Simulizi: Harakati za maisha

SEHEMU YA SITINI NA NANE

Nikiwa napiga kasia zangu barabarani kumuwahi bro aitwaye Scorpion,nilikuwa nawaza mambo mengi sana,hatima ya mimi mwenyewe kuhusu aina ya maisha nayoishi.

Dah,hizi habari mke wangu kama atakuwa kashafikisha kijijini kwetu kwa wazazi wanguuuu,sijui itakuwaje wale wazee ninavyowajua na wamekuwa wakisisitiza mimi kuwa kwenye zone nzuri lakini kwa presha ya mke wangu atakuwa kashawaambia tu,ila nitajua nitajiteteaje.nilijiwazia.

Nikiwa na karibia JNIA nilimpigia Scorpion ili nijue yuko wapi kwenye ile terminal aliyonielekeza,

Hey Dani mimi sijaingia ndani bado,utanikuta nipo pembeni ya barabara karibu na geti la kuingilia terminal 2.alijibu huku nikiongea kasia ya ngalawa yangu na kumuona akiwa na mwenzake mmoja aliyevaa nguo za jeshi la uhamiaji.

Vipi tunaweza kuongelea kwenye gari lako au tutafute sehemu nyingine? aliuliza Scorpion.

Hakuna shida bro,niliwajibu huku wote wakiingia ndani ya gari,lakini moyo wangu ulidunda dunda hata sikujua sababu ni nini ila nikawa makini ,haswa yule jamaa mgeni.

Tulisalimiana huku akionesha uchangamfu wa hali ya juu Scorpion.
Hata yule jamaa yake naye alionesha ni mtu fulani muongeaji halafu kwa muda mfupi nikagundua ni mtu bright.

Sasa Daniel ndugu yanguuuu mimi naenda mwanza mara moja nitakaa takribani wiki moja, huyu unayemuona hapa (yule mwanajeshi)
Anaitwaaaa huku akimpa nafasi ataje jina lake mwenyewe.

Naitwa Malik Alli ni mzaliwa wa mji huu kwani tangu nakua hadi naanza shule mimi na wazazi wangu tuliishi Kariakoo japo wazazi wangu wote wametokea Morogoro.alijitambulisha yule mgeni.

Ni vyema hata wewe ukajitambulisha ili mjuane au nakosea?alitania Scorpion.

Naitwa Daniel (nikitaja jina kamili) nimezaliwa mkoani Iringa,hapa jijini nimekuja kutafuta.nikijitambulisha kifupi.

Wote wakacheka,huku nisijue wanacheka nini ,
Sawa na mimi mnaniita tu Scorpion bila shaka wote hamjui jina langu kamili naitwa Sadam Salimu ,au double S,au Scorpion mdudu mwenye sumu kali ,ukizingua nakuachia balaa,ila bila kupoteza muda nina barua zenu ambazo mtazisoma kwa muda wenu kisha nitawapigia simu.aliongea Scorpion kisha akashuka kwenye gari na kuelekea ndani ya Uzio .akituacha na bahasha kila mmoja mimi na yule mjeda tukishangaana.

Oy bro mimi nilijua huyu mshikaji mpo pamoja,sasa mbona kakuacha?
Niliuliza kwa mshangao!!

Hata mimi nashangaa kwasababu huyu kanipigia simu asubuhi mno akasema tuonane maeneo haya, ndiyo nashangaa hana maelezo zaidi ya hizi barua,vipi tufungue tusome nini?alishauri yule mjeda.

Kwanza umekuja na usafiri gani , niliuliza kwani nilikuwa nataka niondoke barua nitasoma nikiwa hata ofisini.

Mimi nafanya kazi hapa hapa airport na pia leo siyo siku ya kazi kwangu kwani mimi wiki nipo zamu ya usiku.alijibu yule mjeda huku nikigundua ana hamu ya kutaka kujua nini kimeandikwa.

Basi bro mimi nikuache ngoja niwahi kwenye ujenzi wa taifa kila la kheri ndugu kwenye hizi barua zetu.maana ya Mungu mengi.niliongea huku yeye akishuka na kupiga hatua kiukakamavu kuelekea ndani ya ule Uzio.

Nikiwa kwenye foleni kali kwenye makutano ya barabara ya Nyerere na barabara ya Mandela ,na ndicho kipindi Daraja la Mfugale lilikuwa linajengwa nilikumbana na kero huku nikijilaumu bora ningepita chocho nazozijua kuliko adha ya pale .nilitamani nifungue barua nisome lakini kuna sauti iliniambia nisitishe ule mpango kwani naweza kuzua mengine unaweza iko negative contents ikaharibu siku bure.

Nilifanikiwa kufika ofisini muda sahihi kabisa Kisha huyoo mpaka ofisini kwangu, nikafanya setup fulani kwenye vitu vyangu kama ilivyo kawaida hakukuwa na email wala chochote kwenye Desktop nikatulia.
Na kufungua ile barua na kuanza kusoma huku moyo ukiwa unadunda mnooo.

