Simulizi: Mimi na Mimi

Imefika sehemu ya kutambulishwa ukweni kwa lazima ila shadya ametoa shombo sana inafany watu wengi wasiende ukweni😁😁
 
Dah hii story itanifanya niwe mpiga nyeto sasa 😛😛
 
Jc kwenye mna maisha ya kizungu ndomana wakamuelewa miryam licha ya tofauti yenu ya umri kazi ipo ukweni kwako coz ni familia ya kiswahili
 
Pongezi kwa shadya maana taarifa za mahusiano ya JC na MIMI itafika kwa ndugu zake wote kwa negatively way,na hapo ndipo utamu wa simulizi utazidi kunoga😅😅😅
 
MIMI NA MIMI 2

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA AROBAINI

★★★★★★★★★★★★★★


Niliendelea kukaa tu chumbani kwangu nikiwa nasubiri lolote lile kutoka upande wake Miryam, yaani anipigie au labda anitumie ujumbe, lakini haikuwa hivyo mpaka inaingia mida ya saa mbili usiku. Niliweza kusikia gari lake likitoa mvumo wa kuingia hapo kwake pamoja na geti kufunguliwa, kumaanisha kwamba Tesha ndiyo alikuwa ameirudisha familia yao hapo nyumbani, kwa hiyo naelewa huo ndiyo ungekuwa mwanzo wa mambo kuwa moto zaidi baada ya kilichotokea masaa machache nyuma Shadya aliponikuta chumbani kwa bibie.

Sikuwa nahofia lolote, yaani kama ningeitwa hapo ili kuongea, nilikuwa na utayari wote wa kusema nao kwa ujasiri kuhusu upendo wangu kwa Miryam. Shadya alitukuta kwa njia fulani ambayo ingesomeka vibaya, sikatai, lakini siyo kwamba tulikuwa tumefanya kosa. Mimi na Miryam tulikuwa watu wazima, tukielewa vyema matendo yetu, kwa hiyo hapo kilichokuwepo ilikuwa kueleza tu matendo hayo yalimaanisha nini, na labda kuomba tu samahani kwa upande wangu ikiwa kweli nilifanya taswira ya familia iharibike, ila siyo kwamba nilikuwa na hatia kwa lolote.

Niliamini niko sahihi kabisa, na nilikuwa tayari kutetea penzi langu mbele ya maneno yoyote ambayo mtu kama Shadya angeyasema kupingana nami. Ile ishu ya ndugu zake kumpeleka sana Miryam ilitakiwa ikome, ilikuwa imeshatosha sasa, hata Miryam mwenyewe alielewa walikuwa wanampanda mno kutaka kumuamulia maisha yake utadhani hakuyaona. Muda wa kusimama imara kwenye uchaguzi wake ndiyo ulikuwa huu, na tungeungana mkono kwenye hilo kwa asilimia zote.

Ankia akawa amerejea hatimaye na kuja kunisalimia, kisha akaenda kujimwagia kwanza. Ni wakati huu ndiyo askari Ramadhani akawa amenipigia simu kwa mara nyingine, nadhani akiwa amepata nafasi nzuri ya kuzungumza, hivyo nikapokea na kuanza maongezi naye. Moja kwa moja nikaanza kwa kuongelea ishu ya yule Beatha, nikianza kwa kusimulia jinsi ambavyo mwanamke huyo alitumiwa na Bertha kipindi fulani nyuma kama mfanyakazi wake lakini hapo juzi ndiyo nikaja kutambua kwamba alikuwa ni mdogo wake baada ya yeye kunifatilia kwa mwendo mrefu ili anipe ule ujumbe wa Bertha na onyo lake.

Nikamwambia Ramadhan nilihisi huyo Beatha angekuwa na uhusiano fulani na kilichompata Bertha, kwa sababu nilipoongea naye ile siku alionyesha kuwa na aina fulani ya uchu wa kutaka aongoze mambo, akinitishia tu kwamba uwezo wa kuniumiza anao ila hakufanya hivyo kwa sababu ya mamlaka ya dada yake. Ikiwa Bertha kupoteza maisha kwa wakati huu ilimaanisha sehemu fulani ya hiyo mamlaka kwa mambo yao mengine ingekwenda kwa mdogo wake, basi Beatha angekuwa na nguvu ya kufanya lolote lile.

Nikamwambia pia ilibidi amchunguze huyo mwanamke, yaani wamwangalie kwa ukaribu kwa kuwa nadhani kundi lao lililobaki ambalo halikujulikana kama wengine wa madam Bertha waliokamatwa lingekuwa linaendesha operesheni zingine kisiri zaidi, na labda kwa kipindi hiki walikuwa wametulia tu baada ya ule mchakato wa maaskari kuwakamata wakubwa wao.

Ramadhan akaonekana kuelewa, naye akasema tu atalishughulikia. Si unajua maaskari wana njia zao za kuwatafuta na kuwadaka watu wanaowalenga shabaha? Ndiyo ambacho angefanya, na baada ya hapo ingefahamika zaidi. Akasema pia kwamba inawezekana familia yote ya Bertha ilihusiana na yale mambo aliyokuwa akifanya ndiyo sababu aliwaficha kwa akili, lakini kuanzia sasa angetafuta kuwajua watu wote wa karibu na Bertha ili kuona kama aliwaachia urithi (legacy) wake wa zile biashara katika njia nyingine. Bado yangekuwa ni mapambano, na Ramadhan alipenda sana kupata mtihani mpya ndani ya suala hilo hilo ili autatue vyema.

Tulipoagana sasa baada ya kukata karibu nusu saa tukizungumza, nikaona niende tu sebuleni kukaa na Ankia ili kupoteza muda. Mwenye nyumba wangu leo alikuwa akipika tambi, na alitaka tuzile pamoja na mishikaki, hivyo nikampatia elfu kumi na kusema alete mingi kadiri alivyotaka. Akacheka kidogo na kuanza kunisifu kwa kusema inaonekana bado nilikuwa na mood nzuri mno baada ya safari yangu fupi na Miryam ile juzi, lakini katika kauli zake zote sikutoa itikio lolote lenye uchangamfu kabisa, na hiyo ikampelekea kuniuliza kwa nini ni kama sikuwa sawa.

Nikamwambia tu kuna vitu fulani vilikuwa vinanisumbua akilini lakini nilikuwa sawa, na nikamwomba awahi kufata hizo mboga kabla haijawa usiku mno. Akaafikiana na hilo na kuondoka, akiniacha nimebaki kwa kutulia tu kusubiri lolote. Sikutaka kumtafuta Miryam yaani mpaka yeye ndiyo anitafute, ningengoja tu hadi upande wake ndiyo ulete jambo kwangu.

★★

Dakika zikaendelea kutembea tu na kugeuka masaa, hadi Ankia anarejea, tukala, kisha tukaendelea kukaa sebuleni kuangalia runinga. Ilikuwa imeshaingia mida ya saa tano usiku kwa wakati huu, na bado sikuwa nimepata ujumbe wowote kutoka kwa bibie Miryam, lakini Tesha ndiyo akawa amenitumia ujumbe mfupi hatimaye. Tukaanza kuchat, akiniambia kwamba mama zake walikuwa wamekaa pamoja na Miryam hapo sebuleni na Shadya pia, wakizungumzia jambo fulani muhimu sana, na yeye Tesha alikuwa zake chumbani lakini alitambua hayo maongezi yalihusiana na mimi. Ndiyo akawa ameuliza ikiwa wakubwa walijua kuhusu mahusiano ya mimi na dada yake.

