Abdallahking
JF-Expert Member
- Mar 19, 2018
- 3,985
- 10,840
Simulizi: ASANTE KWA KUNIFUTA MACHOZI (HISIA ZANGU)
Mwandishi: JOSEPH SHALUWA
Imeletwa kwenu na: BURE SERIES
*****
SEHEMU YA 1 KATI YA 50
Edo wewe! Acha utani wako bwana... unajua kitakachotokea. Utaniudhi sasa...” akasema Lilian kwa sauti ambayo haikueleweka ilikuwa ya ukali au kudeka.
...Sikujua mwisho wangu ungekuwa hivi
EDO aligeuka tena. Kwa mara ya tatu anafanya hivyo wakati akielekea bafuni. Safari hii alimwangalia Lilian kwa macho yaliyojaa ubembe wa huba.
Alihisi moyo wake ukienda mbio kama saa mbovu!
Lilian alikuwa mbichi kabisa. Mwanamke mrembo kuliko neno lenyewe. Kwa namna Lilian alivyokuwa akimwangalia Edo aliyekuwa akisitasita kuingia bafuni, alionekana dhahiri hakuwa na mpango wa kubadili maamuzi yake.
Moyoni alionekana wazi kusimamia alichopanga. Hakuwa tayari kuyumbishwa! Kweli alimpenda sana Edo, lakini isingekuwa rahisi kwake, kutokana na upendo huo avunje agano lake.
Hapo Edo naye alikuwa na mawazo yake, alijaribu kufikiria ni kwa namna gani angemlaghai Lilian akubali kubadili maamuzi yake.
Kwa hakika ilikuwa kazi ngumu. Kazi ngumu kwelikweli. Pengine ingekuwa rahisi zaidi tairi la gari kupita juu ya mguu wa binadamu bila kuuvunja kuliko jambo lililokuwa mbele yao kufanyika.
Msimamo thabiti!
Lilian alikuwa amekaa kitandani, amevaa gauni zuri, refu la rangi ya buluu ya kung'aa. Tangu ameingia katika chumba cha hoteli hiyo na Edo, saa mbili zilizopita, hakuonekana kuwa na wazo la kutoa nguo zake.
Ni kama alipanga kulala nazo. Ahadi ya wawili hawa ni kutokukutana kimwili hadi watakapofunga pingu za maisha. Ni msimamo ambao Lilian alijiwekea siku zote.
Si kwamba walikutana siku hiyo... la hasha! Hawa ni wapenzi wa siku nyingi; uhusiano wao sasa umefikisha miaka mitatu. Kwa muda wote huo, hakuna siku waliyowahi kukutana kwenye uwanja wa huba.
Lilian pamoja na kuwa na umri wa miaka 22, bado alikuwa hajawahi kumjua mwanaume. Bado alikuwa amefungwa kwenye makaratasi. Kichwani mwake alisema: "Mtu pekee ambaye anapaswa kuchukua zawadi hii ni mume wangu pekee. Siwezi kumwamini Edo, hata kama nampenda.
"Edo atakula vinono vyangu ikiwa atatimiza ahadi yetu ya ndoa. Najua tunasoma, acha tutengeneze maisha yetu kwanza, baada ya hapo atanifaidi tu. Mimi ni wake tu."
Au ataniacha? Lilian akawaza tena.
"Mwenzetu vipi? Mbona umeganda hapo mlangoni?" Lilian akamwuliza Edo ambaye bado hakuwa na dalili za kutaka kuingia bafuni.
"Naingia mama, kwani kuna ubaya gani mtu kumwangalia mpenzi wake?" akajibu Edo.
"Hakuna ubaya kwa kweli, si vibaya mtu kumwangalia mpenzi wake. Nakubaliana na wewe lakini muda baby. Bado hatujala mpaka sasa hivi."
"Najua...njoo basi tuoge wote ili tuokoe muda."
"Edo wewe! Acha utani wako bwana...unajua kitakachotokea. Utaniudhi sasa..." akasema Lilian kwa sauti ambayo haikueleweka ilikuwa ya ukali au kudeka.
Haraka Edo akashika kitasa cha mlango wa bafuni. Akakinyonga kwa nguvu, kisha akasukuma mlango. Akaingia. Muda mfupi baadaye kilichosikika ndani ya bafu lile ilikuwa ni maji yakitiririka kutoka kwenye bomba la mvua.
Bado Edo alikuwa anapanga mashambuzi.
***
Edward Mhagama au Edo kama alivyojulikana na wengi alikuwa kijana mtanashati hasa. Hakuwa mtu wa wasichana sana. Mpaka anamaliza kidato cha nne alikuwa hajawahi kukutana na msichana yeyote kimapenzi.
ITAENDELEA