The President And I(Mimi Na Rais)- Sehemu Ya Kumi Na Tisa
Misheni Imevurugika
Gideon alikuwa kwenye ofisi yake akiendelea kuandaa ile barua ya majibu ya Rais Costa kwa Rais Chriss wa Marekani. Alikuwa akiweka sawa yale marekebisho aliyopewa na Rais Costa ili ikae kama Rais Costa anavyotaka. Hakuwa na wasiwasi wala kuelewa kinachoendelea. Hakujua kama Macha anaweza kumtaja moja kwa moja kwa Rais Costa.
Gideon alikuwa kama kiungo aliyewekwa kati na Joe na Macha, yeye alikuwa akitumika tu na wala hakuwa akiujua mpango kamili umekaaje na unaendaje. Joe na Macha pia waliaminiana tu hakuna aliekuwa akijua nia au dhumuni la dhati la mwenzake kushiriki mpango ule. Walikuwa wakijua dhumuni la pamoja tu kuwa wanaitaka Stanza mpya lakini nini kimewasukuma haswa waitake Stanza mpya hilo kila mmoja alibaki nalo moyoni mwake.
Ukweli ni kwamba mbali ya Joe kuitaka Stanza mpya kilichomsukuma zaidi ni hasira na kisasi kwa mambo aliyotendewa na Rais Costa. Hivyo kwake yeye hata kama Stanza mpya isipopatikana ilikuwa ni lazima Rais Costa ang’oke kwa njia yoyote ile, japo kama mwanadiplomasia mbobezi alitamani itokee bila umwagaji damu.
Yeye Macha alibaki kuwa fumbo, mbali ya nia ya pamoja hakuna aliejua kinachomsukuma kwa hakika na kama kweli alikuwa na nia ya dhati ya kumng’oa Rais Costa ama alikuwa kazini. Watu wa usalama wa Stanza ni hatari sana.
Gideon akiwa amekaa anamalizia kuandaa yale majibu ya Rais Costa akili ilimtuma kuwasiliana na Meja Byabato. Aligundua kuwa tangu alipofanikiwa kumpa ile ‘code’ ya Sienta-Go hajawahi kumrudia kumuuliza nini kinaendelea. Alishika simu yake ya mkononi na kumpigia.
“Meja, salama mkuu?”, Gideon alimsalimia meja Byabato
“Gideon, salama hapa kweli? Meja alimjibu Gideon akionyesha wasiwasi wake wa njia aliyotumia Gideon kuwasiliana nae.
“It’s a secure line Meja” Gideon alimtoa wasiwasi
“It all depends it is secure to whom’’. Please, let us meet in person as we did last time” (Inategemea ni salama kwa nani. Tafadhali tuonane uso kwa uso kama tulivyofanya mara ya mwisho). Meja alimjibu Gideon na kukata ile simu.
Gideon aliingia kwenye mtandao wa WhatsApp na kumuuliza Meja waonane wapi. Meja Byabato alimtajia eneo na walikubalina wakutane usiku wa saa mbili eneo hilo wapate kinywaji na kujadili mawili matatu.
****************************************
Joe na Habibu walikuwa bado nchini China katika jiji la Beijing. Waliishi eneo la Beixinqiao. Eneo hili lipo katikati ya mtaa wa Yonghegong na Dongzhimen. Ni eneo liliojaa migahawa mingi, baa na viwanda vya bia lakini pia ni eneo linalokaliwa na wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali waliopo China kikazi.
Habibu alijitahidi sana kumdodosa Joe ni kwa namna gani alipata chumba kile walichokuwa wakikaa kwasababu hata hati zao za kusafiria zilishaisha muda wa wao kuwa nchini China. Isitoshe wao walikuwa wakitumia hati za kusafiria za kidiplomasia na ukweli walipo hata ubalozi wa Stanza nchini China haufahamu.
Habibu alijitahidi kumwelewesha Joe kuwa kwa wakati huo kama ubalozi wa Stanza utakuwa umetoa taarifa kwa serikali ya China basi watakuwa wapo hatarini lakini pia alitaka aambiwe nini kinaendelea na wataishi maisha hayo kama ya digidigi mpaka lini. Maisha ya kujifungia ndani muda wote bila uhuru yalianza kumchosha Balozi Habibu.
Muda mwingi Joe alionekana akiwa ‘busy’ na simu akifanya mawasiliano ya hapa na pale akipata taarifa na mirejesho kutoka kwa Gideon lakini pia akiwasiliana na mkewe Elizabeth huku akifuatilia kwa ukaribu taarifa za habari za ulimwengu.
