Simulizi:The President and I(Mimi Na Rais)

Simulizi:The President and I(Mimi Na Rais)

The President And I(Mimi Na Rais) -Sehemu Ya Kumi Na Nane

'Confusion'

“Sikiliza mtangazaji, sisi kama taifa na ninarudia tena, sisi kama taifa hatuwezi na hatutakubali kuhadaika na utawala huu wa Rais Costa. Ajira zinazidi kuwa ngumu kwa vijana wetu, demokrasia inaminywa, magereza yameshajaa watu kwa makossa yasiyo na msingi, chaguzi zetu sasa hivi ni geresha tu kila kitu kinakuwa kimeshaamuliwa na Rais Costa. Katiba yetu sasa hivi inachezewa na kubadilishwa kadiri Rais Costa anavyojisikia achilia mbali hali mbaya ya madawa hospitalini na walimu mashuleni.

Hali ni tete, serikali hii imeharibu uchumi, sekta ya uwekezaji ipo hoi bin taabani. Wawekezaji wa nje na ndani wanakimbia. Wafanyabiashara wanahamisha mitaji na kwenda nchi jirani. Lakini akisimama majukwaani atakwambia uchumi unakua.

Wanapika takwimu hawa, uchumi wa Stanza ukiwa unakuwa kwa kasi sana ni asilimia 3-4 lakini kwenye vyombo vya Habari vya ndani na nje wanaripoti asilimia 9 hadi 10. Costa ameharibu uchumi wa nchi hii na itachukua miaka mingine ishirini kuja kuweka mambo sawa.

Mpaka leo mama zetu wanatembea umbali mrefu kutafuta maji halafu tunagereshwa kwa kujengewa vitu badala ya kustawisha watu na Jamii. Madai ya kujengewa na kununuliwa vitu ni eti ndio matumizi ya kodi zetu, ndugu zangu wanastanza hizo ni laghai tu za Rais Costa kujipenyezea hela za kujinunulia visiwa vya kitalii huko ughaibuni”. Alikuwa ni ndugu Julius Kibwe, kiongozi mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Stanza akizungumza wakati wa mahojiano katika kipindi cha Tarumbeta la Alasiri, kipindi cha Luninga kinachorushwa na stesheni ya MULIKA.

“Kibwe hilo la Rais kumiliki visiwa vya kitalii tuliache kwanza Mheshimiwa. Ha ha ha!” Mtangazaji alimkatisha Kibwe asiendelee kulitaja suala la Rais Costa kumiliki visiwa vya kitalii ughaibuni.

Alifanya hivyo kwa sababu ya maelekezo kutoka juu kwa wahariri wote wa vyombo vya habari. Maelekezo yale yaliyotolewa katika njia isiyo rasmi yaliwatisha wahariri wa vyombo vya habari karibu vyote vilivyopendelea kuandika habari za Julius Kibwe.

Wahariri wanne wa kampuni ya YETU SOTE inayochapa magazeti matatu yanayoongoza kwa kusomwa zaidi nchini Stanza ikiwamo ‘Stanza Today’ walisimamishwa kazi kwa muda na menejimenti ya Kampuni yao kwa madai kuwa wapishe uchunguzi wa tuhuma dhidi yao kuwa wanakula njama ili kuandika masuala yakayoidhalilisha serikali ya Rais Costa.

Pamoja na amri hiyo kutoka kwa Menejimenti ya kampuni hiyo, kiuhalisia ilitoka Ikulu ya Stanza ambapo maafisa wa usalama waliagizwa kuutishia uongozi wa kampuni hiyo kuwa ikiwa ungeendelea kuchapisha Habari dhidi ya Costa, basi kampuni hiyo ingefungiwa na magazeti yasingeendelea kuchapishwa tena.

Ili kukubaliana na matakwa hayo ya Costa, maafisa waliagiza kuwa menejimenti iwasimamishe wahariri walioonekana kuruhusu kuchapishwa kwa Habari zinazomdhalilisha Rais na kazi zake.

“Kwanini tusiliongelee. Kama ni pesa zetu zinatumika kwa manufaa binafsi ya Rais kwanini tusiliongelee?”, Julius Kibwe alisisitiza wakati kipindi kikiwa hewani

Wakati Kibwe akiwa anasisitiza kipindi kilitoka hewani na kuwekwa matangazo na wakati matangazo yale yakiendelea kulipita tangazo kwa chini kuwa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao kipindi kile kisingeweza tena kuendelea kuruka hewani.