Nikamwambia ndiyo, bila shaka wangekuwa wamejua. Nikamsimulia kwa ufupi kuhusiana na kilichotokea leo hapo kwao, na kwa mwonekano wa mambo inawezekana Shadya alikuwa akinipondea kinoma kwenye hicho kikao chao. Tesha akanipa pole, ila hakuona ikiwa kuna tatizo lolote kubwa pale, akielewa pia kwamba dada yake angeweka wazi zaidi juu ya mahusiano yetu na bila shaka tungesonga mbele. Wakati nikiwa bado nachat naye, simu yangu ikaanza kuita, na mpigaji alikuwa ni Bi Zawadi.

Nikapokea upesi, hapo hapo sebuleni nikiwa na Ankia, naye Bi Zawadi akaanza kwa kunisalimia vizuri tu. Nikamwitikia kwa utulivu na kumsikiliza, akiniomba niende hapo kwao mara moja "kama sitojali," nami nikasema sawa, nakuja. Nilikuwa ndiyo naenda kusimamishwa kwenye kizimba sasa ikiwa bado mambo hayakuwa mazuri. Nilipokata simu na kumwambia Ankia kwamba ninaenda hapo kwa jirani yetu, akawa ametambua kwamba kuna shida, lakini hakuniuliza sana. Akaniambia nimwahidi kuelezea nini kilichokuwa kinaendelea, nami nikakubali.

Sikuona tatizo lolote, yaani nikatoka hapo ndani na moja kwa moja kufika kwake bibie, na wakati huu saa sita ilikuwa karibu kuingia. Nimefika hapo mlangoni nikagonga hodi, na baada ya kukaribishwa na sauti ya Bi Zawadi nikaingia kuwakuta mama wakubwa, Shadya, pamoja na Miryam wakiwa wameketi sebuleni kwa utulivu tu. Bi Jamila na Bi Zawadi walikaa sofani kwao pamoja, Miryam akikaa pale ambapo nilipendelea kukaa mara nyingi, na Shadya akiwa kwenye sofa la pembeni zaidi. Miryam alikuwa amekaa kwa utulivu tu, akiegamia sofa na kunyoosha miguu kwa kuiunganisha huku akiangalia chini, nami nikaketi hapo hapo karibu yake na kuwasalimu mama wakubwa.

"Shikamooni warembo wangu," nikasema hivyo.

Bi Zawadi akatabasamu kiasi na kusema, "Marahaba baba."

Nikamwangalia Bi Jamila, ambaye hakutaka kabisa kutoa jibu kwa salamu yangu na kubaki ameangalia pembeni tu, nami nikatazamana na Miryam machoni kwa njia ya uelewa wa kwamba mama mkubwa wake alikuwa ameudhika. Nikamwangalia Shadya kwa macho makini, yeye pia akinitazama kwa njia fulani yenye kisirani, kisha nikakishika kiganja chake Miryam na kukikaza kwenye changu. Wote wakaniangalia usoni.

"Mama, asante kuniita. Nahisi kila kitu kishawekwa wazi hapa, na mimi nimekuja kuondoa jambo lolote linalowasumbua kifikira. Chochote mnachohitaji kuniambia, niambieni, chochote mnachotaka kuuliza, niulizeni... nitawaelewesha," nikasema hivyo.

Shadya akasema, "Haujaitwa hapa kuelewesha chochote. Umeitwa ili upewe ukweli wa vitendo vyako vya...."

"Shadya!" Bi Zawadi akamkatisha.

Nikatabasamu kiasi na kuangalia chini. Shadya alikuwa ameanza kunipanda na mimi.

Bi Zawadi akasema, "Ngoja kwanza tuongee nao vizuri. JC baba..."

"Naam mama..." nikamwitikia kwa heshima.

"Tumerudi hapa... Shadya ametuambia jambo fulani ambalo limetutatiza kiasi. Najua unaelewa, na... tunajaribu kuongea na Miryam, lakini... amekaa kimya tu. Haongei nasi kwa sababu ana hasira..."

Baada ya Bi Zawadi kusema hivyo, nikamwangalia Miryam usoni, naye akatazama pembeni kabisa. Nilimwelewa sana.

"Sisi siyo kwamba tunataka labda kuendesha chochote kwenye maisha yake, hapana. Tunajua ni mtu... nyie ni watu wazima. Hatutaki kufanya hili liwe suala zito sana, ndiyo maana nimekuita hapa tuongee kijana wangu. Ni kweli kabisa yote ambayo Shadya amesema kaona leo?" Bi Zawadi akaniuliza hivyo.

"Sijajua kasema ameona nini, lakini najua kaelezea vibaya. Ni kwamba...."

"Nimeelezea vibaya nini?" Shadya akanikatisha kwa sauti ya juu.

"Sina maana mbaya, namaanisha kwamba umechukulia hili suala vibaya. Umejaji mambo vibaya, ndiyo maana hadi Miryam amekasirika. Wewe siyo mtu unayepaswa kumhukumu vibaya, wewe ndiyo unatakiwa ukae umsikilize akikueleza sababu zake kufanya maamuzi fulani, lakini unatanguliza ujuaji ukijifanya unaelewa mambo yote vizuri sana. Kwa nini kutoelewana kusitokee?" nikamuuliza hivyo.

Shadya akabaki kimya na kuendelea kunitazama.

Nikamwangalia Bi Zawadi na kusema, "Sehemu kubwa ya mambo aliyowaambia Shadya ni kweli mama. Nilikuwepo hapa leo. Pamoja na Miryam. Na hiyo ni kwa sababu tunapendana. Hakuna kingine kinachojalisha zaidi ya hilo. Nampenda Miryam, na yeye ananipenda."

Bi Jamila akatuangalia kwa uso ulioonyesha kutatizika sana, naye akasema, "JC unajua unachokisema lakini? Unajua Miryam ni kama dada yako?"

"Mama... umri siyo tatizo. Nimempenda mw...."

"Yeye anachukulia easy kwa sababu ni mambo ambayo wanafanya sana huko kwao, anafikiri hata hapa itakuwa sawa tu. Wafanye yale maisha ya kupendana... kihuni tu, halafu aje amwache Mimi aende kwa wanawake wengine akishamchoka kesho tu, hivyo," Shadya akaongea kwa uchochezi.

Nikafumba macho kiasi, kisha nikaendelea kuwaangalia mama wakubwa na kusema, "Kama nilivyowaambia... hakuna kingine kinachojalisha kwa sababu mimi na Miryam tumependana, na ninataka kumwoa. Halafu kwanza yaani...."

"Umwoe? Unaongelea ndoa ya kanisani kabisa? Wewe JC umwoe Miryam?" Shadya akanikatisha tena.

Nikamwangalia usoni kwa macho makini.

"Kwenye familia yetu hiyo haijawahi kutokea, na haitakiwi. Ndugu zetu wote wakija kujua kuhusu hili, hawawezi kukubaliana nalo. Jamii itawachukuliaje mnafikiri? Usiongelee ndoa hapa kujishaua, kijana kama wewe unataka tu kujionyesha unaweza kumsaidia Miryam kwenye kila kitu, lakini kwenye ndoa HAUWEZI," Shadya akasema hivyo.

"Kinachokuuma ni nini Shadya? Yaani... una shida gani?" nikamuuliza hivyo.

Akabaki kunitazama kwa umakini.