“Habibu mdogo wangu, nimeanza kuwa balozi kwa kuiwakilisha Stanza miaka kumi kabla ya wewe kupewa ubalozi. Najua taratibu za kidiplomasia, nyumba hizi tunazokaa si vyema sana nikakwambia ninazipataje kwasasa lakini fahamu kuwa kabla ya mimi kuhamishwa ubalozi na kwenda kuiwakilisha Stanza nchini Urusi, nilishakaa hapa China kwa miaka saba.
Hiyo itoshe kukuonyesha kuwa hapa tulipo, kwangu ni sawa na Stanza. Nina marafiki, nina ‘connections’ hivyo toa mashaka. Jambo la pili mdogo wangu ni kuwa nimefuatilia kutoka kwa watu wangu wa karibu hapa China wamenihakikishia kuwa Stanza wala Balozi Kimweri hajapeleka shauri lolote kwa serikali ya China ya sisi kutafutwa la sivyo tungeshakuwa tumekamatwa. Unadhani jambo hilo linaashiria nini?”, Joe alimalizia kwa kumuuliza Habibu.
“Maana yake Rais Costa anataka kutumaliza kimya kimya”, Habibu alijibu.
“Exactly, na ndio maana nataka uwe na moyo wa ushujaa. Tumekaribia kuimaliza safari japo bado siuoni mwanga. Nilikuuliza kama unataka tukusalimishe kwa Rais Costa kama mwenzako Pius ukakataa sasa, hang in there. We will be fine’’. Joe alimalizia kumpa risala fupi Habibu.
Walimalizia kuzungumza na walikubaliana watoke waelekee kwenye baa ya jirani ili kwenda kupata bia mbili tatu.
*****************************************
Bwana Zhang Wei na Bibi Whang Xiu Ying ni raia wa China. Ni moja ya wafanyabishara wakubwa wa China wenye kampuni zao na biashara zao nyingi barani Africa. Kuanzia miaka ya 2000 wakati China alipoamua kwa dhamira moja kuingia kwa nguvu na kuwekeza kwenye bara la Africa, Zhang na Whang walikuwa ni wafanyabiashara wa awali kabisa kuanza kuwekeza sana nchini Stanza.
Zhang aliwekeza zaidi kwenye viwanda vya kusindika matunda ili kutengeneza juisi, viwanda vya nyuzi na mbolea. Bi Whang yeye aliwekeza zaidi kwenye teknolojia na miundombinu na kwa hakika walitajirika vilivyo kutokana na uwekezaji huo kwenye nchi nyingi za Afrika hasa Stanza.
Wakati maazimio ya China kuingia Africa chini ya utawala wa Rais wa China Kamaradi Hu Jintao yakiafikiwa miaka ya 2003, Joe alikuwa ni Afisa wa ubalozi wa Stanza nchini China. Stanza ikiwa chini ya utawala wa Rais Jonathan Edward ilikuwa na hofu ya kuwakubali Wachina sawa na nchi nyingi za Afrika.
Japo ni ukweli kwamba mahusiano ya China na nchi za kiafrika yana mizizi mirefu ya enzi lakini propaganda za nchi za kimagharibi zikiongozwa na Marekani ambayo kwa wakati huo ndiye alikuwa mshirika mkubwa wa kibiashara na Afrika zilisababisha viongozi wengi wa nchi za Afrika kuingiwa na hofu na ujio wa China kwa kuhofia kupoteza urafiki na Marekani.
Joe akiwa afisa mdogo wa ubalozi wa Stanza huko China alichangia pakubwa kufanikisha Zhang na Whang wanapata fursa ya kuwekeza nchini Stanza. Ni Joe pia alishiriki kama kiungo muhimu wa kumsaidia aliyekuwa balozi wa Stanza nchini China wakati ule ndugu Benson Rwengereza kutengeneza daraja zuri la kuhakikisha China inaingia Stanza na kuwekeza na hivyo kuleta manufaa kwa Wanastanza.
Ni katika mahusiano hayo ya Zhang na Whang waliendelea kuwa marafiki wakubwa wa Joe kiasi kwamba ilifikia hatua hawakuwa tayari kumuona Joe akipata shida kwani alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio yao.
