Simulizi : Beyond Love (Zaidi Ya Mapenzi)

Simulizi : Beyond Love (Zaidi Ya Mapenzi)

Abdallahking

JF-Expert Member
Joined
Mar 19, 2018
Posts
3,985
Reaction score
10,840
2JIACHIE = BEYOND LOVE (ZAIDI YA MAPENZI).jpg


Simulizi: BEYOND LOVE (ZAIDI YA MAPENZI)
Mwandishi: 2JIACHIE
Imeletwa kwenu na: BURE SERIES

SEHEMU YA 1 YA 50


Tom aliheshimika na kutisha, hakuna mtu aliyechezea shughuli zake kutokana na uhusiano mzuri aliokuwa nao na viongozi Serikalini, akiwa mdhamini wa Chama Tawala. Hakuna mtu ambaye hakumfahamu, kila alipopita watu walionyeshana vidole, alikuwa na marafiki wengi kupita kiasi. Ilipotokea akaa peke yake kwenye baa au hotelini, ndani ya dakika mbili tayari alishazungukwa na watu, kila mtu akiagiza alichotaka kutumia, kwa Tom kulipa haikuwa tatizo, fedha alikuwa nayo. Tabia hii ilimfanya awe na wapambe wengi kila alikokwenda, akilindwa na watu ambao wala hakuwapa kazi hiyo.

Hayo ndiyo yaliwahi kuwa maisha ya Tom, lakini vitu vyote hivyo havikuwepo tena, vilikuwa vimeyeyuka na yeye kujikuta amelala kitandani kwa miaka mitano bila kuwa na fahamu, akiwa amepooza mwili wote isipokuwa kichwa tu! Marafiki wote aliokuwa nao walimkimbia, mwanzoni kila mtu alifikiri angekufa wiki ya kwanza lakini akaendelea kuwepo mpaka mwaka ukaisha, ukaja wa pili, hatimaye wa tatu akiwa hana fahamu. Fedha zote alizokuwa nazo zikiwa zimetumika kumtibu kwenye hospitali mbalimbali duniani bila mafanikio yoyote, hatimaye mke wake mrembo, Mayasa Kamani ambaye kwa hakika walitumbua maisha pamoja wakati wa raha, akaja kumbwaga kwenye Hospitali ya Muhimbili na yeye kuingia mitini akiwa ameuza kila kitu kilichokuwa kimebaki.

Mama yake Tom, mjane bibi Bhoke Wambura, ilibidi asafiri kutoka nyumbani kwao Tarime kuja kumuuguza mwanaye, naye hakudumu sana akawa amefariki kwa ugonjwa wa shinikizo la damu mwanaye akiwa hana fahamu na kuzikwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwenye makaburi ya Kinondoni kwani haikuwepo hata senti moja ya kutosha kusafirisha maiti kwenda Tarime, Tom akabaki kitandani peke yake, marafiki zake wala hawakuulizia aliendeleaje na wauguzi wala hawakujishughulisha naye sana wakijua alikuwa ni mtu aliyesubiri siku yake, kwa miaka miwili zaidi aliendelea kulala kitandani.

Ilikuwa ni asubuhi siku ya Jumapili, wodi ya Mwaisela ikiwa kimya kabisa, wagonjwa wakiwa wametulia vitandani mwao. Mwanamke mwembamba mrefu, afya yake ikiwa imedhoofika alikuwa akimgeuza Tom kitandani ili amwoshe sababu alikuwa amejisaidia kwenye mashuka, hakuwa muuguzi bali mtu aliyejitokeza kumtunza Tom baada ya kukosa ndugu hata mmoja. Ghafla alishangaa alipomwona Tom amefumbua macho, lilikuwa ni jambo geni kabisa ambalo halikutegemewa kutokea, akashtuka na kumuachia, Tom akazungusha macho yake huku na kule chumbani na baadaye kumkazia sana macho mwanamke huyo.

“Wee Malaya nani amekuambia uje nyumbani kwangu? Hivi wewe mwanamke husikii? Nilishakuambia sikupendi kwanini unanifuatilia? Ondoka hapa, Mayasa akikuta utasema nini? Unataka kunichonganisha na Mayasa wangu? Ondoka upesi vinginevyo nitakupiga!” Tom aliongea akijaribu kunyanyuka kitandani, akashindwa, hapo ndipo akagundua hakuwa na hisia hata kidogo kuanzia shingoni hadi miguuni, hakuelewa ni kitu gani kimetokea.

“Tom! Tulia kwanza, huelewi kilichotokea ndani ya miaka mitano iliyopita, niko hapa kitandani kwako kwa sababu nilichonacho moyoni juu yako ni zaidi ya neno nakupenda, zaidi ya mapenzi; This is Beyond Love!” Aliongea mwanamke huyo akibubujikwa na machozi.

Tom hakuwa na habari juu ya kilichotokea maishani mwake, hakuelewa alikuwa amelala kitandani bila fahamu kwa muda wa miaka mitano, fikra zake zilimtuma kuhisi alikuwa amelala kitandani nyumbani kwake mahali ambako alishampiga marufuku Mariam kufika. Alipozungusha macho yake huku na kule ndani ya chumba alicholala, aliwaona watu wengine wakiwa juu ya vitanda na harufu ilikuwa mbaya tofauti kabisa na nyumbani kwake, akaelewa alipokuwa amelala ni hospitali, mara moja akaanza kuzivuta kumbukumbu zake juu ya kilichotokea mpaka akajikuta yuko mahali pale.

Picha iliyokuwa kichwani mwake kwa haraka, aliyoikumbuka kama kitu kilichotokea mwisho ni yeye akiwa ndani ya gari lake aina ya Vogue, akiwa amefunga vioo vyote huku akipulizwa na kiyoyozi, muziki laini uitwao Hello wa mwanamuziki Lionel Richie ulikuwa ukipigwa taratibu kutoka kwenye spika ambazo hazikuonekana. Shingoni alikuwa amevaa mkufu uliotengenezwa kwa mchanganyiko wa dhahabu, rubi na Almasi ambao thamani yake ilikuwa milioni ishirini na tano.

Si hivyo tu, usoni kulikuwa na miwani ya jua kutoka Kampuni ya DG, thamani yake ikiwa ni milioni moja saa yake ilikuwa ni ya milioni tano, nywele zake zilikuwa zimetengenezwa na kuwekewa dawa iliyozifanya zimeremete na kuwa na mawimbi, alipojiangalia kwenye kioo kilichokuwa juu mbele yake kwenye gari, alitabasamu na kumshukuru Mungu kwa jinsi alivyomuumba akiwa kijana mwenye kuvutia, yeye mwenyewe aliamini hakuwepo mwanamke wa kupindisha kama angeamua kumtokea.

Akijiangalia kupitia kwenye kioo hicho, alifanikiwa kuona gari nyeusi aina ya Rav 4 ikija nyuma yake, hakutilia maanani sana akiamini mwenye gari alikuwa na safari zake na alipojaribu kuangalia vizuri, alimwona msichana mzuri akiwa amekaa nyuma ya usukani.

Tom alizidi kukanyanga mafuta gari hilo likimfuata kiasi cha mita kumi tu nyuma yake mpaka akafika kwenye lango la kuingilia kwenye jumba lake la kifahari eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam, akakanyaga breki na kubonyeza kitufe fulani kando ya mlango ili lango kuu lifungunge aingize gari lake, ghafla bila kutegemea kabla hajakanyaga moto, lango likiwa wazi, alishangaa kuwaona watu wawili waliovaa kininja wakiwa wamesimama kila upande wa gari lake, mmoja akipigapiga dirishani na kumwomba afungue, mshtuko mkubwa ulimpata, akaanza kutetemeka akiwa hajui nini cha kufanya.

Akiwa katika hali hiyo akifahamu kabisa alikuwa ametekwa, mmoja wa watu hao waliotoka kwenye gari lililokuwa nyuma yake, alikipiga kioo cha dirisha kwa kitako cha bunduki, chote kikavunjika na Tom kuwekewa mdomo wa bunduki aina ya SMG shingoni.

“Ndugu yangu, naomba usiniue kama ni gari chukua, niachie roho yangu niko tayari kukuongezea na vito vyote vya thamani nilivyovaa na hata fedha ya mafuta kama utahitaji!”

“Sihitaji fedha yako, nimefuata roho yako!”

“Nani amekutuma?”

“Hilo sio swali!”

Kilichofuata baada ya hapo ni milio miwili ya risasi, moja ikazama kichwani kwa Tom na nyingine shingoni, akaanguka kwenye kiti huku akitokwa damu nyingi. Majambazi wakamchukua na kutupa nje ya gari, wote wawili wakaingia ndani na kuondoka na gari lake kwa kasi ya ajabu, Tom akiachwa amelala ardhini akivuja damu nyingi bila kuwa na fahamu, wakati hayo yakitokea ilikuwa ni saa tatu na nusu ya usiku kwani alikuwa akiwahi nyumbani kuangalia taarifa ya habari ya ITV, saa nne kamili.

Hiyo ndiyo ilikuwa kumbukumbu ya mwisho iliyomwijia kichwani mwake baada ya kujaribu kukumbuka ilikuwaje akawa hospitalini, kichwani mwake alifikiri tukio la kuvamiwa lilitokea jana yake kumbe alikuwa amelala kitandani kwa miaka mitano mfululizo bila kuwa na fahamu akiwa amezungushwa huku

ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 2 YA 50

na kule duniani kutafuta matibabu, Uingereza, Marekani, Ujerumani, India kote walishindwa kumsaidia ndipo akarejeshwa nyumbani Tanzania, mkewe Mayasa akambwaga hospitali ya Muhimbili na kutokomea akiwa ameuza kila kitu na kumwacha masikini.

“Yuko wapi mke wangu mpenzi Mayasa?”

“Mayasa hakukupenda wewe Tom, alipenda mali zako, zilipokwisha akaamua kukukimbia, mimi niko hapa pembeni mwa kitanda chako kwa sababu niliyokueleza, la kwangu ni zaidi ya penzi!” Aliongea Mariam akilia kwa uchungu, kumbukumbu za mambo yote ambayo Tom alimfanyia zilimwijia, akamwangalia na hasira ikapanda, lakini akakumbuka neno la mwisho alilolisema kabla hajatoka porini kwamba “Nimemsamehe Tom!”

Hali ilikuwa ya utulivu jijini Dar es Salaam, watu wengi walikuwa wakirejea majumbani mwao kutoka kazini, giza lilishaanza kuingia. Katika wakati kama huo watoto wengi maeneo ya Vingunguti, Manzese, Tandika na kwingineko walikoishi watu wenye maisha ya kawaida, walikuwa wakioshwa tayari kwa chakula cha usiku na kwenda kulala, ndio maana vilio vya watoto wengi ambao hawakutaka kuoga vilisikika, labda siku ambayo kwenye nyumba nyingi ulipikwa wali, siku hiyo hakuna mtoto aliyelia, akiogopa kuambiwa ‘mpelekeni akalale’

Nyumbani kwa mzee Maftah Abdallah, aliyekuwa na nyumba kubwa yenye vyumba zaidi ya kumi na tano vilivyojaa wapangaji hali ilikuwa tofauti, watoto walikuwa bado wakicheza na kukimbizana huku na kule uwani, miongoni mwa watoto hao alikuwepo Mariam na Thomas, Mariam akiwa mtoto wa mwenye nyumba na Tom akiwa mtoto wa bwana Chacha, mpangaji aliyefanya kazi ya ulinzi kwenye kiwanda cha Soda cha Pepsi, kilichokuwepo huko huko Vingunguti.

“Tucheze mchezo wa baba na mama, mimi mama wewe baba!” ilikuwa ni sauti ya Mariam akimwambia Tom, ambaye hakukubaliana na mchezo huo, badala yake akawaita watoto wengine wa wapangaji waungane nao kucheza mchezo wa kujificha na kutafutwa, maarufu kwa jina la kombolela, watoto wote wakakubaliana, Mariam akatakiwa kujifunika na viganja vyake machoni na watoto wengine wote wakaenda kujificha, Tom akajificha kwenye nyumba ya kuku.

“Tiari bado?” Mariam aliuliza.

“Bado” watoto wengine ambao walikuwa bado hawajajificha waliitikia.

“Tiari bado?” Mariam akapataza sauti na kuuliza tena mara ya pili,

“Tiari!” Sauti za watoto zilisikika kutoka sehemu mbalimbali walizokuwa wamejificha, akaanza kuwatafuta mmoja baada ya mwingine, ndani ya muda wa nusu saa alishawaona wote lakini akabaki Tom peke yake, Mariam hakukata tamaa akizunguka huku na kule kufunua kila sehemu akimtafuta lakini hakumpata mwisho giza likazidi kuingia, watoto wengine wakaanza kuchukuliwa na wazazi wao kwenda kuoshwa.

“Labda kwenye nyumba ya kuku?” Alijiuliza Mariam ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka saba, mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Vingunguti na Tom miaka kumi mwanafunzi wa darasa la pili katika shule hiyo hiyo.

Taratibu akaanza kuisogelea nyumba ya kuku, ndani yake hapakuwa na kuku hata mmoja, wote walishakufa, akapiga magoti chini na kuanza kutambaa akiingia ndani yake, macho yake hayakuamini alipomwona Tom amelala kwenye kona, akataka kupiga kelele kuashiria kwamba amemwona, kabla hajafanya hivyo kiganja cha Tom tayari kilishaufunika mdomo wake kuzuia asiseme chochote.

“Mimi baba wewe mama, sawa?”

“Sawa!”

“Tulale kama vile baba na mama!”

“Sawa!”

Karibu wapangaji wote wa mzee Maftah walikuwa na chumba kimoja, wakiwa wamegawa katikati kwa pazia ili watoto walale upande wa pili, kwa wenye mtoto mmoja kama ilivyokuwa kwa Chacha na mkewe, hawakuona sababu ya kufanya hivyo, walilala na mtoto wao chumba kimoja wakijidanganya kwamba walikuwa ni watoto wadogo wasioelewa chochote, jambo ambalo halikuwa na ukweli, katika umri wa miaka kumi, Tom aliona kila kitu ambacho wazazi wake walifanya usiku wakiamini yuko usingizini na hicho ndicho alitaka kukifanya na Mariam. Akapanda juu yake.

“Mariaaam!Mariaaaam!Mariaaaam!” ilikuwa ni sauti ya Bi. Mwamtumu Maftah, mke wa baba mwenye nyumba akimtafuta mwanae wa mwisho ili aoge, Mariam hakuitika, aliendelea kubaki kimya Tom akiwa juu ya kifua chake, bila kuelewa jambo alilokuwa akifanya, kwao kilichokuwa kikitokea ni kuwaigiza baba na mama bila kuelewa maana yake.

“Mariaam!” aliendelea kuita lakini sauti ya mtoto wake haikusikika.

Ghafla akipita kando ya kibanda cha kuku alisikia minong’ono ya watoto “baba Khadija, niachie mwenzio watoto hawajalala” moyo wake ukashtuka, akarudi kinyumenyume mpaka kwenye kibanda hicho, akasikia sauti ya mtoto wa kiume “Wewe mama Tom, ritomu rimesharara, sogea huku” hiyo ilikuwa ni sauti ya Tom akimwigiza baba yake, mama yake Mariam hakuyaamini masikio yake baada ya kuhakikisha kabisa kwamba ni binti yake mdogo wa miaka sita na mtoto wa mpangaji wake walikuwa ndani ya kibanda cha kuku wakifanya mambo yasiyolingana na umri wao, akakimbia mbio hadi ndani kumwita mume wake.

“Hebu sikiliza mwenyewe kinachoendelea ndani ya hiki kibanda!” alimwambia mume wake ambaye baada ya kutega sikio, naye pia hakuamini, lilikuwa ni jambo la ajabu mno, hasira zikampanda.

“Hebu kawaite wazazi wa Tom, huyu mtoto wao atatuharibia mwanetu, mtoto ana miaka kumi keshaanza mambo haya? Wallah hatumtaki ndani ya nyumba yetu, lazima wahame!”

Mzee Chacha na mkewe walipoitwa hata wao hawakuamini walichokiona, walishindwa kuelewa ni lini Tom alikuwa amejifunza jambo la hatari kiasi hicho, alikuwa mdogo mno kuelewa mambo ya watu wakubwa, hawakuwa na habari kwamba kila kitu walichokifanya chumbani wakidhani amelala yeye alikiona na ndicho alichokuwa akikifanyia kazi.

“Hizi nyumba zetu za kupanga hizi? Kulala chumba kimoja na watoto ni balaa, inaleta shida sana kwenye malezi!”

“Unaongea kitu gani wewe Chacha, kwa hiyo unataka kutoa kisingizio kwamba nyumba ya kupanga ndio imefanya mwanao atake kuniharibia binti yangu? Usinitanie, jiandaeni kuhama, siwataki tena kwenye nyumba yangu!” mzee Maftah alifoka, Chacha na mkewe wakaweka mikono yao midomoni kwa mshangao, hakuamini kauli waliyoisikia kama kweli ililingana na kosa lililofanywa na watoto.

Maneno hayo hayakuwa utani, mzee Maftah aliandika notisi na kuwakabidhi siku hiyo hiyo akiwataka wahame ndani ya nyumba yake. Hawakuwa na la kufanya zaidi ya kukubali suala likawa ni wapi wangehamia, miezi mitatu baadaye notisi yao ilipokwisha walihamia kwenye nyumba nyingine jirani kabisa na shule ya msingi Vingunguti, mwendo wa dakika tano tu kufika shuleni, Tom akafurahi lakini akiwa na masikitiko mengi moyoni mwake sababu ya kutenganishwa na Mariam, alikuwa amezoea sana kucheza naye.

Mzee Maftah na mkewe walifikiri kuwatenganisha Tom na Mariam ingesaidia, jambo ambalo halikuwa kweli, ukaribu wao uliendelea kama kawaida wakiwa shuleni! Waliongea, walicheza na kufurahi pamoja lakini hawakudiriki tena kufanya mambo yaliyowasababisha wachapwe
 
SEHEMU YA 3 YA 50

Tom aliogopa mno, alama za fimbo bado zilikuwepo mwilini mwake na kila siku aliporejea nyumbani alionywa na wazazi wake kutojishughulisha na mambo hayo tena, akipewa kila aina ya vitisho ili aogope tendo la ndoa, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Mariam, naye alitishwa kupita kiasi.

Kwa miaka mitano iliyofuata mpaka Tom anamaliza darasa la saba, hawakuwahi kabisa kuongelea suala la mapenzi. Akafaulu kuendelea kidato cha kwanza kwenye shule ya sekondari Ukonga, hapakuwahi kutokea mwanafunzi mwingine aliyefaulu vizuri kiasi hicho, alisifiwa na kila mwalimu, alipewa zawadi mbele ya wazazi na wanafunzi wote na wakatakiwa waige mfano wake! Ilikuwa ni heshima kubwa sana kwa mzee Chacha na mkewe kusimamishwa mbele ya wageni wote waalikwa siku ya kuwapongeza wanafunzi wote waliofaulu.

“Hongera sana Tom!” Mariam alimwambia baada ya sherehe hiyo.

“Ahsante! Inabidi pia wewe uongeze bidii, una uwezo wa kufanya vizuri, jiepushe na mambo yaliyosababisha tukachapwa baada ya kufumwa kwenye nyumba ya kuku, si unakumbuka?”

Badala ya kujibu Mariam alitabasamu na uzuri wote wa sura yake ukaonekana, kimoyomoyo Tom akakiri kwamba Mariam alikuwa msichana mzuri na kuweka ahadi kwamba kama akifanikiwa kufanya vizuri katika masomo yake na kufika Chuo Kikuu hatimaye kupata kazi nzuri angemuoa, hakutaka kuyaweka maneno hayo wazi, alitaka kila kitu kibaki siri mpaka wakati muafaka ufike.

“Nitajitahidi sana kufuata nyayo zako Tom!”

Sababu ya umasikini hata kutimiza mahitaji ya shule, ilikuwa ni kazi ngumu kwa Tom,baba yake alijitahidi kufanya mpaka kazi za kuzibua mitaro akafanikiwa kupata ada peke yake, mpaka zikiwa zimebaki siku nne shule ifunguliwe, Tom alikuwa hajapata sare za shule na godoro. Hakuwa na mahali pa kukimbilia, ikabidi amfuate Mariam na kumwelezea kilichotokea, msichana huyo akamchukua mpaka kwa baba yake na kulia akiomba amsaidie, kwa kumwonea huruma mtoto wake, mzee Maftah alimnunulia Tom mahitaji yote yaliyobaki na kuondoka kwenda shule siku nne baadaye.

“Nakushukuru sana Mariam, bila wewe sijui kama ningekwenda shule, nitaukumbuka sana mchango wako maisha yangu yote!”

“Usijali, nahisi moyoni mwangu kuna upendo wa aina fulani kwako Tom!”

“Kweli?”

“Kabisa”

“Basi tuangalie kitu gani Mungu ataleta mbele ya safari”

Mariam alikuwa amefanya ndoto yake itimie, kwa Tom alionekana ni malaika mkombozi kwani bila yeye asingeweza kuendelea na masomo ya sekondari. Akamshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea, nyumbani aliwasimulia wazazi wake jinsi alivyopata msaada, hata wao hawakuwa tayari kuamini kama baba yake Mariam aliyewafukuza kwenye nyumba sababu Tom na Mariam walikutwa ndani ya nyumba ya kuku wakicheza mchezo wa baba na mama ndiye aliyempa fedha mtoto wao kukamilisha mahitaji yote ya shule.