Umma wa wafuatiliaji wa kipindi kile kinachopendwa sana kwa kurusha na kuchambua habari nzito za kitaifa walilalamika na kuanza kupata hamasa ya kwanini Kibwe amezuiwa kuelezea kashfa ile. Wengi walianza kuamini kuwa vyombo vya Habari vinaminywa ili kuficha uchafu na uovu unaofanywa na serikali ya Rais Costa.

Huku nyuma ya kamera katika studio za MULIKA kuliibuka mjadala mzito kati ya Julius Kibwe na wahariri kwanini wameamua kusitisha mahojiano yale. Walimweleza wazi kuwa tuhuma anazozitoa zinamuhusu kiongozi mkuu wa nchi na kuwa haiwezekani wamuache aendelee kumtuhumu bila kuwa na vielelezo pasi shaka.

Mkurugenzi wa Mulika alitoka ofisini kwake haraka na kuelekea studio ambapo Kibwe alikuwa akifanya mahojiano na mtangazaji. Kibwe alipomuona Mkurugenzi alimgeuzia kibao.

“Sasa ndugu Machege Marwa afadhali umekuja. Anayemtuhumu Rais ni mimi ama ninyi? Hapa ni sawa na kuninukuu tu kwani kuna kosa ninyi kuninukuu? Ninyi niachieni mimi hili suala kama ni kukamatwa nitakamatwa mimi na kuhojiwa nitoe ushahidi sio ninyi” Kibwe alikazia.

“Kibwe tunaelewa yote hayo lakini tunakuomba utumie majukwaa yako ya mitandao ya kijamii na mikutano ya hadhara kulisema hilo sisi hatutaweza kukuruhusu. Katika hili hapana” Mkurugenzi Mtendaji alimsisitiza.

“Mnaogopa.Amewafanya nini Costa?” Kibwe aliuliza kwa hasira huku akinyanyuka kwenye kiti tayari kuondoka. Wote walibaki kimya.

“I will take this matter to the parliament”, Kibwe alimalizia na kuanza kuagana na wenyeji wake ili aondoke.

Julius Kibwe alilidhamiria suala hili.
******************************************

“Shemeji yani huwezi amini nimetoka ofisini kwako tumepishana tu njia”, Gideon alikuwa akiongea na Sara alipokutana nae kwenye korido.

Sara alikuwa akiondoka baada ya kugusa mlango wa Gideon na kukuta umefungwa. Wakati yeye akiwa anamtafuta Gideon ofisini kwake na yeye Gideon alikuwa akimtafuta kwenye ofisi zake.

“Haya, ulikuwa unanitafuta kwa lipi shemeji yangu?”, Sara mke wa Rais Costa alimuuliza Gideon.

“Nina mambo mengi Sara, embu tuingie ofisini”, Gideon alimjibu Sara huku akifungua mlango na kuingia na Sara ofisini kwake.

“Kama nilivyokwambia shemeji kuwa nitatafuta ukweli wa suala la Costa kutaka kutalikiana na wewe na kumuoa Ketina. Sasa leo nimepata ‘shocking’ story kuwa anampa ubunge kwa kutumia zile nafasi zake tano za bure na labda atampa uwaziri”, Gideon alimwambia Sara huku akiwasha luninga iliyokuwa imetundikwa pale ofisini kwake.

“Kwa hiyo anamsogeza karibu? Hivi Costa ananijua ananisikia? Sara aliuliza kwa kebehi na ghadhabu.

Kabla Gideon hajajibu luninga iliwaka na habari ya Rais Costa kumteua Ketina kuwa mbunge ndiyo ilikuwa ikimaliziwa kusomwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu ya Stanza ndugu Alpha Wauwau.

“Hivi shemeji kumbe unayosema ni kweli?”, Sara alionekana kutoamini kilichokuwa mbele ya macho yake.

“Kwa hiyo shemeji mimi huwa unaona nakudanganya?”, Gideon alimjibu Sara katika muktadha wa kutaka aendelee kumuamini zaidi na zaidi.

