JOTO LA MOTO
JF-Expert Member
- Apr 11, 2018
- 758
- 555
TITLE: DOKTA IVO
MTUNZI: JOTO LA MOTO
SEHEMU YA KWANZA
NJE-KUNDUCHI BEACH HOTEL-KWENYE BWAWA LA KUOGELEA-MCHANA.
KAZI, kijana mtanashati, miaka 35,akiwa amevalia bukta ndefu ya bluu iliyobana sambamba misuli yake ya miguu, huku akiwa kifua wazi anatembea pole pole kuelekea kwenye bwawa la kuogelea.
Pembeni yupo Nora,Mwanadada mmoja mrembo mwenye muonekano wa kisomali kama sio kihabeshi, miaka kati ya 24 na 27, amejilaza juu ya kitanda kidogo cha mbao kilichopo mita chache kutoka lilipo bwawa lile, mkononi akiwa na glasi yenye juisi ya machungwa, huku macho yake kayaelekeza kwa Kazi.
Kazi anafika kwenye ubao maalum wa kunesanesa uliopo pale kwenye bwawa na kwenda mpaka ulipoishia ubao ule juu ya bwawa,ananesanesa mara kadhaa kisha kwa ustadi mkubwa anaruka juu na kuchumpa kwenye maji. Tukio lile linamfanya Nora kutoa tabasamu moja matata linaloashiria kuvutiwa na anachokiona, huku kwa mapozi akifyonza juisi kutoka kwenye glasi yake akitumia mrija.
Kazi anaogelea kwa ustadi mkubwa mpaka katikati ya bwawa na kisha anageuka kuangalia alipotokea, macho ya Kazi yanatua moja kwa moja kwa Nora hali inayopelekea macho yao kugongana, Nora analegeza macho yake mithili ya Mtu anayejaribu kutuma ujumbe fulani kwa Kazi, hali hii inamfanya Kazi kubaki ameduwaa kama Mtu aliyenaswa na umeme, “Mr Kazi” sauti nzito ya kiume inamshtua Kazi na kumfanya ageuke haraka pembeni na kumuona Bw Jako, Bwana wa makamo, mwembamba wa miaka kama 50 hivi, akiwa amevalia miwani nyeusi na suti maridadi ya kijivu mikono yake ikiwa mifukoni.
Kazi anapiga mikambi kuelekea ukingoni mwa bwawa aliposimama Bw Jako, Jako anatoa bahasha ya kaki kutoka mfuko wa koti lake. “kuna ujumbe wako hapa kutoka ofisini” anasema Jako, “lakini nipo likizo Mr J” anasema Kazi, “sasa unataka nifanyeje..mjumbe hauwawi?” anasema Jako huku akimpa Kazi mkono na kumsaidia kutoka mule kwenye bwawa.
Kazi na Jako wanaelekea zilipo meza na viti mita chache kutoka pale, “kuna muda wa kazi na muda wa kupumzika” anasema Kazi, “unaita haya ni mapumziko?” anasema Jako huku akisindikiza maneno yale kwa kicheko kifupi cha kebehi, “ona wale..wale sasa ndio wapo kwenye mapumziko” anasema Jako huku akimuonyesha Kazi pale alipojilaza Nora, huku kando ya Nora anafika Kijana mmoja mtanashati, wa miaka kama 25 hivi,anafika pale alipo Nora na kuonekana akianzisha mazungumzo na Nora.