Baada ya sakata la Pius kusaliti kambi ya Joe, ilibidi awasiliane na marafiki zake hawa. Aliwaeleza kuwa yupo nchini China kwa muda kidogo kwa mambo ya kidiplomasia na masomo hivyo aliwaomba wamsaidie nyumba ya kuishi kwa mwezi mmoja mpaka mitatu.
Wafanyabiashara hawa walikuwa na nyumba nyingi katika miji tofauti tofauti. Nyumba hizi zilikuwa za kibiashara hivyo ombi la Joe lilikuwa ni dogo sana kwao. Walimruhusu kukaa na kumwambia popote watakapokuwa wanakwenda kama kuna nyumba zao basi watakuwa tayari kumpa makazi Joe.
Isitoshe, walikuwa wakigharamia chakula na huduma zote ambazo Joe alikuwa akihitaji. Joe alishawasababishia utajiri mkubwa na wao walikuwa wakimwambia kwa kichina Wǒmen méiyǒu shé me kěyǐ huíbào nǐ de yaani hawana cha kumlipa Joe.
*********************************************
Rais Costa alisikia kuchanganyikiwa alipotajiwa kuwa Gideon anahusika kwenye mpango wa kumpindua. Alishindwa kuelewa inakuwaje mtu anaemwamini kiasi kile anaweza kuwa anapanga njama kama zile. Lakini alianza kuunganisha nukta baada ya kukumbuka suala la Meshack kumvamia Sylvanus. Akipata jibu ni nani atakuwa amewasiliana na Meshack, alimwamini Macha. Rais Costa alitaka kutoka kwa hasira.
“Costa unakwenda wapi”, Macha alimwita Rais Costa kwa jina lake bila kutanguliza heshima yoyote.
“Huyu mshenzi Gideon hawezi kunichezea namna hii”, Costa alijibu huku akibonyesha kitufe kinachowapa ishara vijana kuwa wafungue mlango anataka kutoka.
“Sylvester, unarudia kosa lilelile ulilonitendea mimi, kutaka kuchukua maamuzi bila kutafakari”, Macha alimwambia Rais Costa.
“Macha usinitukane, I am your president! Ina maana Stanza inaongozwa na kichaa? Unaniambiaje nafanya maamuzi bila kutafakari?”, Rais Costa alimfokea Macha.
“Samahani Mheshimiwa Rais lakini nakuomba uketi sijamaliza kukwambia ninayotaka kukwambia”, Macha aliomba radhi. Alikumbuka kuwa anaongea na mkuu wa nchi hivyo alipaswa kuongea nae kwa nidhamu.
“Mh. Rais, Gideon ni kiungo tu wa mpango huu ambaye nilikwishamng’amua lakini wapo wengine, nina uhakika na kama nilivyoshughulikia suala la jeshi kutaka kukupindua na kuhakikisha ninang’oa mpaka mizizi suala hili pia latakiwa kushughulikiwa hivyo kwasababu bado wewe na mimi hatujui limejichimbia mizizi kiasi gani.
Masuala haya kwa sisi watu wa usalama tunashauri usiyapeleke kwa pupa, ni mambo nyeti na pengine yamepangwa kiustadi na labda hata kuna mkono wa nje. Gideon si mtu wa kumchukulia hatua bali ni mtu anayepaswa kutufanya tuwajue wengine kwenye mpango huu’’, Macha alipumzika na kumeza mate.
Wakai Macha akiongea Rais Costa alikuwa akimkodolea macho kwa umakini huku akitafakari mambo mengi. Alikuwa akiunganisha nukta kichwani lakini ni kama muunganiko ulikuja na kukata, yaani tungeseama alikuwa akiwaza maruweruwe kwasababu ya taarifa nyingi na mchanganyiko anazoendelea kupokea kuhusu jaribio la mapinduzi.
Hoja ya Macha kutaka kujua mzizi wote wa wanaotaka kumpindua ilimwingia, hoja ya kutomgusa Gideon alisita kidogo. Hoja ya Gideon kuhusika nayo ilikuwa ikisumbua kukubalika kweye ubongo wake lakini akikumbuka suala la Meshack ni kama anaielewa hoja ile. Hakika alianza kutoka jasho pasi kujijua.
“Umejuaje kama Gideon anahusika, mbona ni yeye aliyeomba mimi kuonana na wewe?” Rais Costa alihoji.
“Hajui kama mimi najua na imekuwa vyema kuwa hivi, lakini hivi karibuni utafahamu kwanini anahusika”, Macha alijibu.
