SEHEMU YA 54
“bwana ni mwema na mwenye huruma,hakuna mwenye haki atakayeaibika akiwa naye moyoni mwake……..hayo ndiyo bwana amenitendea,sala zenu zimenifikisha hapa nilipo,nilitakiwa kuwa nimezikwa zamani sana lakini bado ni hai bwana asifiwe!!.....hakuna mwanadamu yeyote anayeweza kuukatisha uhai wa kiumbe ambaye bado bwana anahitaji huduma zake katika hii dunia,ulemavu wa mwili sio sawa na ulemavu wa akili,ilimradi naweza kusema na nikasikika basi amani ya bwana iwe naye aliyeunyanyua mkuki na kunichoma nao katika mgongo wake,hata yeye ni mwanadamu aliyeumbwa na Mungu aliyeniumba mimi basi kama yupo hapa mimi namwambia nampenda sana na nimemsamehe zamani sana kwani lazima ana sababu zake zakufanya hivi kwani mimi ni nani hata nisitendwe hivi??? Hakika mimi si kitu na wala sijakamilika” alizungumza mchungaji maneno ambayo yaliwagusa wengi sana,ukimya ulikuwa wa hali ya juu kwikwi za hapa na pale zilitawala kwa walioshindwa kujizuia kulia.
“najua nitaumia sana kwani nilipenda kumchezea bwana kwa shangwe katika viwanja hivi lakini kamwe sitajutia kwani hata walemavu wanaweza pia kucheza kwa mbinu zao ambazo hivi karibuni nitajifunza na kuzielewa……” aliendelea mchungaji kabla ya kukatishwa kidogo na mtumishi aliyekuja kumnon’goneza.
“hamna shida mwambie aje tena ajisikie huru!!” alijibu mchungaji baada ya kuambiwa ujumbe flani na mtumishi.
“karibu karibu sana” alikaribishwa jukwaani kijana huyu mtanashati ambaye alikuwa hana uoga wowote na macho yake mekundu kutokana na kulia muda mrefu yalielezea uchungu aliokuwa nao.
“katika maisha ya kila siku ushuhuda ni kitu ambacho kinaongeza imani na kwangu mimi,ushuhuda ni zaidi ya mahubiri ya kawaida sasa wakati napumzika kidogo kuna ushuhuda tunatakiwa kuusikiliza kutoka kwa mmoja wa waumini wetu” alisema mchungaji kisha akamkabidhi kipaza sauti mtumishi mwingine.
“kabla sijazungumza lolote ningependa familia yangu pia iwe hapa kwani hawa ndio mashahidi wangu,na kama nawe pia ni shahidi wa hili nitakalosema tafadhali usisite kupanda jukwaani” alianza kijana huyo,hakuwa mwingine bali Timoth ambapo Noela na Oscar kwa furaha walipanda jukwaani.
“maisha ya ndoa niliyaogopa kuanzia mwanzo sikutarajia kuoa mapema lakini jitihada za mchungaji Marko pamoja na mama yangu mzazi hatimaye nikamuoa mke wangu huyu kipenzi anaitwa Noela ni mwanakwaya wetu pia,nimefurahia mengi katika uhusiano wangu huu lakini leo kwa uchungu na kwa msukumo wa moyo wangu nachukua nafasi hii kuyazungumza machungu niliyoishi nayo kwa muda mrefu sana,hisia potofu zilivyoyumbisha maisha yangu na kuivuruga kabisa akili yangu. Sitaficha lolote nitauelezea umma ukweli wote atakayeumia na aumie kwani ni kwa muda mrefu naumia mwenyewe” alisisitiza Timoth na kuzidi kuvuta umakini wa watu pale ambao taratibu walianza kusahau kuhusu mchungaji Marko na sasa macho yao yalikuwa kwa Timoth