Kazi anashusha pumzi mithili ya Mtu aliyekata tamaa ya jambo fulani, anageuka kwa Jako, “hiyo barua ni ya nini?” anauliza Kazi huku akiketi kwenye moja ya viti vile, “kadi ya mchango wa harusi”, anasema Jako huku akimpatia Kazi ile bahasha huku naye vile vile akiketi, “acha utani bro”, anasema Kazi huku akifungua bahasha ile na kutoa karatasi iliyokuwa ndani, “wewe unaoa lini Mzee?” anauliza Jako, Kazi anabaki kimya akionekana kuzingatia ile barua anayoisoma, zinapita sekunde kadhaa Kazi anaisogeza barua pembeni na kushusha pumzi nzito. “kwa nini Mzee kawaacha watu wote kanichagua mimi niliye kwenye likizo?” anasema Kazi, “labda ni kwa sababu wewe ni bachela au labda anakuamini sana kuliko wengine?” anasema Jako huku akitoa pakiti ya sigara mfukoni na kutoa sigara moja na kuiweka mdomoni, anatoa kibiriti cha gesi na kuwasha ile sigara kisha anapiga pafu moja na kupuliza moshi hewani. “nimekuuliza unaoa lini Mzee?“ anauliza Jako, “nitaoa vipi wakati sipati hata muda wa kutumia likizo yangu?” anasema Kazi, “mbaazi ukikosa maua husingizia jua” anasema Jako kwa sauti ya chini, “mmeshaandaa kila kitu?” anasema Kazi baada ya kushusha pumzi ya kichovu, “tiketi ipo tayari na muamala utasoma muda wowote”, anasema Jako, “na uwe makini maana huyo Bwana ni kigogo wa vigogo pale Arusha ni mfupa uliomshinda Fisi” anaongeza Jako huku akibofya simu yake na kusimama kumuonesha Kazi picha iliyopo kwenye ile simu, “huyu Dogo anaitwa Muso.. ana taarifa nyingi muhimu za uchafu wa huyo bwana” anasema Jako huku akimpatia Kazi simu ile, “maelezo mengine yapo kwenye email yako” anaongeza Jako na kisha anapiga pafu kadhaa za sigara, “bila shaka utamaliza kazi mapema ili uje kuendelea na mapumziko yako”, anasema Jako kwa sauti yenye mirindimo ya kebehi.
Kazi anamaliza kuangalia picha ile kwenye simu na kuirudisha simu kwa Jako, “kila la kheri kamanda”, anasema Jako huku akipokea simu yake, anaiweka mfukoni na kuanza kuondoka pole pole, Kazi anabaki ametulia huku amejiiegemeza kwenye kiti kama Mtu anayetafakari jambo, zinapita sekunde kadhaa Kazi anaangalia pale alipokuwepo Nora na kuona kitanda kikiwa bila Mtu, anainuka na kuelekea vyumba vya kubadilishia nguo.
Muda mchache baadae Nora anarudi na kujilaza tena kwenye kile kitanda, amamuita Muhudumu, “yule Kaka aliyekuwa pale yuko wapi?” Nora anauliza, “ameshaondoka” anasema Muhudumu, “shit” anasema Nora kwa sauti ya kukata tamaa.
JIJINI ARUSHA-NDANI YA NYUMBA ALIYOFIKIA KAZI-MCHANA
Kazi na Muso, kijana mdogo, 22, wameketi wote wakiwa na vinywaji mbele yao, Kazi akiwa na kifaa maalum (I pad) akionekana kubofya mara kwa mara akifuatia maelezo ya Muso,“kwa nini umeamua kumgeuka huyu rafiki yako wa muda mrefu?” anauliza Kazi, Muso anashusha pumzi, “nimemchoka tu bro” anasema Muso. “huo sasa ndio ujasiri..Vijana mnatakiwa kuwa hivi..mkiona Mtu anaharibu mambo mtoe taarifa bila kujali nafasi yake” anasema Kazi, “Kwa niaba ya jeshi la Polisi nakupongeza kwa hilo..na ninaamini utanipa ushirikiano mpaka tutakapomfikisha Dokta Ivo kwenye mikono ya sheria” anaongeza Kazi, “tupo pamoja Bro” anasema Muso, “hebu niambie kwa kifupi kuhusu shughuli za Dokta Ivo?” anasema Kazi, “ni mfanya biashara maarufu hapa Arusha..ana biashara za wazi na za chini ya kapeti” anasema Muso, “zipi za wazi unazozijua?” anasema Kazi, “ananunua na kuuza madini ya Tanzanite..ana Migahawa kadhaa hapa mjini..ana kampuni ya ujenzi” anasema Muso, “na za chini ya kapeti ni zipi?” anauliza Kazi, “ana vituo vya kuchezesha kamari ambapo huwa wanaruhusu hata Watoto washiriki na hakuna anayemchukulia hatua yoyote..pia nasikia ana kiwanda bubu cha kuzalisha bidhaa gushi..na anauza dawa za kulevya” anasema Muso, zinapita sekunde kadhaa, “endelea..zipo nyingingine” anasema Kazi, “hizo ndio ninazozifahamu bro” anasema Muso, Kazi anashusha pumzi, “ok..walau tuna kwa kuanzia” anasema Kazi. “na kwa muda huu wote utalazimika kuwepo hapa nyumbani tufanye hii kazi” anasema Kazi, “sawa bro..ila kuna jambo moja” anasema Muso, “ni lipi?”, “kuna rafiki yangu anaitwa Gabu..naomba tuwe nae hapa..maana ni Mtu wangu wa karibu na huwa tunakuwa naye mara nyingi” anasema Muso na kumfanya Kazi atulie kwa muda, “anajua kama uliwasiliana na IGP kuhusu Dokta Ivo?” anauliza Kazi, “anajua kila kitu..hata yeye hampendi Dokta Ivo” anasema Muso, “ok..anaweza kuja..ila awe tayari kufuata masharti yangu” anasema Kazi, “nitahakikisha inakuwa hivyo bro” anasema Muso.
