kuruka huo ukuta na kufanikiwa kurukia upande wa pili na kumuacha mbwa upande mwingine. Kwako itakua ni furaha kwamba umejiokoa na huyo mbwa lakini je una uhakika na huo upande wa pili wa ukuta uliodondokea utakua salama zaidi ya uliotoka?

Je unahakika hakuna mbwa wengine wakali wanakusubiri zaidi ya uliemkimbia? Je upo tayari kwa mbio zingine au ndio utakua mwisho wako kwa hao mbwa wa upande wa pili utakao kutana nao? Ulipomaliza kidato cha nne na kufaulu ni sawa na kuruka ukuta na kumuacha mbwa wa kwanza na tafsiri yake sio kwamba umemaliza, upande wa pili wa ukuta uliporukia (over the fence) kuna changamoto zake nyingi tena zinaweza zaidi ya ulizozivuka (not always evergreen) ndio maana ya tafsiri ya maneno yale. Ulipaswa kujiandaa kiakili na kabla ya kuanza masomo yako kwamba mbio zimeanza tena upya badala yake uliona kwamba umemaliza” Maneno haya aliyasema kwa ukali mno ambao sikuwahi kumuona hapo awali.

Baada ya kuachana nae nilitenga muda na kutafakali niliyoambiwa na mama pamoja na huyu anko hapa nilijiona kabisa kuna kazi ya ziada natakiwa kufanya na alamu ikagonga tena kichwa “sijachelewa muda ni sasa kubadilisha na kutengeneza kulipoharibika”

Nikafanikiwa kumaliza kidato cha sita salama na kufaulu, Mungu ni mwema nikapata ufadhili wa masomo yangu ya chuo (Scholarship) nikafanikiwa kuhitimu masomo yangu ya chuo. Wakati nipo chuo nikabeba jukumu la kumsomesha mdogo wangu kwa allowance nilizokua napata chuoni. Dogo nae hajamuangusha mama bado naendelea kupambana nae yupo chuoni kwa sasa endapo Mungu atambariki mwakani atakua anamaliza masomo yake ya udaktari ngazi ya diploma (Clinical Medicine) huku na mimi nikijiandaa kufanya degree yangu ya pili ya hapo mwakani ya masuala ya Usalama wa TEHAMA.

Anko anaendelea vizuri japo umri umemtupa mkono kwa sasa, mama yangu wa hiari bado anaendelea vema anasogeza umri astaafu na yeye. Mama mzazi amepata Amani na utulivu japo bado afya yake si imara sana matatizo yale ya awali ya moyo yaliendelea na kufikia kiwango kikubwa sana hadi kufikia kuwekewa “pace maker” lakini Mungu ni mwema uwezo wa kupata matibabu kupitia kadi ya bima ya afya na kwa kuchangia fedha wakati mwingine zinapohitajika pale Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete siku zake zinasonga.

Maelezo ya Chapisho hili ni ya kweli kwa asilimia 85. Lengo ni kuhamasisha hasa vijana kutokata tamaa katika maisha. Lakini pia kwa ambao wamebahatika kufanikiwa katika maisha yao waone namna bora ya kugawana Baraka na wengine kama yule mama alivyotenda. Lakini hata kama hauna uwezo wa mali unaweza pia kuwa mshauri (mentor) kwa mtu mwingine na ukawa sababu ya yeye kufanikiwa katika maisha yake kama yule anko alivyotenda kwangu.

"Over the Fence is not always evergreen"
 
Upvote 0
Back
Top Bottom