Bi Zawadi akasema, "Shadya ana hofu tu, JC. Hataki Miryam aumie, ndiyo sababu. Hata mimi kiukweli nimeshangaa, lakini siyo kwamba tunajaribu ku...."

"Shangazi, usiwe mpole kwa huyu kijana, hata kama amefanya mangapi, la leo halikuwa sawa hata kidogo. Hata kama Miryam ni mtu mzima, bado ni mtoto kwetu, na JC amemrubuni tu... me nawaambia. Miryam... nikasirikie tu mama, lakini ni muhimu utusikilize sisi kwanza," Shadya akamwambia hivyo.

Nikamwangalia Miryam usoni, yeye akiwa ameweka uso makini na macho yake chini, nami nikamuuliza, "Uwasikilize kuhusu nini?"

Miryam akabaki kimya na kuangalia pembeni.

Ni hapo ndipo Tesha akawa ametokezea kwenye kona ya ukuta uliolekea huko jikoni, naye akaegamia hapo na kusema, "Jamani, kwani tatizo liko wapi?"

"Na we' Tesha unafanya nini hapa?" Bi Jamila akamuuliza hivyo.

"Ningeendelea kutulia chumbani, ila Shadya ana kelele mno," Tesha akasema hivyo.

"Shika adabu yako Tesha! Jiheshimu," Shadya akamwambia hivyo.

Tesha akanyanyua mikono juu kiasi, lakini akaendelea kusimama hapo hapo kwa kuegamia ukuta.

Nikaendelea kumwangalia Miryam na kumuuliza, "Ni nini ulichoshauriwa Mimi?"

Miryam hakutaka kabisa kujibu, yaani alikuwa anajizuia kutoa hisia zake, na kiukweli hilo likanifanya nijihisi vibaya.

"Mimi nitakwambia JC," Bi Zawadi akasema hivyo.

Nikamwangalia.

"Kwa kweli, hili suala lako na Miryam tunaona kama vile halifai... na... yaani, haijakaa sawa baba," Bi Zawadi akaniambia hivyo kwa upole.

Nikaangalia chini na kutabasamu kiasi.

"Kwa nini isifae ma' mkubwa?Msisingizie umri bwana, hawa wote ni watu wazima. Kama kupendana wamependana... haijalishi umri. Mtawazuia sasa?" Tesha akamuuliza Bi Zawadi.

"Tesha, ni bora ukae kimya. Haya ni ya watu wazima," Shadya akamwambia hivyo.

"Kwani me ni mtoto Shadya? Huyu ni dada yangu, namjua vizuri. Na tena hadi na nyie mnamjua vizuri. Mshawahi kumwona analeta mwanaume yeyote hapa? Mshawahi kusikia ametoka na mwanaume yeyote toka amekuja kuishi nasi hapa... kututunza? Ma' mkubwa... Shadya... mmemletea da' Mimi wanaume wangapi kumfosi aolewe lakini akawakataa kwa sababu alitaka kutuangalia sisi kwanza? Leo mmegundua kuna mtu anampenda, ndiyo imekuwa dhambi?" Tesha akasema hayo.

Mama wakubwa wakawa wametazama pembeni kwa njia za huzuni, naye Shadya akasema, "Ni rahisi kwako kuongea kwa sababu haujui familia hii imejengwa vipi. Si upogo bize tu kunywa pombe, utajuaje? Haipo, yaani haipo kwenye familia yetu mwanamke aolewe na mtu amemzidia umri. Tena kumkuta chumbani kwake akiwa amesha...."

"Kama kuwaambia angewaambia tu, wala ishu ya kumkuta chumbani na JC isiwe sababu ya kusema uhusiano wao muuone kuwa batili. Mkumbuke hapa ni kwake. Da' Mimi amefanya mangapi kwa ajili yetu jamani? Kweli tushindwe kufurahi kwa ajili yake akiwa amepata mtu wa...."

"Basi Tesha... inatosha. Hebu kaa kimya..." Bi Zawadi akamwambia hivyo kwa huzuni.

Tesha akatulia na kuangalia chini.

"Haya mambo siyo ya kuzungumzia hivi, eh... kwa kweli... Mimi... mwanangu unavyokaa hivi kimya unaniumiza sana. Ongea kitu basi," Bi Zawadi akasema kwa njia ya kubembeleza.

Miryam akaendelea kufunga mdomo tu.

Nikasema, "Tesha yuko sahihi mama. Umri siyo tatizo. Narudia tena... umri siyo tatizo."

Nilipokazia maneno hayo, nilimwangalia Shadya, naye akasema, "Siyo tatizo kwako kwa sababu umeshamdanganya Mimi weee, mpaka kuanza kufanya naye niliyokuta mnafanya leo. Halafu baadaye uje kumwacha, si ndiyo?"

Nikamwangalia usoni kwa njia makini na kumwambia, "Okay, labda uniambie ni nini kipya ambacho umeona tumefanya kilichokukera sana leo."

"Umeona jinsi anavyonisemesha? Yaani ana dharau! Me nilimwona mstaarabu, ila si mmeona?" Shadya akasema hivyo.

Nikamwangalia Bi Zawadi na kuuliza, "Eti cheupe wangu... ni kweli? Me ninawadharau?"

Bi Zawadi akabaki kunitazama kwa huzuni.

"Sijui kwa nini mnachukulia hili suala vibaya mama zangu... lakini nitawaambia kitu kimoja. Sijali nini, wala nani, nachojali ni kwamba ninampenda Miryam, na yeye ananipenda... na nitafanya kila kitu kuendelea kuwa naye," nikasema hivyo kistaarabu.

"Mmesikia hiyo?! Heeee! Hajali tumesema nini wala nini. Yuko tayari kufanya lolote, hata akimfanya Mir...."

"Na wewe Shadya nisikilize," nikamgeukia na kumwambia hivyo kwa uthabiti.

Akanitazama kwa umakini.

Nikamwambia, "Nakuwa mtulivu kwenye maneno kwa sababu nakuheshimu, nawaheshimu nyote, lakini siyo kwamba siwezi kuongea. Mimi na Miryam siyo watoto, na sijaja hapa kuomba ruhusa ya mtu yeyote yule kumpenda huyu mwanamke, kwa sababu nimeshampenda, na yeye ananipenda. Maneno yako hayo, mambo yote ambayo huwa unakaa na kina mama Doris ili kuvunja taswira nzuri ya huyu mwanamke, anayajua..."

"Jayden..." hatimaye Miryam akaongea kwa kusema jina langu.

Nikamwangalia usoni, akiwa ananitazama kwa namna ya kusema nisiongelee hilo suala, nami nikamwambia, "Hapana Miryam... lazima niongee ukweli."

Miryam akabaki kuniangalia kwa njia ya kutatizika, hata Tesha, Bi Zawadi, na Bi Jamila wakanitazama kimkazo.

Nikasema, "Yote mnayokuwa mnakaa kuyasema kuhusu huyu mwanamke, anayajua. Mtu ambaye Miryam anamwona kama mama yake, anakaa kusema kwamba hataolewa kwa sababu amelaaniwa, kwamba wazazi wake waliopoteza maisha ndiyo wamemwachia laana ya kuwatunza nyie. Ikimaanisha nini? Ikiwa wewe Shadya na mama Doris mnaona hiyo kuwa laana, basi ni nyie ndiyo mliomsababishia asiolewe kwa kuwa mzigo wa hiyo laana ni nyie, na ni yeye ndiyo anaubeba...."

"Jayden, acha..." Miryam akaniambia hivyo kwa sauti uthabiti.