Yeeees,
Waaaoooooh!!
Kilichoandikwa nilikielewa,nilikipenda na kukifurahia ila tu sikuwa na uhakika kama jina la Daniel Alex ni miongoni mwa watu niliowekwa kwenye mkeka ,hakika ilikuwa ni siku ya aina yake,nilianza kuvuta taswira ya vitu vingi nilijikuta natamani nimpigie simu yule afande niliyekutana naye pale airport ili nijue alichokutana nacho ni mlima au mteremko? Lakini nikakumbuka hatukubadilishana namba za simu hivyo zoezi likaishia pale.

Nilitoka nje ili nikapate breakfast kama ilivyo kawaida yangu huwa sipendi kifungua kinywa cha kwenye taasisi yetu badala yake huwa naenda nje kabisa kwenye restaurant nayoikubali mwenyewe.

Nilifika getini mlinzi akafungua mlango lakini mimi nilikuwa nimeganda nikiangalia nyuma nikilitafakari lile jengo letu nikiwa na mambo kadhaa kichwani,niliwaza vitu vingi mno kisha nikashituliwa na mlinzi.

Boss vipi kuna kitu umesahau naona unaangalia nyuma unakotoka.aliuliza kisha nikatoka nje bila kumjibu chochote.

Ndugu msomaji huwezi amini hata breakfast yenyewe sikuipata vilivyo nilikuwa na wenge la furaha,furaha ambayo ilizidi kipimo,nikaacha kula ile supu na kurudi ndani,niliinuka na kwenda kuchukua kitabu fulani kilichoandikwa na Mfaransa mmoja ambapo huwa nakisoma nikiwa nimepunguza majukumu yangu.

Lengo kulikuwa na mstari mmoja ambao huwa naupenda siku zote,kwani huwa unanihamasisha na kunipa nguvu ya kuamini kwamba ipo siku moja isiyokuwa na jina ambayo itabadilisha mustakabali wa maisha yako ambayo umeyaishi miaka mingi .

Mwandishi akiwa anamtaka msomaji asikate tamaa kwa anachofanya kwani huenda kikampa hatua moja mbele,na hata kama siyo hatua bali hata mabadiliko tu ya pale alipo ,kama alisimama basi atakaa,kwahiyo atakuwa kapata pumziko fulani.
Nilisoma kisha nikatabasamu huku kiherehere fulani cha kumtaka nimpigie simu wife kikinijia lakini nikasema weweeee!! Moyo ukome huenda chakula kipo mezani kweli,lakini hata maji ya kunawa bado,nataka kukaribisha watu! Tena unaweza kunawa na usile ,ni kawaida sana kwenye maisha.

Boss alinipigia simu,akinitaka niende ofisini kwake.nikafanya vile

Tulisalimiana huku akiniangalia na kutabasamu,kisha akaendelea

Kwani wewe Daniel nyumba ya iko wapi au unaishi wapi kwenye huu mji.aliuza.

Boss mimi sina nyumba bali nina kibanda ,ok ninaishi nje ya mji pembeni kidogo ya barabara ya kilwa.nilimjibu.

Daniel kwanza usipende kujidharau
Hivyo kusema labda nyumba yako siyo ya maana cha msingi unaishi kwako hata kama ni shimoni.

Nyumbani siyo sehemu unapoishi tu bali ni sehemu unapopamiliki mwenyewe, unaweza kuwa unaishi Apartments,mansion kubwakubwa,au Crystal palace ya kifahari lakini kama siyo kwako basi wewe utahesabika huna unachomiliki.

Ila tuachane na hayo nilichokuitia ni kwamba tulikubaliana tukutane saa kumi leo hii kwahiyo ifikapo Mida hiyo basi tutakutana pale, ikiwezekana mtaarifu na mkeo awepo lengo ni kuwapatanisha nyinyi kama familia ili maisha yaendelee.lakini pia najua unaishi Uswahilini hivyo jitahidi upunguze Uswahili,ukichofanya kimekishushia na kukupunguzia heshima sana na kupunguza hata imani kwa waajiri wako.
Unaweza kwenda.tukutane Mida hiyo tujue tunamalizaje,kwani suala hili nimeamua kulibeba.

Jifunze,
Elimika,
Burudika.

Loading.......
 
SEHEMU YA SITINI NA TISA

Kutokana na kile nilichokisoma kwenye barua niliyopewa na Scorpion asubuhi,niligundua boss hajui chochote,hivyo nilikaa kimya niliendelea na kazi zingine huku nikiona familia ya Jane ni wapumbavu tu na hata nilichofanya nikijiona nilikuwa sahihi.kifupi ile barua ilishanipa jeuri.

Nilimpiga simu wife kuwa Mida fulani atatakiwa awepo hotel fulani lakini pia ahakikishe kijana anakuwa makini ikiwemo kutomfungulia yeyote asiyefahamika lakini pia abebe kiasi fulani cha pesa kwani nilijua lazima kutakuwa na kutozana pesa.

Naam,ule muda wa kukutana hotelini uliwadia,watu tukakutana huku watu wote wakijibu salamu yangu kasoro Jane ambaye alijifanya yuko busy na simu lakini niligundua haraka.

Alikuwepo mume wa Jane na ndugu zake jane wawili.
Pia mimi na mke wangu ,pia alikuwepo mtu mmoja ambaye alikuwa sambamba na mume wake Jane alijitambulisha kama mwanasheria,jumla tukawa watu nane akiwemo boss wangu.

Kikao kilianza huku mke wangu mguu wake ukiwa umenikanyaga na hatoi lengo nitakapojaribu kupandisha ukali au presha yeyote basi iwe rahisi kunikonyeza.