Tom alisindikizwa na wazazi wake hadi Ukonga na kukabidhiwa kwa walimu wake, ulikuwa ni mwanzo mpya wa maisha. Kwa alivyokuwa amevaa, haikuhitaji maelezo yoyote kuelewa alikuwa ni mtoto wa masikini. Alibezwa na kupuuzwa na wanafunzi wenzake wengi wao wakiwa ni watoto wa matajiri jijini Dar es Salaam, hii ilimtia Tom hasira na uchungu lakini hakutaka kulipiza kwa mtu yeyote, nguvu zake zote zikaishia kwenye masomo ingawa alitengwa na wanafunzi wenzake.

Miezi mitatu baadaye walipofanya mitihani ya majaribio, matokeo aliyopata Tom yaliwashangaza walimu mpaka wanafunzi, alishika namba moja, akiwa amepata alama mia moja katika kila somo! Heshima ikaanza kupanda, wanafunzi wakaanza kumsogelea na kumfanya rafiki wakimtaka msaada. Hakuwa na kinyongo, alikuwa tayari kumsaidia kila mwanafunzi aliyemwomba kitu bila masharti yoyote, idadi ya marafiki ikaongezeka na Tom akazoea shule ingawa hakumwondoa Mariam katika akili yake, kila siku alikuwemo, alimuwaza wakati wa kula, kunywa na kulala! Alikuwa ni mtu muhimu sana kwake.

Shule ilipofungwa alirejea nyumbani kwa wazazi wake, baba yake alikuwa bado akiendelea na kazi ile ile ya ulinzi kwenye kiwanda cha Soda cha Pepsi na mama yake alifanya kazi ya kuponda kokoto, hiyo ndiyo kazi ambayo Tom alichagua kufanya ili kupata fedha za matumizi shule ikifunguliwa. Kila siku asubuhi aliondoka nyumbani na mama yake kwenda sehemu ilipokuwa ikijengwa barabara na kuchukua mawe kisha kuyasomba hadi karibu na nyumbani kwao ambako walianza kuyaponda kwa kutumia nyundo, kila siku Tom alifanya kazi hiyo na mama yake bila kuchoka.

“Mama kazi hii mpaka lini?”

“Hatuna jinsi mwanangu!”

“Lakini nitakuja kuwapumzisha wazazi wangu, kwani mmehangaika muda mrefu sana!”

“Jitahidi tu kusoma mwanangu!”

“Nitafanya hivyo mama!”

Alitamani sana kumwona Mariam lakini akaogopa kwenda kwao, kumbukumbu za kusababisha wazazi wake wafukuzwe kwenye nyumba bado ziliendelea kuishi akilini mwake, lakini mwisho alipokumbuka wema wa Mariam na wazazi wake walipompa fedha za mahitaji ya shule, aliamua kuweka hofu pembeni na kumuaga mama yake asubuhi moja na kutembea kwa miguu hadi nyumbani kwao, ilikuwa siku ya Jumapili, ambaye hapakuwa na uwezekano wa Mariam kutokuwepo nyumbani.

“Shikamoo mama!” alimwamkia mama yake.

“Marahabaaaa…nani huyu? Tom?”

“Ndio mama”

“Karibu mwanangu habari za shule?”

“Nzuri tu mama”

“Umeongezeka urefu!”

“Ahsante mama! Hamjambo hapa nyumbani?”

“Hatujambo!”

“Mama nimekuja kuwapeni shukrani zangu kwa wema mlionitendea! Sijui baba yupo?”

“Hapana ametoka asubuhi, usijali sana, tulikuwa tukitimiza wajibu, mbona sisi tulishasahau?”

“Mimi nakumbuka mama, nimemkuta Mariam?”

“Yupo…Mariaam!” alijibu mama huyo na kuanza kuita.

“Bee mama!” sauti ya Mariam ilisikika kutoka ndani.

“Njoo huku nje una mgeni!”

Ukimya ukatokea, baadaye Mariam akatokeza nje, alipomwona Tom furaha ilimjaa, akaruka juu na kushangilia huku akimkimbilia lakini alipomfikia alishindwa kumkumbatia baada ya kuona macho ya mama yake yakimwangalia kama vile alitaka kujifunza kitu! Wakashikana mikono na kusalimiana kwa heshima, kama alivyofanya kwa mama yake, Tom pia akamshukuru Mariam kwa wema aliomtendea na kumtaarifu kwamba alikuwa amefunga shule lakini alikuwa akiendelea vizuri, pia akachukua kadi yake ya matokeo na kumwonyesha.

“Umekuwa wa kwanza?”

“Ndio!”

“Amekuwa wa ngapi?” mama aliuliza.

“Wa kwanza mama, Tom ana akili sana, hongera!”

“Ahsante, wewe unaendeleaje?”

“Vizuri ingawa sikuwa wa kwanza, nilishika nafasi ya kumi!”

“Hongera pia, jitahidi mpaka uende sekondari!”

Waliongea mengi lakini mama hakutaka kuondoka, alikuwepo kusikiliza kila kitu kilichotoka midomoni mwao, Tom alipoaga mama hakumruhusu Mariam kumsindikiza, wakashikana mkono na akaondoka kurudi ndani huku akimshuhudia Tom akitembea kwenda nyumbani kwao, fikra za mapenzi zilikuwa zikijengeka ndani ya mioyo ya watoto hao, hakuna kilichokuwa kimebadilika siku walipofumwa ndani ya nyumba ya kuku, pamoja na kuwatenganisha baada ya wazazi wa Tom kufukuzwa nyumbani kwa baba yake Mariam walipokuwa wamepanga, bado waliendelea kupendana.
 
SEHEMU YA 4 YA 50

Nyumbani Tom alimsimulia mama yake kila kitu wakiponda kokoto, siku hiyo kazi hazikufanyika sawasawa, akili yote ikiwa kwa Mariam. Alimfikiria kila aliponyanyua nyundo juu na alimfikiria kila aliposhusha chini na kuvunja jiwe, ubongo wake ulijaa neno “Mariam!Mariam!Mariam” aliamini kwa upendo aliokuwa nao, huyo ndiye msichana aliyemfaa hata baadaye katika maisha yake, ingawa alikuwa bado ni mtoto mdogo alijikuta akifikiria hivyo akiamini upendo aliokuwa nao Mariam ulikuwa ni wa kweli, mtoto wa tajiri kumpenda masikini halikuwa jambo rahisi kukutana nalo.

Maisha yakaendelea, mara kwa mara Mariam akielekea kwenye masomo ya ziada alipita sehemu ambapo Tom na mama yake waliponda kokoto, alimwonea huruma lakini hakuwa na jinsi ya kumsaidia zaidi ya kuchukua sehemu ya nauli yake na kumwachia ili yeye na mama waitumie kununua chakula au maji. Ulikuwa ni upendo wa ajabu, hata mama yake Tom alikiri kwamba Mariam alikuwa na moyo tofauti kabisa na watoto wengine wa matajiri aliowafahamu.

“Kwa jinsi baba yake alivyo na majumba mengi hapa Dar es Salaam, lazima angekuwa na maringo ya kutisha!”

“Hayuko hivyo mama, ana moyo wa huruma sana Mariam!”

“Basi endeleeni na uhusiano huo huo, msigombane wala usije ukamuudhi!”

“Sawa mama!”

Shule zilipofunguliwa Tom aliagana na Mariam na kurejea shule ambako kazi ilikuwa ni moja tu; kusoma ili kulinda heshima aliyokuwa nayo na pia aliamini hiyo ndiyo njia pekee ya kumfikisha juu na kuendelea kuheshimiwa zaidi na jamii iliyomzunguka hata akiwa mkubwa, hakutaka maisha kama ambayo yeye na wazazi wake waliishi, alipenda sana kubadili historia, awe mtoto wa masikini aliyefanikiwa na kuwatia moyo watoto wengine ambao wangekuwa katika maisha kama ya kwake ili kuonyesha kwamba mafanikio ni ya kila mtu.

Utaratibu uliendelea kuwa ule ule, nafasi ya kwanza ilikuwa ni ya kwake mpaka anamaliza kidato cha kwanza na kuingia cha pili, kila mtu alimpenda, walimu walimfurahia na waliamini kabisa ni yeye ndiye angeweza kuiletea heshima shule yao kwenye mitihani ya kidato cha nne kama angeendelea na kasi hiyo hiyo. Kidato cha pili kilikuwa kizuri sana kwake, hasa kwa kuwa pia Mariam alikuwa amefaulu na kujiunga na shule hiyo hiyo kwa kidato cha kwanza, yeye ndiye akawa mwenyeji wake. Furaha ikawa imeongezeka, wasichana wote walioonekana kuwa karibu naye wakimtaka mapenzi, hakusita kuwatambulisha kwa Mariam ili wajue Paka alikuwa ameingia, Panya wote waondoke.

“Huyu ndiye Mariam uliyekuwa ukimwongelea?” wasichana waliuliza.

“Ndio”

“Ni mzuri!”

“Ahsante, hata mimi najua” Tom alitania.

Urafiki wao ulizidi kukomaa na matatizo ya Tom kiuchumi yakapungua kwani Mariam alimsaidia kwa kila kitu, kila alichotumiwa iwe ni chakula, dawa ya meno ama fedha waligawana na kutumia pamoja. Shukrani zake kwa Mariam alizitoa kwa njia ya kumfundisha masomo aliyoyapitia kidato cha kwanza, yeye pia akaanza kufanya vizuri akashika namba moja kwenye kila mtihani, hii iliwafurahisha sana wazazi wa Mariam kiasi kwamba kila walipokuja shuleni kuwatembelea ilikuwa ni lazima waonane na Tom kumpa shukrani zao.

“Tunakushukuru sana Tom na tunaomba utusamehe kwa yote yaliyotokea ukiwa mtoto mdogo nafikiri wazazi wako huwa wanaliongelea sana suala hili nyumbani!”

“Yalishapita wazazi, ulikuwa utoto tu ule!”

“Basi ni vyema endeleeni hivyo hivyo, kila tutakachomtumia Mariam pia kitakuwa cha kwako!”

“Ahsante mama!”

Hiyo ikawa kama ni ruhusa kwao, mapenzi yakaongezeka ingawa hawakudiriki hata siku moja kubusiana wala kufanya ngono na hakuna kati yao aliyewahi kumwambia mwenzake anampenda kingono! Walikuwa marafiki wa kweli ambao kwao neno “Mapenzi” lilikuwa ni zaidi ya kufanya tendo la ndoa, mwaka wa kwanza ukapita wakiwa pamoja, hatimaye ukaja wa pili, Tom akaingia kidato cha nne na kuendelea kufanya vizuri katika masomo yake kuliko ilivyokuwa kwenye vidato vilivyotangulia, walimu wote walimtegemea yeye kupeperusha bendera ya shule ya sekondari Ukonga Kitaifa, nafasi ya kwanza Tanzania nzima iliaminika kuwa yake.

“Tom!”

“Yeah!”

“I am so proud of your success!” (Najivunia mafanikio yako!)

“Thanks!” (Ahsante)

“And I know you are going to perform well in your final exams!” (Na ninajua utafanya vizuri kwenye mitihani yako ya mwisho!)

“I know! My mind is stronger than any challenge ahead” (Najua, akili yangu ni imara kuliko changamoto yoyote mbele yangu!)

“Today I want to tell something!” (Leo nataka kukuambia kitu)

“What is it girl?” (Nini hicho?)

“NAKUPENDA!”

“Najua unanipenda na mimi nakupenda pia!”

“Sikupendi kama tunavyopendana!”

“Unanipendaje?”

“Vile kivingine!”

“Kivingine aje?”

“Tom!”

“Sijakuelewa!”

Mariam alitumia uwezo wake wote wa kujieleza akijaribu kukitoa kilichokuwemo ndani ya moyo wake ili Tom aweze kuelewa ni kiasi gani alimpenda na alihitaji nini kutoka kwake lakini bado Tom alimkatalia, hakuwa tayari kabisa kujiingiza katika uhusiano zaidi ya uliokuwepo, bado aliikumbuka picha ya tukio la utotoni walipofumwa ndani ya nyumba ya kuku wakiigiza kufanya mapenzi, jambo lililosababisha yeye na wazazi wake wafukuzwe kwenye nyumba ya wazazi wa Mariam kwenda kupanga sehemu nyingine, bado taswira ilikuwemo kichwani na ilimfanya amwogope Mariam, hakuwa tayari kukororofishana tena na wazazi wake waliojitolea kuwa wafadhili wa masomo yake kwa miaka yote aliyokaa shuleni.

“No!No Mariam, we cant be more than this!” (Hapana! Hapana Mariam, hatuwezi kuwa zaidi ya hapa)

“Think twise darling!” (Fikiria mara mbili mpenzi)

“Even if I think about it a dozen times it won’t change a thing!” (Hata nikifikiria mara kumi na mbili, bado haitabadilisha chochote!)

“I love you Tom, with all my heart, please accept me as your lover!” (Nakupenda Tom, kwa moyo wangu wote, tafadhali nipokee kama mpenzi wako!)

“It is not possible darling, let’s just remain good friends, helping one another to achieve our dreams!” (Haiwezekani mpenzi, tuendelee kuwa marafiki, tukisaidiana kutimiza ndoto zetu!)

“I know, but …!(Najua lakini…)

“That is the truth!” ( Huo ndio ukweli) Tom alisisitiza.

Wote wawili walikuwa bado bikra, mpaka wakati huo Tom akiwa kidato cha nne na Mariam cha tatu, walikuwa bado hawajakutana na mtu yeyote kimwili! Halikuwa jambo rahisi sana kwa mtu kuamini, lakini huo ndio ulikuwa ukweli, Tom alikuwa amedhamiria kuutunza mwili wake kama ilivyokuwa kwa Mariam mpaka watakapomaliza Chuo Kikuu, wote wawili wakiwa wamesahau kwamba miili yao ilikuwa ikikua na mihemko kuongezeka, kilichokuwa kikimtokea Mariam hakikuwa ridhaa yake ni mabadiliko ya mwili yaliyokuwa yakimsukuma, alihitaji sana kufanya tendo la ndoa na mtu pekee wa kufanya naye hakuwa mwingine isipokuwa Tom, alimpenda kwa moyo wake wote.
 
SEHEMU YA 5 YA 50
Kumkatalia msichana mwenye umbile na sura nzuri kama Mariam ilihitaji moyo, haikuwa rahisi sana kwa vijana wengi hasa wa umri kama aliokuwa nao Tom, yeye pia mwili wake ulikuwa ukichemka ni kweli alivutiwa na Mariam kwa kila kitu lakini alijitahidi kadri ya uwezo wake kupambana na hisia zote zilizokuwa zikimpata, Mariam alikuwa mzuri, kuanzia juu hadi chini hapakuwa na mahali pa kumkosoa na kila alipopita mbele ya kundi la wavulana walionekana kupagawa, hakika alikuwa na mvuto wa kutisha, huo ndio ambao Tom alikuwa akipambana nao.

Hakustahimili sana jambo hilo, mwezi mmoja baadaye alijikuta amepunguza msimamo na kuruhusu angalau kuwa wanabusu kwenye kona usiku baada ya kujisomea, hii ilikuwa ni faraja tosha kwa Mariam aliyeamini lazima nia aliyokuwa nayo ingetimia! Kila siku usiku ilikuwa ni lazima wafanye jambo hilo kabla ya kwenda kulala, jambo pekee ambalo Tom hakuwa tayari kulitenda ni ngono.

“Siwezi Mariam, nilishaweka nadhiri ya kutokukutana na mwanamke mpaka niingie Chuo Kikuu!” alimwambia Mariam siku moja wakiwa gizani kabla ya kwenda kulala, alikuwa akishinikiza wakutane kwenye choo cha shule na kufanya tendo hilo.

“Kidogo tu! Wala haitachukua muda, nakupenda Tom tafadhali kubali!”

“Unaweza kupata mimba halafu wazazi wako wakanichukia tena! Huyo ni shetani Mariam lazima upambane naye, ukimruhusu sana hutamaliza masomo yako, ni afadhali umekutana na mimi ninayeweza kukupa ushauri!”

“Nina kondomu, tutaitumia!”

“Umeitoa wapi?”

“Nilipewa na msichana mmoja darasani kwetu!”

“Hata kama una kondomu siwezi kukubali, tendo la ndoa kabla ya ndoa ni dhambi!”

“Tom utabaki kwenye msimamo huo mpaka lini? Mbona wenzetu wanafanya na wanafunzi wengi pia wananifuata mimi nakataa?”

“Naomba uendelee kukataa hivyo hivyo, hiyo ni kwa faida yako!”

Msimamo wa Tom uliendelea kubaki huo huo mpaka mwisho wa muhula ukafika, shule ikafungwa na wote wakarejea nyumbani. Alijisikia mshindi moyoni mwake baada ya majaribu makubwa ya Mariam ambaye tayari alishaanza kuonyesha chuki kwa sababu ya kukataliwa. Wakiwa nyumbani waliendelea kuwasiliana kama kawaida, wakienda kwenye masomo ya ziada pamoja, wazazi wa Mariam walimfurahia na Tom, hawakuwa na wasiwasi naye kwa kitu chochote, wakiamini angemsaidia mtoto wao kutimiza ndoto bila kuelewa kilichokuwa kikiendelea kichwani mwa Mariam.

Usiku wa manane wiki moja kabla shule haijafunguliwa, Tom alizinduliwa usingizini na kelele za mlango ukigongwa, aliposikiliza vizuri ilikuwa ni sauti ya mama yake. Halikuwa jambo la kawaida mama yake kumgongea usiku, ilipotokea kuna shida ni baba aliyekwenda chumbani kwa Tom kumwamsha, hii ilimshtua na kumfanya anyanyuke haraka kwenda kufungua mlango akiwa amevaa bukta tu.

“Vipi mama?”

“Imebidi tu nikuamshe!”

“Kwani kuna nini?”

“Baba yako!”

“Kawaje? Kalewa halafu anakupiga?” Tom aliuliza kwa mshangao, mara kadhaa huko nyuma ilipotokea baba yake akanywa pombe nyingi alimfanyia fujo mama na hata kufikia hatua ya kumpiga jambo ambalo Tom hakulipenda hata kidogo.

“Hapana anaumwa!”

“Anaumwa?”

“Ndio!”

“Nini?”

“Mkojo umekataa kutoka anasema tangu jana mchana, walinzi wenzake wamemrudisha kutoka kazini!”

Tom hakuongea zaidi, wala kuuliza chochote alichokifanya ni kuchomoka chumbani na kupita sebuleni akielekea chumbani kwa wazazi wake, nyumba yao ilikuwa ni ya vyumba viwili na sebule. Halikuwa jambo la kawaida kwake kuingia chumbani kwa wazazi wake lakini siku hiyo alilazimika kufanya hivyo, akamkuta baba yake amelala sakafuni akitupa miguu huku na kule na kulalamika maumivu ya tumbo, mwili wote ulikuwa umelowa jasho, akitua harufu kali ya mkojo! Ingawa alijua kabisa Tom hakuwa na uwezo wa kumsaidia alianza kulia akiomba ampunguzie maumivu, hali ilimchanganya Tom, akamgeukia mama yake aliyekuwa akilia.

“Mama tufanyeje?”

“Twende hospitali!”

“Tutapata wapi daladala saa hizi?”

“Sijui!”

“Tusaidiane kumbeba mpaka stendi, Mungu atajua huko huko!”

“Sawa mwanangu!”

Wakakubaliana, mzee Chacha alikuwa mzito sana kwao lakini walijitahidi kadri ya uwezo wao na kumbeba juu juu wakipita kwenye madimbwi ya maji sababu mvua kubwa ilikuwa imenyesha jijini Dar es Salaam siku hiyo. Njia nzima mzee Chacha alikuwa akilia kama mtoto mdogo, hata hivyo wakafanikiwa kufika stendi na kumlaza chini, tayari ilikuwa saa tisa na nusu za usiku kwa mujibu wa saa ya plastiki ambayo Tom alikuwa amevaa mkononi, kila gari lililopita walijaribu kulisimamisha lakini hakuna lililosimama, wote wawili wakachanganyikiwa.

“Mama!”

“Naam mwanangu”

“Acha nikimbie nyumbani kwa akina Mariam nikamwombe baba yake atusaidie gari!”

“Wazo zuri sana, laiti ungekuwa umesema mwanzo, hivi sasa tungekuwa hospitali!”

“Nilipitiwa!”

Pamoja na giza lote lililokuwepo Vingunguti sababu ya mawingu ya mvua angani, Tom hakuogopa, ni kweli hakuzoea kutembea usiku kwa kuogopa vibaka lakini siku hiyo aliweza. Akakimbia moja kwa moja hadi nyumbani kwao na Mariam na kuanza kugonga kwenye lango kuu la kuingilia lakini hakuna mtu aliyemsikia wala kufungua, akalazimika kuzunguka nyuma ya nyumba na kugonga kwenye dirisha la kwanza alilokutana nalo bila kujua nani aliyelala ndani ya chumba hicho.

“Nani?” ilikuwa ni sauti ya Mariam.