“Ule mpango wa kumpindua alionituhumu kuhusika uliufuatilia? Ni wa kweli au ilikuwa tu namna ya kutaka kunipa tuhuma ili aniache? Kina nani wanahusika?”. Sara aliuliza maswali mfululizo. Na hapo alikuwa amekuja kwenye mtego Gideon aliotaka aingie.

“Sasa shemeji suala hili ni nyeti kidogo. Nimelifuatilia na nimeujua ukweli, ndiyo maana hata mimi nakusudia kujivua nafasi yangu kama mshauri wa Rais nirudi zangu Ulaya nikaendelee na mambo yangu maana nisingependa kugeuka kuwa adui wa ‘regime’ mpya”, Gideon alianza kidogo kidogo.

“Regime mpya? What do you mean? Kwani ni kina nani?”, Sara alihoji kwa shauku.

“Ni watu wengi kumbe wapo kwenye mpango huu, lakini kwa nilivyosikia taarifa zilizo chini ya kapeti ni kuwa wanakwama kwasababu hawajapata mtu ambaye yupo karibu Zaidi na Rais, hasa wewe. Inawezekana pia ndiyo sababu Costa anahofia kuwa wewe unahusika. Madai yapo kuwa wangependa uwasaidie na walipanga kwa kusaidia kumuondoa Costa wangekupa nafasi ya kugombea kama Makamu wa Rais katika Uchaguzi mkuu ujao.

Walipanga kuongea na wewe muda mrefu lakini waliingiwa hofu kuwa ingewezekana ukafikisha kwa Rais. Hapo ndo walipokwama. Taarifa hizi nimefikishiwa na watu ninaowaamini, na nimeanza kuziamini.

But anyway, I do not want to be at the middle of all this chaos, so whatever it is, it is nothing of my business, I am going to be abroad anyway.” Gideon alichombeza huku akijitoa kiaina katika mpango ule ili asije kufahamika na Sara moja kwa moja kabla ya kuthibitisha nia yake ya kutaka kushiriki mpango ule.

“Shemeji sikiliza, kuliko mimi kushuhudia Costa ananitaliki na kumuoa Ketina bora aondoke madarakani. Haya madaraka ndiyo yameanza kumpa kiburi. Kitu ambacho sitaweza kufanya ni kusaidia kumuua Costa, kwa sababu ni baba wa watoto wangu, lakini kama ni kuondoka madarakani tu na aondoke.

Siwezi kuvumilia fedheha ya kuachwa na kudhalilika. Unawafahamu wahusika? Nataka kuzungumza nao”, Sara alionekana kukerwa na kwenda moja kwa moja kwenye nia yake.

“Sasa mimi sifahamu kiongozi wao ni nani, lakini pia Sara huu ni mpango hatari. Nisingependa kuwa sehemu ya wanaotekeleza mapinduzi haya. Lakini nikimjua tu basi nitajenga nae mazoea na kukusemea wewe. Lakini shemeji nikuombe kitu kimoja suala hili ni nyeti na ni uhaini kwa mujibu wa katiba ya Stanza ya mwaka 1965, kwa hiyo isije ukajikoroga ukaropoka mbele ya Costa, itakuwa mwisho wa maisha yako, pengine hata na mimi’’ Gideon alijihami.

“Siwezi shemeji, hili ni suala lenye maslahi kwangu, kwako na hata kwa taifa letu. Kwanza nakushangaa unapojitoa na kutotaka kujiunga nao, kwanza usikute Costa amekutuma uniingize mtegoni”, Sara alimjibu Gideon.

‘’Hapana Sara, unafahamu uadilifu na utiifu wangu kwako kwa miaka mingi sasa. Nikutege ili ninufaike nini? Au nitaolewa na Costa baada ya wewe kuachana nae?’’

‘’Mmmh, sawa shemeji. Endelea kunihabarisha’’. Baada ya hapo Sara aliaga ili aondoke.

“Sasa ulikuwa unanitafuta kwa ajili ya nini shemeji?”, Gideon alimuuliza Sara baada ya kuona anaondoka bila kumwambia alikuwa anamtafuta kwa ajili gani.