Bahati nzuri kila kitu kilienda freshi kabisa ,pakuomba msamaha niliomba huku yule mwanasheria akidai mkono mtupu haulambwi hivyo lazima kibinadamu na kiuungwana nimpe takrima fulani Jane .

Ndugu zanguni hii wala siyo faini wala nini bali ni namna ya kumfariji ndugu yetu,dada yetu,ambaye ndiye aliyedhalilishwa,na hii kesi kama ingefika mahakamani huenda Mr Daniel angekuwa kwenye wakati mgumu mno lakini kwakuwa tumeamua kuimaliza kibinadamu basi unapaswa kutoa chochote ili kusafisha moyo wa Jane muhanga wa hili jambo.kwanza itakupa uhuru Daniel na itamfariji na Jane pia.
aliweka kituo yule aliyejiita mwanasheria.

Kwahiyo ni kiasi gani ndugu naweza kutoa, niliuliza.

Hii siyo faini kwamba imepangwa kisheria,na hapa hatupo kwaajili ya kukandamizana au kumuonea mtu bali ni muhusika atataja mwenyewe,iwe elfu moja,elfu kumi n.k.aliweka kituo yule mwanasheria.

Baada ya kusema hayo alipewa nafasi Jane ataje kiasi ambacho anahisi kitamfaa,
Aliinuka huku akijifanya anachechemea lengo watu wamuone aliumia sana.

Kwanza niwashukuru nyote kwa kuweza kunijali na kuonesha mapenzi kwangu,lakini pia nimshukuru huyu ndugu yetu ambaye ni boss wa Daniel kwa kuweza kuwa na utu wa kulimaliza hili suala.
Kiufupi bado nina maumivu kadhaa kwenye ubavu wa kulia lakini pia mguu wa kulia nao haujakuwa sawa.lakini najua mwenyezi Mungu ataniponya.

Pia niseme tu ukweli kwenye kikao hiki hakuna aliyenishawishi moja kwa moja mimi kukubali kuelewana na Daniel,si mume wangu wala nani bali ni mwanamke mwenzangu ambaye amekuwa akipiga simu kwa ndugu zangu lakini pia kwangu akinisihi na kuniomba nisitishe mpango wangu wa kumshitaki .sasa kwa kumalizia tu ni kwamba ninaomba anipe million tano ili angalau nikafanye checkup vizuri maana nina maumivu kila sehemu ya mwili wangu.na hapo ndipo nitakuwa nimemsamehe.aliweka kituo Jane .

Kwanza nilishtuka huku nikigundua mle ndani kila mmoja kashituka si kwamba waliona ile pesa ni nyingi ila ni kwamba Jane alikuwa kama anatoka kwenye mstari wa makubaliano yetu na ni kama alikuwa ananikomoa fulani.

Baada ya hapo mume wa Jane , mwanasheria wao na Jane mwenyewe walitoka wakaenda kujadili pembeni karibu dakika kumi nzima lakini baada ya kurudi walidai wamemsihi ila Kagoma akidai yeye anataka fidia ya pesa husika aliyoitaja.

Wakati huo mimi na mke wangu tulikuwa kimya sana,kisha boss wangu akavunja ukimya....

Ndugu zanguni nadhani tunachofanya kinaweza kisiwe sahihi kwasababu wote tulikubaliana kuwa tumalize kiundugu na kifamilia,ili maisha mengine yaendelee na pia kumbukeni gharama zote za hapa tulipo zote ni juu yangu mimi nadhani hakuna yeyote anayejua bili inalipwa na nani hivyo tunaomba basi tubaki kwenye mstari wa utu ili mradi kila kitu kiende sawa.aliweka kituo boss wangu.

Baada ya hapo mimi nilivunja ukimya na kusema nipo tayari kulipa ile pesa,na sijui ni hasira gani ilinipata ila ndiyo hivyo tena niliropoka.

Kwanza niwashukuru nyote kwa kuweza kukubali kuelewana na hatimaye kumaliza hili suala najua uhuru hupatikana kwa gharama,watu wengi Duniani wanahitaji uhuru,
Wawe huru kufanya mambo yao.

Kuna watu hawaolewi kwasababu wanahitaji kuwa huru na mambo yao
Hawahitaji kubanwabanwa.

Kuna watu hawaoi wala kutengeneza familia kwasababu tu hawataki kubanwabanwa wanahitaji kuwa huru.

Hivyo kwa mifano hii Daniel nahitaji kuwa huru , ni siku chache tu hapa nilikuwa kama mkimbizi asiye na vibali vya kukaa kwenye nchi za wengine yote haya ni kwasababu sikuwa huru. Hivyo niseme tu kuwa nipo tayari kulipa hiyo hela ili tu niwe huru. Niliweka kituo.

Mke wangu alinikanyaga akiwa anaonesha kukerwa kwanini nakubali kulipa pesa yote ile kwani pengine tungeomba tupunguziwe ingewezekana lakini pia Kila mmoja aliniangalia huku ikionekana Nina jeuri ndiyo maana nimekubali kulipa .
Hata boss wangu alinitazama huku uso wake ukiongea jambo.

Baada ya hapo niliomba niende chemba na mke wangu tutete jambo.
Huku tukiwaacha wengine pale.....