“Mariam?”

“Ndio!”

“Mimi ni Tom!”

“Tom?”

“Ndio!”

“Unafanya nini saa hivi nje?”

“Baba yangu anaumwa!”

“Anaumwa nini?”

“Ameshindwa kukojoa!”

“Mungu wangu! Sasa?”

“Nimekuja kuomba msaada wa gari!”

“Baba amesafiri, tutafanyaje sasa?”

Tom alikuwa gizani akijaribu kutafakari juu ya nini cha kufanya ili kuhakikisha kwamba baba yake anapelekwa hospitali baada ya kuambiwa na Mariam kuwa gari lilikuwepo lakini baba yake ambaye dereva alikuwa amesafiri, hivyo hapakuwa na dereva wa kuifanya kazi hiyo. Akamwomba Mariam atoke nje ili wapate kushauriana kwa sababu akili yake yeye ilikuwa imekoma kufanya kazi.

“Sidhani kama mama atakubali nitoke nje!”

“Sasa?”

‘Tuongelee hapa hapa!”

“Hakuna njia yoyote unayoweza kuitumia kunisaidia?”

“Nakuhurumia sana Tom lakini sidhani kama naweza, mimi najua kuendesha gari lakini sio sana, hata mara moja sijawahi kuendesha gari mbali na hapa nyumbani tena baba akiwa hayupo!”

“Kwa hiyo unaweza kuendesha?”

“Kidogo naweza!”

“Sasa kwanini usijaribu?”

“Naogopa kugongana na magari barabarani!”

“Lakini hakuna magari mengi hivi sasa!”

“Mh! Tom unanishawishi kufanya jambo la hatari sana”

“Mariam take risk for me!” (Mariam thubutu kwa ajili yangu)

“Hebu subiri!” Mariam aliongea akishuka kitandani kisha kunyata hadi sebuleni ambako aligusa juu ya kabati mahali ambako siku zote ufunguo wa gari ulihifadhiwa na kukuta upo, akauchukua na kunyata tena hadi chumbani ambako alimwomba Tom amsubiri nje ya lango.

“Sawa!”

Baada ya kuvaa nguo zake, Mariam alinyata kwa mara nyingine akitumia ustadi wa paka mpaka akaufikia mlango na kuufungua bila kelele
 
SEHEMU YA 6 YA 50

yoyote kisha kutembea hadi kwenye lango la kutokea nje, pia akalifungua na kutoka. Tom alikuwa akimsubiri, akamsogelea na wakakumbatiana, Mariam alipomwangalia vizuri aligundua machozi yalikuwa yakimtoka.

“Usilie Tom!”

“Nampenda sana baba yangu!”

“Najua!”

“Naomba unisaidie baba afike hospitali, nakufanyisha kosa lakini sina jinsi, wewe peke yake ndiye msaada ninaoutegemea, tafadhali nisaidie ili baba yangu apone, Mariam unataka niendelee na shule?”

“Ndio!”

“Basi nisaidie ili baba yangu apone, akifa sina uhakika kama naweza kuendelea kusoma!” aliongea Tom akilia, maneno hayo yakauchoma moyo wa Mariam mpaka ndani kama vile mkuki wa moto, naye akalengwalwengwa na machozi..

“Sasa sikiliza!” Mariam alisema.

“Ndio!”

“Nafungua lango kuu, kwa sababu sitaki kuliwasha gari likiwa mahali lilipo, mama atasikia muungurumo, hivyo basi itabidi tulisukume sisi wenyewe kulitoa ndani mpaka pale mbele kwenye mteremko ndipo tuliwashe, huo ndio mtihani tulionao, tukifanikiwa basi mimi niko tayari kuthubutu kuendesha gari kwenda hospitali, si ni Amana Ilala?”

“Ndio!’

“Uko tayari kusukuma gari?”

“Natamani lingekuwa limeshafika nje” Tom aliongea akionyesha utayari wake.

Bila woga Mariam akanyata tena na kuingia ndani ambako kwa taratibu sana alizungusha komeo la lango na kufanikiwa kufungua bila kelele ndipo akamwita Tom aingie ndani, wote wawili kwa nguvu zao zote walizokuwa nazo na hata za akiba, walishirikiana na kufanikiwa kusukuma gari hilo dogo aina ya Nissan Datsun hadi nje ambako waliendelea kusukuma mpaka mbele mita kama hamsini hivi, kilichowasaidia ni mteremko, ndipo Mariam akaingia na kuketi kwenye usukani, mara moja akawasha na gari likaitika. Tom alibaki mdomo wazi, hata siku moja hakuwahi kufahamu kwamba msichana huyo alikuwa na uwezo wa kuendesha.

“Nani alikufundisha kuendesha gari Mariam?”

“Ni baba, lakini hajawahi hata siku moja kuniruhusu niendeshe peke yangu!”

“Haya twende basi!”

“Umesema wako sehemu gani?”

“Stendi”

Mariam aliendesha gari kwa ustadi mkubwa, wakipita kwenye barabara zenye madimbwi mpaka wakafanikiwa kufika stendi na kuwakuta wazazi wa Tom wakisubiri, wote wamelowa na mvua, baba akiendelea kulia kwa maumivu makali aliyokuwa nayo yaliyosababishwa na mkojo uliogoma kutoka! Mama yake Tom hakuamini alipoona gari linasimama na mwanae kushuka, macho yake alipoyatupa kwenye usukani alimwona Mariam ameketi, hakutaka hata kuuliza swali lolote, alichokihitaji wakati huo ni kufika hospitali tu.

Baada ya kuegesha gari Mariam alishuka, wote wakasaidiana kumpandisha mgonjwa garini, zoezi lilipokamilika wote wakapanda, gari likawashwa tena na safari kwenda hospitali ya Amana ikaanza. Akiwa nyuma ya usukani Mariam alitetemeka lakini hakutaka kuionyesha hali hiyo, mpaka wakafika Tazara ambako alikata kushoto kuelekea Buguruni ambako alikata kulia kuingia barabara ya Uhuru bila kukutana hata na gari moja barabarani, akanyoosha moja kwa moja hadi hospitali ya Ilala Amana, yeye mwenyewe hakuamini kama alikuwa amewafikisha.

“Nakushukuru Mungu!” alitamka maneno hayo kimoyomoyo alipoegesha gari mbele ya jengo lililoandikwa OPD na wauguzi wakafika wakiwa na machela.

“Vipi?” mmoja wao akauliza.

“Tuna mgonjwa!”

“Anaumwa nini?”

“Ameshindwa kukojoa!”

“Poleni!”

Wauguzi wakapanda ndani ya gari na kwa kusaidiana na Tom pamoja na Mariam walimshusha mgonjwa na kumlaza juu ya machela ambayo ilisukumwa moja kwa moja hadi kwenye chumba cha daktari, akalazwa kitandani na daktari kuanza kumchunguza kwa makini, alishangazwa na jinsi mfuko wa mkojo ulivyokuwa umetuna.

“Mzee hujakojoa tangu saa ngapi?”

“Tangu juzi!”

“Pole sana…masista hebu nileteeni Catheter na vifaa vyote vya Catheterization haraka” Daktari aliagiza.

“Sawa daktari!” Mmoja wao aliitikia na kuondoka mbio aliporejea alikuwa amebeba sinia lenye vifaa pamoja na mpira wa kutolea mkojo, vyote akaviweka kwenye meza iliyokuwa kando ya kitanda, daktari akawaomba ndugu wa mgonjwa watoke nje ili apate kufanya kazi yake.

Tom, Mariam na mama yake wakatoka nje. Alichokifanya daktari ni kuchukua mpira na kuuingiza kwenye uume wa mzee Chacha na kuusukuma moja kwa moja mpaka kwenye mfuko wa mkojo, ilikuwa ni kazi ngumu kidogo kuliko alivyofanya kwa wagonjwa wengine lakini ulipoingia mkojo mwingi ukatoka kwa nguvu na kuanza kujaa kwenye mfuko wa plastiki ambao mpira wa kutolea mkojo ulikuwa umeunganishwa nao. Mzee Chacha akashusha pumzi na maumivu yote yakaisha.

Nje ya chumba cha daktari, Mariam na Tom waliendelea kuongea mama akiwa kimya, fikra zote zikiwa zimetekwa na tatizo la mume wake. Hakuwa na uhakika kama angeweza kupona, ilikuwa ni mara ya kwanza kushuhudia binadamu ameshindwa kukojoa, hakuna kitu alichotamani kama mume wake kupona kwani maisha katika jiji la Dar es Salaam yasingewezekana bila yeye kuwepo, mshahara wake wa ulinzi ulikuwa mdogo lakini uliweza kuitunza familia yao.

“Tom!”

“Naam”

“Acha mimi nirudishe gari la wao kabla hakujakucha, mama yangu huwa ana kawaida ya kuamka saa kumi na mbili kamili, hivi sasa ndio nasikia Adhana inalia, acha nirudi, ili mradi nimeshakufikisha hapa, endeleeni na matibabu nitakuja kukuona asubuhi!”

“Nakushukuru sana Mariam, msaada ulioutoa ni mkubwa sitausahau, nakupenda kuliko unavyofikiria!”

“Nakupenda pia na ndio sababu nayafanya yote haya!”

“Endesha vizuri njiani, naomba Mungu asaidie ufike nyumbani salama!”

“Amina!”

Wote wakasimama na kukumbatiana, walipoachiana ndipo Mariam alimfuata mama yake Tom na kumuaga, yeye pia alitoa shukrani nyingi na kumtaka pia afikishe shukrani hizo kwa wazazi, hakuwa na habari kabisa kwamba gari liliibiwa. Mariam akashukuru na kuingia ndani ya gari, kuwasha na kuondoka kwa mwendo wa kawaida.

Mbele aliingia barabara kuu ya Uhuru na kunyoosha kama alivyokuja mpaka akafika Tazara kwenye mataa, macho alipoyatupa mbele aliona taa za kijani zikiwaka, akawa na uhakika ilikuwa ni zamu yake, kwa haraka aliyokuwa nayo wala hakutaka kuangalia upande mwingine wowote, akakata kona kuelekea uwanja wa ndege, hakujua kama kulikuwa na daladala la kutokea Mbagala likija kwa kasi bila kujali taa alishtuka, aliona mwanga mkali machoni.

“Mamaaaaaaa! Nakufa!” ndio maneno pekee aliyoyasema ukatokea ukimya.

***

“Tumeutoa mkojo sasa hivi anajisikia vizuri, lakini ni lazima tufanye uchunguzi ili kufahamu ni kwanini alishindwa kukojoa, hapa kuna uwezekano kukawa na moja kati ya matatizo mawili, aidha ana Stricture au Benign Prostatic Hypertrophy!” daktari aliongea baada ya kuwaita Tom na mama yake kutoka nje.

“Sijakuelewa daktari” Tom alisema, maneno yaliyokuwa yametolea yalikuwa ni mazito sana kwa elimu yake ya kidato cha nne.

“Inawezekana kuna kovu ambalo limeziba njia ya mkojo, hii inaitwa Stricture au Tezi ya Prosteti imepanuka sababu ya uzee na kuuziba mrija wa kutoa mkojo nje sababu unapita ndani yake!”

“Mungu wangu si ni magonjwa makubwa sana hayo?”
 
SEHEMU YA 7 YA 50

“Hapana, yanaweza kutibika kwa njia ya upasuaji lakini ni lazima tufanye kwanza uchunguzi kupata uhakika! Subiri kuche, ili afanyiwe vipimo vya Ultra-sound ili tuone kama kuna tatizo lolote tumboni, sawa?”

“Sawa daktari!”

“Kwa hivi sasa naandika cheti akalazwe wodi ya wanaume!”

“Ahsante daktari!” mama yake Tom aliitikia.

Kulipokucha hapakuwa na kazi nyingine iliyofanyika hospitali kwa mzee Chacha zaidi ya vipimo, daktari aliandika kwenye faili lake afanyiwe kipimo cha kupiga picha tumboni kilichoitwa kwa kimombo Ultra-sound, saa tatu kamili wauguzi walifika na kumbeba kwenye machela kumpeleka kwenye chumba cha kipimo hicho, mrija wa mkojo ukiwa mahali pake. Kila kitu kikafanyika na akarejeshwa wodini baada ya dakika arobaini na tano, Tom na mama yake walikuwepo kusubiri, mioyo yao ikiwa na hamu kubwa ya kujua tatizo lililokuwa likimsumbua mgonjwa wao.

“Tom!” Dk. Magesa alifika na kumwita nusu saa baadaye, mkononi akiwa ameshikilia faili juu yake likiwa limeandikwa Chacha Mitiro, Tom akaelewa lilikuwa ni faili la baba yake.

“Naam daktari”

“Njoo wewe na mama tuongee!”

Akamgusa begani mama yake alikuwa akisinzia kwenye msingi nje ya wodi na kumwomba anyanyuke wafuatane, wakaingia wodini ambako wauguzi walikuwa bado wakimsaidia mzee Chacha kupanda kitandani. Daktari akaanza kufungua faili lililokuwa mikononi mwake, wakati anamaliza wauguzi nao walishamaliza kumlaza mgonjwa kitandani ndipo daktari akaanza kulielezea vizuri tatizo lililokuwa likimsumbua mzee Chacha.

“Mzee anaumwa, ana uvimbe tumboni!”

“Uvimbe wa nini?” mama yake Tom aliuliza.

“Tezi ya Prostate, kwa ilivyovimba nahisi atakuwa na Saratani, kwani uvimbaji wake sio wa kawaida, nahitaji kumchukua kwenda chumba cha upasuaji leo mchana ili nipate kuchukua kipande cha nyama kwenye tezi hiyo nikipeleke hospitali ya Ocean Road kuhakikisha ninachokiwaza!”

“Sawa tu daktari!”

“Kwa hiyo naomba muwe wavumilivu, kwa hivi sasa atatumia dawa za kuzuia maambukizi lakini pia atakojoa kwa kutumia mpira, tukishapata majibu ndio tutajua sasa ni nini kifanyi…!” daktari hakuimaliza sentensi yake hadi mwisho akashangaa kuona mzee Chacha akikakamaa kitandani kama mtu mwenye degedege kali, lilikuwa jambo la ajabu sana kulishuhudia kwani mara nyingi waliopatwa na tatizo hilo walikuwa ni watoto wadogo.

“Mungu wangu baba kawaje tena?” Tom aliongea akimwangalia daktari.

“Hebu nipeni sindano ya Valium!” daktari aliwaeleza wauguzi huku akimlaza mzee Chacha vizuri kitandani kuhakikisha haumi ulimi wake, muda mfupi baadaye muuguzi alirejea na chupa ya dawa pamoja na bomba la sindano, akamkabidhi daktari ambaye aliivunja na kuinyonya dawa yote kwa kutumia bomba kisha kumchoma mzee Chacha, muda mfupi baadaye akatulia na kulala usingizi.

“Sijui ni kwanini anapatwa degedege? Nahitaji kujua hili suala, sijawahi kuona mtu aliyeshindwa kukojoa akapatwa na hali hii, lazima kuna tatizo jingine hapa!”

“Tusaidie kumchunguza vizuri daktari, huyu ni baba yangu ndiye anayenisomesha, akifa mimi nitakuwa nimekwama moja kwa moja!”

“Unasoma darasa la ngapi Tom?”

“Kidato cha nne!”

“Ulikuwa wa ngapi kwenye mtihani wako?”

“ Wa kwanza!”

“Hongera, unataka kuwa nani ukimaliza masomo yako?”

“Kama wewe”

“Daktari?”

“Ndio!’

“Kazi ya wito hii mwanangu!”

“Nafahamu lakini nataka kusaidia watu, kuna masikini wengi kama mimi!”

“Nakutakia kila la kheri, sasa saa tano kamili watakuja kumchukua wamlete chumba cha upasuaji nichukue hicho kipimo, sawa?”

“Sawa daktari!”

Kama ilivyopangwa saa tano kamili machela iliingizwa wodini na mzee Chacha akapandishwa juu yake kisha kupelekwa moja kwa moja hadi chumba cha upasuaji Tom na mama yake wakifuata nyuma na kusubiri nje ya chumba hicho wakiwa na wasiwasi mwingi! Ndani akaingizwa kwenye chumba kimoja kidogo kwa ajili ya kazi hiyo ambako alimkuta Dk. Magesa akimsubiri, kazi ikaanza kufanyika na kukamilika ndani ya kipindi cha nusu saa, haukuwa upasuaji kama ambavyo Tom na mama yake walifikiri bali kifaa fulani kiliingizwa kwa kutumia mashine mpaka kwenye tezi hiyo na kuchukua kipande cha nyama, kikawekwa ndani ya chupa tayari kwa kupelekewa hospitali ya Ocean Road.

Mgonjwa aliporudishwa wodini, mawazo ya Tom yalirejea tena kwa Mariam akaanza kufikiria juu ya wema wote alimtendea, hakujua kabisa angefanya kitu gani ili msichana huyo apate kuzielewa shukrani zake! Hakuwa na jinsi zaidi ya kumpenda, tayari alishaanza kumkubali na kuona kama ingewezekana baadaye katika maisha yao, alikuwa tayari hata kubadili dini yake lakini amuoe Mariam kuwa mke wake wa maisha, mambo aliyomtendea yalikuwa makubwa mno.

“Ananipenda kwa ukweli kabisa!” aliwaza.

Baadaye mama yake aliondoka na kumwacha Tom wodini, kama kawaida aliendelea kumuwaza Mariam akimsubiri kwa hamu, alijua mchana huo ni lazima angefika sababu aliahidi siku hiyo badala ya kwenda kwenye masomo ya ziada angerudi wodini kumwona baba yake Tom. Mpaka saa kumi na moja wakati mama analeta chakula cha jioni, Mariam alikuwa hajaonekana, Tom akahisi labda wazazi wake hawakumruhusu kwani isingekuwa kawaida asifike kabisa kwa upendo aliokuwa nao moyoni mwake.

“Mariam amekuja?”

“Bado”

“Kwanini?”

“Sifahamu mama, lakini atakuja tu!

Walikaa na mama yake mpaka muda wa kuona wagonjwa ukapita bila Mariam kuonekana, mama akaondoka kurudi nyumbani akimwacha Tom mwenye mawazo mengi kichwani mwake, si kwa sababu baba yake alikuwa akiumwa peke yake bali kwa sababu pia Mariam alikuwa hajaonekana, alimpenda mno, alitamani kuwasiliana naye angalau kwa simu lakini hakuwa na namba, matumaini akayahamishia siku iliyofuata ambayo pia Mariam hakuonekana, wasiwasi wake ukazidi kuongezeka.

“Haiwezekani, au kwa sababu kaona baba yangu kaugua? Ndio maana ananitelekeza? Lakini Mariam hawezi kufanya hivyo, ana upendo wa kweli, sijui tu ni kitu gani kimempata!”

Siku tatu baadaye alizobaki wodini akimwangalia baba yake kuanzia sababu mama hakuruhusiwa kulala kwenye wodi ya wanaume, Mariam alikuwa hajaonekana! Badala ya huzuni hisia za chuki zikaanza kumwingia Tom, moyoni akajua alikuwa ametelekezwa kwa sababu baba yake alikuwa mgonjwa. Siku hiyo ndiyo majibu kutoka Ocean Road yalikuja na kuthibitisha kabisa kwamba baba yake Tom alikuwa na Saratani iliyocheleweshwa kupata matibabu na kusambaa karibu kwenye viongo vyote muhimu vya mwili ukiwemo ubongo.

“Ndio maana anapatwa na degedege kumbe ubongo wake umekwishashambuliwa na Saratani!” Dk Magesa aliongea na Tom pamoja na mama yake ofisini.

“Atapona?” Tom aliuliza.

“Kwa kweli ni kazi ngumu kidogo, kwanza itabidi ahamishwe hapa kupelekewa hospitali ya Ocean Road ambako watamwanzishia matibabu ya Saratani, Mungu akisaidia anaweza kupona!”

“Tunashukuru daktari!”

Maelezo hayo baadaye yalitolewa kwa mzee Chacha katika lugha ya kumpa matumaini na wakapakiwa

ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 8 YA 50

ndani ya gari kwenda hospitali ya Ocean Road, Tom akiwa ameacha maagizo kwa wauguzi kwamba ikitokea Mariam akaonekana na kuulizia basi aelekezwe mahali walikokuwa, wauguzi wakaahidi kumsaidia kufanya hivyo. Safari ya hospitali ya Ocean Road ikaanza, siku zote Tom alipita nje ya hospitali hiyo akielekea feri lakini hakuwahi kuwaza kwamba siku moja angeingia humo akiuguliwa na baba yake, hakuamini kama Saratani ingeweza kuingia ndani ya familia yake, aliuona ugonjwa wa watu wengine.

Matibabu yalianza siku hiyo hiyo kwa njia ya vidonge, mionzi na dawa za sindano ambazo badala ya kuonekana kumsaidia mzee Chacha zilimdhoofisha zaidi, afya yake ikaharibika kabisa na kupoteza uzito mwingi ndani ya muda mfupi! Nywele zote zikanyonyoka kichwani sababu ya ukali wa dawa alizokuwa akipewa.