“Siyo kwamba siamini, naamini sana kwa sababu hivi ninavyoongea na wewe yule kijana wako Meshack amemvamia Sylvanus tuliyemtuma kwenda kumdhibiti Joe na hakuna aliyekuwa anajua mwingine zaidi yangu na Sabinas isipokuwa siku nilipokuwa ninasaini ile ruhusa ya Joe kuuawa Gideon alikuwepo ingawa sina hakika kama aliona, hivyo bado napata shaka sana”, Rais Costa alifunguka mazima kwa Macha.
“Meshack alifanikiwa kumdhibiti Sylvanus?”, Macha alihoji ili apate kujua nini kiliendelea kwa kuwa habari hiyo hakuwa ameipata.
“Nadhani Sylvanus alimuua Meshack japo bado sijapata taarifa sawasawa”, Costa alijibu.
Macha aliposikia juu ya uwezekano wa Meshack kuwa ameuawa alishtuka kwa ndani ndani. Aliumia sana. Meshack alikuwa ni kijana mwaminifu na kipenzi wa Macha, na ikiwa ni kweli ameuawa basi ni wazi ni pigo kwa kambi yao ya mapinduzi.
“Ndiyo maana nakushauri Mh. Rais utulie nilishughulikie hili suala mpaka mwishowe. Ni wazi basi hata Meshack alikuwa akihusika na sasa nadhani unanielewa ninavyosema mpango huu ni mkubwa. Sabinasi peke yake kamwe hawezi kuujua kwa undani na kwa haraka kama mimi niliyekwishaanza kuufatilia”, Macha aliongea kwa shida maana mdomo wake ulikuwa umevimba.
“Macha sitaweza kukaa na kutazamana na Gideon. Sitaweza”, Rais Costa alijibu kwa hasira.
“Hata mimi sikutaka nikushauri hivyo. Ipo Sehemu nzuri ya kumuweka Gideon ambayo nitapata nafasi ya kufuatilia nyendo zake kwa ukaribu”, Macha alimwambia Rais Costa.
“Wapi Macha? Wapi nimuweke ambapo sitapata hasira kila nimwonapo na uniambie ni baada ya muda gani utakuwa umeweza kugundua wahusika wote ili niwachukulie hatua” Rais alihoji kwa hasira.
“Gideon ni mbobevu wa masuala ya Sayansi ya Siasa ni mtu mwenye weledi sana wa uongozi, mimi nilikuwa nadhani mteue awe Katibu Mkuu wa Chama chetu cha Ukombozi Stanza. Kwa uchapakazi wake huko atakusaidia sana kuleta mapinduzi na wanachama wa kutosha nadhani unajua mipango mikakati yake kisiasa Mh. Rais”, Macha alishauri.
“Unasema nini wewe? Yani mtu anaepanga kunipindua nikampe utendaji mkuu wa chama?”, Rais Costa aling’aka.
“Mh. Rais kwenye chama kuna viongozi wengi na hawezi kufanya lolote la ajabu. Lengo langu la kukwambia umpeleke kule ni mawili. Mosi, nataka umtoe karibu na serikali ili kama kuna watu huku anaoshirikiana nao akose muunganiko nao, lakini pia kama wataendelea kuwasiliana basi watakuwa wakitumia simu ambazo mimi nitaanza mchakato wa kuzifuatilia. Sababu ya pili ni kutaka asione ametupwa nje na hivyo kukatisha mpango ama kumwachia mtu mwingine ambaye itanichukua muda kumtambua hivyo nataka ajione ni sehemu ya utawala wako mpaka pale tutakapomaliza kuwajua washiriki wote.
"Wewe una uwezo wa kuteua leo na kutengua kesho, una wasiwasi gani?”. Macha alisisitiza
Rais Costa alibaki kama dakika mbili akimtazama tu usoni Macha. Hesabu zilikuwa zikikataa kubalansi lakini alikuwa hana namna. Kwake Macha alikuwa ni mkweli kwa wakati huo.
Walizungumza na kukubaliana mengi na Macha. Macha alimwambia Rais Costa hataki kurudia nafasi yake ya Ukurugenzi wa Idara na hivyo amruhusu Sabinasi aendelee ila yeye ataimaliza hiyo kazi maalumu ya kuhakikisha anawaweka hatiani wote wanaoshiri kwenye mpango wa kumpindua Rais Costa kisha atastaafu. Aliomba kijana wake Daudi wa mambo ya mawasiliano nae aachiwe huru na kutaka wapewe ruhusa ya kufikia baadhi ya vitu ili vimrahisishie kazi.