Hivi wewee upoje?umewezaje kukubali kulipa pesa yote hiyo?
Yule Jane katamka tu hakukuwa na ulazima wowote wa kukubali kirahisi vile,mmmh tena kila mtu kashakuona
wewe ni mjeuri na kiburi,na mbaya zaidi upo na boss wako huoni hii itakuweka kwenye mazingira magumu?alinilaumu mke wangu.

Usijali kuhusu boss wangu,kwanza huyu ni msimamizi tu siyo ndiyo kila kitu wewe unadhani maboss zangu wangekubali kukaa kwenye vikao hivi,
CEO mwenyewe yupo ughaibuni wiki ya tatu sasa.

Eenhee una kiasi gani hapo cha pesa . niliuliza.

Hapa nina milioni moja tu,sasa wewe mwenyewe umekubali pesa nyiiiingi kiasi hicho ,punguza kujiamini mume wangu kila siku pesa utakuwa unawatafutia watu tu sasa itakuwaje hii si ada ya mtoto ya mwaka mzima cha ajabu unawapa watu tu.
alilalamika sana wife.

Nilirudi kwenye kikao kisha nikawaambia kwa muda ule nina kiasi cha pesa kama asilimia ishirini tu,nyingine nitawapa baada ya siku kadhaa.kisha wote waliangaliana kisha mume wa Jane akachukua kile kiasi na kumkabidhi mkewe.

Baada ya Jane kupokea zile pesa akaziweka kwenye mkoba na kuinuka akaja nilipo na kutamka maneno yafuatayo......

Mimi nilikuwa nakuletea taarifa kutokana na ajali ya gari la mkeo baada ya kuona linatoa moshi kwenye injini hata hivyo tulikubaliana kuwa alinde gari Kisha mimi nikufuate wewe ili ukatoe maamuzi Ukiwa kama mwanaume ,pia nilimdanganya mume wangu nikimwambia nipo nyumbani lengo nisimuache mwanamke mwenzangu kwenye nyakati ngumu angenielewa vipi? Simu tumekupigia zaidi ya mara mia lakini haikupokelewa.
lakini Cha ajabu ukiishia kunipiga na kunisababishia maumivu makubwa.
Ila nimekusamehe na hata hicho kiasi kilichobaki nimesamehe ili nikuombe kitu shemeji yangu, bahati haijirudii mara mbili jaribu kubadili tabia zako. aliweka kituo Jane.

Watu wote walipiga makofi wakimpongeza Jane lakini pia mimi nilimshukuru kwa msamaha sana tena sana tu.

Baada ya hapo Jane na mke wangu walikumbatiana kitambo kidogo wakiwa na hisia fulani , baada ya tukio lile kupita niliwashukuru wote huku Kila mtu akionesha hana kinyongo na mimi.

Baada ya hapo niligusia juu ya usalama wangu haswa baada ya kusikia mpango mbaya wa kuchoma nyumba yangu moto , lakini wote walinihakikishia kuwa haitotokea hilo
huku wakiniasa kuwa niache au nipunguze kuwa na uhasama na watu kwani linaweza kufanywa tukio la ajabu na mtu mwingine Kisha Mimi nikawahisi watu wengine kwakuwa tu Niko na bifu na watu wengi.
Kifupi niliwaelewa sana Kisha boss akaingia kwenye gari lake na kusepa, Kisha Mimi na wife tukaaga. Huku tukiwaacha wale watano wakiagiza vinywaji vya aina mbalimbali, huenda ile pesa walitumia pale pale.

Tukiwa kwenye gari wife alikuwa anashukuru Mungu kama kawaida yake baada ya tukio lile kupita.
Vipi barua inasemaje? sehemu ijayo ina majibu, usikose!!

Jifunze
Elimika
Burudika.

Itaendelea..............
 
Itaendelea lini??
 
Ila mwanangu maisha yako kama series vile
una bahati sana ya upendeleo
 
Muendelezo baada ya x mass na boxing day 😂
 
Shukran mzee Kwa muda wako
 
SEHEMU YA SABINI

Maisha ni lazima yaendelee, lazima yasonge mbele kukosea kupo, kujikwaa kupo tu.
jambo la muhimu ni kuinuka na kuendelea mbele kwa maisha ndivyo yalivyo hakuna kukata tamaa.

Baada ya kufika nyumbani niliugundua ukimya wa mke wangu Kila nikimuongelesha na kujipendekeza kwake, akawa mbali na mimi mno. nikaona ni tatizo ila litaisha tu.ni hasira kutokana na mambo yote yaliyotokea hivyo atakuwa sawa tu. nilijipa imani.

Kesho yake asubuhi niliamka mapema sana kuliko kawaida ikiwa ni namna ya kumkimbia mke wangu ambaye tayari sikuwa na raha naye.
kutokana na kuwahi sana sikukumbana na adha yeyote ya foleni huku nikienjoy ngalawa yangu.

Naam, kama ada kama kawaida niliendelea na majukumu yangu kama kawaida huku ile barua aliyonipa Scorpion nikiisoma Kila nikipata muda, na moyo ukawa unapiga kila nikiichungulia barua ile, Kuna muda niliwaza mbali nikiona pengine yaliyoandikwa mule ni ya uongo.