Kila mara Tom alipomwangalia baba yake alishindwa kuvumilia na kutoka nje ambako alibubujikwa na machozi akitamani angalau Mariam angeonekana na kumpa maneno ya faraja lakini haikuwa hivyo, hatimaye wiki mbili zikakatika hali ya mzee Chacha ikizidi kuwa mbaya, madaktari wakashauri mgonjwa arudishwe nyumbani hasa baada ya kugundua alikuwa ni mtu wa Tarime na mke wake hakuwa tayari azikwe jijini Dar es Salaam kama kingetokea kifo jambo ambalo kila mtu alikuwa akilitarajia.

“Sawa tu daktari nimekubali, tatizo letu kubwa ni nauli, hatuna fedha kabisa!”

“Mimi na wafanyakazi wenzangu tutawachangia fedha kidogo lakini pia ninyi mnaweza mkajitahidi kutafuta kwa ndugu jamaa na marafiki!”

“Tutajitahidi!”

Alichokifanya mama yake Tom ni kuuza vyombo vyote vya ndani, akaenda Pepsi kazini kwa mume wake na kuomba msaada, Mkurugenzi wa kiwanda hicho akampa shilingi laki moja na nusu na kuja nazo hadi hospitali ya Ocean Road ambako wafanyakazi walimkabidhi shilingi laki moja, jumla akawa na shilingi laki sita pamoja na zilizopatikana kwa kuuza vyombo, mipango ya safari ikaanza kuandaliwa.

Siku mbili tu baadaye bila Tom kuonana na Mariam, moyo wake ukiwa umejaa hasira, walipanda daraja la tatu la treni kuelekea Mwanza ambako wangeunganisha kwa basi hadi Tarime, kwa jinsi hali ya mzee Chacha ilivyokuwa mbaya ilibidi abiria wote waliokuwa naye kwenye kiti, wanyanyuke kumpisha alale, hakuna aliyekuwa na uhakika angefika mzee huyo angefika Mwanza siku tatu baadaye akipumua.

Ulikuwa ni mlio mkubwa mno kwa mtu yeyote aliyekuwa jirani na eneo hilo kutosikia, watu wengi waliokuwa jirani walianza kukimbia kwenda mahali magari yalipogongana, baadhi wakiwa na nia ya kuokoa lakini wengine wakifikiria kuiba mali yoyote ambayo wangeikuta. Magari yaliyokuwa yakipita kwenye Barabara ya Nyerere kwenda au kutoka Uwanja wa Ndege yalishindwa kuendelea na safari sababu barabara ilikuwa imezibwa na magari mawili yaliyogongana uso kwa uso katikati ya barabara, hii iliwafanya abiria wote waliokuwa kwenye magari washuke kwenda kutoa msaada.

Kwenye daladala kulikuwa na abiria wengi walioumia, dereva wake akiwa amelaza kichwa kwenye usukani, damu zikimtoka puani na mdomoni, tayari alishakufa! Taratibu wakamwondoa na kumlaza chini. Sababu tairi za mbele za daladala zilikuwa zimesimama juu ya gari dogo lililogongwa, ilibidi watu wajitolee kulisukuma kurudi nyuma ili kutoa nafasi ya kuangalia kama kulikuwa na watu wengine ndani ya gari dogo. Hayo yalifanyika wakati abiria waliojeruhiwa wakipakiwa ndani ya magari mengine tayari kwa kupelekwa hospitali ikiwa ni pamoja na dereva wa daladala aliyekufa.

“Mungu wangu kuna mtoto mdogo, tena kwenye usukani, sijui ndiye aliyekuwa akiendesha? Mbona mdogo sana?” Mtu mmoja aliuliza baada ya daladala kuondolewa juu ya gari dogo.

“Ni mdogo mno huyu, hawezi kuwa dereva kama ni hivyo basi itakuwa aliiba gari, hawa watoto wa matajiri ndio wanasababisha sana ajali barabarani, si ajabu alikuwa ametoka zake disko akiwa amelewa!” Mwingine aliitikia.

Mariam alikuwa amelala ndani ya gari lililogongwa, akiwa kimya kabisa huku damu nyingi zikimtoka hasa kwenye paji la uso palipoonekana kuvimba, damu nyingine ilikuwa ikimtoka puani na masikioni. Kwa jinsi alivyokuwa amebanwa ilikuwa kazi ngumu kidogo kumtoa, hata hivyo baada ya muda si mrefu walifanikiwa na kumlaza chini kisha kuanza kumgusa kifuani kuona kama alikuwa na uzima.

“Anahema!” Aliongea mwanaume aliyekuwa akimgusa kifuani.

“Basi hajafa, tumkimbizeni hospitali!”

“Ni jambo jema, mleteni huku kwenye gari yangu nimpeleke mara moja Muhimbili!” Mwananchi mmoja alijitolea, Mariam akabebwa juu juu na kwenda kupakiwa kwenye gari dogo aina ya Mark II, safari kwenda hospitali ikaanza ambako walikuta pia majeruhi wengine wamekwishawasili.

Mapokezi hawakuona sababu ya kuuliza maswali mengi kwa jinsi hali ya mgonjwa ilivyokuwa mbaya, haraka akakimbizwa mpaka kwenye chumba cha daktari ambaye baada ya kumwona aliamuru akimbizwe haraka sana Chumba cha Upasuaji, kisha yeye kuwasiliana na madaktari wengine ambao walikutana kwenye chumba hicho na Mariam kuwekewa Mashine ya Hewa ya Oksijeni kisha kupandishwa kitandani ambako kazi ya kwanza iliyofanyika ni kuziba mishipa yote iliyokuwa ikivuja damu kuzuia upotevu mkubwa.

“Haraka sana mfanyieni CT-Scan!” Dk. Majaliwa, Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Uti wa Mgongo, alisema.

“Sawa daktari, acha tuwapigie simu hawa watu waje kuifanya kazi hiyo mara moja!”

“Fanyeni hivyo haraka kwani kwa dalili ninazoziona nahisi kuna tatizo kwenye ubongo wake!”

“Sawa daktari!”

Dakika ishirini baadaye Bingwa wa Kipimo cha CT-Scan alifika kwenye Chumba cha Upasuaji cha Hospitali ya Muhimbili na vifaa vyake na kumfunga Mariam kichwani, kisha yeye na madaktari wote wakaanza kuangalia, haikuhitaji muda mrefu sana kugundua kilichokuwa kikiendelea chini ya fuvu la Mariam; damu nyingi ilikuwa imevuja chini ya fuvu, kichwa chacke kilijipiga kwenye chuma sehemu ya paji la uso na ubongo kuumia kwa ndani.

“She has a subdural haemorrhrage!” (Anavuja damu chini ya fuvu!) Dk. Majaliwa aliongea baada ya kuitazama picha kwenye kompyuta.

“So?” (Kwahiyo?)

“She needs an urgent operation!” (Anahitaji upasuaji wa haraka)

“Are we ready?” (Tuko tayari?)

“Yes!” (Ndiyo)

“Can the people from laboratory do urgent blood grouping and cross matching check? As well as HB level?” (Watu wa maabara wanaweza kupima kundi lake la damu na anaweza kuongezewa na kundi gani? Pia kiasi cha damu alichobakiza?) Dk. Majaliwa alisema na wote wakakubaliana, watu wa maabara wakaitwa haraka na kuifanya kazi hiyo.

Hapakuwa na mtu wa kujiuliza mtu waliyekuwa wakimshughulikia aliitwa nani, mtoto wa nani na alitokea wapi. Kwao alikuwa ni mgonjwa na kazi yao kubwa ilikuwa ni kuokoa maisha yake, hilo ndilo madaktari walilotaka kulifanya. Damu ilipopatikana, vipimo vya moyo wake vikawa viko sawa, Mariam aliingizwa kwenye
 
SEHEMU YA 9 YA 50

chumba kingine kikubwa cha upasuaji ambako kazi ya kupasua kichwa chake, kuufikia ubongo na kuiondoa damu yote iliyoganda chini ya fuvu ilifanyika na kukamilika ndani ya masaa sita, madaktari wakiwa wamesimama wima!

Baada ya hapo Mariam aliondolewa Chumba cha Upasuaji na kupelekwa chumba cha wagonjwa mahututi, hali yake ilikuwa mbaya, hakuna aliyekuwa na matumaini kwamba angeweza kupona kwani mapigo yake ya moyo yalikuwa yakipanda na kushuka. Kwenye chumba hicho alilazwa na kuwekewa mashine ya hewa ya oksijeni, damu ikiendelea kudondoka kuingia kwenye mishipa yake huku vipimo vyote vikifuatiliwa kila baada ya nusu saa kuona namna alivyoendelea, kadri muda ulivyozidi kusonga ndivyo mapigo yalivyozidi kuporomoka.

“I don’t know if she will make it!” (Sijui kama atapona!) Muuguzi mmoja alimwambia mwenzake baada ya kusoma majibu ya mwenendo wa moyo kwenye mashine.

“Hivi ni mtoto wa nani kwanza?”

“Mpaka sasa haijajulikana!”

“Mh! Wazazi wake wakijua watachanganyikiwa!”

****

Saa kumi na mbili kamili alfajiri mama yake Mariam alizinduka usingizini na kuketi kitandani, siku hiyo kilikuwa kimetokea kitu cha ajabu ambacho kwa muda mrefu hakuwahi kukiona kwa mtoto wake. Ilikuwa ni kawaida ya Mariam kuamka asubuhi kabla ya wazazi wake kwenda kuamkia, baada ya hapo alirejea kitandani kulala, siku hiyo ilikuwa tofauti na siku nyingine zote; mpaka muda huo Mariam alikuwa hajagonga mlango kusalimia, mama yake akaingiwa na wasiwasi na kufikiri pengine alikuwa mgonjwa.

Alichokifanya ilipotimu saa moja kamili ni kutoka chumbani kwake na kunyoosha moja kwa moja chumbani kwa Mariam; mlango ulikuwa wazi! Jambo jingine ambalo halikuwa kawaida, hakutaka kusita, akaingia ndani na kusimama katikati ya chumba, Mariam hakuwepo! Moyo wake ukaanza kudunda kwa nguvu, badala ya kutembea akatoka akikimbia hadi nje ambako alianza kuita jina la mtoto wake lakini hakuitikiwa, hali hiyo iliwafanya wapangaji wengine watoke nje kwenda kuuliza ni kitu gani kilikuwa kimetokea.

“Sio kawaida ya Mariam kutokuwepo nyumbani asubuhi, simwoni!”

“Labda amekwenda kufanya mazoezi?”

“Angeaga, mwanangu namfahamu sana tabia zake!”

“Sasa atakuwa wapi? Labda huku nje?” Mmoja wa wapangaji alisema akitembea kwenda nje, nyuma yake akifuata mama yake Mariam na wapangaji wengine watatu.

“Mungu wangu hata gari halipo, huyu mtoto kaenda wapi na gari?”

“Mimi nilisikia usiku lango la kuingilia likifunguliwa na kitu kama gari likisukumwa, sikutia mashaka sana kwani mawazo yangu yalinituma kuamini baba alikuwa amerudi labda alikuwa akitoka kwenda mahali fulani!”

“Basi huyo atakuwa ni Mariam, alikuwa anatoroka usiku, lakini kwenda wapi?” Mama yake Mariam alizidi kuuliza, tayari machozi yalishaanza kumbubujika.

“Watoto wa kike mama, huwezi jua labda yeye na wenzake walikuwa wanatoka!”

“Nitamwambia nini baba yake akirudi?” Mama huyo alisema akizidi kulia.

Baada ya safari ya siku mbili, hatimaye siku ya tatu treni ilipiga honi eneo la Mwanza South, watoto wakatoka ndani ya nyumba kushangilia, hiyo ndiyo hali iliyojitokeza kila treni ilipoingia mjini Mwanza! Hawakujua kilichokuwemo katika moja ya mabehewa ya daraja la tatu yaliyojaza watu, wengi wakichungulia madirishani, huku wakivuja jasho jingi miilini mwao.

Mzee Chacha alikuwa katika hali mbaya mno, tangu waondoke Dar es Salaam alikuwa akihangaika njia nzima na kudai hewa ilikuwa haimtoshi, kazi ya Tom na mama yake ilikuwa ni kumpepea kwenye kiti alicholala! Zaidi ya mara tano alishapoteza fahamu na kuzinduka, kila mtu alimwonea huruma. Hatimaye walikuwa wakiingia Mwanza, mzee Chacha akipumua jambo ambalo hakuna aliyekuwa amelitegemea kwa jinsi hali yake ilivyokuwa mbaya.

“Afadhali!” Mama yake Tom aliongea treni iliposimama.

“Namshukuru Mungu!” Tom alijibu.

Kilichofanyika abiria wote walipoisha ndani ya behewa ni kumshusha Mzee Chacha na kumlaza chini wakifikiria nini cha kufanya. Jesica Makanyaga, msichana waliyesafiri naye akiwapa kila aina ya msaada njiani aliwauliza ni wapi walikotaka kwenda baada ya kutoka stesheni, Tom akamsimulia kila kitu juu ya baba yake kisha kumwomba msaada wa usafiri mpaka stendi ya mabasi.

“Lakini mimi nafikiri msiunganishe na safari kwenda Tarime!”

“Tufanye nini sasa mwanangu?”

“Mgonjwa wenu anaumwa sana, yafaa apelekwe kwanza hospitali!”

“Wazo lako ni zuri lakini sisi ni wageni kabisa hapa Mwanza, hatumfahamu mtu yeyote na hatuna fedha kabisa!”

“Nitawasaidia, kumpakia huyu mzee ndani ya gari kwa kweli ni kumtesa kwanza nashukuru Mungu tumefika Mwanza salama, naomba mnisubiri!” Alisema msichana huyo na kuanza kutembea kwenda nje, aliporejea muda mfupi baadaye aliongozana na kijana mrefu mwenye mzuzu.

“Huyu ni kaka yangu, anaitwa James, yeye ana gari hapo nje tutamchukua mgonjwa kumpeleka Hospitali ya Sekou Toure atibiwe kwanza!”

“ Mungu awabariki sana, sijui jinsi ya kuwashukuru!” Tom aliongea huku akimwangalia Jesica usoni, msaada wa gari aliopewa ukamkumbusha Mariam, chuki zikaongezeka.

“Hakuna shida, twendeni tu!”

Wakasaidiana kumbeba mgonjwa hadi nje ambako mlango wa gari aina ya Landcruiser ulifunguliwa na mzee Chacha akaingizwa ndani akiwa hajitambui, safari kwenda hospitalini ilianza. Dakika ishirini na tano baadaye walishafika na mgonjwa kupokelewa kisha kuonwa na daktari ambaye alipopewa historia yake alishauri aongezewe chupa kadhaa za maji ya glukosi ili mwili wake upate nguvu, baada ya hapo wangeendelea na safari yao. Wakalazwa kwa siku mbili, ndipo hali ya mzee Chacha ikatengemaa kidogo.

Hawakuwa na jambo lolote la kusubiri mjini Mwanza, ikabidi waunganishe safari yao kuelekea Tarime, Jesica na James kama walivyofanya mwanzo, waliwasaidia kutoka wodini mpaka stendi ya basi na kuwapandisha kwenye basi liitwalo Tanganyika Bus service, wakaagana kwa huzuni huku Tom akiwapa shukrani nyingi kwa msaada waliompa na kuahidi kuwakumbuka katika maisha yake yote, saa moja baadaye safari ilianza mzee Chacha akiwa amelala peke yake kwenye kiti cha watu watatu.

Njiani hali yake ilikuwa mbaya, nafuu yote iliyopatikana iliondoka, alilalamika maumivu makali sababu ya kurushwarushwa na basi lililokuwa likiendeshwa kwa kasi kukimbizana na basi jingine kuwahi abiria mbele, hata hivyo walifanikiwa kuingia Tarime saa kumi jioni, mzee Chacha akiwa hoi, hakuwepo ndugu yeyote wa kuwapokea stendi ya basi kwani hakuna taarifa iliyotangulia, lakini wasamaria wema waliomfahamu mzee Chacha walijitolea kutafuta kitanda na kukifanya machela, kisha wakambeba moja kwa moja hadi kijijini.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Tom kufika kijijini kwao, hata mara moja tangu kuzaliwa kwake hakuwahi kukanyaga Kijiji cha Nyamongo ambako wazazi wake walitokea! Kitu cha kwanza kilichomshangaza ni maisha, yalikuwa duni mno, hapo ndipo akafuta kichwani ufahamu aliokuwa nao kwamba maisha yake jijini Dar es Salaam yalikuwa mabaya kuliko binadamu mwingine yeyote.
 
SEHEMU YA 10 YA 50

“Kumbe kuna watu wanaoishi maisha magumu kuliko mimi, kifupi Dar es Salaam kwa watu wa hapa ni kama mbinguni!” Aliwaza.

“Tom mbona umebadilika?”

“Kwanini hamkuwahi kunileta nyumbani mama?”

“Tusa..mehe…ane mwa…nangu! Ni mak..osa ya..ngu,” baba yake aliongea kwa taabu kubwa.

Hakuwepo mtu mwingine nyumbani, bibi na babu wa Tom walishafariki miaka mingi na kuacha nyumba peke yake, hapo ndipo ambako pangekuwa nyumbani kwa mzee Chacha, mke wake na Tom tangu siku hiyo. Hivyo ndivyo ilivyotokea, Tom na mama yake ndio wakawa watafutaji wa mahitaji yote, wazo la shule likafutika kabisa kichwani. Kila siku aliamka asubuhi na kwenda kwenye mgodi wa dhahabu wa Nyamongo, ambako alifanya kazi ya kuosha mchanga wa dhahabu uitwao Marudio kwa kutumia Zebaki, kiasi kidogo cha dhahabu alichopata aliuza na fedha kumpelekea mama yake, ikatumika kununua chakula pamoja na dawa.

Mara chache alifikiria shule na kutamani kuendelea kwani alikuwa na uwezo wa kusoma mpaka Chuo Kikuu lakini fikra za kuwaacha wazazi wake katika hali waliyokuwa nayo zilimfanya aamue kuchagua maisha tofauti na kusoma, siku zikazidi kusonga baba yake akiteseka kitandani bila msaada wowote zaidi ya dawa ya maumivu, hatimaye miezi sita baadaye Tom akiwa amezoea maisha ya mgodini, bila taarifa yoyote ya Mariam, BABA YAKE ALIKATA ROHO USIKU WA MANANE NA KUIACHA DUNIA, Tom hakuamini.

Katika maisha yake yote Tom hakuwahi kufikiria dunia bila baba yake, lilikuwa ni jambo lisilowezekana. Mara nyingi alisikia watu wamefiwa na wazazi wao, au wengine yatima kabisa lakini aliamini hayo yalikuwa matatizo ya watu wengine, yeye akijiweka kando. Lakini usiku huo alimshuhudia baba yake akiwa amelala kwenye jamvi, mwili umebaki mifupa na ngozi, mama yake alikuwa kando akilia kwa uchungu huku akiliita jina la mume wake, picha hiyo ilimuumiza sana Tom ambaye macho yake bado yalikuwa yameangalia kifuani kwa baba yake akiamini lazima kifua kingenyanyuka na kupanda tena, kuashiria kwamba baba yake alikuwa bado akipumua.

“Haiwezekani! Baba hajafa!” Alijikuta akitamka maneno hayo huku akimgusa kifuani na kumwita kwa jina, baba yake hakuitika.

“Ni kweli amekufa! Baba yako hayupo nasi tena tumebaki peke yetu, huu ndio mwisho wake mwanangu ametangulia mbele ya haki!” Mama aliongea akimtengeneza mzee Chacha mdomo na macho.

Mzee Chacha alipokata roho ilikuwa katikati ya usiku, wakiwa wawili peke yao ndani ya nyumba, lakini walipoanza kulia kwa sauti majirani walianza kufika kutaka kufahamu ni kitu gani kilikuwa kimetokea. Walipoambiwa mzee alikuwa amefariki wengi walisikitika lakini wakashauri mambo yote yaachwe mpaka asubuhi ya siku iliyofuata ndipo taarifa zisambazwe kijijini.

Hilo ndilo lililofanyika, Tom na mama yake wakilia kwa uchungu, majirani wakakusanyika kwa wingi na uamuzi wa kuzika ukafikiwa kwenye majira ya saa nne asubuhi, kaburi likachimbwa na saa kumi jioni mzee Chacha akalazwa shimoni na mchanga kufukiwa juu yake, baada ya hapo majirani wengi walisambaa kurejea majumbani mwao wakiwaacha Tom na mama yake peke yao.

“Mama mbona wameondoka wote?”

“Hatuna ng’ombe!”

“Za nini?”

“Tungekuwa na ng’ombe wangebaki, umasikini mbaya mwanangu, ukikua hakikisha unapata fedha na kutajirika, binadamu wana tabia ya kuwaheshimu wenye nacho, mimi na wewe hatuna kitu ndio sababu tumeachwa peke yetu!” Mama yake Tom aliongea akijifuta machozi, maneno hayo yakapenya moja kwa moja kichwani mwa Tom na kuhifadhiwa.

Hakuna mtu aliyekuja kuwaona tena baada ya hapo, walikuwa wao wawili wakifarijiana, kila siku alfajiri ilikuwa ni lazima wanyanyuke kwenda kwenye kaburi la mzee Chacha na kusujudu wakimwomba Mungu amrehemu kule alikokuwa! Siku zikazidi kusonga, hatimaye wakaizoea hali na miili yao kupata nguvu, Tom akatamani kurejea tena machimboni kuendelea na kazi yake ya kuosha mchanga wa Dhahabu, tayari alishazoea kazi hiyo na aliridhika kabisa na kipato kidogo alichopata, hakufikiria shule hata kidogo, wala Mariam, alikuwa kwenye ulimwengu mwingine ambako Mbinu ya kupata mafanikio haikuwa elimu peke yake.