"Mi' nimewahi kusema hivyo lini?" Shadya akajitetea kiwasiwasi.

"Tulimsikia mama yake Doris akisema hayo mambo, na alikuwa akiongelea mawazo yenu kwa ujumla. Mama zangu? Watu mnamwonaje huyu mwanamke? Kwa kila kitu ambacho amefanya kuwa pamoja nanyi mpaka sasa, Bi Jamila, umemtaka aipate furaha kwa muda mrefu, umetaka sana kuona anampata mtu ambaye atamwoa... leo kampata, mnataka kumzuia tena?" nikaongea kwa hisia.

"Jayden please..." Miryam akanena hivyo kwa kufadhaika.

"Wewe siyo huyo mtu JC! Haiwezi kuwa wewe," Bi Jamila akaniambia hivyo.

"Kwa nini? Ni kwa sababu ya umri kweli, au kwa sababu tu mmeshaanza kuogopa kwamba nikimwoa Miryam ndiyo itakuwa kama namwondoa kwenu milele? Kwamba atawapiga chini sasa...."

"Jayden...."

"... kwa kuwa ataanza kutumia muda wake mwingi pamoja nami zaidi yenu? Si ndiyo? Point ilikuwa nini sasa kujaribu kumfosi aolewe?" nikaongea kwa hisia.

Miryam akainamishia uso wake kiganjani kwa kufadhaika, na mama zake waliniangalia kwa mkazo mwingi sana wa kihisia.

"Huu unageuka kuwa uonevu, kwa sababu mnashindwa kueleweka ni nini mnataka. Hata kama ningekuwa sijamzidi umri, naelewa kungekuwa na pingamizi tu, ni maneno yasiyokuwa na maana yoyote ambayo yanasemwa kuhusu Miryam ndiyo yanavunja imani yenu katika maamuzi yoyote anayochukua, na kwa kuwa yeye ni mkimya, sikuzote mtataka kumwendesha tu. Well niko hapa sasa kuwathibitishia wote kwamba mnayowaza siyo... na nitamwoa Miryam hata mki...."

"Jayden, enough!" Miryam akanikatisha kwa sauti kali iliyoonyesha hasira.

Nikamwangalia usoni, wote yaani tulimwangalia, na alikuwa akinitazama kwa macho yaliyojaa machozi na hisia nyingi zenye kuvurugika.

Akatoa kiganja chake kwangu na kuniambia, "Naomba uende."

"Mimi, ninajaribu ku...."

"Nimesema ondoka, Jayden!" akanifokea.

Nilibaki nikimtazama kwa hisia za maumivu, kutoelewa yaani, nami nikamwangalia Tesha na kuona akitutazama kwa wasiwasi. Miryam akaegamiza paji lake kwenye kiganja huku akifumba macho kwa huzuni, nami nikainamisha uso wangu kwanza nikiwa nimechomwa sana na kitendo hicho alichofanya mbele ya mama zake, kisha nikanyanyuka na kuondoka sehemu hiyo kama mfukuzwa awaye mimi kweli.

Nilirudi kwa Ankia nikiwa nimeanza kuingiwa na hasira kali sana. Ilikuwa hasira ya moyoni yaani, na aliyeisababisha alikuwa Miryam. Yaani kwa mara ya kwanza akawa amenifanya nihisi hasira kumwelekea. Kitendo chake kiliniumiza, yaani nilikuwa najaribu kutetea mapenzi yetu na kuwafanya watu wake wa familia waone ni namna gani huyu mwanamke amekuwa akivumilia mengi, lakini badala ya Miryam kuniunga mkono, hata ingawa niliruhusu hisia ziniongoze kusema mengi hapo, yeye bado akaamua kusimama imara kwa ajili yao, na siyo kwa ajili yetu. Iliniumiza.

Nikaingia ndani, saa sita hiyo, Ankia akiwepo sebuleni bado, naye akanisemesha lakini nikapitilizia chumbani nikiwa nimeudhika vibaya mno. Nikaenda kujimwagia nikiwa na hasira bado, Ankia akinitazama tu kwa ukimya hadi niliporejea na kuelekea chumbani tena, na huko nikajifungia na kulala upesi nikiwa nimevurugika sana kihisia. Nilihisi hasira mpaka kuchoka yaani, kwa hiyo nikaulazimisha usingizi ili niepuke kuvurugika zaidi.


★★★


Asubuhi ya Ijumaa ikawa imefika. Niliamka kwenye mida ya saa moja hivi, na hiyo ni baada ya kusikia simu yangu ikiita bila kuacha kwa muda mrefu. Ndiyo nikanyanyuka kivivu na kuichukua, kukuta mpigaji ni daktari mwenzangu ambaye nilifanya naye kazi huko Muhimbili. Nikapokea na kumsikiliza alipokuwa akinipa utaratibu fulani mpya aliokuwa amekabidhiwa na mamlaka ya hospitali, na katika kushughulikia masuala mengi yaliyohusiana na huo utaratibu, akawa ameniambia kwamba ningehitajika kuwa tayari kurudi kazini kabla ya muda wa likizo niliyopewa kumalizika. Zilikuwa zimebaki wiki kama tatu, ila sasa hivi ningepaswa kurudi ndani ya wiki mbili.

Nikamwambia nimeelewa, na ndani ya hizi siku chache ningeenda huko hospitali kuangalia mambo yalivyobadilishwa kiutaratibu, halafu mengine yangefuata. Nikamuaga vyema baada ya kumwambia amsalimie daktari Roshan kwa ajili yangu, kisha baada ya hapo nikatoka kwenda kukojoa na kurudi ndani tena. Ankia alikuwa ameshaamka, na hatukuongea mengi zaidi ya salamu tu ila najua alielewa nini kingekuwa kinaendelea. Aliniangalia kwa macho yaliyoonyesha uelewa wa ni kwa nini nilikasirika, labda angekuwa ameshamuuliza Miryam na kuambiwa, ama kama Miryam hakumwambia basi huenda Tesha.

Nikaingia tu chumbani tena na kuanza usafi kwa kupanga vitu vyangu, maana zilikuwa zimepita siku chache sijakisafisha chumba. Nikamwomba Ankia fagio la kudekia, nikajishughulisha hapo wee mpaka chumba kikawa na mwonekano bora zaidi, nami nikaziweka pembeni nguo na mashuka yaliyohitaji kufuliwa kwa ajili ya kesho, Jumamosi, yakarabatiwe vizuri sana. Ankia akawa amemaliza kutengeneza chai na kuniita tunywe pamoja, nami sikupinga. Tukakaa sebuleni pamoja, na ndiyo akaniambia sasa kuwa alijua ni nini kilikuwa kimetokea kutoka kwa Tesha, na akanipa pole kwa jinsi ambavyo mambo yalikwenda mrama huo usiku wa jana.

Sikutoa komenti yoyote, yaani nilikuwa namega na kumegua mihogo-mkaango iliyotiwa pilipili na chai huku nikimsikiliza tu alipoongea, na akaniuliza leo ningefanya mambo yapi hapa nyumbani. Nikamwambia nisingekaa hapa leo, yaani nikimaliza kunywa chai, naoga, navaa, naondoka kwenda kuzurura mbali huko kwa marafiki zangu ambao sikuwa nimeonana nao kitambo, na labda ningerudi usiku kabisa. Aliponiambia nijaribu kumtafuta Miryam ili tunyooshe mambo kabla sijaondoka, nikanyanyuka tu na kwenda chumbani, na baada ya hapo shwaaa... bafuni.