Nilijaribu kumzoom Scorpion, kama ana Power na Energy ya kuweza kuwa kwenye nafasi ile ya kumpitisha mtu, lakini sikupata majibu , kwasababu kwanza scorpion alikuwa mtu fulani wa kawaida, lakini pia sikumfahamu vyema, nilimjua juujuu tu, ingawa yeye alikuwa anaweza kusimulia habari zangu na mienendo yangu kiasi cha kunishangaza sana.
Kifupi sikumjua vyema Scorpion.

Muda fulani nilipokea simu kutoka kwa dada wa kazi, hii ilinistua kidogo kwasababu huwa si mwepesi kunipigia simu, isipokuwa kwenye dharula na pia ni utaratibu wangu wa miaka mingi kutokuwa karibu na madada hawa,all men wanajua nini hutokea kwenye familia zetu hizi. nilipokea kwa hofu kidogo.

Habari za muda shemeji ,
Shikamoo., alianza kwa kusalimia dada wa kazi.

Hebu nenda kwenye point moja kwa moja , Kuna habari gani?
niliuliza.

Tangu asubuhi dada hayupo sawa, Kuna muda analia tu na Kila nikimuuliza hasemi, na amekuwa mkali sana leo, kifupi hayupo sawa.
na hapa naongea ametoka akiwa na begi lake dogo sijui ni wapi anaelekea . aliweka kituo dada wa kazi.

Nilikata simu ile ya dada wa kazi Kisha nikampigia mke wangu lakini licha ya kujaribu mara nyingi simu haikupokelewa.
Moyo ukaingia ganzi fulani lakini pia hasira ilijaa kifuani, nilijua mke wangu ananifanyia visa na ananifanyia utoto , ananinyanyasa.

Nilipiga simu kwa dada wa kazi ili nijue ni wapi kaona mke wangu anaelekea lakini akasema hajui kwani ni taxi imemfuata na kuelekea highway ikawa ni shida wao kujua.

Ilikuwa ni shida nyingine mpya baada ya ile ya Jane kuisha, japo kilichomo kwenye mioyo yao sikujua kwenye hii Dunia ya visasi.

Wakati nikiwaza hayo yote huku nikiwa sijui mke wangu nimtafute kwa njia gani, simu iliita jina likiwa ni CEO wetu, ilinistua huku nikikohoa kidogo kutafuta pozi la kuongea na boss mkubwa kabisa ambaye alikuwa ughaibuni kwa wakati huo.

Kwanza alianza kwa kunipongeza kwa kuniongezea daraja pale kazini,hii ni kutokana na kujituma na kukubali kufanya baadhi ya kazi ambazo kwa nafasi yangu ilikuwa ni kama dharau lakini nikawa nakubali ,hali ambayo ilifanya watu wanione na kuona nastahili kuwa kwenye angle fulani. huku sauti yake ya chini na ya kujivuta iliyojaa mamlaka ikiunguruma.
Tuliongea mengi huku nikijizuia nisijekujikanyaga kwa lolote kutokana na hali ya unyonge niliyokuwa nayo.
huku akinitaka nijiandae kwa safari ya kwenda kwenye semina fupi ya wiki tatu kwenye Moja ya Nchi za kusini mwa jumuiya ya SADC.

Ilikuwa ni moja ya safari moja nzuri na iliyo kwenye ndoto zangu , kwanza nilikuwa naenda kwenye Nchi fulani ndogo lakini maarufu barani Africa lakini pia sijawahi kufika ikiwa ni mara ya kwanza kukanyaga nchi hiyo.

Baada ya kupata utulivu fulani kwa kiasi chake, haswa kutokana na mawazo juu ya wife kutoka bila sababu za msingi hakika ilinisumbua, ilinipa hasira , niliwaza mambo mabaya sana.

Dah huu ni mkosi gani tena!!
Natakiwa kusafiri lakini cha ajabu badala ya mke wangu atulie tufurahie hatua tuliyopiga yeye ameamua kunidharau, Sasa nitafanyaje?
Nawezaje kusafiri bila kumuacha mke wangu nyumbani?
Nawezaje kwenda wakati waifu hayupo?
Dah kwani ni laana au kitu gani kinanifuatilia kwenye maisha yangu mbona Kila siku matatizo hayaishi kwangu? nilijiuliza mengi sana.

Taarifa ya mimi kuonesha natakiwa kubadilishiwa majukumu ilienea kwenye viunga vya taasisi yetu Kila mmoja alinipongeza sana japo kwao ilikuwa ni tetesi na bado sikuwa kwenye nafasi husika bado,lakini Mimi nilishajua kwa uwezo wa Mungu Kila kitu kitakuwa sawa tu.

Jioni nikiwa naingia kwangu kinyonge nilikutana na kijana wangu, aka ambaye ndiye ninayemtumia kwa mipango kadha wa kadha niliongea naye tukiwa pale nje huku akinifariji kuwa mke wangu atarudi tu.
Mke wangu nilimpenda hata yeye alinipenda ila alishachoka visa na vituko vyangu na hili lilinigusa na kuniumiza mno.

Mapenzi yanauma, yanaumiza sana, haswa kama unayempenda akawa hayupo radhi kuwa na wewe, achilia mbali wapenzi.