“Mwanangu usiniache peke yangu?”

“Sina jinsi mama, wewe mwenyewe umesema umasikini mbaya, kama nimeshindwa kusoma basi acha nitafute utajiri kwa njia nyingine! Naomba baraka zako”

“Hapana Tom! Huwezi kuondoka, wewe peke yako ndiye niliyebakiza hapa Duniani, wewe ukifa huko machimboni nitafanya nini mimi?”

“Mama, unamwamini Mungu?”

“Ndio!’

“Basi yeye ndiye atakayenilinda na kama kuna maisha mbele basi yatakuwepo na kama kuna kifo basi sitakikwepa!” Tom aliongea maneno mazito akimwangalia mama yake usoni ambaye alionekana kutoamini kama maneno hayo yalitoka mdomoni mwa Tom, kwake alikuwa mtoto mdogo mno kuongea mambo mazito kiasi hicho.

“Hapana, sikubali mwanangu, kaa tu hapa hapa tufe na umasikini wetu!”

Tom hakuwa na la kufanya, asingeweza kumkatalia mtu aliyemleta duniani. Siku zote alifundishwa kuwaheshimu wazazi hivyo akabaki kimya kufuata maelekezo ambayo mama yake alitoa, kamwe asingeweza kuyakiuka, aliamini kufanya hivyo ingekuwa kupoteza baraka za wazazi ambazo zilikuwa muhimu sana katika ya mwanadamu, ingawa aliyafanya yote hayo kwa shingo upande hakutaka kumwonyesha mama yake, siku zote aliendelea kutabasamu akimbembeleza amruhusu kwa hiari yake lakini mama hakukubali.

Siku zikazidi kusonga kazi yao ya kuwapatia riziki ikiwa ni kufanya vibarua kwenye mashamba ya majirani wenye uwezo, malipo yakiwa ni chakula. Tom hakuipenda kazi hiyo, hakumaanishwa kufanya hivyo siku zote za maisha yake, alikuwa na akili nyingi ambazo zingemwezesha kupata fedha badala ya kuendelea kufanya vibarua vya kulima. Mara kadhaa alitamani kutoroka aende machimboni bila ridhaa ya mama yake lakini aliogopa, mwisho akaamua kuwa anajifungia chumbani kila siku jioni na kuanza kulia.

“Mbona unalia Tom?”

“Mama ninao uwezo wa kubadilisha maisha yako, ukaishi kitajiri kuliko mzee Wambura na Magige tunaowalimia kwenye mashamba yao!”

“Sasa hiyo ndiyo sababu unalia mwanangu?”

“Ndio! Naomba uniache niende machimboni, ipo siku utakuja kufurahi kwa sababu uliniruhusu!”

“Utajitunza?”

“Ndio mama!”

“Utaendelea kumcha Mungu?”

“Ndio mama!”

“Hutawaonea watu wengine?”

“Ndio mama!”

“Hutaiba?”

“Ndio mama!”

“Kweli?”

“Kabisa mama yangu, hata mimi nasikitika kukuacha, nakupenda mno lakini sina jinsi inabidi nitakafute maisha!”

“Basi mwanangu, hebu nipe mikono yako yote miwili!” Mama aliongea na Tom akanyoosha mikono yake yote miwili na kuviweka viganja vyake mbele ya mama ambaye alivishika na kuanza kuvitemea mate.

“Mungu akutangulie popote utakapokwenda mwanangu!”

“Amina mama!”

“Kila utakachokigusa kiwe chako!”

“Amina mama!”

“Watu wakusifu na kukuheshimu!”

“Amina mama!”

“Uwe na maisha marefu na Mungu akukinge na maovu!”

“Amina mama!”

“Ahsante mwanangu, sasa unaweza kwenda una baraka zangu zote!”

“Ahsante mama yangu, sitakuangusha!”

“Sawa!”
 
SEHEMU YA 11 YA 50



Walipomaliza maongezi hayo ilikuwa saa saba za usiku wakiwa wameketi kando ya moto ndani ya nyumba yao, Tom akamshuhudia mama yake akiingia chumbani na yeye kutandika jamvi sebuleni, haukupita muda mrefu sana usingizi ukampitia na kuamka saa kumi na nusu za usiku, mara moja akaanza kugonga chumbani kwa mama yake na kumuaga, mama akatoka nje na kumsindikiza mpaka mita kama mia moja hivi kutoka nyumbani, akamshuhudia Tom akipita katikati ya vichaka na kupotea.







Tukio la kupotea kwa Mariam pamoja na gari lilikuwa limemchanganya mama yake kupita kiasi, hakujua nini cha kumwambia mume wake akirejea kutoka safarini Mwanza alikokuwa amekwenda kibiashara kwani alielewa ni kiasi gani alimpenda mtoto wake Mariam, asingekubali jibu jingine lolote zaidi ya mwanae kuwa mzima! Akili yake ilikuwa imesimama kufanya kazi, majirani pamoja na wapangaji walikuwa wamemzunguka wakimtuliza huku wakijadili juu ya nini cha kufanya, hatimaye walifikia uamuzi wa kuondoka nyumbani kwenda kituo cha polisi cha Vingunguti kutoa taarifa juu ya kupotea kwa Mariam pamoja na gari.



“Anajua kuendesha?” Mkuu wa kituo aliwauliza.

“Hapana! Alijaribu kujifunza kidogo lakini hakufuzu, hivyo siwezi kusema anajua kuendesha” mama yake alijibu huku akibubujikwa na machozi,

“Ana mpenzi?”

“Hapana, yupo kijana mmoja wanasoma naye lakini ni rafiki wa kawaida, angekuwa mpenzi wake lazima angeniambia maana mimi na yeye huwa hatufichani kitu, ni marafiki! Jamani mwanangu Mariam uko wapi? Naomba uwe hai…” mama huyo alimalizia kwa kilio huku majirani wakizidi kumtuliza.

“Gari lilikuwa nyumbani jana jioni wakati wa kulala?”

“Ndio”

“Yeye mwenyewe mtoto?”

“Alikuwepo, tuliingia naye ndani kulala na mlango ukafungwa!”

“Huwa ana tabia ya kutoka nje usiku, tuseme kwenda muziki au kitu cha kufanana na hicho?”

“Hapana, ni mtoto wa ndani tu, kitu anachopenda kufanya ni kusoma!”

“Sawa, kaeni hapo kwenye kiti mniache nifanye mawasiliano na Makao Makuu ili niulize kama kuna tukio lolote la wizi au utekaji lililotolewa taarifa, lakini nionavyo mimi huyu binti atakuwa aliiba gari kama wanavyofanya watoto wengine wengi wa matajiri akaenda zake muziki, si ajabu yuko kwa mpenzi wake amepitiwa na usingizi, usiwe na wasiwasi wowote mama atapatikana tu!”

“Hajawahi kufanya jambo la aina hii, kamwe hawezi kuanza leo, mwanangu Mariam hana tabia hiyo, niambieni tu kama amekufa!”



“Hapana mama Mariam, usiseme hivyo, unamwom bea mtoto mabalaa, waache maaskari wafanye kazi yao” Mmoja wa majirani aliongea akimpigapiga mama Mariam mgongoni na kumsaidia kuketi kwenye benchi, wote wakimsikiliza askari akiongea na Makao Makuu kwa simu ya upepo, bahati nzuri sana sauti ya upande wa pili pia ilikuwa ikisikika.



“Kuna ajali ilitokea…ova…jana usiku…maeneo ya Tazara…ova… binti mmoja alikuwa akiendesha gari hilo…akagongana uso kwa uso na daladala lililokuwa likitokea Mbagala…ova…akaumia vibaya sana…gari hilo hivi sasa limeegeshwa kituo cha polisi Buguruni…ova! Sijui kama unayemtafuta ndiye huyo?”

“Namba za gari afande”

“Ni TZ 22210!”

“Uwiiiii!Mwanangu! mwanangu Mariam! Amepata ajali…afande…afande…muulize kama yupo hai au amekufa, gari hilo ni la kwetu!” tayari mama yake Mariam alishanyanyuka kwenye benchi na kusogea kaunta ambako aliongea na askari aliyekuwa akiwasiliana.

“Afande huyo binti alikuwa na hali gani?”

“Kwa taarifa nilizopewa, matumaini ni kidogo na kuna uwezekano atakuwa alikufa pale pale!”

“Mungu wangu! Muulize yuko hospitali gani?”

“Eti afande yupo hospitali gani?”

“Alikimbizwa Muhimbili”

“Ahsante afande, acha niende huko huko Muhimbili” Mama yake Mariam aliongea na kuanza kukimbia kutoka kituoni, hakwenda hatua nyingi sana majirani wakawa wamemkamata na kuanza kutembea naye taratibu hadi nje ya kituo ambako waliingia ndani ya gari na safari kwenda Muhimbili ikaanza mama Mariam akilia na kutamka maneno kwamba hakujua nini cha kumweleza baba wa mtoto akirejea kutoka safari, alijisikia mzembe kupita kiasi, yeye mwenyewe akawa anamatani kufa.



Muhimbili waliegesha gari lao mbele ya Idara ya wagonjwa wa nje na kuanza kukimbia kwenda Idara ya wagonjwa mahututi, hawakuhitaji kuuliza chochote mapokezi, walikuwa na uhakika kwa jinsi hali ilivyokuwa lazima alikuwa amelazwa kwenye wodi hiyo na si mahali pengine popote. Maandishi “USIINGIE NDANI BILA RUHUSA” yaliwafanya wote wabaki wamesimama nje ya wodi hiyo bila kujua la kufanya ingawa walikuwa na uhakika kabisa Mariam alikuwemo ndani, dakika kumi na tano baadaye walishuhudia mwanaume mfupi mwenye mvi akitembea haraka sana kuelekea kwenye wodi hiyo, nyuma yake akiwepo mwanamke mwingine, wote walionekana kuwa na wasiwasi.

“Habari za leo kaka?” Mama yake Mariam aliuliza.

“Nzuri tu habari zako?”

“Sio nzuri”

“Kuna nini?”

“Namtafuta binti yangu, alipatwa na ajali alfajiri ya leo na kukimbizwa hapa Muhimbili!”

“Anaitwa nani?”

“Mariam!”

“Kuna binti mmoja yuko ndani lakini sifahamu jina lake maana hana uwezo wa kuongea, aliletwa alfajiri baada ya gari lake kugongana na gari jingine, sasa sina uhakika kama ndio huyo! Nimepigiwa simu sasa hivi kwamba hali yake ni mbaya sana, imebadilika ghafla” mzee huyo aliyetambulika kama daktari bila kujieleza sababu ya kifaa cha kupimia mapafu na moyo alichokuwa amekivaa shingoni alimjibu mama yake Mariam huku uso wake ukionyesha wasiwasi.

“Ni huyo hu…!” mama yake Mariam aliongea lakini kabla hajaendelea sana mlango ulifunguliwa, muuguzi aliyevaa nguo nyeupe akachungulia nje macho yake yakionyesha wasiwasi mwingi.

“Dk.Mbise!” Akaita.

“Yes Aminata!”

“Mgonjwa amekufa!” ilikuwa ni sauti ya muuguzi akimwita daktari aingie ndani haraka.





Dk.Mbise hakuongea chochote zaidi ya kuanza kukimbia kuingia ndani ya wodi akimwacha mama yake Mariam taaban, mwili wake ukaishiwa nguvu, giza likayafunika macho yake na taratibu akaporomoka sakafuni! Majirani na wapangaji wake alioongozana nao kwenda polisi na baadaye hospitali ndio waliombeba tena kumkimbiza idara ya wagonjwa wa nje kwenda kumwona daktari ambaye baada ya kumpima kifuani na mashine ya kusikilizia mapigo ya Moyo, alionyesha wasiwasi.

“Mh!”

“Mbona unaguna daktari?”

“Huyu mgonjwa huwa anashinikizo la damu?”

“Hajawahi kusema, labda mume wake angekuwepo swali hilo lingepata jibu, kwani vipi daktari? Moyo haupigi?”



Daktari hakuongea chochote, alibaki kimya akimwangalia mgonjwa machoni kwa wasiwasi mwingi, alionekana mwenye siri moyoni ambaye hakutaka kuwashirikisha watu waliokuwemo ndani ya chumba, mwisho akawaamuru wote watoke nje yeye abaki na wauguzi peke yao.





Wakiendelea na maongezi, mlango wa chumba cha wagonjwa mahututi ulifunguliwa, muuguzi akatokeza nje akionyesha wasiwasi mwingi na kumuomba daktari aingie haraka chumbani kwani mgonjwa tayari alikuwa amekufa! Daktari huyo aliyejulikana kwa jina la Dk. Mbisse aliingia ndani haraka akimuacha mama yake Mariam, muda mfupi baadaye mama huyo alianguka chini na kupoteza fahamu,
 
SEHEMU YA 12 YA 50

ikabidi watu waliokuja naye wambebe juu juu mpaka idara ya wagonjwa wa nje ambako daktari alipomuona tu alionyesha wasiwasi na kuanza kuuliza maswali huku akimuangalia mgonjwa usoni.





“Mh!” Daktari aliguna tena na kuzidi kuwatia wasiwasi watu waliompeleka mama yake Mariam kwenye chumba chake, hisia kwamba alikuwa amepoteza uhai zilianza kuwaingia vichwani mwao, wakiwa nje waliendelea kusikiliza kupitia dirishani kila kitu kilichoendelea.

“Shinikizo lake liko juu sana, sijawahi kuona presha ya aina hii, ni lazima aanzishiwe dawa sasa hivi vinginevyo atapasuka mshipa kichwani, inavyoonekana ni mgonjwa wa presha wa muda mrefu ila alikuwa hajitambui!” Sauti ya daktari iliwafikiwa majirani waliokuwa wameketi nje kwenye benchi wakisubili kupewa maelezo.

“Dawa gani tunamuanzishia daktari?”

“Mpeni Rosartan na Aprinox haraka iwezekanavyo, halafu muendelee kumpima shinikizo lake kila baada ya nusu saa na nipewe taarifa, kama kuna tatizo lolote niiteni haraka iwezekanvyo, mmenisikia?” Daktari aliuliza.

“Ndio daktari!”

“Haya mpelekeni chumba cha wagonjwa mahututi haraka iwezekanavyo!”

“Sawa daktari!”

Mama yake Mariam akashushwa kitandani na kulazwa juu ya machela kisha kusukumwa kuelekea chumba cha wagonjwa mahututi, majirani na marafiki wakifuata nyuma kutaka kufamu kilichotokea. Walifurahi baada ya wauguzi kuwaeleza kwamba mama yake Mariam alikuwa hajafa, bali shinikizo lake la damu lilikuwa limepanda mno, hivyo lilihitaji kushushwa ili aweze kurejewa na fahamu zake.

Chumba cha wagonjwa mahututi mama yake Mariam alilazwa kwenye moja ya vitanda vilivyokuwemo, akawekewa mashine ya hewa ya Oksijeni iliyofunika pua na mdomo wake kisha dawa zilizoandikwa na daktari zikaanza kutolewa kwenye njia ya mshipa na vidonge. Kitanda kilichokuwa jirani na mahali alipolazwa mama huyo, palikuwa na pazia la rangi ya kijani lililozungushwa kwenye kitanda huku madaktari na wauguzi wakionekana kuhangaika, baadaye Dk. Mbisse alitokeza nje na kumuona mama yake Mariam.

“Mh! Huyu mama si nilikuwa naongea naye hapo nje?”

“Ndio!”

”Imekuwaje tena?”

“Baada ya kuongea naye tu alianguka chini na kupoteza fahamu!”

“Farida makosa yak ohayo!”

“Kwanini daktari?”

“Ulitoa ujumbe vibaya, nadhani alifikiri mtoto wake amekufa, siku nyingine ukiwa unatoa taarifa za aina hiyo lazima uangalie kwanza mazingira, mgonjwa alikuwa amepoteza fahamu tu wewe ukafikiria amekufa halafu ukaniita kwa kusema “Daktari mgonjwa amekufa!” Hiyo ni kinyume cha taaluma, siku nyingine usifanyi hivyo, sawa?” Dk Mbisse aliongea kwa sauti ya chini.

“Sawa daktari nimesikia, sitarudia tena!”

“Hebu nimuangalie kidogo!” Dk Mbisse aliongea akikisogelea kitanda cha mama yake Mariam, alipokifikia alianza kumpima shinikizo la damu, hata yeye alipomaliza pia aliguna na kumpigia simu daktari aliyemuona kwa mara ya kwanza, wakajadiliana na kukubaliana kuongeza dozi ya dawa kwani shinikizo lilikuwa juu mno.

*********

Mama yake Mariam alirejewa na fahamu masaa sabini na mbili baadaye, ikiwa katikati ya usiku, akaangaza macho yake huku na kule chumbani akijaribu kutaka kuelewa ni wapi alipokuwa. Fahamu hazikumwijia upesi mpaka alipouona mrija wa dripu ukiteremka na kuingia kwenye mshipa wa mkono wake, hapo ndipo akaelewa kwamba alikuwa hospitali. Kikohozi kikamkaba na kujikuta akikohoa, hicho ndicho kilimfanya mtu aliyekuwa kando yake azinduke usingizini, macho yao yakagongana na mtu huyo akatoa tabasamu.

“Pole sana mke wangu, ndio Dunia ilivyo!”

“Baba Mariam!”

“Naam mke wangu!”

“Nisamehe kwa yote yaliyotokea, sikumruhusu Mariam atoke, aliiba gari nikiwa usingizini!”

“Usijali hayo mke wangu yamekwishatokea!”

“Yuko wapi Mariam?”





*********

Machimboni Tom aliendelea na maisha yake, kazi yake kubwa ikiwa ni kuosha mabaki ya mchanga wa dhahabu ulioachwa na matajiri akitumia madini ya Zebaki, kiasi kidogo cha fedha kilichopatikana alikitumia kwa chakula na kumtumia mama yake matumizi! Hakuwa na mahali pa kulala, siku zote usiku ulipoingia alilala kando ya mto karibu kabisa na mahali alipofanyia kazi zake. Haikuwa rahisi kwa mtu yoyote kuelewa alikuwa kijana mwenye uwezo mkubwa darasani, aliamua kukatisha masomo sababu ya umasikini, jambo hilo wala hakutaka kuliongelea akiwa na marafiki zake.

Alikuwa mkimya kupita kiasi, asiye na maneno mengi wala ugomvi na vijana wenzake jambo ambalo kwa machimboni lilikuwa ni kawaida, karibu kila kijana alitembea na kisu na wengi walikuwa wamejaa majeraha miilini mwao sababu ya kuchomana visu! Hapakuwa na kituo cha polisi wala mahali pa kutoa malalamiko mtu alipoonewa, wanawake walifanyiwa unyanyasaji wa kutisha wakibakwa mbele za watu lakini hakuna aliyechukua hatua, hayo ndiyo yalikuwa maisha ya machimboni ambayo Tom alilazimika kuishi ndani yake sababu alikuwa akitafuta mafanikio baada ya njia ya kupitia shule kushindikana.

“Naweza, naweza kufanikiwa pia kwa njia hii, kuna watu wengi tu Duniani walioacha shule na wakafanikiwa, ni kweli shule ni muhimu lakini inaposhindikana si mwisho wa kila jambo, bado upo uwezekano wa kufanikiwa kama binadamu akitumia akili yake!” Hayo ndiyo yalikuwa mawazo yake kila siku asubuhi kabla ya kwenda kazini, hakuwa amekata tamaa na aliamini siku moja angepata mafanikio makubwa sana na kurejea tena Dar es Salaam ambako angemtafuta tena Mariam mpaka ampate na kumuonyesha kwamba kitendo cha kumkimbia akiwa na shida hakikuwa cha kiungwana hata kidogo.

“Ipo tu siku changudoa yule atanitambua! Nitamuonyesha mie ni nani, yeye si anajidai na utajiri wa baba yake, mimi nitakuwa nazo zangu mwenyewe, hivi sasa naamini Duniani hakuna mapenzi ya kweli, watu wanadanganyana tu, kwa jinsi Mariam alivyokuwa akiniambia maneno mazuri vile, kumbe yote yalikuwa kamba? Siamini, sitampenda mwanamke tena, naapa!” Tom alisema moyoni mwake akiosha mchanga kando ya mto, bado chuki dhidi ya Mariam iliula moyo wake, alimchukia msichana huyo kuliko kitu kingine chochote chini ya jua la Mungu.





Tom alifanya kazi kwa nguvu akiwa na usongo wa kupata utajiri ili siku moja arejee Dar es Salaam na kumwonyesha Mariam kwamba maisha na mafanikio yalikuwa ni kwa kila mtu, si kwa watoto wa matajiri peke yao. Ndio maana alikuwa na nidhamu katika kila fedha aliyoipata, hakujishirikisha katika mambo mabaya kama ulevi na uvutaji wa bangi, ambayo yalifanywa karibu na vijana wote wa machimboni.
 