“Shemeji nishasahau nikikumbuka nitakupigia simu”, Sara alimjibu Gideon akiwa mlangoni akiendelea kuondoka.
*****************************************

“Guys kuna jambo nitataka mnisaidie. Jambo hili niseme wazi sitawaambia lote lakini nitataka kila mtu anisaidie kile tu nitakachokuwa nimempangia na kumuomba. Kitu chenyewe kitakuwa ni nje ya kazi na kitakuwa kinakiuka miiko na maadili ya kijeshi hivyo nataka kusikia kauli kutoka kwenu kama mpo tayari kunisaidia au vinginevyo kabla sijasema lolote”, Meja Byabato aliuliza.

Kulipita ukimya wa kama dakika mbili hivi kila mmoja akishangazwa na kutafakari ni jambo gani Byabato alitaka kuwaagiza na kama wangekuwa tayari kutekeleza watakachoagizwa. Suala kuu lililowaumiza kichwa ni kauli kuwa jambo hilo linakwenda kinyume na miiko na viapo vya kazi zao.

“Niambie”, mmoja alijibu

“Kama na wewe mkuu upo kwenye hilo jambo mi sina shida”, Mwingine alidakia

“Linaweka maisha yetu rehani?”, Kingasi, mmoja wa wale vijana alihoji kwa tahadhari.

“Kazi yako tu yenyewe tayari ishaweka maisha yako rehani. Kinachokutisha ni nini?” Kijana Gwakata Msingazi, aliyekuwa wa kwanza kuitikia alimjibu Kingasi.

“Aaaah sijakusemesha wewe bwana mbona unazingua?”, Walianza kukoromeana.

“We kama unaona noma kumsaidia kufanya kazi na Meja toka nje. Sisi wengine huyu alituokota tukiwa kama Watoto wa mbwa yatima huko mtaani, alituleta jeshini, ametulea na kutufunza hadi tulipofikia hapa leo hii”, Walianza kulumbana.

“Guys, tulieni. Nataka jibu moja”, Byabato aliwatuliza. Walinyamaza

“Nipo tayari mkuu”, mmoja alijibu

“Fresh”, wa mwisho alimalizia.

“Ok. Najua ninyi ni wapiganaji na sio warushaji wa ndege hapa kwenye tawi letu hili la anga. Na nadhani mnajua yapo matawi mawili ya namna hii. Sasa basi, kuna jambo linaweza kutokea siku za usoni na nitataka ninyi mliopo hapa mnisaidie kulizima na kulizuia”, Meja aliongea kwa sauti ya chini lakini ya kuunguruma.

Alikuwa akiongea huku akiwatoea macho wale vijana wake wanne waliokiri utii kwake wa kumsaidia. Alikuwa akiwaambia huku akiwasoma saikolojia yao kama wanakubaliana nae kweli ama anaona woga kwenye macho yao. Kadiri alivyokuwa akiongea alikuwa akiona hawana shaka na hilo hivyo aliendelea.

“Nitaongea na mkuu wa kamandi nzima ya anga kuwa mgawanywe, wawili waende kambi ya milima ya Sempamba na wawili wabaki hapa. Kazi kubwa mtakayofanya ni kujenga urafiki na marubani wa ndege za first responders, hao ndio hasa nataka wakawe ‘target’ yenu. Kwa hiyo mkiwa kule marubani hawa ni lazima wawe marafiki zenu sana, huwa hawazidi watatu kwenye kila kambi kwa hiyo tunao kama sita hivi na ninyi mpo wanne.

Mtakachofanya kutokea leo na kuendelea bila mwisho mpaka hapo nitakapowaambia ni kufatilia nyendo zao. Siku yoyote kuanzia sasa kunaweza kutokea lolote na hivyo first responders wakahitajika kuzuia kwa amri kutoka juu. Mimi nitawapa taarifa na ninyi mtakuwa na kazi ya kuwadhibiti wasirushe hizo ndege. “Meja aliwaambia.

Jeshi la Stanza, kikosi cha anga (Air Wing) kina kambi mbili kubwa, moja ipo jiji kuu la Stanza Peron na nyingine ipo milima ya Sempamba. Kutokana na utaratibu wao wa kijeshi wa kuingia kwenye mapigano ambao wao huuita kwa kimombo ‘Atacking Protocal’, huwa wamegawanyika katika makundi matatu.