Hapa namzungumzia Mume au Mke , ambaye akinuna unajua yupoje, akicheka yupoje, na Mazoea yenu ya muda mrefu sana, lakini pale inapofikia anakukimbia bila kusema chochote ni ngumu sana kuikubali hali halisi kirahisi.

Niliingia chumbani na kuthibitisha kuwa mke wangu kaondoka kwani begi fulani na baadhi ya mikoba sikuiona, lakini pia hata kwenye meza yake ya urembo baadhi ya vitu sikuviona hii ilinifanya nijue kuwa kaelekea mbali sana.

Nilipiga simu mara nyingi ila mafanikio yakawa hakuna,
Nilituma sms nyingi lakini ilikuwa sawa na bure sikujibiwa chochote kile, nikajikaza kiume, sikutaka kumsimulia yeyote yanayonisibu huku kwa mara ya kwanza nikilala sebuleni nikiwa na viatu na nimechomekea vilevile, niliamshwa na adhana iliyotoka kwenye msikiti wa mtaani kwangu pale.

Nilikurupuka na kuingia chumbani huku nikiwaza mambo mengi sana , moyo uliniuma mno nilichukua simu na kuanza kumpigia mke wangu kwa fujo sana lakini hali ilikuwa vile vile, niliingia bafuni Kisha nikatoka.na kujiandaa , ile nataka nitoke tu simu iliita nikairukia nikidhani ni wife kumbe siye ,

Alikuwa ni fundi wa gereji akiwa anaongea kwa kufoka sana,,

Hivi bro unakumbuka nilikwambia hapa siyo sehemu ya kuhifadhi magari Sasa kwanini mpaka leo hupigi simu wala hufiki hapa tuanze kazi kama ulivyosema?
Na nilijua tu maana wengi wenu mko hivyo mnatelekeza mikweche yenu , Sasa nakwambia njoo utoe takataka yako Mimi hapa Sina nafasi Wala parking. aliongea kwa jazba sana yule fundi.

Lakini nilimuomba msamaha kiupole huku nikiahidi kila kitu kitakaa sawa tu na nitampa pesa kazi aianze mara moja.

Nilifika ofisini Kisha nikawa na kazi mbili kumpigia mke wangu huku nafanya mambo mengine lakini mafanikio yakawa hakuna mke wangu hakupokea simu wala hakujibu sms yeyote.

Kuachwa kunauma,
Kukimbiwa kunaumiza,
Mapenzi yanauma mno.
Usicheze hisia za mtu aliyeko moyoni mwako ni hatari sana revenge yake ni ni risk kwa afya ya akili na mwili.

Jifunze,
Elimika.
Burudika.

Inaendelea.............
 
SEHEMU YA MWISHO.

Ilifikia hatua nikataka kuwashirikisha watu maana maji yalishafika kooni ama shingoni , Daniel nina jeuri, kiburi na najiamini ila kwa mke wangu nilikwama, loh!!
Mwanamke ni kiumbe mwenye nguvu ya ajabu mno tena sana wanaume acha tufe mapema.

Watu wengi sana wanateswa na mapenzi lakini kutokana na vifua vyao na Siri zao wanajikuta wanaumia ndani kwa ndani, all weman wakipenda wamependa, wakiamua kuvumilia wanavumilia, tena unaweza sema labda hawana pa kwenda, ila usiombe wakakuchoka , yaani mwanamke akifikia mwisho wa kuwa na wewe mmmmh, weka mbali na watoto.

Ndani ya siku tatu mke wangu hakupokea simu, niliwaza na kuwazua, nikipanga na kupangua lakini haikusaidia chochote.
Nilikula ili nisijekufa ila sikuiona ladha ya chakula.

Nakumbuka asubuhi sana meneja aliniita na kunitaka nijiandae na safari huku akinikumbusha kupeleka CV zangu upya ofisini , sikujua maana yake lakini nilitimiza nachoambiwa,
Nikapewa siku nne za kujiandaa na safari huku niliruhusiwa kubeba Kila kilicho changu mle ofisini, kwani niliambiwa nikirudi huenda nikafikia sehemu tofauti na ile.

Nakumbuka nilienda kwa katekista mmoja aliye mtaa wa pili kutoka kwangu , nikawa namueleza habari za wife, kuwa simpati kwenye simu kwani katoroka na pia hapokei simu.

Kwanza Katekista alishangaa huku akidai siyo muda mrefu mke wangu alikuwa anaongea na mke wake na anaonesha ni mwenye amani na walijua yupo tu nyumbani na pia hajawaambia kama hayupo , lakini pia walinilaumu kwa kitendo cha kukaa muda wote pasi na kutoa taarifa popote maana ilikuwa ni ndoa hivyo alichokifanya mke wangu hakikuwa sahihi na angetafutwa na pia angejibu mashtaka.
alifafanua katekista.

Baada ya hapo mke wa katekista alikuja Kisha akapiga simu mbele yangu, mke wangu akapokea kisha simu nikapewa Mimi lakini baada ya kusikia simu yangu alikata.
Katekista na mkewe waliangaliana Kisha nikatoka bila kuwaaga , lakini simu yangu iliita mpigaji akiwa mke wangu,

Nilitulia huku nikipark ngalawa pembeni, huku nikipanga kuwa na nidhamu na maongezi yale.