SEHEMU YA 13 YA 50



“Yeke mura! Mang’ana?” (Vipi mshkaji mambo?) Tom alimsalimia Mwita kulipokucha asubuhi wakijaanda kuondoka kwenye kibanda chao kidogo kwenye mto kuendelea na kazi yao ya kuosha Marudio.

“Maia!” (Safi tu)



Ilikuwa ni saa kumi na mbili asubuhi, wote watatu wakaamshana na kuanza kuondoka kuelekea mtoni, kila mmoja wao akiwa na uchungu moyoni mwake, wote walikuwa ni watoto wa masikini waliotamani sana kufanikiwa katika maisha yao, wakiwa njiani Tom aliwaeleza mambo mbalimbali aliyoyasoma kwenye vitabu vya watu waliofanikiwa kama Donald Trump, Robert Kiyosaki na Bill Gates, alieleza kwa lugha rahisi ili wapate kumwelewa na pia wasigundue kwamba alikuwa na elimu kuwazidi, jambo ambalo hakutaka kabisa ligundulike, siku zote alitaka kufanana na watu waliomzunguka ili iwe rahisi kufanya nao kazi.

“Ili ufanikiwe ni lazima uwe na ndoto, ninaposema ndoto simaanishi kulala na kuota, uwe unatamani kuwa kama mtu fulani na ufanye kazi kwa nguvu kufikia kiwango hicho cha maisha, uwe tayari kupitia kwenye dhiki zote alizozipitia mtu huyo, tatizo letu tunatamani kuwa kama Yesu Kristo lakini hatupo tayari kusulubishwa msalabani, tunataka kwenda Mbinguni lakini hatuko tayari kufa… wewe Mwita unataka uwe kama nani maishani mwako?”

“Gachuma!” Mwita alitamka kwa ujasiri, Gachuma alikuwa mfanyabiashara maarufu sana miongoni mwa kabila la Wakurya, wengi walimchukulia kama mfano wa kuigwa.

“Uko tayari kupitia matatizo yote aliyoyapitia Gachuma?”

“Sana tu”

“Wewe Gimonge unataka kuwa kama nani?”

“Kuna rijamaa rimoja ra Mwanza rinaitwa Rikishimba” Gimonge alisema kwa Kiswahili chenye lafudhi ya Kikurya akimtaja mfanyabiashara mmoja wa Mwanza



Wote walikuwa na ndoto za kufikia hatua fulani maishani mwake, kila siku asubuhi mpaka jioni waliongea mafanikio, magari mazuri, wanawake wazuri, nyumba nzuri, nguo nzuri pamoja na heshima ambayo wangepewa kama wangefanya vizuri maishani mwao. Walijiona wadogo ambao kesho yake wangekuwa wakubwa, hawakufanya mchezo hasa Tom ambaye kila alipomfikiria mama yake nyumbani machozi yalimtoka, alitamani sana kubadilisha maisha ya mama yake ili naye apate kuheshimiwa na majirani waliombeza na kumdharau kwamba yeye na mume wake walikimbilia mjini ambako maisha yaliwashinda.



Kidogo alichopata Tom alikitumia na mama yake, sehemu nyingine akatunza kama akiba akiwa na lengo la kufungua biashara ndogo machimboni lakini hakufanikiwa, kwani fedha ilipoongezeka na kufikia mtaji wa kufungua duka, alipata taarifa kwamba mama yake ni mgonjwa, akaondoka machimboni kwenda kumwona. Hali aliyomkuta nayo ilikuwa ya kusikitisha, alikuwa amepungua kupita kiasi na miguu imevimba, uso wake ukiwa mweupe na mashavu yametuna na macho yakiwa na rangi ya njano.

“Pole mama”

“Ahsante mwanangu, hali yangu si nzuri, ni bora umekuja ili unipeleke hospitali”

“Hakuna shida mama, nina fedha kidogo hapa ambayo nimepata, bila shaka itakusaidia!”

“Ahsante sana mwanangu”



Walikubali na siku iliyofuata Tom alikodisha baiskeli na kumbeba mama yake mpaka Tarime Mjini ambako alimpeleka hospitali ya Wilaya, uchunguzi ukafanyika na kugundua kwamba mama huyo alikuwa na tatizo kwenye Wengu lake, lilikuwa limepanuka na kuongezeka ukubwa, jambo lililofanya liwe na uwezo usio wa kawaida wa kuvunjavunja chembechembe za damu.

“Kwa kitaalam hali hii inaitwa Splenomegally!” daktari alimwambia Tom mbele ya mama yake.

“Atapona?”

“Atapona lakini itachukua muda mrefu, kwa hivi sasa itabidi alazwe wodini kuongezewa damu na pia tufanye uchunguzi zaidi kutafuta sababu ni kwanini Wengu limevimba!” Dk. Richard Mitiro alimwambia Tom ambaye uso wake ulionyesha kukata tamaa.

“Itagharimu shilingi ngapi matibabu yake?”

“Si fedha nyingi, lakini atahitahi mtu wa kumwongezea damu”

“Nina shilingi elfu hamsini tu, ila damu ninayo nyingi”

“Zinatosha, ngoja niandike kwenye fomu uende maabara kupima damu tuone kama inafaa kumwongezea mama yako”

“Sawa daktari”



Mama alichukuliwa na kwenda kulazwa wodini, Tom akapelekwa maabara ambako damu yake ilichukuliwa na kuchunguzwa ikilinganishwa na ya mama yake ambayo pia ilichukuliwa baadaye na kuonyesha alikuwa na uwezo wa kumtolea chupa tatu, mchana wa siku hiyo hiyo akatoa damu na mama yake akaanza kuongezewa mpaka siku iliyofuata jioni ndio zoezi hilo likakamilika. Tom alishindwa kuondoka, ikabidi abaki na mama yake hospitali kwa muda wa wiki nzima majibu yalipotoka na kuonyesha kuvimba kwake kwa Wengu kulisababishwa na tatizo kubwa kwenye damu yake.

“Itabidi umpeleke Mwanza!”

“Mwanza? Daktari, Mwanza?” aliuliza kwa mshangao mkubwa.

“Ndio kijana”

“Hauwezi kunisaidia tu hapa hapa? Sina uwezo wa kumpeleka mama Mwanza kwa matibabu”

“Kauze hata ng’ombe!”

“Hatuna ng’ombe hata mmoja daktari”

“Inabidi ujitahidi, hali ya mama si nzuri, anahitaji uchunguzi wa kina zaidi ya uwezo tulionao hapa Tarime, hospitali ya Bugando itafaa zaidi maana wao wana vifaa vikubwa kuliko tulivyonavyo sisi”

“Ninaelewa daktari, tatizo fedha”

“Kawaone ndugu nyumbani”

“Sina ndugu”

“Sijawahi kuona Mkurya asiye na ndugu”

“Wazazi wangu walitengwa”

“Na nani?”

“Na ndugu zao”

“Sababu?”

“Walikimbilia mjini wakaacha kuwasiliana nao, baba alipougua na kufariki ndio tukarudi huku na mimi ndiye mtoto pekee kwa wazazi wangu”

“Nakushauri ukafanye mpango,” daktari alizidi kusisitiza.



Alichokifanya Tom ni kuondoka ofisini kwa daktari na kwenda moja kwa moja kitandani kwa mama yake, hakutaka kulia wala kuonyesha udhaifu lakini mama yake aligundua na kumuuliza ni kwa sababu gani alikuwa kwenye hali hiyo ya masikitiko, akashindwa kumficha na kulazimika kuuweka ukweli wote wazi kwamba walitakiwa kwenda Mwanza kwa uchunguzi zaidi! Mama yake alibubujikwa na machozi ya uchungu, hakuwa ametarajia kabisa taarifa kama hizo kwani alifahamu hawakuwa na uwezo wa kufanya jambo hilo.

“Tutatoa wapi fedha?”

“Sijui mama, lakini nashauri tuondoke kwenda nyumbani, nikakuache ili mimi nikimbie machimboni Nyamongo kujaribu kuhangaika, labda naweza kufanikisha kwa msaada wa Mungu” aliongea Tom, safari hii alishindwa kuyazuia machozi, mashavu yake yakalowa na mama yake kuanza kuyafuta.

“Usijali mwanangu, Mungu yupo!”

“Sitaki ufe mama, sitaki kubaki peke yangu”

“Mungu atasaidia”





Jioni ya siku hiyo hiyo kwa baiskeli ya kukodi Tom alimbeba mama yake na kumrejesha nyumbani ingawa hali yake ilikuwa bado dhaifu, huko hawakulala usiku mzima wakiwa wameangaliana, Tom akiwa na wasiwasi sana na maisha ya mama yake! Hakutaka afe na aliamini ilikuwepo njia ya kulifanya jambo hilo. Kulipokucha, ingawa kwa shingo upande, Tom aliaga na kumwacha mama yake akiwa amelala hoi kitandani, hakuwa na uhakika kama wakati wa kurudi angemkuta akiwa hai lakini ilibidi afanye hivyo kwani kuendelea kumwangalia peke yake kitandani isingesaidia.
 
SEHEMU YA 14 YA 50

“Mama acha tu niende, utajitahidi kidogo kidogo kuwa unanyanyuka na kupika, lazima nikatafute fedha, nitakuwa nakuja mara kwa mara kukuona, nikipata kiasi cha kutosha tu nitakuja nikupeleke hospitali!” Tom alisema maneno hayo akibubujikwa na machozi, kwake kilichokuwa kikitokea kilikuwa ni sawa na kumuaga mama yake kwa mara ya mwisho, ndani ya moyo wake alifahamu siku atakaporejea angekuta maiti imelala kitandani ikiwa imeharibika! Mawazo hayo yalimfanya afumbe macho kwa kuogopa.

“Nenda tu mwanangu, lililopangwa na Mungu hatuwezi kulibadilisha”

“Ahsante mama, buriani”

“Buriani mwanangu”

Tom akatoka na kufunga mlango nyuma yake kisha kuanza kutembea kwa unyonge akipita porini mpaka akafika machimboni Nyamongo, hakuwakuta Mwita na Gimonge kambini kwao, akaelewa tayari walikuwa kazini mtoni wakiosha marudio! Akazidi kutembea mikono akiwa ameshika nyuma, machozi yakimbubujika mpaka mtoni ambako hakuwakuta Mwita na Gimonge jambo ambalo halikuwa la kawaida na kulikuwa na watu wachache sana mtoni siku hiyo, akazidi kushangaa. Muda mfupi baadaye akapita mtu mmoja na kulazimika kumsimamisha.

“Wako kwenye shimo namba tatu!”

“Kuna nini?”

“Limetema vibaya mno, watu wote hivi sasa wana fedha!”

“Mungu wangu!” Tom alitamka neno hilo na kuanza kukimbia kuelekea kwenye shimo aliloambiwa, hakuna kitu alichohitaji katika maisha yake wakati huo kama kupata fedha ili aweze kumpeleka mama yake hospitali, alijisikia mwenye bahati mbaya kutokuwepo wakati shimo hilo likitema dhahabu.



Alikuta kundi kubwa la watu likiwa zimezunguka shimo hilo, hali ilikuwa tofauti kabisa na alivyotarajia kwani mahali ambako watu wengi walikuwa wamepata fedha alitegemea kuwa na vicheko na furaha lakini wengi wa watu walikuwa wakitokwa na machozi! Moyo wake ukashtuka, hata hivyo akapenya katikati ya watu kwenda mbele ambako alikuta miili kumi ikiwa imelazwa chini, muda huo huo akaguswa begani, alipogeuza kichwa chake alikutana na Mwita, mashavu yake yakiwa yamelowa na machozi.

“Vipi tena?”

“Mwenzetu kafa!”

“Nani?”

“Gimonge”

“Kimetokea nini?”

“Shimo limetitia na kuwabana watu ndani yake, bahati mbaya yeye na vijana wengine ndio walikuwemo!”

“Ha! Dhahabu zimo?”

“Nyingi mno lakini watu wameogopa kuingia kwa sababu linaendelea kutitia taratibu!”

“Wee! Kwa hiyo hata nikiingia sasa hivi dhahabu zimo?”

“Ndio”

“Hebu nipe hiyo RPG yako pamoja na tochi!” Tom alimwomba Mwita vifaa vya kuchimbia, kichwani mwake taswira ya mama yake mzazi akiwa kitandani akiteseka kwa maumivu huku akisubiri kifo kwa sababu hapakuwa na fedha ilimwijia.

“Za nini?”

“Wewe nipe tu”

Mwita bila kujiuliza mara mbili alimkabidhi Tom vifaa vyake, katikati hali ambayo hakuitarajia alishangaa kumwona rafiki yake akikimbia mbio katikati ya watu na kwenda moja kwa moja kuzama ndani ya shimo lililokuwa likititia, watu wakashika mikono kichwani mwao katika hali ya mshangao, mtu mwenye akili timamu asingeweza kufanya jambo la aina hiyo wakati maiti kumi zilikuwa zimelala chini. Muda huo huo shimo likaanza kutitia, watu wote wakakimbia kwenda pembeni kuepusha maisha yao.







Kwa masaa kadhaa shimo liliendelea kutitia hali iliyowatia hofu sana wachimbaji waliokuwa jirani na mashimo hayo, hawakuhitaji akili nyingi sana kufahamu kwamba Tom alikuwa ameshafariki na hataonekana tena!

Watu walihuzunika sana, walishindwa kuelewa ni kwanini Tom alikuwa kujitoa kafara kiasi kile, kila alikuwa akizungumza lake. Walishindwa kuelewa ni akili ya aina gani aliyoitumia kuingia shimoni wakati alikuwa akiona maiti zimelala juu ya mashimo hayo baada ya kutitia.

“Lakini kwanini hamkumzuia?” Mmmoja wa vijana waliokuwa wakijadiliana alisema.

“Huu ni uzembe wa hali ya juu,” mwingine akadakia.

“Au mlimdanganya?”

“Hapana, aliingia mwenyewe!”

“Kwanini mlimuachia?”

“Hakuna aliyekuwa akijua nia yake, aliomba tochi na RPG kisha ghafla tukashangaa anakimbilia shimoni, akaingia!”

“Mh! Lakini huyu jamaa mjinga sana!”

“Sana, ni kama alikuwa akitaka kufa!”

Mazungumzo yale yaliwaumiza sana mwita na Gimonge, hawakuona kama walikuwa na sababu ya kuendelea kuyasikiliza. Walichokifanya ni kuchepuka pembeni kama wanajadilina jambo fulani kisha baadaye wakaondoka na kwenda nyumbani.

“Vipi kaka, unadhani jamaa atapona kweli?” Mwita alikuwa wa kwanza kumuuliza rafiki yake Gimonge.

“Sidhani, kwa hali ilivyo?”

“Eh...!”

“Siyo rahisi kutoka akiwa hai!”

“Sasa?”

“Nafikiri cha kufanya hapo ni kwenda kujaribu kama tutaweza kumtoa, lakini ikishindikana hadi kesho, ni wazi kwamba atakuwa amekufa!”

“Akifa itakuwaje ndugu yangu?”

“Hakuna kitu kingine zaidi ya kwenda kumweleza mama yake hali halisi!”

“Sawa!”

“Turudi machimboni!”

“Twende!”

Waliporudi machimboni hali ilizidi kuwa mbaya kwani shimo lilizidi kutitia, hapakuwa na matumani ya Tom kutoka akiwa mzima. Kila mtu aliamini Tom alikuwa amekufa.

******

Asubuhi ya siku iliyofuata Gimonge na Tom walikuwa safarini kwenda kwa mama yake na Tom kumpa taarifa za msiba wa mwanaye. Kila mmoja alikuwa hafahamu jinsi gani mama yake Tom angezipokea taarifa hizo kwa majonzi.

Hadi kufikia saa nane walikuwa wameshafika nyumbani kwa mama yake na Tom ambaye walimkuta akiwa hoi kitandani.

“Shikamoo mama!”

“Marhaba wanangu, hamjambo?”

“Hatujambo, pole sana kwa kuumwa!” Mwita akamwambia.

“Ahsante, hata hivyo nimeshazoea, hapa nasubiri siku yangu ya kufa tu, najua sitapona!”

“Usiseme hivyo mama, Mungu yupo na wewe, amini kwamba kwake kila kitu kinawezekana!”

“Vipi mbona mpo hivyo?” Mama Tom aliwauliza baada ya kuona wana majonzi ingawa walikuwa wakijaribu kuyaficha.

“Hakuna kitu!”

“Semeni tu wanangu, hamuweza kunificha!” Mama Toma akasema kwa uchungu, tayari alishahisi kwamba kulikuwa na tatizo!

“Mwambie...” Mwita akamwambia Gimonge.

“Mwambie wewe!”

“Hapana mwambie wewe!” Waliendelea kubishana kwa muda mrefu sana, kiasi mama Tom akazidisha wasiwasi.

“Ni nini lakini wanangu, ni vyema mkaniambia kuliko kubishana, maana hata kama mtachelewa kuniambia lakini lazima mwishoni mtaniambia tu!”

“Mama...Tom amefariki!”

“Unasema?”

“Tom amefariki mama, hatuna haja ya kukuficha!”

“Ilikuwaje?”

“Alisikia shimo linatoa madini, yeye akaingia ingawa lilikuwa linatitia, tangu jana hajatoka na tumeshatoa maiti nyingi lakini yake hatujaiona!”

“Tom mwanangu unaondoka na kuniacha mama yako nakufa! Unakufa kabla hujaiona maiti yangu....Eeeh Mungu naomba umpokee mwanangu, najua na mimi nitamfuata muda siyo mrefu!” Mama Tom alilia sana lakini baadaye akawaomba wale vijana aongozane nao Nyamongo.

“Kufanya nini tena?” Mwita akamwuliza.

“Nataka kuona mahali mwanangu alipolala!”

“Lakini unaumwa mama!”

“Najua lakini nitajikaza, lazima nione mahali mwanangu alipolala kabla na mimi sijafa!”

“Mama kwa hali yako hutaweza kutembea!”

“Mtatumia machela kunibeba!” Hawakuwa na sababu ya kubishana naye tena, wakakubaliana naye.

Machela ikatengezezwa jioni ile ile na siku iliyofuata walimbeba na kuanza safari ya kwenda Nyamongo. Walifika jioni majira ya saa 10:15.

“Nipekeni machimboni!”

“Kwanini tusiende asubuhi?”
 
SEHEMU YA 15 YA 50

“Siwezi kulala kabla ya kuona mahali alipolala mwanangu, lazima nione leo hii hii!” Hakuna aliyepingana naye, walijua ni kiasi gani alikuwa na uchungu.

Wakambeba na kuongoza moja kwa moja machimboni. Walipofika, mama Tom aliangalia shimo alilofia mwanaye huku machozi yakimtoka. Alionekana akiwa kimya kwa sekunde chache kisha akafuta machozi yake na kugeuza shingo na kuwatizama watu waliokuwa wamezunguka eneo lile.

“MWANANGU HAJAFA! TOM YUPO HAI?” Mama Tom akasema kwa sauti kubwa.

“Mama hivi unaona hapo kuna mtu atakayeweza kutoka akiwa hai?”

“Nasema Tom hajafa!” Yalikuwa maneno ambayo yaliyowachanganya wengi, hakuna aliyeweza kujua sababu za mama huyo kukazania kwamba mwanaye hakufa.

Kitu akabaki ameduwaa.

****

Pamoja na kukandamizwa na mchanga akiwa ardhini, Tom alikuwa akijitahidi kuchimba kidogo kidogo kwenye mwamba ili aweze kutoka. Pamoja na mateso yote aliyokuwa akiyapata ya kukosa pumzi, hata mara moja hakuachia mfuko wake wa salufeti uliokuwa na dhahabu.

Alijitahidi sana kujiokoa lakini pumzi ilikuwa ikimuishia, akilini mwake alikuwa akihuzunika sana kufa na kumuacha mama yake akiwa katika hali ngumu.

“Najua mama yangu utateseka sana, lakini hakuna jinsi naamini ni mipango ya Mungu, siwezi kuzuia kifo changu ikiwa Mungu mwenyewe wa mbinguni atakuwa amenipangia, sina ujanja tena, naelekea kifo changu sasa!” Tom akajisemea moyoni mwake.

Hakuwa na kitu cha kubadilisha ukweli kwamba alikuwa anakufa! Kitu pekee kilichokuja akini mwake ilikuwa ni kutafuta toba kwa Mungu wake. Kwanza aliamua kumsamehe Mariamu, hakutaka kufa akiwa na kinyongo na watu. Baada ya hapo akakumbuka sala ya Baba Yetu, akaanza kusali ili akifa aende Mbinguni.

‘Baba yetu uliye Mbinguni,

Jina lako litukuzwe,

Ufalme wako uje,

Mapenzi yako yatimizwe hapa duniani,

Kama yatimizwavyo huko mbinguni,

Utupe leo riziki zetu,

Utusamehe makosa yetu,

Kama tunavyowasamehe waliotukosea,

Usitutie majaribuni,

Bali utuokoe na yule muovu,

Kwakuwa ufalme ni wako,

Na nguvu,

Na utukufu,

Hata milele,

Amen.’

Alipomaliza sala hiyo akavuta pumzi ndefu sana kisha akazishusha taratibu akihisi kifua kumbana. Akayafumbua macho yake kisha akaufungua ule mfuko wa salufeti, akasikia mapigo ya mopyo wake yakipiga paaa!