Kundi la kwanza huitwa first responders, hizi ni ndege za kivita zinazotumwa eneo la tukio kwa sababu kuu mbili, moja yaweza kuwa kuweka hali ya usalama ama kumpa onyo adui kuwa amezungukwa na hivyo ajisalimishe au aache anachotaka kukifanya. Sababu ya pili yaweza kuwa jeshi la nchi kavu limeelemewa na hivyo linahitaji msaada wa jeshi la anga hivyo ndege hizi huja kwa ajili ya kusaidia wale walio chini.

Kundi la pili ni lile waliloliita ‘second deployment’, hizi ni ndege kubwa kidogo na huja na wanajeshi wengi zaidi na silaha zake pia ni nzito kiasi. Ndege hizi haziwezi kupelekwa mahala bila kujiridhisha kuwa zile za first responders zimeshindwa kurudisha hali ya usalama eneo la tukio.

Kundi la tatu na la mwisho waliliita ‘total destruction’, hizi ni ndege kubwa zaidi ya kundi la kwanza na la pili na mara nyingi hazipelekwi eneo la tukio kama bado askari wao wapo hapo, kwa hivyo askari wote huambiwa wakimbie ama kutoka eneo hilo halafu ndio hizi ndege zinaingia.

Sababu ni moja tu, kama lilivyo jina lake zikifika eneo la tukio zinakuwa na lengo moja tu, kuangamiza kila kilichopo ikiwamo maadui, yaani ‘non-discriminatory bombings. Adui ni ngumu kukwepa pigo la hizi ndege. Hubeba silaha nzito sana za maangamizi.

“Boss, kwani ni issue gani hiyo mbona kama unaonekana ni mpango muovu sana. Kuzuia first responders kurusha ndege katika hali wanayotakiwa kurusha unajua ni hatari sana”, Kabasa alihoji.

“Hakutakuwa na hatari na ndiyo maana nimesema hutakiwi kuzuia tu ni mpaka niwe nimewaambieni maana kutakuwa na sababu maalumu”, Meja alijibu

“Ni issue gani?”, mmoja alikazania aambiwe.

“Siwezi kuwaambia kwasasa nitakapofanikisha suala la kuwahamisha wawili waende kambi ya pili nitakuwa nikiwasiliana nanyi kwa utaratibu maalumu. Ila niseme mpaka kufikia hapa mmeshakula yamini. Yeyote atakayetoa siri hii basi amejiapiza kufa. Tunakubaliana hilo?” Meja aliongea kwa msisitizo.

“Yes Kamanda” wote walijibu kikakamavu ishara ya kukubali amri na kiapo cha utiifu.

“Vipi hiyo misheni ikifeli si ndo tunauawa sasa mkuu?”, Gwakata alichombeza akiwa ameshafikiria mwisho kutokana na njia watakayopita.

“Kwanza ikifanikiwa muwe na uhakika wa kupanda vyeo kwa kasi ya ajabu, nawahakikishia. Ila ikishindikana kama ulivyosema ni mawili ni aidha utokomee kusikojulikana ama utauawa. Lakini nitashangaa sana kama mtafanya misheni hii kijinga namna hiyo mpaka mjulikane. Kama mtu ataona hajui namna gani afanye bila kugundulika basi tutawasiliana”, Meja aliamua kusema ukweli

Meja aliwashukuru na walikumbatiana na kuagana. Kila mmoja alitoka kimya bila kuongea na mwenzake. Maswali yalikuwa mengi yaliyokosa majibu. Mambo yalikuwa mengi muda ni mchache.
***********************************

Mara baada ya Sara kuondoka, Gideon alipumua kwa pumzi nzito. Aliona ni kama ametekeleza sehemu kubwa ya mtihani aliokuwa nao wa kuhakikisha Sara anaigia kwenye mstari.

Haraka aliingia kwenye game na kumpa taarifa zote Joe ili asikie ni hatua gani anatakiwa kuendelea nayo. Ilikuwa ni muhimu sana kwa Gideon kusikiliza ushauri wa Joe kwa sababu ramani nzima alikuwa nayo Joe na Macha na kuwa yeye alikuwa kati kama kiungo mchezaji.