Sikutaka kuanza na stress zozote kwa hii siku, yaani leo nilihitaji tu kufanya kitu wanaita "carefree," nisijali nini wala nini. Jamani, kama kujitahidi nilikuwa nimeshajitahidi mno, Miryam kunielewa alikuwa ameshanielewa mno, ni maneno mengi kadiri gani niliyokuwa nimemwambia kumfanya aone umuhimu wa sisi kupambania mapenzi yetu bila kujali nini wala nani? Hadi kwetu nilikuwa nimeshampeleka. Lakini yeye mbele ya familia yake yaani sijui alikuwaje, mpaka kumwelewa ilianza kuwa ngumu. Na hiyo jana, badala asimame imara na mimi kuniunga mkono, eti yeye tena akachagua kutetea upande wa familia yake uliopinga mapenzi yetu. Nini sasa? Halafu tena nianze "Miryam, sijui nini..." hamna. Na mimi nilikuwa nachoka!

Kwa hiyo leo kweli ningeenda tu kujiachia huko, maana huku niliona kama vile nimeanza kujilazimisha sana kuonyeshea watu umuhimu wangu. Nilikuwa najitahidi mno kutokuwa yule mtu niliyekuwa mwanzoni kwa ajili yake Miryam, ila yeye tena akawa ananivunja moyo. Kwa hiyo nini, kisa Shadya au nani kasema hataki, basi ndiyo tutatetemeka sasa, ama tuachane? Yaani kiukweli Miryam angepaswa kueleweka, mimi sijui msimamo wake ulikuwa wapi, lakini kama angeendelea kujiweka nyuma-nyuma namna hii, basi ingefikia hatua ningepaswa tu kumuuliza anauonaje uhusiano wetu. Kabisa yaani, ikiwa ulijalisha chochote kwake. Maana hiyo tabia ilikuwa inageuka kuwa ugonjwa usiopona sasa.

Bwana eh, nikaoga zangu vizuri kabisa na kuanza kutia viwalo safi mwilini, T-shirt ya Manga nyeusi na suruali ya jeans ya samawati, na hii ikiwa inaelekea kuingia mida ya saa nne sasa. Wakati nikiwa nachana nywele, nikaona kwamba mama alikuwa ametuma ujumbe simuni muda sana tokea nimeanza usafi, na kabla sijachukua simu kuusoma mlango wa chumba changu ukagongwa. Kwa kufikiri ni Ankia nikamwambia aingie tu, asinisumbue na maigizo yake ya kupiga hodi utafikiri yeye mgeni, na mlango ukafunguliwa kwa mimi kuangalia hapo kukuta ni Miryam ndiye aliyekuwa mgeni. Unayempenda akaja, lakini kwa wakati ambao hukuiona haja!

Miryam alikuwa amesimama hapo mlangoni, mwonekano wake ukiwa ule wa kutoka, bila shaka kwenda kazini kwake. Alivalia ile blauzi yake nyepesi iliyokuwa na mtindo kama ngozi ya twiga, pamoja na suruali yake nyeupe ya jeans laini iliyobana umbo lake matata vyema. Nywele zake alizibana nyuma ya kichwa na kuacha mkia uliozidondosha nyingi nyuma ya shingo, na macho yake mazuri kwenye uso wake wenye urembo wa hali ya juu yalinitazama kwa njia yenye subira kutokea hapo alipokuwa amesimama, akitaka nimsemeshe chochote kile.

Lakini nikaacha kumwangalia na kuendelea kuzipiga-piga nywele zangu kimarekebisho zaidi huku nikijiangalia kiooni, nikiwa makini kweli yaani, nami nikawa naona bila kumwangalia alipoanza kupiga hatua zaidi kuingia hapa chumbani na kuufunga mlango, kisha akaja hadi alipofika pembeni yangu na kusimama. Sikumtazama tena. Nikiwa naonyesha wazi kwamba sikujali uwepo wake hapo, nikaweka chanuo pembeni na kuanza kuvaa saa, kisha nikachukua raba nyeupe na kuketi kitandani ili nivae upesi.

"Jayden..." akaniita kwa sauti ya chini.

Nikaendelea kutia kiatu mguuni bila kutoa itikio lolote.

"Jamani Jayden, si nakuita?" akasema hivyo kwa upole.

Nikamaliza kuvaa viatu na kusimama, nami nikachukua simu yangu nikitaka kuusoma ujumbe wa mama.

Miryam akaweka kiganja chake juu ya simu yangu kama kuifunika, naye akasema, "Jayden please... usiwe hivyo. Naomba tuongee."

Nikashusha mkono ulioshika simu na kutazama juu kwa ufupi, kisha nikamwangalia usoni kwa njia makini.

"Mbona unaniangalia hivyo?" akaniuliza.

Nikaacha kumwangalia na kuiweka simu mfukoni.

Akanishika mkononi na kusema, "Jayden nakuomba tuongee vizuri. Jana... yaliyotokea, yaani wote tulikuwa rash, nilikuwa na hasira, na we' ulikuwa na hasira, ndiyo maana nikakwambia uondoke ili mambo yasipindukie kubaya zaidi... inaeleweka. Naomba tuyaweke hayo pembeni ili tuongee."

"Nakusikiliza Miryam. Sema unachotaka kusema, me niondoke," nikamwambia hivyo bila kumtazama.

"Jayden... ina maana... nilikukasirisha kihivi, kusema tu uondoke hiyo jana?" akaniuliza.

Nikamwangalia kwa macho makini na kuuliza, "We' unahisije?"

Akabaki kunitazama kwa huzuni.

Nikataka kumpita, lakini akanishika pande za mikono na kusimama mbele yangu kwa ukaribu ili kunizuia.

"Jayden, nisikilize..."

"Miryam, niachie, kuna sehemu nawahi..."

"Usinisome vibaya... tafadhali mpenzi wangu. Sikuwa na nia mbovu kukwambia uondoke ma...."

"Kuniambia?!" nikamkatisha kwa kumuuliza hivyo kiukali.

Akaniachia na kurudi nyuma huku akinitazama kwa macho yenye hofu.

"Hukuniambia niondoke Miryam... ulinifukuza. Mbele ya mama zako. Niambie ikiwa nimejichanganya kwenye hilo," nikasema hivyo kwa hisia.

"Jayden..." akaniita kwa sauti ya chini.

"Miryam nashindwa kukuelewa! Nifanye nini? Eh? I was there... fighting for us to show our love legit in front of your family, na nilidhani utasimama pamoja nami, lakini wewe tena.... akhh!" nikawa nimepandwa na hisia kali sana.

"Jayden, I'm sorry. Nisamehe... sihhh... sikutaka yawe magomvi ile jana, ndiyo maana nikakwambia uondoke. Nilitaka kuongea...."

"Ulitaka kuongea nini? Muda wote ulikuwa kimya, nikafikiri unanihitaji karibu yako ili tuwaonyeshe ndugu zako msimamo wetu, ila ulipofika muda wako wa kuongea... badala usimame nami... wewe tena ukaamua kunishindilia chini! Ni kwa nini?" nikaongea kwa hisia chungu kiasi.

Miryam akawa ananiangalia kwa macho yaliyojaa huzuni sana.