“HAPANA, LAZIMA JAMBO FULANI LIFANYIKE NIWEZE KUTOKA HUMU SHIMONI! NIKITOKA LAZIMA NITAKUWA TAJIRI MKUBWA NA HATA MAMA YANGU ATAPONA! MUNGU ALIYENIUMBA AMBAYE NILIKUWA NAMUOMBA MUDA MFUPI ULIOPITA NDIYE ATAKAYENITOA HUMU SHIMONI NIKIWA HAI!” Tom akawaza akilia kwa uchungu.







Maneno ya mama yake Tom yaliwashangaza sana watu wengi waliokuwa machimboni, wengi walimpuuza! Isingewezekana mtu kuwa shimoni kwa siku tatu halafu akawa mzima. Maneno ya mama Tom yalikuwa sawa na usiku wa giza.

“Mh!” Mmoja aliguna.

“Vipi?”

“Huyu mama anazeeka vibaya!”

“Kweli!”

“Lakini damu nzito kuliko maji ndugu zangu, huwezi kujua kwanini huyu mama anaamini mwanaye hajafa, maana kama angekuwa amekufa, angeona ishara yoyote moyoni mwake,” kijana mmoja alisema kwa sauti kubwa, mama Tom akamsikia.

“Nisikilizeni jamani, Tom hajafa! Nina uhakika huo, moyo wangu hauniambii kabisa kwamba mwanangu amekufa!” Mama Tom akasema huku machozi yakimtoka kwa uchungu.

“Jamani sasa tufanyeje?” Mmoja wa vijana waliokuwa pale machimboni alisema.

“Nafikiri ni vyema kama tukiendelea kuchimba, huenda tukampata!”

“Sawa!” Vijana wakaitikia na kazi ya kuanza kuchimba ikaanza.

Gimonge na Mwita walikuwa wakiongoza wenzao kuchimba pembeni ya shimo ambalo Tom alikuwepo! Walichimba kwa muda mrefu sana bila mafanikio. Kila walipotaka kuacha, mama Tom alipiga kelele akisema kwamba wanamuacha mwanaye afie ndani ya shimo.

“Lakini juhudi zetu mama umeziona, Tom hawezi kuwa hai katika hili shimo! Ni maiti ngapi tumezitoa? Shimo lenyewe linazidi kutitia, siyo rahisi Tom akawa mzima mama, amini ninachokuambia!” Gimonge akamwambia mama Tom.

“Hapana...hapana...mimi ni mtu mzima wanangu, ninachowaambia ni kwamba Tom hajafa na ni vyema kama mkiendelea na juhudi za kuchimba, mwananu yupo hai ingawa atakuwa na hali mbaya sana!”

“Kwahiyo?”

“Endeleeni kuchimba!”

“Sawa mama, hatuna budi kukuridhisha!” Kazi ya kuendelea kuchimba ikaendelea.

Wengi wa vijana waliokuwa wakichimba walikuwa wakifanya hivyo kwa ajili ya kumridhisha mama Tom tu, lakini hawakuwa na matumaini ya kumtoa Tom akiwa mzima.

*******

Hewa ilizidi kumuishia Tom. Njaa, kiu na joto vilizidi kumsumbua lakini kila alipochungulia kwenye mfuko wake uliokuwa na dhahabu zinazong’aa alijiona ana kila sababu ya kujitahidi sana ili aweze kutoka akiwa salama akafurahie utajiri.

Tom aliendelea kupagua majbali pamoja na mchanga kwa mikono akielekea kutoka juu kupitia upande wa pili wa shimo. Alijitahidi sana kutoka eneno ambalo lilikuwa likititia, aliendelea kufanya hivyo kwa muda mrefu hadi aliposikia ardhi ikitingishika!

Alihisi kama kulikuwa na mtu akilima au akichimba kitu chini ya ardhi aliyokuwemo. Hapo alijua huenda shimo lilitaka kutitia tena! Akajisogeza pembeni zaidi kupisha mtetemeko na kishindo alichokuwa akikisikia. Ghafla akashangaa kuona sululu ikitita na kutoa pembeni ya sehemu aliyokuwemo, tobo likaonekana!

Tom hakuamini!

Alikuwa ni Gimonge, Mwita na vijana wengine wakichimba. Tom akapata furaha ya ajabu sana. Akaaza kupumua kwa kasi ya ajabu sana.

“...Huyu hapa!” Mwita akapaza sauti yake.

“Nani?”

“Tom!”

Mama yake Tom aliposikia hivyo alitamani kuamka kumfuata lakini alishindwa, aliishia kulia kwa sauti kubwa. Tom akabebwa na kutolewa hadi juu ambapo alianza kupepewa! Wakati yote hayo yakifanyika, hakuwa tayari kuuachia mfuko wake wa dhahabu uliokuwa mkononi mwake. Mwita alipotaka kumsaidia, alishangaa Tom akikataa.

“Wewe umechoka sana, acha nikusaidie!”

“Hapana, nitabeba mwenyewe!”

“Mamamaaaaaaa......” Tom alipaza sauti baada ya kumuona mama yake akiwa amelala kwenye machela, huku macho yake yakiwa yamejaa machozi.

“Tom mwananguuuuuuuu.....” mama Tom naye akapaza sauti yake.

“Pole sana mwanangu!” Ilikuwa ni mapema sana wewe kufa, napaswa mimi nitangulie kwanza, nikuache ukihangaikia maisha yako.

“Mama Mungu amesikia kilio chetu mama, utaishi maisha ya furaha katika kipindi chote ulichobakisha duniani! Mama tumeuaga umasikini...” Tom akasema huku akimfungulia mama yake ule mfuko wa slufeti uliokuwa na dhahabu!

Mama yake Tom hakuamini macho yake, akamkumbatia mwanaye wakilia kwa furaha. Katika vitu ambavyo Tom hakujaribu kabisa kuvifanya ni pamoja na kuuachia ule mfuko aliokuwa ameushika! Isingekuwa rahisi kufanya jambo la hatari kiasi hicho, alikumbatiana na mama yake, lakini mfuko wake ukiwa mkononi mwake.

Kilichofanyika baada ya hapo ilikuwa ni Tom kuandaliwa uji mwepesi kisha akapewa akanywa na kupata nguvu, baada ya hapo akapewa maji ya kunywa.

Hakutaka kulala kijijini Nyamongo, baada ya kupata nguvu wakakodisha Landrover iliyowapeleka hadi mjini ambapo Tom aliuza dhahabu kidogo, fedha aliyopata aliwagawia Mwita na Gimonge kisha kiasi
 
SEHEMU YA 16 YA 50

kilichobaki alikitumia kama nauli ya kwenda Nairobi kuuza madini yake.

Alipofika Nairobi alikwenda moja kwa moja kwa Sonara wa Kimataifa kuuza madini yake. Hakuamini macho yake pale alipokabidhiwa kiasi cha shilingi bilioni 7 za Tanzania, Tom akashika kiasi hicho kikubwa cha fedha akiwa na umri wa miaka 20. Kitu kilichokuwa akilini mwake kilikuwa ni afya ya mama yake.

Mara moja akakodi ndege na kwenda nayo hadi nyumbani kwao ambapo alimchukua mama yake na kumpeleka Nairobi kupata matibabu. Alimpeleka katika hospitali kubwa iliyosifika Afrika Mashariki nzima kwa kutoa tiba za uhakika ingawa walikuwa gharama za hospitali hiyo zilikuwa kubwa sana.

Baada ya vipimo kufanyika na mama Tom kupewa kulazwa, Tom aliitwa ofisini kwa daktari na kupewa majibu ya vipimo vya mama yake ikiwa ni pamoja na gharama za matibabu.

“Huyu mgonjwa ni nani wako?”

“Mama yangu!”

“Mama yako?”

“Ndiyo!”

“Pole sana mwanangu!”

“Nashukuru, hivi anasumbuliwa na nini?”

“Anasumbuliwa na uboho wa kweye mifupa!”

“Ni nini hiyo na inakuwaje?”

“Hiyo kitalaamu tunaita Bone Marrow, ambayo huathiri ute wa kwenye mifupa hivyo kusababisha upungufu wa nguvu za kuzalisha chembe hai nyeupe za damu na hapo ndio chanzo cha tatizo hilo kutokea!”

“Sasa?”

“Ni matibabu tu!”

“Atapona?”

“Ni matumaini yetu, lakini anatakiwa kufanyiwa ukarabati katika mifupa yake, kitaalamu tunaita Bone Marrow Transplant!”

“Naomba afanyiwe mapema tafadhali!”

“Tatizo ni gharama yake, sijui kama utaweza kumudu!”

“Ni kiasi gani?”

“Milioni 40 za Kenya!”

“Zitakuwa kiasi gani kwa fedha za Tanzania?”

“Milioni 400!”

“Hakuna shida, nipo tayari kutoa kiasi chochote kwa ajili ya mama yangu! Fedha haina thamani aliyonayo mama yangu!” Tom alisema akionyesha huzuni sana.

“Hakuna tabu, acha tukaanze hiyo kazi leo hii!”

“Nitashukuru sana dokta, kazi njema!”

Matibabu ya mama Tom yalianza mara moja, wiki mbili baadaye aliruhusiwa baada ya hali yake kutengemaa. Alipewa dawa kwa ajili ya kutumia nyumbani. Safari hii hawakurudi kijijini walipokuwa, badala yake walikwenda Dar es Salaam.

Tom akafungua akaunti katika Benki ya CRDB Tawi la Lumumba na kuhifadhi fedha zake. Akaanza mipango ya maisha yake mapya. Alinunua nyumba nyingi sana jijini Dar es Salaam na Kibaha. Akateua nyumba moja iliyopo Mbezi Beach kwa ajili ya kuishi na mama yake.

Katika nyumba hiyo kubwa ya kifahari, waliishi yeye, mama yake na msichana wa kazi tu! Tom akawa maarufu Dar es Salaam nzima, akaanza kutoa misaada katika Vituo vya Watoto Yatima. Akawa anadhamini michezo mbalimbali, jina lake likawa kubwa Dar es Salaam nzima, jina lake likabadilika, hakuitwa Tom tena, sasa alijulikana kwa jina jipya.

Alikuwa akiitwa Papaa Bill, likiwa ni kifupisho cha jina Bill Gates, bilionea wa Marekani. Jina lake likawa maarufu katika nyimbo za Dansi na Bongo Fleva. Tom (Papaa Bill) akaanza kufanya biashara mbalimbali jijini Dar es Salaam na Afrika Mashariki, safari za kwenda nje ya nchi zikawa haziishi. Jina lake likazidi kuwa kubwa sana, akawa Mjasiriamali aliyealikwa kufundisha katika vyuo, shule, makanisa na Jumuiya mbalimbali juu ya elimu ya Ujasiriamali na jinsi alivyoweza kupata utajiri na kudumu nao. Tom akaawa Papaa Bill kwelikweli! Utajiri wake ukaongezeka maradufu.

Jioni moja akiwa mezani wanapata chakula cha usiku na mama yake, alimweleza juu ya mkutano aliotakiwa kuufanya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam siku iliyofuata. Mama yake alimtia moyo sana.

“Itakuwa saa ngapi?”

“Ni semina ya siku nzima, nashindwa kuelewa itakuwaje, maana chuo kizima watakuwa wakinisikiliza!”

“Tatizo lipo wapi mwanangu, mbona mara nyingi umekuwa ukienda kutoa semina kwa watu?”

“Siyo Chuo Kikuu mama, kwanza ni wengi halafu pili ni wasomi, natakiwa kuandaa pointi za msingi sana kuweza kuwateka watu wenye elimu kunizidi mimi!”

“Usiwe na wasiwasi mwanangu, Mungu atakutangulia!”

“Ahsante sana mama! Nakupenda sana!”

“Nakupenda pia Tom!”

“Siamini kama umepona mama, lakini moyo wangu unaumi sana kula mafanikio haya bila baba. Ingekuwa furaha sana baba naye angekuwa nasi, sijui kwanini Mungu alimchukua mapema kiasi kile?!” Tom alisema machozi yakimlengalenga.

“...Mwanangu...Mungu hufanya kila jambo kwa makusudi yake, amini kwamba ana sababu za kumchukua baba yako...usijiumize mwanangu, Mungu atatutia nguvu! Hata hivyo ukianza kumlaumu kwa kumuita utakuwa unamkufuru! Kaka ni yeye ndiye aliyemuumba, kwanini asiamue kumchukua kwa wakati wake? Mwanangu umesahau kwamba sote tunaelekea huko huko na siku moja tutakutana naye? Tulia mwanangu, usijali tutakutana naye siku moja!” Mama Tom alisema kwa uchungu sana akimwangalia mwanaye.

“Sawa mama!” Tom akaitika kwa upole, hakuweza kukaa zaidi, Tom akaingia chumbani kwake kulala na mama yake pia.

******

Ukumbi wa Nkurumah ulikuwa umejaa wanafunzi wengi sana pamoja na Wahadhiri wakimsikiliza kwa makini Papaa Bill (Tom) alivyoweza kupata utajiri. Historia ya maisha yake iliwahunisha wengi.

Haikuwa rahisi watu kuamini kwamba Papaa Bill na fedha zake aliwahi kupitia maisha ya taabu kiasi kile. Baadhi yao hasa wanawake walishindwa kuzuia machozi yao, wakajikuta wakilia kwa huzuni wakati wakimsikiliza Papaa Bill.

“Hata jina la Papaa Bill, nilipewa hapa mjini baada ya kuwa maarufu na utajiri nilionao. Jina langu halisi ni Tom!” Papaa Bill alisema watu walimsikiliza makini.

Hakuna hata mmoja aliyekuwa akikohoa, kila alitaka kusikia kila neno lililotoka kichwani mwa Papaa Bill.

******

“Tom?!” Msichana mmoja aliyekuwa katikati ya wanafunzi alisema kwa sauti huku akioonyesha kushtuka sana.

“Vipi?”

“Namfahamu huyu Tom!”

“Acha kujipendekeza, mara hii unasema unamfahamu? Au kwasababu umeona ni tajiri?”

“Niache bwana, namfahamu naamini akiniona atanikumbuka!” Msichana huyo alisema maneno hayo huku akikazana kwenda mbele aliposimama Bill akihutubia.

Hakujali kama maneno yale yalisikika au lah, shida yake ilikuwa kuonana na Bill. Akajipenyeza katikati ya watu hadi akafika mbele kabisa aliposimama Bill, alishtuka sana kumuona msichana huyo.

”Mariam?!”

“Tom?!”

“Ni wewe?”

“Ndiyo!”

“Wewe ni mtu mbaya sana!”









Yalikuwa maneno makali sana yaliyomchoma moyo Mariam, hakuelewa sababu iliyomfanya Tom amwambie yeye ni mtu mbaya! Aliamini alikuwa mtu mwema sana katika maisha ya Tom, hasa kutokana na ukweli kwamba alishapata matatizo makubwa sana kutokana na kumsadia Tom.

Mariam akamwangalia Tom kwa macho ya mshangao, watu wakiwa kimya kuangalia kilichotokea, kuna waliochukizwa na kitendo cha Mariam kwenda mbele kwani kiliharibu mtiririko mzima wa semina.

“Tom, mimi ni mtu mbaya?”
 
SEHEMU YA 17 YA 50

“Yeah! Wewe ni mtu mbaya sana katika maisha yangu! Naona sasa umeona thamani yangu baada ya kusikia nimekuwa tajiri! Unajua baadhi ya watu wenye uwezo huwa mnajisahau sana, mnaona kama utajiri ni kwa ajili yenu na maisha ya shida ni ya watu wa chini siku zote!

“Mungu huyo huyo aliyewapa ninyi utajiri, ambao ulininyanyasa na kutoa thamani ya utu wangu, ndiye aliyenibariki na hivi sasa nina fedha!” Tom alisema kwa uchungu sana.

“Usiseme hivyo Tom!”

“Kumbe nisemeje?”

“Hujui yaliyotokea, nina habari mbaya sana!”

“Sawa...niache kwanza nimalize semina, hayo mambo mengine yafuate baadaye!”

“Sawa!” Mariam akaitika kwa shingo upande, huku machozi yakimtoka machoni mwake.

Akaondoka na kwenda kukaa mahali alipokuwa mwanzoni. Furaha yake ikatoweka kabisa, hakuwa na amani tena, shida yake ilikuwa kuhakikishiwa kuwa na mwanaume aliyempenda, Tom!

Hakuna aliyekuwa akifahamu kilichokuwa kikiendelea, ilikuwa ni siri ya Tom na Mariam peke yao, wao ndiyo waliojua kilichokuwa kikiendelea. Semina ikaendelea ambapo Tom alieleza siri ya mafanikio ya utajiri wake na jinsi anavyoweza kutunza fedha na kuendelea kuwa tajiri.

“Tatizo siyo kupata fedha, kikubwa ni jinsi gani ambavyo unatumia fedha zako! Labda niwaeleze jambo moja, baada ya kupata kiasi kikubwa cha fedha ni rahisi sana fedha hizo kupuputika kwa matumizi ambayo siyo ya lazima.

“Hata ukiwa na fedha nyingi kiasi gani? Kama hutatulia na kupanga mikakati, basi lazima mwisho wa siku utalia. Jambo la kwanza kabisa katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio ni nidhamu ya fedha!

“Lazima fedha iheshimiwe, usiamini una fedha nyingi sana kiasi cha kuanza matumizi ambayo siyo ya lazima. Nidhamu ya fedha inaanzia unapokuwa na kiasi kidogo kwanza, matumizi yako yapoje?

“Hupaswi kuidharau shilingi mia, maana ni mwanzo wa kuelekea kwenye elfu moja. Anza sasa kuwa na nidhamu ya fedha, utaona faida yake. Jambo lingine ni kuweka mikakati ya nini ufanye huku utafiti ukiwa silaha ya kila jambo linalohitaji fedha kabla ya kulifanya.

“Fanya utafiti wako kwanza, ni kweli ukitoa fedha zako hazitapotea? Ni kweli ni biashara nzuri inayolipa? Unaweza kufanya utafiti kwa wengine ambao wamewahi au wanafanya biashara ambayo inafanana na hiyo unayotarajia kuifanya kabla ya kuingia kwenye biashara husika.

“Tunza fedha, nenda kwa mahesabu, kila kitu kifanyike kwa rekodi, utaona mafanikio yake. Ndugu zangu, kama nilivyotangulia kusema awali kwamba, kupata fedha au utajiri siyo jambo gumu sana, lakini kinachowashinda wengi ni jinsi gani ya kuweza kudumu na huo utajiri bila kutetereka. Kwangu mimi naamini tunaweza na si imani yangu kwamba kuna mmoja kati yenu atashindwa kuwa na nidhamu ya fedha ili mwisho wa siku aweze kupata utajiri!” Tom alisema akishangiliwa.

Watu walikuwa makini sana kumsikiliza kwa kila alichokuwa akiongea, kwa wanafunzi pamoja na Wahadhiri wa Chuo Kikuu, ilikuwa faraja kubwa sana kwao kupata semina elekezi juu ya kufikia mafanikio.

Tom alikuwa na fedha nyingi sana, alikuwa tajiri mwenye uwezo mkubwa wa fedha na mwenye mali zinazoendelea kuzaliana. Ukiachana na maduka mbalimbali aliyokuwa amefungua jijini Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Tanga, Moshi, Mwanza na Dodoma alikuwa akimiliki kampuni ya kuuza na kununua madini mbalimbali iliyoitwa Tom Minerals Ltd iliyokuwa eneo la Posta jijini Dar es Salaam.

Alimjengea mama yake nyumba ya kifahari Musoma ambapo alimwekea mifugo na maduka ambayo aliyasimamia. Maisha ya kubahatisha yakawa yamefutika kabisa, mama yake Tom akaishi maisha ya kitajiri yaliyojaa furaha na amani.

Tom alikuwa akilipwa kiasi cha shilingi milioni 10 kwa saa kila anaposimama kutoa semina na ushuhuda wa maisha yake. Kila siku alikuwa akiendelea kukua na kukua!

Baada ya kumaliza semina, Tom akiongozwa na wapambe wake, walitoka wakiliendea gari lake. Mariam alikuwa akimfuata na kumuita jina lake lakini Tom hakugeuka. Alipolifikia gari lake, akafunguliwa mlango na kuingia.

Mariam akaendelea kulia akiomba asikilizwe, hata hivyo maneno yale Tom hakuyasikia kwakuwa alifunga vioo vyote. Mariam alipozidi kulia, Tom akafungua dirisha moja na kumwangalia kwa jicho la huruma.

“Hebu mwacheni, mruhusuni aje!” Tom akasema, wapambe wake hawakuwa na kipingamizi tena, wakamruhusu Mariam ambaye alisogelea gari la Tom akizidi kulia.

“Mfungulieni mlango!” Tom akaagiza.

Mlango ukafunguliwa, Mariam akaingia ndani ya gari, mlango ukafungwa na vioo vikapandishwa. Tom akawasha kiyoyozi kisha akafungulia redio yake kwa sauti ya chini sana.

“Nini kipya unataka kunieleza Mariam? Nimeshakuambia wewe ni mtu mbaya sana katika maisha yangu, sioni kama kuna sababu ya kuendelea kusumbuana. Haiwezekani kipindi nikiwa na matatizo unikatae halafu sasa hivi nina mafanikio ndiyo unajifanya unanililia. Huo naufananisha na unafiki! Acha unafiki Mariam!” Tom akasema kwa hasira ya wazi akimtizama Mariam machoni.