NDANI YA OFISI YA DOKTA IVO-MCHANA.
Ndani ya ofisi moja kubwa nzuri iliyosheheni samani za kifahari na vipande vya madini ya Tanzanaite kwenye moja ya kabati dogo zuri la kioo lililopo kati kati ya ofisi ile, vinavyotoa mvuto wa kipekee.
Dr Ivo, Bwana wa makamo mtanashati, wa miaka kama 55 hivi, ameketi akipitia moja ya faili lililopo mezani kwake. Simu ya mezani inaita, anaiinua na kuiweka sikioni, “Mgeni wako ameshafika Boss” inasema sauti ya kike kwenye simu, “mwambie aingie” anasema Dr Ivo na kurudisha simu mezani, sekunde chache baadae mlango unagongwa na kufunguliwa, anaingia Kazi, “Karibu sana Mr Kazi” anasema Dokta Ivo huku akisimama na kuelekeza mkono wake kwa Kazi, “nashukuru sana Dokta” anasema Kazi huku akijongea na kupokea mkono wa Dokta Ivo, “karibu kiti” anasema Dokta Ivo huku akimuelekeza kwenye moja ya viti vilivyopo mbele ya meza yake, “nashukuru sana..ila nadhani nitaokoa muda..naomba niende moja kwa moja kwenye kazi iliyonileta hapa” anasema Kazi, Dokta Ivo anainua mkono wa simu ya mezani na kubofya mara moja, “niitie Sinta” anasema Dokta Ivo na kurudishia mkono wa simu mezani, “karibu” anasema Dokta Ivo huku akionyesha mkono kwenye meza ya pembeni iliyosheheni thermos kadhaa, vikombe, Jagi za juisi, vitafunwa mbali mbali na makopo kadhaa ya kahawa, milo, cocoa n.k.”usijali Dokta..nipo sawa” anasema Mr Kazi, “habari ya Dar?” anasema Dokta Ivo, “tupo tunapambana Kaka” anasema Kazi na mara mlango unafunguliwa anaingia Sinta, Dada mrembo, 25, mwenye umbo la kuvutia, “Sinta huyu ndio mgeni wetu kutoka Dar..anaitwa Kazi Wajibu” anasema Dokta Ivo, Kazi anamuangalia Sinta na kushindwa kuficha hisia zake huku akipokea mkono wa Sinta, “karibu sana” anatamka Sinta kwa sauti nyororo na ya upole, “nashukuru sana Dada Sinta” anasema Kazi, “ok..huyu ndiye ofisa uhusiano wetu, atakutambulisha kwenye vitengo vyote unavyohitaji kufika kwenye kampuni yetu..na ndiye atahakikisha unajisikia upo nyumbani” anasema Dr Ivo, “nadhani upo tayari” anasema Sinta, “tangu jana” anasema Kazi na kumfanya Sinta kutoa tabasamu moja pevu linalosababisha kuonekana kwa meno yake meupe yaliyopangika vizuri mdomoni, “karibu” anasema Sinta huku akielekea mlangoni na kutoa ishara kwa Kazi amfuate, Kazi anaenda hatua mbili na kugeuka kwa Dokta Ivo, “karibu Arusha Mr Kazi” anasema Dokta Ivo baada ya kuona Kazi amesita kwenda na kugeuka kwake, “upo vizuri Kaka” anasema Kazi, “ila kumbuka sio kila king’aacho ni dhahabu” anasema Dokta Ivo na kumfanya Kazi kubadili uso kama Mtu anayejaribu kutafakari maneno yale, “nadhani tuonane baadae Mr Kazi” anasema Dokta Ivo na kukatisha ile ganzi ya Kazi na kumfanya aelekee mlangoni na kutoka.
.......itaendelea......