Leo, Oktoba 5, 2026, Kenya inaadhimisha World Teachers’ Day katika Uwanja wa Kasarani, chini ya kauli mbiu: “Standing with teachers: 60 years of protecting the profession, advancing its status and shaping our futures.”
Lakini kuna kinaya kikubwa. Wakati viongozi wakiwa Kasarani wakisherehekea na kuzungumzia umuhimu na hadhi ya walimu, vyuo vikuu vya umma nchini Kenya viko kwenye mgomo.
Kutoka katika jukwaa hilo, Waziri wa Elimu, Julius Migos Ogamba, amewataka wahadhiri wanaogoma kutii amri ya Mahakama na kurejea kazini.
Mgomo huo ulianza Oktoba 2, ukiongozwa na vyama vya UASU, KUSU na KUDHEIHA, ambavyo vinapinga kutokamilika kwa mazungumzo pamoja na kutotekelezwa kwa makubaliano ya pamoja ya ajira (CBA) ya mwaka 2025–2029.
Lakini CBA yenyewe ndiyo kiini cha mgogoro.
Kwa upande wa UASU, Serikali haijaweka ahadi ya maandishi kwamba CBA ya 2025–2029 itafadhiliwa kupitia National Exchequer. Kwa lugha rahisi, wahadhiri wanataka uhakika kwamba fedha za kutekeleza makubaliano hayo zitatengwa na Serikali Kuu, badala ya kuachwa kuwa suala lisilo na uhakika baadaye.
Pengo la fedha nalo ni kubwa.
UASU imekataa pendekezo la takribani shilingi bilioni 9.76, ikisema kiasi hicho hakiwezi kugharamia CBA ya miaka minne yenye madai mapana zaidi, yakiwemo ulinganifu wa posho na kuboreshwa kwa mipango ya mikopo, hasa mikopo ya magari na nyumba.
Hapo ndipo mgogoro unapokuwa mkubwa kuliko suala la mshahara wa mhadhiri mmoja.
Ni nani anayebeba gharama ya kutokubaliana?
Mwanafunzi — masomo na kalenda ya chuo vinavurugika.
Mhadhiri — anasema hawezi kuendelea na kazi bila makubaliano kuhusu mishahara na maslahi yake kutekelezwa.
Serikali — inakabiliwa na swali kuhusu uwezo wake wa kugharamia na kuendesha mfumo wa vyuo vikuu vya umma.
Na sasa, katika siku ambayo dunia inaangazia umuhimu wa kuheshimu na kulinda taaluma ya ualimu, viongozi wako jukwaani wakisema “Standing with teachers”, huku upande mwingine wa mfumo wa elimu ukiwa umesimama.
Je, hii ni coincidence tu, au ni picha halisi ya changamoto zinazoukabili mfumo wa elimu ya juu nchini Kenya?
Kama Serikali inasema, “Rudini kazini, kuna amri ya Mahakama,” huku wahadhiri wakisema, “Tuonyesheni kwanza mpango wa kufadhili CBA,” nani anapaswa kuchukua hatua ya kwanza kutatua mtafaruku huu?
Na kwako, World Teachers’ Day ya mwaka huu imekuja na ujumbe gani?
Ni siku ya kusherehekea na kuheshimu walimu, au ni ukumbusho kwamba mfumo wa elimu wenyewe bado una matatizo makubwa yanayohitaji kutatuliwa?