"Point uliyoonyesha hapo kwako jana ni kwamba maneno na hata masengenyo kutoka kwa watu wa familia yako, yako above all! Kwamba wakisema fanya hivi, utafanya, usifanye vile, hautafanya... hata kama ikikugharimu. Sasa ni kwa faida gani? Eh? Ni faida ipi iliyofanya nije pale, nikushike mkono, nitoe declaration yote kwa wote kuhusu mapenzi yetu, halafu in the end me ndiyo nionekane mbaya? Oh, nisingejali hata kama nani angeniona vipi, lakini we' tena ndiyo ukaushusha msimamo wetu mbele ya fam.... ohh... God!"

Nikashindwa hata kuendelea kuongea kwa kuhisi kuchoka na kuangalia pembeni, huku mapigo ya moyo yakidunda kwa nguvu kweli, maana hasira niliyohisi ilikuwa inalazimisha kutoka kwa kasi sana. Nilipomwangalia Miryam tena, nikakuta amejishika viganja kwa chini huku akidondosha machozi, kwikwi za kilio zikitikisa kifua chake kiasi huku akinitazama kwa huzuni sana.

Nikaingiwa na simanzi, nami nikamwambia, "Una... ah, aisee! Miryam... unanipa wakati mgumu kuelewa unacho.... acha kulia basi... ah... unalia nini sasa? Eh?"

Akainamisha uso wake kiasi na kusema, "Si we' unanifokea..."

"Na... a.. ahh... sikufokei, Miryam najaribu kukufanya uone kwamba...." nikaishia hapo na kumtazama kimaswali kwanza.

Akawa ananiangalia kwa huzuni bado.

"Yaani... unalia kwa sababu nakufokea?" nikamuuliza hivyo.

Akaonyesha kuwa na huzuni bado kwa kuangalia chini tu.

Hapa kulikuwa na hali yenye utata, lakini kauli yake aliyoitoa ikawa imenifanya nihisi kucheka kidogo, maana kiukweli ilichekesha. Lakini nikajizuia na kusema, "Ih! Ahah... haki ya Mungu!"

Nikaziba na mdomo nikiwa siamini kama kweli huyu mwanamke alilizwa na mimi kisa tu nimepandisha sauti, na yeye akawa ananiangalia kwa macho yenye kujihami hivi.

Nikamsogelea karibu na kusema, "Okay, okay, usilie... usilie Mimi, sijisikii vizuri ukilia. Usilie, samahani. Samahani kufoka."

Nilimwambia hivyo kwa upole huku nikimkumbatia, naye akarudisha kumbatio langu kwa wororo.

"I'm sorry. Nimeenda mbali. Nachanganywa tu na mambo mengi, nashindwa... nashindwa kuelewa sometimes," nikamwambia hivyo kwa sauti yenye upole, huku nikisugua mgongo wake kumbembeleza.

Miryam wangu alijua kudeka!

Akiwa bado kanikumbatia, akasema, "Nisamehe pia. Najua nilikufanyia vibaya, ila ilikuwa necessary tu Jayden. Sikutaka wakuone kuwa hauna heshima, maana kiukweli hayo yote hata me yalinikasirisha... lakini nimewaweka wazi juu ya msimamo wangu."

Nikamwachia taratibu na kufuta machozi yake, na miili yetu ikiwa karibu zaidi, nikamuuliza, "Unamaanisha nini?"

"Niliongea nao wote. Niliongea na Shadya kumwambia iwe mwanzo na mwisho ye' kurefusha mdomo wake juu ya mambo yangu yasiyomhusu. Nikaongea na mama hao pia... nikawaweka wazi kwamba ninakupenda, na niko tayari kupitia yote pamoja nawe iwe ni kwa faida au hasara... na nikawaomba wakubaliane tu na hilo kwa sababu sitabadili huo msimamo," akaniambia hivyo.

"Kweli?"

"Ndiyo. Ni kweli."

"Ahh... mbona sasa hukufanya hivyo wakati niko...."

"Wakati upo nilikuwa nataka nikuache uongee, nilijua mama zangu wanakuelewa sana, kwa hiyo hata kwa hili nilidhani wangekuelewa wewe vizuri zaidi pia. Nilidhani maongezi yangeenda vizuri, maana me nilikuwa nimekasirishwa sana na maneno mengi aliyoongea Shadya kabla hata hujafika, ndiyo sababu nilikuwa kimya, na ni kwa sababu tu ya heshima ndiyo maana nilikaa kimya maana ninge... ahh... sikutaka yaani hiyo misunderstanding iwafanye wakujaji vibaya. We were in the heat of the moment, nilitaka tu kukuambia uondoke, lakini kwa sababu ya hasira yangu ikawa kama nimekufukuza, lakini si kwamba nili...."

"Basi, basi Mimi... nimekuelewa," nikamwambia hivyo na kumshika usoni.

Akanishika mkononi pia na kusema, "Najua nilikuchanganya, na kwa hilo nisamehe tu. Ila maana yangu haikuwa kwamba nitakubaliana na pingamizi lolote lile kuhusu sisi. Siwezi kukubali. Hakuna mtu atatutenganisha Jayden."

Nikatabasamu kiasi kwa kufarijika.

"Niliwaambia hivyo jana. Nikanyoosha mambo, lakini... mama mkubwa anaonekana kama hajapenda sana hii ishu hata nikisema nini," akaniambia hivyo.

"Bi Jamila?"

"Ndiyo. Nilipoongea nao, Shadya akawa mpole, na ma' mkubwa Zawadi akasema ameelewa, lakini huyu mwngine ndiyo akaenda tu kulala bila kuniambia anaonaje. Hata leo hajataka kunisemesha," akaniambia hivyo.

Nikamwachia taratibu usoni na kusema, "Labda bado tu anashangaa. Tumpe muda eh? Hata hao wengine si walishangaa mwanzoni, lakini kama wameelewa, ni vizuri. Na yeye atayeyuka tu."

"I hope so. Sitapenda tukisonga mbele huku mama zangu wako conflicted yaani, nataka wote waone hili suala kuwa sawa. Nataka iwe ni amani mpaka mwisho Jayden," akaniambia hivyo kwa hisia.

"Na itakuwa hivyo Mimi. Ona, najua hapa mwanzoni inaweza ikawa ni ngumu, ila nitakuja kuzungumza nao tena, zamu hii vizuri, maana sitaki iwe...."

Maneno yangu yakakatishwa baada ya simu yangu kuanza kuita kutokea mfukoni mwa suruali.

"Ngoja..."

Nikamwambia hivyo na kuitoa simu mfukoni, kukuta mama ndiyo ananipigia. Nikamwonyesha bibie, naye akanitikisia kichwa kuwa nipokee, na nikafanya hivyo. Baada ya salamu fupi, mama akawa ameuliza kama niliuona ujumbe aliokuwa amenitumia mapema, lakini nikamwambia sikuwa nimeusoma bado. Ndiyo akawa amenipa taarifa iliyofanya nitabasamu kiasi, nami nikamwangalia Miryam usoni kwa furaha.

"Jas amejifungua!"

Nikamnong'oneza hivyo Miryam pembeni ya simu, naye akatabasamu kiasi kwa furaha. Nikaendelea kuongea na mama, nikiulizia muda ambao Jasmine alifanikisha kujifungua salama na ni hospitali ipi waliyokuwa wamempeleka ili niende huko upesi kumwona dada yangu na wapwa wangu wageni kwenye hii dunia. Mama akawa ameniambia wako kwenye hospitali fulani ya kibinafsi huko mbele kupita Goba kuelekea Bunju, iliyoitwa Rebinansia, na baada tu ya yeye kuniambia hivyo, tabasamu langu likafifia. Miryam akaniangalia kwa kujali sana, akifikiri kuna tatizo, nami nikaagana na mama nikisema ningeenda huko upesi hivyo tungeonana baadaye.