Mke wangu kumbuka nakupenda, kumbuka kwasasa sisi ni watu wazima jaribu kuwaza na kufikiria ni taswira gani tunawaonesha watoto wetu, vipi wakisikia hizi taarifa huoni zitaathiri maendeleo yao ya shule?
niliongea kwa sauti ya chini yenye kujihurumia.

Acha maigizo Daniel,
Nakuita Daniel kwasababu hata sifa ya kuwa mume wangu sidhani kama unayo lakini nikwambie tu kuwa , Sina mengi zaidi ya kusema sihitaji kuwa na wewe, hapa napumzisha akili yangu tu kisha taratibu za kuachana au kuvunja ndoa zitafuata, siwezi ishi na wewe tena , ni mlevi, hujiheshimu, na huniheshimu, ni mtu mwenye majanga kila siku , unatengeneza maadui kwa makusudi Kila siku, jamii haikukubali inakuona kama inaishi na mtu mwenye wazimu na kichaa,.

Niliolewa na wewe kwasababu ya Sheria mtu akifika umri fulani lazima awe na mwenza wa kuanzisha maisha, ni kweli wewe ni mtafutaji, ni mtu mwenye kuijali familia na mambo mengine mengi lakini hukujali hisia zangu, Kila nilichojaribu kukifanya ulipinga, Leo hii hata marafiki zangu wengi walinikataa sababu yako, mtu pekee nilikuwa namuelewa ni Jane ambaye naye ukamuumiza,na kumsababishia maumivu makubwa. Sasa baba imetosha wewe tafuta mke uoe Mimi siwezi kuishi na wewe , tutakuja tufe kwa moto humo ndani si nasikia Kuna watu walipanga kuchoma nyumba yako?

Sasa kwanini nife wakati inawezekana kukuepuka na hata wanangu nimewaambia wasirudi hapo hata likizo ikifika, hata hao wafanyakazi wako nimewaambia waondoke na huyo dada wa kazi nilimpa na nauli yake aondoke kabisa.aliweka kituo mke wangu.

Sasa uko wapi nije maana Nina maongezi na wewe , tafadhali nihurumie mke wangu umeondoka kipindi nakuhitaji sana. Kumbuka Kila lenye mwanzo halikosi mwisho. nilimbembeleza lakini alikata simu huku licha ya kupiga mara kadhaa sikufanikiwa.

Niliwaambia wanajumuiya wake juu ya maamuzi ya mke wangu lakini walidai hawawezi kunisaidia kwasababu kwanza huwa sisali na pia tabia zangu zinajulikana mno hivyo itakuwa ngumu.

Nikahamia kwa wachungaji ambao walinipa moyo kuwa ni shetani yupo kazini na muda wowote mke wangu atarudi kama zamani .

Baada ya hapo niliondoka nchini nikiwa bado sijafanikisha lolote juu ya kurudi kwa mke wangu.

Nikiwa kwenye Moja ya Nchi nzuri yenye kudumisha mila na tamaduni
za muafrika , nilienjoy na kujifunza vingi sana, huku nikificha huzuni na kulazimisha furaha ili tu nisije kuwa kituko kwenye semina ile muhimu.

Siku moja nikiwa nimelala usiku, nilimpigia mke wangu kwa namba nyingine, ya Nchi ya kule akapokea ...

Mimi ni mume wako Niko nchi ya (nikitaja jina) vipi kwema huko!! nilisalimia

Ni kwema, vipi Nini kimekupeleka huko? aliuliza.

Nimeamua kutoka kwasababu wewe unaniumiza mno , nimeamua kuja kupunguza mawazo, mke wangu tafadhali ikiwezekana rudisha moyo wako kumbuka tutaharibu saikolojia ya watoto wetu. Niliweka kituo huku nikigundua ule ukali wa mwanzo umepungua.(nilimdanganya sikutaka ajue kama ni mambo ya kiofisi)

Usinichekeshe, wataharibika kivipi , na mbona wanajua kama sipo na wewe, ningekufa wasingesoma?
Nilipita shule zote wanakosoma na nimeshawaambia Mimi sipo nyumbani, lazima wajue na wazoee tu niwafiche ili iweje?

Tuliongea mengi huku msimamo wake ukiwa vile vile hakutaka kabisa ushirikiano na mimi.


Naam, siku za semina ziliisha huku nikiwa na madini kibao, hakika Mungu ni mwema, nakumbuka nilirudi Nchini huku nikihuzunika maana mtu pekee wa kunipokea alipaswa awe mke wangu lakini
Kweli shetani anajua anachokifanya.

Baada ya kwenda ofisini niliambiwa natakiwa kuandaa taarifa fulani kama feedback kutokana na nilichojifunza
Kule hivyo nikapewa wiki mbili,
Wiki ya kwanza nitaenda pembeni ya mji kwaajili ya kufanya kwa vitendo kile nilichojifunza lakini , wiki ya pili nitaandaa taarifa nyingine inayohusu computer.

Nikiwa pembeni ya mji nilikumbuka ni Kijiji nakifahamu niliwahi kufika kwaajili ya kumtafuta mtaalamu au mganga wa jadi ambaye alinikatalia kuwa ni kazi alishaiacha na kuamua kumrudia mwenyezi MUNGU.