Alihakikisha jumbe zile zimemfikia Joe na yeye alianza kurekebisha ile barua ya majibu ya Rais Costa kwa Rais Chriss wa Marekani.
****************************************

“Mh. Rais nilitaka nikufikishie taarifa hizo. Watu uliowaweka karibu yako, ndiyo watu watakaokufitini na kukuangusha. Inavyoonekana mpango huu ulisukwa kwa umaridadi ili kukugombanisha na watu wako wa karibu uliowaamini na kuchomeka watu wengine ili watengeneze mazingira ya kukupindua Mh Rais, Stanley Macha aliendelea kuongea kwa taabu.

“Umenitesa, umeniumiza pasi kutaka kunisikiliza lakini kwasababu mimi bado nina mapenzi ya kweli kwa taifa langu na utiifu kwako Mh Rais, nimeona bado ninalo jukumu la kukusaidia” Aliendelea kuongea kwa kuanza kumtengeneza Rais Costa kisaikolojia.

Maongezi ya Macha yalianza kuteka hisia za Rais Costa. Alianza kujiona mkosaji kwa kumtesa Macha bila hata kutaka kumsikiliza.

“Mpango wa kukupindua ni ukweli upo wahusika uliowasikia ni hakika tena wapo na wengine ambao nimeona leo nikutajie maana wapo karibu na wewe na kamwe bila kuwadhibiti mapema hutaweza kuwashinda. Mimi niliamua kuwaaminisha kuwa ni sehemu yao ili kuwadhibiti. Kwa bahati mbaya, walio na nia mbaya wamekufanya uamini kuwa mimi ndiye adui, lakini hukusikiliza upande wangu wa hadithi.

Costa, unakumbuka ni mimi niliyezuia jaribio la kwanza la jeshi kutaka kukupindua? Kwanini unahisi kuwa sikushiriki kukamilisha mapinduzi wakati ule ambao nafasi ilikuwa wazi kukuondoa? Macha alisema maneno yaliyomuacha Costa njiapanda.

Lakiki pia maneno yake yalizidi kumtia simanzi Rais Costa, alianza kufikiri pengine Macha hahusiki na hakupaswa kupitia mateso yote yale bila kuwa na hatia. Wanaomfahamu Costa wanajua kuwa ni Rais anayeendeshwa kwa kila aina ya hisia; hasira, furaha, huruma na ukatili.

Na kwa wakati wote, maamuzi yake mengi yalifanyika kwa hisia kuliko mantiki au hata sheria. Alikuwa ni kiongozi aliyejawa na hisia kuliko ufikiri, na watu waliomzunguka na kumfahamu kwa muda mrefu kama Macha walikuwa wanajua jinsi ya kumuingia kwa kucheza na hisia zake.

Ni kitu kibaya sana watu wanaokuzunguka wakikujua unaendeshwa na hisia badala ya kufikiri na mantiki. Hisia ni rahisi kuchezewa lakini ni ngumu kuchezea ufikiri wa mtu.

“Nitajie ni nani anahusika Macha, nitajie ikiwa unataka niamini kuwa wewe huhusiki na mpango huu.’’, Rais Costa wakati huu alionekana kuanza kumuamini Macha na kutaka kumsikiliza.

Macha alikaa kimya kwa muda kidogo kisha akamjibu Rais Costa kwa ufupi, “Gideon…Gideon anahusika na anawafahamu wahusika wengine wote”, Macha alitamka.

Rais Costa alisimama kutoka katika kiti alichokaa kwa mshtuko na kusogea nyuma hatua mbili kutoka kiti kilipo.

Maafisa usalama waliokuwa wanafuatilia muenendo wa kimatendo ndani ya chumba kile, ingawa hawakusikia kilichoongelewa walifungua mlango kwa haraka wakifikiri kuwa Macha amemdhuru Rais Costa.

Walipomkaribia Rais Costa alinyoosha mkono wake juu kidogo kuwataarifu kwa ishara kuwa hakuna lililoharibika na mambo yalikuwa shwari. Costa aliendelea kumuangalia Macha bila kuamini kile alichosikia masikioni mwake.

‘’Gideon!!!!……son of a bitch. I had my reservations about him’’, Costa aliongea kwa sauti ya chini lakini iliyojaa ghadhabu kuu na kuanza kuondoka mule chumbani bila hata kumuaga Macha.
*********************************************
Mambo Yameanza Kuwa 'Varangati'. Nini Kitaendelea Katika Simulizi Hii Ya Kusisimua? Tukutane Wiki Ijayo.

the Legend☆
 
Back
Top Bottom