Niliposhusha simu, nikaangalia pembeni kwa njia makini yaani, na Miryam akaniuliza, "Kuna nini Jayden?"

Nikamwangalia na kusema, "Naam?"

"Mbona hivyo? Kuna tatizo lolote?" akauliza tena.

"Hapana. Hamna tatizo. Ahah... Jas kajifungua mapacha bwana," nikasema hivyo.

Akatabasamu na kuuliza, "Wa kike au wa kiume?"

"Wa kiume. Wote wa kiume. Ma' anasema Jas kawakurupua saa kumi usiku, ndiyo wakamkimbiza hospitali. Alipata-pata shida kwenye usukumaji ila akafanikiwa kujifungua wote salama kufikia saa moja hapo. Dah! Mungu mkubwa!"

"Sana!" Miryam akasema hivyo.

"Kibonge amejitahidi. Ndo'... itabidi niende huko sa,'" nikamwambia.

"Twende pamoja," akaniambia.

Nikabaki kumtazama machoni kama vile sikuwa nimemsikia.

"Vipi? Jayden!" akanishtua kwa kunitikisa kiasi mwilini.

"Aa... yeah, aa... ni sawa. Ila, si unaenda kazini?" nikaongea kwa kubabaika kiasi.

"Mm? Yaani Jasmine kajifungua, halafu nisiende kumwona kisa kazi? Acha mambo yako. Ngoja nikatoe gari nje..." akasema hivyo na kuashiria kutaka kuondoka.

Nikamshika mkono na kusema, "No, sikia... twende tu tuchukue usafiri. Gari liache."

"Kwa nini?"

"Usiende kabisa kazini leo. Tupite kwangu, nitakurudisha," nikamwambia hivyo kwa hisia.

Akatabasamu kiasi na kusema, "Ushaanza kunifanya niwe mtoro wa kazi."

"Nachukulia umekubali then. Au siyo?"

Akaniangalia kiudadisi na kuuliza, "Mbona kama kuna kitu unaficha? Unataka kufanya nini?"

"Mawazo yako tu. Sema kama umekubali," nikamwambia hivyo na kumbinya kiunoni kiasi.

Akacheka kidogo kwa pumzi, naye akasema, "Sawa. Tutapita. Hata hivyo bado tuna mengi ya kuongea. Ni vizuri tukiwa sehemu private."

"Fresh kabisa. Hapa si tuko tayari? Tunaweza tu kwenda?" nikamuuliza.

"Eeh, twende," akakubali.

Kwa hiyo ikawa ni kuondoka kwa Ankia upesi baada ya hapo, na bado mwenye nyumba wangu alikuwepo akijiandaa kwenda dukani kwake. Mwanzoni wakati Miryam ameingia inawezekana Ankia alikuwa amesikia utata wa suala letu pale chumbani, lakini sasa kutuona tunatoka tukiwa tumeshikana mikono ndiyo kukamfanya atambue kuwa ugomvi ulikuwa umesuluhishwa. Nikamwambia kuhusu dada yangu kujifungua, naye akatoa hongera zake na kututakia safari njema huko tulikokuwa tunaenda.

Tukatoka hapo kwake Ankia kwa mtindo huo huo wa kushikana mikono, na Miryam aliona aende kwanza pale kwake ili akaweke mambo fulani sawa na nini, kisha ndiyo akanirudia huku nje na mwendo ukaanza. Tulipendeza sana kutembea pamoja, na kwa sasa hivi hatukushikana mikono, ila wenye macho ya utambuzi hawangeweza kuacha kuona ukweli wa uhusiano uliokuwepo baina yangu mimi na bibie. Kwenye familia yake bado hali ingetakiwa kuwekwa sawa zaidi, na tena kuna ishu ya Mariam ambayo hatukuwa tumeigusia bado, ila kwa wakati huu umakini wetu ungekuwa kwa Jasmine kwanza.

Kuna jambo nililokuwa nikitarajia kukutana nalo huko kwenye hiyo hospitali aliyoisema mama muda mfupi nyuma, jambo ambalo sikuzote lilikuwa lenye uzito kwangu, ila kwa sasa ningekuwa tayari kulipa za uso.

★★

Tukachukua usafiri mpaka Rangi Tatu, kisha tukasubiria pale stendi kupanda daladala za kuelekea Mwenge. Miryam akampigia Soraya kumwambia kwamba asingefika dukani leo, hivyo ikifika tu saa sita na mwanamke huyo akahitaji kwenda msikitini ama wapi, afunge tu sehemu hiyo ya kikazi na wangekuja kuonana kesho; bila kusahau kumwambia ampe taarifa yoyote mpya iliyomhitaji ajue, na Soraya akawa ameafikiana na hayo. Watu kadhaa walikuwa wakitutazama mno kama ilivyokuwa kawaida, na hizo daladala za kuelekea Mwenge zilichelewa kiasi kufika, lakini si muda mrefu kutokea hapo gari likawa limefika, nasi tukapanda na kupata siti za kukaa.

Mwendo wa kuelekea huko Mwenge ulichukua muda mrefu, shauri ya misongamano ya mara kwa mara, mpaka tunafika kwenye kituo fulani kabla ya kumaliza safari nzima ilikuwa imeshaingia saa saba mchana. Kwenye hiki kituo tulichofikia tulisimama kutokana na gari kuharibikia njiani yaani, kwa hiyo tukashuka tu na kusubiri daladala zilizoelekea Bunju ambazo zingepita upande huo. Nilitaka tuchukue usafiri binafsi, lakini Miryam akaonelea kupanda daladala ndiyo ilifaa. Tukafanikiwa kupata moja na kusimama, na sikupenda hii ya kusimama nikiwa pamoja na Miryam lakini yeye mwenyewe ndiye aliyesisitiza hivyo, mpenda mambo simple, kwa hiyo mwendo ukaendelea hadi tulipokifikia kituo cha hospitali ya Rebinansia.

Hiyo hospitali ilikuwa kubwa, ya gharama kweli, halafu ya kibinafsi. Majengo yalikuwa maghorofa yenye umaridadi wa hali ya juu kweli, na kulikuwa na ujenzi wa chuo kikubwa hapo pia. Niliwahi kuja mara kadhaa kipindi cha nyuma kwenye hii hospitali kwa hiyo nilipajua vizuri sana, na wakati huu palikuwa pameboreshwa hata zaidi ya kipindi cha nyuma yaani. Kwa hiyo mimi na bibie tukaelekea huko, watu karibia wote walioingia na kutoka eneo la hospitali wakiwa na mionekano ya "kwenda shule" yaani, karibia kila mtu alijiweka katika hali zile za matawi, na ilikuwa sahihi maana gharama za hapo hazikuwa za mchezo, hivyo wengi wangejitahidi kuonyesha wanaendana nazo.

Nikawa nimempigia mama simu kumjulisha kuwa nimefika na kumuuliza wapo ghorofa gani, naye akaniambia ghorofa la tatu upande wa wodi za wanawake waliotoka kujifungua, ila kwenye chumba binafsi namba nane cha "ma-VIP." Haya bwana, mimi na Mimi wangu tukaelekea hadi kwenye milango ya lifti, nikitembea utafikiri hospitali yote ilikuwa yangu, basi tu eti kujiamini kwa sababu niko na bibie wangu. Tukapanda mpaka huko juu na kukitafuta hicho chumba, na tulipopata usaidizi wa muuguzi mmoja kutuelekeza, tukawa tumekutana na mwanaume mmoja aliyesimama usawa wa kaunta la wauguzi hapo nje ya vyumba, mweusi wa maji ya kunde, ambaye alivalia kwa njia ya kitanashati sana, na aliponiona akatabasamu.