Baada ya kumaliza kilichonipeleka, niliamua kwenda kumsalimia , akiwa kashanisahau , ila baada ya kumkumbusha alifurahi sana.

Enhee matatizo yako ulishayamaliza ? aliuliza.

Mzee wangu , kiukweli yaliisha ila kwasasa yapo mengine ambayo yananinyima raha mno ,Tena ni Bora Yale ya zamani nilikuwa nafarijiwa na mke wangu, lakini kwasasa mke wangu ndiye kanikimbia, yaani yapata mwezi na kitu sasa. Nilifafanua.

(Kwanza akacheka sana tu)
Loh mwanangu kweli una matatizo, lakini si uoe mwingine, mbona wanawake ni wengi mno , isitoshe wewe ni mwanaume unayeonekana si haba Sasa kwanini uhangaike na wanawake, hujui dawa ya moto ni Moto? aliuliza.

Mzee wangu,
Ingekuwa nimemuoa miaka mitano, au miaka ya hivi karibuni , ningemuacha lakini tatizo nimezeeka naye, yaani naona anguko mbele yangu ikiwa nitaoa kwa kutaka kuziba pengo, na pia sipo tayari kuoa kirahisi hivyo. Nilijibu Kisha akakubali kwa kutikisa kichwa.

Sasa mwanangu Mimi nitakusaidia kwa hilo, unajua Mungu hataki ramli chonganishi na shirki zingine ila kwa hili ngoja tumuombe Mungu, zipo sura za kuomba ustahimilivu kama wako kwanza nakuonea huruma sana ujue mke anauma na mbaya zaidi hujui kajificha kwa nani hapo na wivu unatafuna mifupa yako. alifafanua huku akizidi kuniumiza.

Tukakubaliana kuwa nikaoge niwe safi Kisha nirudi nikiwa nadhifu.
Kisha nikaenda pale gesti bubu nikajiswafi na kurudi kwa yule Mzee ambaye naye nilimkuta akiwa kwenye kanzu yake nzuri na safi licha ya watu wa vijijini kuwa na muonekano fulani rural.

Tuliingia ndani akaanza kusoma Aya kwa kiarabu huku akiwa ni mwenye hisia Kali , ilifikia hatua Hadi machozi yalimtoka huenda alimaanisha alichokuwa anakisoma.

Baada ya hapo akasema nimfuatishe akisoma maneno fulani, nikafanya vile Kisha tukaagana huku akinihakikishia kuwa kama huyo mkeo ni halali yako na Mungu alipanga uwe na wewe basi atarudi, ikiwa ni kinyume chake nayo ni kheri pia kwani mwenyezi Mungu anajua Kila analolifanya, tukapeana namba za simu Kisha nikaondoka. Nikiwa na tumaini jipya.

Basi niliendelea kumsumbua kwa kumpigia simu , hatimaye akaniambia alipo, alikuwa kwa ndugu zake fulani ambao ni wenye uwezo mzuri tu kipesa hawapo kinyonge ,japo ilikuwa ngumu kuwashawishi kumchukua lakini hekima na busara nilizotumia huku nikimshirikisha Mungu kwa Kila hatua, nikafanikiwa kumrudisha nyumbani.

Maisha mapya ofisini yalikuwa poa sana tena mno, heshima iliongezeka , wigo wa kufahamiana na watu uliongezeka, na mengine mengi mazuri, ila kumbuka tangu mke wangu arudi tulikaa vyumba tofauti kwa takribani mwezi mzima, huku nikigundua mapenzi yake kwangu yalishuka kwa kiasi kikubwa kama siyo kuporomoka kabisa.nilionesha
Udhaifu wa wazi kwa mke wangu
Kiasi cha kunigeuzageuza kama samaki kwenye kikaango.

Lakini ni udhaifu wangu ,wapo ambao mke hawasumbui kwa wanaacha mara moja lakini nao wana madhaifu sehemu nyingine,ndicho tulivyo ,mimi nikilizwa na hiki mwingine atalizwa na kile,ambacho huenda ni cha kijinga kwangu.

Dharau, vitisho vya kukimbiwa tena na mambo kibao ilikuwa ni kawaida kuambiwa, kifupi ni baadaye sana nilifanikiwa kuirudisha ndoa yangu kama zamani huku nikiwa natii vitu kibao ili tu ninusuru ndoa yangu.wanaume wenzangu wanajua.

Maisha yaliendelea hivyohivyo ,Kila kitu kikirudi taratibu, na kulingana na umri wangu vipo nilivyopunguza kama pombe,vipo nilivyoviacha na kufanikiwa kurudisha amani na upendo kwenye familia, jamii na hata Imani kwa waajiri wangu.

Harakati ni nyingi huwezi kuandika Mikasa ukaimaliza hii ni sehemu ya mwisho kwenye simulizi hii,
Huku lengo kubwa likiwa ni kujifunza, kuelimika na kuburudika pia.

1. Ndugu wasomaji na wafuatiliaji, kwa wote niliowakwaza haswa kuchelewa kwa simulizi mnisamehe tu,mambo ni mengi mno na pia members waliokwazana wenyewe kwa wenyewe, msameheane
Ni kawaida tu kwenye maisha.

2.Makosa ya kiuandishi, typing error na mengineyo mnisamehe sometimes haraka haraka inachangia.

Nawapenda sana wote.

Jack Daniel.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…