“Hapana Tom, nakupenda sana Tom wangu, Mungu ndiye shahidi wa ninac hokiongea. Nilitaka kupoteza maisha yangu kwasababu yako! Hujui kilichotokea!”

“Kwani ulipatwa na nini?”

“Siku ile wakati narudi kutoka hospitalini, nilipata ajali mbaya ya gari, nikakimbizwa hospitalini na kulazwa. Nilikuwa na hali mbaya sana maana nilipoteza kabisa fahamu kwa miaka mitano!

“Nililala kitandani kwa muda wote huo nikiwa sijui kinachoendelea, ni kama nilikuwa nimekufa! Nilipata majereha makubwa sana katika ubongo wangu hivyo kushindwa kupata fahamu katika kipindi chote hicho. Niliteseka sana, lakini nilipopata fahamu na hali yangu kurejea kawaida ndipo nikarudi tena hapa chuo, ndiyo maana unaniona nina umri mkubwa zaidi kuliko wanafunzi wengine!” Mariam alisema huku machozi yakitiririka machoni mwake kwa kasi sana.

“Pole sana Mariam, nakupenda sana Mariam!”

“Hata mimi Tom, sijaona mwanaume mwingine zaidi yako, sikuambii haya kwasababu ya utajiri ulionao sasa, kumbuka hata kipindi ulipokuwa huna kitu nilikuwa nakupenda kwa mapenzi haya haya ninayokupenda leo!

“Nirudishe moyoni mwako tafadhali, nipe nafasi nyingine Tom, naamini kwa kuwa na wewe maisha yangu yatakuwa ya furaha tena baada ya kuishi bila kuwa na furaha kwa miaka mingi sasa!” Mariam akamwambia Tom.

“Lakini umeshachelewa!”

“Kivipi?”

“Subiri!”

Tom akatoa simu yake mfukoni kisha akabonyeza namba fulani, akaanza kuzungumza na mtu. Dakika moja baadaye, msichana mrembo sana mwenye sifa zote za kuitwa mrembo akaingia kwenye gari ya Tom. Alikuwa mrefu, mwenye hips pana, makalio makubwa yaliyobebwa na kiuno chembamba sana.
 
SEHEMU YA 18 YA 50



Msichana huyo alikuwa amevaa suruali nyepesi nyeusi, blauzi ya pink pamoja na viatu vya wazi vyenye rangi ya pinki. Macho yake yalifunikwa kwa miwani kubwa ya giza! Alikuwa na midomo minene, iliyopambwa na mafuta maalum ya kupambia midomo, nyusi zilizochongwa kwa ustadi wa hali ya juu zilizochorwa kwa wanja mweusi zilizidisha uzuri wake.

Alikuwa msichana mrembo kwelikweli, manukato yake yalikaribia kupasua pua za Mariam! Yalikuwa manukato ya bei mbaya yenye harufu nzuri kuliko kawaida. Alipofika aliketi na kumtizama Mariam kwa dharau.

“Unasemaje Tom?” Msichana huyo akasema akionekana kuchukizwa na Mariam kuingia kwenye gari la Tom.

“Nataka kukutambulisha!”

“Sawa...”

“Mariam huyu ni mchumba wangu mpenzi ninayempenda sana, anaitwa Juliana. Ndiye mwanamke niliyenaye kwasasa ambaye kwakweli nampenda sana. Tupo mbioni kufunga ndoa ili tuishi kama mke na mume!” Tom akamwambia Mariam. Alipomaliza akamgeukia Juliana.

“Juliana, huyu anaitwa Mariam, alikuwa mpenzi wangu wa zamani kabla sijakutana na wewe!”

“Mh! Kumbe ulikuwa na mwanamke mbaya hivi? Ulifikiria nini lakini kuwa na uhusiano naye? Huyu ni kama alikuwa anakusababishia nuksi tu, katika maisha yako? Huyu ni takataka tu, hastahili kabisa kuwa na wewe!” Juliana akasema huku akifungua mlango tayari kwa kurudi kwenye gari lake.

“Tom mimi mbaya, takataka? Ndiyo umeamua kumuita mwanamke wako ili anitukane? Sawa bwana, Mungu yupo!” Mariam akasema akilia sana.

Muda huo huo akashuka kwenye gari na kukimbia akielekea mtoni. Hakuna aliyejua alichokifuata.







Maneno yale kutoka kwa Juliana yalikuwa sumu kali kwa Mariam, kwanza alijiangalia kuanzia chini hadi juu, kisha akamwangalia na Juliana baadaye akayarudisha macho yake kwa Tom, hakuamini alichosikia, aliona kama alikuwa katikati ya ndoto kali na huenda muda wowote angezinduka.

Alishuka haraka sana kwenye gari kisha akapiga hatua za haraka akielekea katika mto uliokuwa chini ya Jengo la Utawala. Kila mtu alimshangaa, alionekana kama mwendawazimu.

Kilichokuwa kikimuuma zaidi ni kitendo cha kumsaidia Tom kwa moyo wake, tena wakati akirudi kutoka kumpeleka baba yake na Tom hospitalini akapata ajali ambayo ilimlaza kitandani kwa miaka kadhaa.

Hakuona thamani yake tena, kila kitu alikiona kichungu, hakuwa na hamu ya kuendelea kuishi duniani. Alipofika mtoni alikaa chini akiwaza jinsi gani atakavyoweza kumaliza hasira zake, haikuwa rahisi kupata jibu la haraka. Tom alikuwa amempa kovu ambalo lisingepona kabisa.

“Nimemkosea nini mimi jamani, kosa langu ni nini? Kwanini ananinyanyasa kiasi hiki? Kwanini ananikosesha amani kiasi hiki? Amenionaje kwanza, yaani napoteza kabisa mwelekeo wa maisha yangu!” Mariam akawaza.

Aliendelea kulia akiwa hajui la kufanya, maisha yake sasa yalishakuwa machungu. Lakini baada ya kuwaza muda mrefu, akapata jibu; jibu lenyewe lilikuwa baya sana. Aliwaza kujiua!

“Ndiyo lazima nife...sioni sababu ya kuendelea kuishi katika dunia yenye tabu kiasi hiki, dunia yenye watu wenye roho mbaya ambao hawataki kuangalia thamani ya maisha ya wenzao, bora nife!” Mariam aliwaza akifikiria njia nzuri ya kujitoa uhai bila maumivu.

“Watu wanaojinyonga mara nyingi hutamani kukata kamba, lazima nifikirie njia nzuri ambayo haitaniumiza, lazima niondoke duniani kimya kimya, tena bila maumivu makali. Nataka kufa taratibu...ndiyo bora nife, hakuna sababu ya kuendelea kuishi nikiteseka!” Aliwaza Mariam.

Alidhamiria kufa, lakini hakutaka kusikia maumivu wakati roho yake ikitengana na mwili, lakini alikuwa akiwaza sana njia ya kujiua! Ni njia gani hiyo? Hakuwa na majibu, lakini ilikuwa lazima ipatikane.

* * * * *

Watu walikuwa wamezunguka gari la Tom wakisikiliza mzozo uliokuwa ukiendelea kati yake na Juliana, tayari Juliana alishaanza kuleta fujo baada ya kumuona Mariam, alilalamika kwamba eti alikuwa akidhalilishwa!

“Nimekwambia ni msichana wangu wa zamani, kwani kuna tatizo gani?”

“Wewe huoni tatizo?”

“Lipi? Sioni tatizo mimi!”

“Sasa sikiliza, wakati mwingine sipendi na sitaki unifanyie ujinga kama wa leo, tafadhali sana Tom, na kama hunitaki ni bora ukaniambia ukweli ili nijue moja!”

“Usiseme hivyo mpenzi wangu!”

“Kumbe nisemeje?”

“Sikiliza tuachana na haya mambo, tunaonyesha picha mbaya, nenda kwenye gari lako tuondoke!”

“Siendi kabla haya mambo hayajaisha!”

“Unataka yaisheje?”

“Kwani wewe unafikiriaje?”

“Basi twende tutazungumza nyumbani!”

“Sawa!” Juliana akajibu kwa hasira kisha akatoka na kwenda kwenye gari lake.

Kila jicho la watu waliokuwepo mahali pale lilikuwa likimwangalia Juliana. Alikuwa mwanamke mzuri sana kwa mwanaume yeyote rijali. Alikuwa mrefu, mwenye hips pana, makalio ya kumtosha na mwendo wake ulizidi kuwakosha raha wanaume.

“Mh! Huyu msichana mzuri sana jamani!” Mmoja wa watu waliomuona akipita alisema.

“Ni kweli kaka! Kweli pesa ni kila kitu, yaani ukiwa na pesa unaweza kuwa na mwanamke yeyote umtakaye!”

“Hivi umemuona vizuri usoni?”

“Ndiyo, ana macho mazuri ajabu, halafu anajua kuyatumia! Hakyanani huyu nikimpata chumbani, hakuna kulala yaani usiku mzima ni kupeana maraha tu!”

“Mh! Mshkaji sasa wewe umefika mbali!”

“Hakuna umbali wowote, ni mambo ya kawaida sana kwa mwanaume yeyote mwenye viungo vyote vizima mwilini!”

“Umeshinda kaka!” Hayo yalikuwa mazungumzo ya vijana wawili waliokuwa wakimtizama Juliana aliyekuwa akitembea kwa maringo akielea gari lililokuwa limeegeshwa karibu na la Tom.

Alipolifikia akafungua mlango na kuingia, Tom akafunga mlango wa gari, kisha akamwambia dereva aondoe gari! Tom akaondoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

******

Utajiri wa Tom ukawa gumzo kwa wanafunzi wa chuo, stori zote siku hiyo zilikuwa zikimhusu Tom! Kila mtu alikuwa akimmiminia sifa kutokana na uwezo mkubwa kifedha aliokuwa nao. Tom alikuwa mfano wa kuigwa.

“Lakini ana maendeleo sana!” Mmoja wa wasichana waliokuwa wakijadiliana kuhusu Tom alisema.

“Sana, halafu ana mwanamke mzuri sana!”

“Yaani acha tu, yaani ndiyo upate bahati ya kuwa na boyfriend kama yeye mh! Yaani mji mbona ungechimbika?”

“Lakini hapana bwana, watu wenye fedha wana matatizo yao bwana, waone hivyo hivyo!”

“Matatizo gani?”

“Kufungua zipu!”

“Tena ni viboko ile mbaya!”

“Ukiamua kuwa naye, lazima ukubali kuteswa, kutukanwa na kuchangia na wengine, lakini ukiwa na yale mambo ya kupenda umependa utake kuwa mwenyewe, thubutu haiwezi kutokea! Wanaume wenye pesa zao tabu tupu, asikudanganye mtu!” Walizungumza kwa muda mrefu sana wasichana hao, lakini baadaye mmojawao akamkumbuka Mariam.

“Halafu nilimuona kama Mariam akimfuata mbele wakati jamaa akitoa mada!”

“Eti alikuwa anamwambia anamkumbuka!”

“Mh! Mie sikuona jamani, ikawaje?”

“Jamaa akamtolea nje!”

“Si nilisikia baadaye alipotoka nje alimfuata tena?”

“Enhee! Lakini yaliyomkuta huko balaa!”

“Ilikuwaje?”

“Alimfuata jamaa, akamfungulia mlango, baadaye Tom akamuita mwanamke wake! Mzuri huyo asikuambie mtu.
 
SEHEMU YA 19 YA 50

Basi bwana, sijui walikuwa wakizungumza nini, nikashangaa Mariam akitoka kwa hasira na kuondoka zake!” Lilian, mmoja wa wasichana hao alisema.

“Akaenda wapi?” Pamela akauliza.

“Kakimbilia huko chini!”

“Wapi?”

“Mtoni!”

“Alikuwa katika hali gani?”

“Kama amekasirika hivi, maana inaonekana aliambia kitu kilichomuuza sana!”

“Mungu wangu!”

“Mbona umeshtuka?”

“Yaani mnaona ni jambo dogo hilo, tunaweza kumpoteza mwenzetu kwa mzaha hivi hivi!” Pamela akasema huku akikimbia.

Wenzake nao walimfuata wakikimbia hadi mtoni. Baada ya kutafuta kwa muda, walifanikiwa kumuona Mariam akiwa amelala chini akilia. Wakati mwingine alikuwa akjipigiza chini kwa hasira.

“Mariam vipi?” Pamela akamuuliza.

“Niache rafiki yangu!”

“Kwanini nikuache, niambie kuna nini?”

“Nina matatizo makubwa sana!”

“Matatizo gani tena?”

“Si unakumbuka niliwahi kukusimulia kuhusu maisha yangu?”

“Nakumbuka sana!”

“Unakumbuka kwamba nililala kuitandani kwa zaidi ya miaka minne nikiwa nimepoteza fahamu!”

“Nakumbuka!”

“Sijui kama unakumbuka sababu iliyonisababuishia matatizo yote hayo!”

“Ulisema...nakumbuka Mariam!”

“Ilikuwa ni nini?”

“Mapenzi...” Pamela akasema kwa sauti ya taratibu sana.

“Mwanaume mwenyewe ni Tom!”

“Tom?!”

“Ndiyo! Tom ndiyo chanzo cha matatizo yote hayo, lakini leo hii naambulia matusi!”

“Tom amekutukana?”

“Siyo yeye!”

“Sasa mbona umesema ni Tom?”

“Ni Juliana!”

“Juliana ndiyo nani?”

“Mwanamke wake, yule aliyekuja naye!”

“Mbona siamini kama anaweza kukutukana? Amekuambiaje?”

“Eti mimi mbaya, sina hadhi ya kuwa na Tom, yaani mimi mbaya...mimi mbaya? Sina hadhi ya kuwa na Tom? Siamini macho yangu, siamini kabisa, naona ni bora nife!” Mariam alipomaliza kusema maneno hayo akaanguka chini kama mzigo!

Akapoteza fahamu. Wakajaribu kumtingisha lakini hakushtuka, macho yake yakaanza kulegea pole pole kisha akayafumba kabisa, ute mwepesi ukaanza kumtoka kinywani mwake, shingo yake ikalegea kabisa. Mariam hakujigusa tena.

Wakapiga kelele za kuomba msaada.







Dakika kumi tu baadaye tayari watu walikuwa wameshajaa katika eneo lile. Hawakuwa na sababu ya kuuliza kilichotokea kwani hali aliyokuwa nayo Mariam pale chini iliwahuzunisha sana, mara moja akabebwa juu juu na kupelekwa eneo la Utawala.

“Nini kimetokea?” Mmoja wa wanafunzi aliuliza.

“Hayo siyo maswali kinachotakiwa sasa hivi ni kumuwahisha hospitali kwanza!”

“Lakini ni vizuri tukafahamu!”

“Ndiyo maana nimesema tumpeleke kwanza hospitali!” Pamela akaendelea kusisitiza.

Pamela na wenzake wakaongoza moja kwa moja hadi ofisini kwa Mkuu wa Chuo ambapo alitoa taarifa na gari likatolewa mara moja. Muda mfupi baadaye safari ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ikaanza. Hawakuchukua muda mrefu sana kufika hospitalini hapo wakitumia Barabara ya Sam Nujoma baadaye Ali Hassan Mwinyi kisha walipofika eneo la Daraja la Salender wakakata kulia wakielekea Hospitali ya Muhimbili.

Hawakuwa na sababu ya kukaa mapokezi, moja kwa moja aliweka juu ya machela na kusukumwa kuelekea wodini.

“Nini kimempata?” Mmoja wa wauguzi aliuliza.

“Alianguka!”

“Kwanini?”

“Alipatwa na mshtuko!”

“Wa?”

“Ni mambo ya uhusiano!”

“Kawaida ya wasichana!”

“Naomba utusaidie apone!”

“Usijali hii ndio kazi yetu, mmesema mnatokea wapi?’

“Chuo Kikuu!”

“Tulisikia Papaa Bill alikuwa anatoa semina ya Ujasiriamali pale!”

“Ndiyo, tena yeye ndiye amesababisha yote haya!”

“Kivipi?”

“Aliwahi kuwa mpenzi wa Mariam!”

“Mungu wangu!”

“Kwa hiyo alivyokuja pale alikuja na mwanamke mwingine anayeitwa Juliana. Hata hivyo Mariam alivyomfuata alimtambulisha kwamba ana mpenzi mwingine, mbaya zaidi Juliana alimtukana Mariam hiyo ndiyo sababu iliyosababisha matatizo yote haya!”

“Poleni sana, kwani Papaa Bill alikuwa hajui kwamba Mariam alikuwepo chuoni?”

“Alikuwa hajui!”

“Mbona sielewi kivipi?”

“Walipotezana muda mrefu sana na hata hivyo Papaa Bill alivyokuja Mariam hakujua kama ndiye mpenzi wake wa zamani!”

“Kwanini asijue?”

“Papaa Bill siyo jina lake halisi!”

“Kumbe anaitwa nani?”

“Tom!”

“Ok nimeanza kuelewa, tupeni nafasi kidogo tufanye kazi yetu!”

Pamela na wenzake wakatoka nje na kuwaachia wauguzi waendelee na kazi ya kumpatia matibabu Mariam. Jopo la madaktari watatu walikuwa bize kuhakikisha hali ya Mariam inakuwa nzuri. Kazi ya kupandisha mapigo yake ya moyo ilianza mara moja na matumaini yakaanza kuonekana.

Baadaye Muuguzi aliyekuwa akizungumza na akina Pamela alitoka nje uso wake ukionyesha alikuwa na jambo la kuzungumza nao. Macho yake yalionyesha wasiwasi mwingi jambo ambalo liliwazidishia hofu Pamela na wanafunzi wengine waliokuwepo.

“Muuguzi nini kinaendelea huko ndani?” Pamela alikuwa wa kwanza kuuliza.

“Punguzeni hofu, Mariam anaendelea vizuri!”

“Ameamka?”

“Bado lakini hali si mbaya!”

“Ahsante Mungu!”

“Mnaweza kwenda na kurejea kesho asubuhi!”

“Ahsante sana na Mungu akubariki!”

“Nanyi pia!”

****

Majina ya Tom na Mariam yalikuwa gumzo chuo kizima, kila kona walikuwa wakizungumziwa wao, hakuna hata mmoja aliyeelewa siri iliyokuwepo kati yao. Wengi walimwonea huruma sana Mariam lakini kuna ambao walimwona kama mtumwa wa mapenzi anayemng’ang’ania Tom kwa sababu ya fedha alizokuwa nazo.

Kilichokuwa nyuma ya pazia hakuna aliyekifahamu kwani ilikuwa ni siri kubwa iliyojificha katikati ya moyo wa Mariam ambaye alimweleza siri hiyo rafiki yake pekee Pamela.

“Hivi anaendeleaje Mariam?”

“Hajambo!”

“Ametoka?”

“Bado ila ameshapata fahamu!”

“Mh!”

“Mbona unaguna?”

“Sababu iliyompeleka hospitali!”

“Sasa hiyo ni ya kuuliza?’

“Ndiyo kila mtu anajua alianguka lakini sababu ya kuanguka kwake ndiyo inayonitatiza!”

“Si mapenzi?” Mwingine akadakia.

“Ishu sio mapenzi bali ni nani anayempenda!”

“Jamani huyu naye si Papaa Bill!”

“Sasa haoni kama hawaendani naye?”

“Msiingilie mambo ya watu hivi mnajua nguvu ya mapenzi ninyi?” Pamela aliuliza kwa ukali.

“Rafiki yako naye amezidi kujipendekeza kwa watu wenye fedha zao, halafu anajifanya mgumu utafikiri binti mlokole, hajawahi kusimama na mwanaume hata siku moja lakini hii inashangaza mpaka akazimia?”

“Ndiyo maana nasema hamfahamu kitu kinachoendelea hivyo kaeni kimya!”

“Sasa kama unajua si utuambie?”

“Ya ngoswe muachie ngoswe mwenyewe mmekuja kusoma au kujua ya watu?”

“Mh! Na wewe una majibu...shauri yako wewe mwendekeze tu huyo shoga yako!”

“Fyuuuu bakini na umbea wenu!” Pamela akasema huku akisonya na kuondoka zake.



***

Siku tatu baadaye Muuguzi aliyekuwa akipita raundi ya asubuhi alishangazwa na hali ya Mariam ambaye alikuwa ameanza kufumbua macho na kupepesa huku na kule. Mara moja muuguzi akasogea katika kitanda cha Mariam kisha akaketi.

“Pole!”

“Ahsante!”

“Unajisikiaje sasa?”

“Sijambo, kwani hapa ni wapi?”

“Hospitali!”

“Hospitali?”

“Ndiyo!”

“Nililetwa hapa kufanya nini?”

“Uliletwa hapa ukiwa hujitambui umepoteza fahamu!”

“Mungu wangu!” Akili ya Mariam ikafanya kazi kwa haraka. Akavuta kumbukumbu tataribu.



Nataka kwenda kwa Tom...

Napanda kwenye gari lake...

Namkumbusha mimi ni nani...

Ananiambia ana mchumba...

Baadaye anamwita...

Ni mwanamke mrembo sana...

Anaonekana ana dharau...
 
Back
Top Bottom