Huyu alikuwa ndiyo Kevin, mume wa dada yangu Jasmine, baba wa hao mapacha. Alikuwa mrefu kunifikia, mwenye mwili mzuri wa mazoezi ingawa tumbo la kitambi cha mbali lilituna kiasi, na sasa alivalia shati jeupe ndani ya kizibao chekundu cha suti, na suruali yake ilikuwa nyekundu ya hiyo hiyo suti. Mwonekano wake ulitosha kutuambia kwamba alikuwa ametokea kwenye sehemu ya kikazi na kuja hospitalini baada ya kupata taarifa za mke wake kujifungua, nasi tukakutana hapo na kuunganisha mikono kisalamu huku mimi pia nikitabasamu.

"Mr... nakuona," nikamwambia hivyo kirafiki.

"Ah, hata me nakuona mdogo, unajikoroga tu. Uso unazidi kuwa wa njano kila kukicha," Kevin akaongea kimasihara.

Mimi na Miryam tukacheka kidogo, nami nikamwambia, "Haujaniona muda mrefu ndiyo maana."

"Ahah... dada habari?" Kevin akamsalimu Miryam.

"Salama. Za kwako?" Miryam akamjibu.

"Nzuri tu," jamaa akajibu.

"Mimi, huyu ni kaka mkubwa Kevin. Mume wake dada yangu. Kev, huyu ni Miryam. Mke wangu," nikamwambia hivyo.

"Ahaa... safi sana. Nimefurahi kukujua shemeji," Kevin akasema hivyo.

"Mimi pia Kevin. Hongera sana we' na Jasmine," Miryam akamwambia hivyo.

"Shukrani sana. Dah! Nina furaha sana leo!" Kevin akasema hivyo na kujishika kiunoni.

Sote tukacheka kidogo kwa pamoja, nami nikamwambia, "Si wapo huko ndani?

"Eeh, wote wapo."

"Wote? Na mabaunsa wako?"

"Ahahah... wapo eeh, utaratibu mzuri hapa, wako wamesinzia," Kevin akajibu.

"Mbona uko hapa sasa? Twende ndani," nikamwambia hivyo.

"Nilikuwepo humo, ndiyo nimetoka sasa hivi kumsubiria mama kwa hapa, yupo anapanda juu sasa hivi... ndiyo amefika hospitali," Kevin akasema.

"Ahaa, sawa," nikaelewa.

"Nyie ingieni tu, tunakuja," akatuambia.

Nikamshika begani na kusema, "Haya poa, ngoja tuwaone hao. Nitaanza kuwafinya mashavu mapema."

Tukacheka kidogo kwa pamoja, na ile ndiyo tunataka kuelekea huko chumbani, sauti nayoifahamu vizuri mno ikaita jina langu kutokea nyuma.

"Jayden!"

Miryam aligeuka, na hata Kevin akatazama nyuma yangu, lakini mimi sikugeuka upesi na kuendelea kutulia kama vile sijasikia kuitwa huko. Kisha nikawa nasikia sauti za hatua kwa viatu vya kuchuchumia ikija upande wangu, na sauti hiyo iliyoniita ilikuwa ya mwanamke.

Nikageuka hatimaye, nikiwa makini zaidi wakati huu, nami nikamwona mwanamke kijana niliyemtarajia. Mrefu kwa urefu uliofaa mwanamke, mweupe, mwenye macho ya kungu na midomo minene iliyopigwa lipstick nyekundu, akiwa amevalia kikoti cheupe kirefu kumtabulisha kuwa daktari, ambacho kilifunika gauni jeusi lililoishia magotini mwake. Miguu yake ilikuwa myeupe kweli, akivalia kiatu cha kuchuchumia chekundu, na alikuja upande wangu akiwa anatabasamu kiasi. Alikuwa na miondoko ya taratibu kwa njia ya mwanamitindo fulani hivi, akiwa ana shepu nzuri na mwili usio mnene ila ulionawiri vizuri tu, na alisukia nywele ndefu na laini za kizungu kichwani alizozibana juu ya kichwa chake.

Akaja mpaka karibu yangu, akiwa na kamtindo fulani hivi ka kuipiga-piga mikono yake pande za mapaja kwa kila hatua aliyopiga, na alikuwa akifuatwa na muuguzi wa kike mfupi-mfupi aliyevalia nguo za blue, akiwa amembebea vifaa fulani vya kihospitali, na huyu mwanamke daktari akafungua mikono yake kunielekea, kisha akanikumbatia kwa wororo kuwaonyesha wengine kuwa tulifahamiana. Sikutoa itikio lolote upesi zaidi ya kumwangalia Miryam usoni tu kutokea kwenye mgongo wa huyu mwanamke, na bibie alitutazama kwa utulivu tu, asiwe na longolongo lolote.

"Jamani wewe! Ahah... hata kama ndiyo kupotea, a-ah..." daktari huyu akasema hivyo.

Alikuwa na sauti laini, na alipenda kuongea taratibu kama vile anavuta kila neno alilotamka kwa makusudi.

"Anajua kweli kujichimbia," Kevin akasema hivyo.

"Yaani!" huyu daktari akamwambia hivyo.

Nikarudisha tu kumbatio lake kistaarabu, naye ndiyo akaniachia na kuniangalia usoni kwa hisia nzuri. Alinukia!

Akiwa ananiangalia kwa upendezi, akasema, "Umekuwa mbaba zaidi. Na unapendeza."

Nikajitahidi kutoa tabasamu kwa kujilazimisha tu.

Akamwangalia Miryam pembeni yake, halafu akamwambia, "Za saa hizi dada?"

"Salama tu. Za kwako?" Miryam akamjibu kwa utulivu.

"Ni nzuri," mwanamke huyu akamjibu Miryam hivyo, kisha akaniangalia kiudadisi na kuuliza, "Dada yako?"

"Mke wangu," nikamwambia hivyo kiuhakika.

Akapandisha nyusi kiasi kwa mtazamo wa kushangaa, naye akasema, "Wooow... okay."

Halafu akamwangalia Miryam usoni tena, ambaye alikuwa ametulia na akimtazama huyu daktari kwa njia makini kiasi.

"Hongera yako dada," akamwambia Miryam hivyo na kumpa mkono ili waitikise kufahamiana.

Miryam akakishika kiganja chake huyu daktari, akiwa ameanza kumwangalia kwa umakini sana.

Mwanamke huyo akamwambia, "Naitwa Stella."

Miryam akanitazama machoni kwa njia yenye utafakari kiasi, akiwa kama ananiomba nimhakikishie, na kwa jinsi ambavyo nilimwangalia, akawa ameupata huo uhakika. Hapo ndiyo alikuwa amekutana kwa mara ya kwanza na mama wa mtoto wangu, Stella!







★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★


Pata Full Story WhatsApp au inbox

Whatsapp +255 678 017 280

Karibuni sana
 
Stella anamtukana Jc kwa ndan 😁😁 kuwa unanikomoa
 
Kumbe Stella pisi kali hivyo Sasa huyo junior JC si ndo kabisa MR handsome of world,ahh we jamaa ni danger sana🫡🫡🫡
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…