Rais Costa alikuwa ni mtu rahisi kujazwa upepo na kujaa, alitawaliwa na hisia kuliko mantiki na hivyo alikubaliana na Macha kwa yote. Alisikitika sana kwa kitendo chake cha kumtesa bila kumsikiliza. Alimbembeleza pia kama akitaka aendelee na Ukurugenzi wa Idara aseme lakini Macha alishauri kuwa wakati wake wa kutumikia nafasi hiyo umefikia kikomo.
Alimwambia kwa yaliyotokea anawachia tu wadogo waendeleze gurudumu na kuwa kazi hiyo ya kumuweka Joe, Gideon na wengine wote wanaohusika na mpango ule haramu itakuwa kazi yake ya mwisho, ama kwenye lugha ya kigeni wanasema ‘Last assignment’.
Rais Costa alitoa ishara kuwa mlango ufunguliwe na alitoka akiambatana na Macha wakitembea taratibu kuelekea nje. Kagiza kalikuwa kameanza kuingia kwa mbali.
“Pius anaendeleaje? Amesharejea?”. Macha alimuuliza Rais Costa.
“Yes, infact we had a discussion with him and General Ndutta that shortly, he will succeed Ndutta as our new CDF” (Ndio tena nilikuwa na mazungumzo nae yeye na Jenerali Ndutta kuwa wiki chache zijazo nitamteua Pius kama mkuu wetu wa majeshi ya ulinzi na usalama kurithi mikoba ya Ndutta) Rais Costa alimjibu Macha.
“Ni jambo sahihi. Pius ameonyesha uaminifu mkubwa. Angeweza kukubaliana na Joe na kazi ingekuwa kubwa zaidi. Kwa hivyo ni lini utamtangaza”, Macha alihoji.
“Well, I told General Ndutta when he is comfortable, and transition plan is in place they will let me know. I did not want him to feel that this is a forced retirement. He served this country with honor and loyalty and he deserve to be treated as such”
(Nilimwambia Jenerali Ndutta siku akiwa tayari ataniambia. Unajua sikutaka aone kana kwamba ninamlazimisha astaafu. Ameitumikia nchi hii kwa mapenzi na uaminifu mkubwa na anapaswa kufanyiwa hivyo), Rais Costa alimjibu Macha huku wakiwa wamefika mlango wa kutokea nje.
Wakiwa wanasindikizwa na Sabinasi pamoja na walinzi wa Rais walikuta tayari msafara wa Rais umeshajipanga tayari kwa kuondoka.
“Sabinas, Macha amerudi kwa kazi maalumu. Tafadhali mpe ushirikiano wowote atakaohitaji”, Rais Costa alikuwa akimpa maelezo Sabinas Paulo anayekaimu nafasi ya Macha kwa wakati huo katika Idara ya Usalama wa Taifa Stanza.
“Sawa mkuu. Ni bosi wangu bado huyu. Ha ha ha!” Sabinas aliitikia kwa kujichekesha kinafiki.
Macha alimkata jicho la chini chini kwani alijua fika kicheko kile ni cha kinafiki mbele ya Rais.
Rais Costa aliagana na wote na kuingia kwenye gari na kuondoka kurudi Ikulu ya Stanza pale jiji la Peron
*****************************************
Jioni ya siku hiyo kama walivyokubaliana Gideon na Meja Byabato walitafutana ili waonane na kuongea.
“Meja hebu niambie kinachoendelea kwa upande wako maana mimi nipo tu kati kati natoa taarifa huku napeleka huku sasa hali hii siipendelei sana. Nataka kujua kinachoendelea kila upande”
“Gidi mbona mimi sikuwa najua kama wewe ndio utaniletea ile code? Mambo haya huenda kwa namna hii, unachotakiwa kufanya ni kutimiza wajibu wako na kumwachia mwingine atimize wake. Wewe hujasomea masuala haya ya usalama lakini ni kitu cha kawaida kabisa hiki”
“Sawa Meja naelewa lakini sasa nisichoelewa ni kama tunakaribia mwisho, tupo katikati ama tumeshashindwa kwa sababu unakuwa huelewi nini kinaendelea wapi”
“Hilo lisikusumbue kichwa Gidi. We fahamu kuwa nilichotumwa nimeanza kukitekeleza. Mambo haya hufanyika hivi ili kuzuia kama kuna anaetaka kuharibu ama kuwachomea wenzake asipate ushahidi ama kuzuia mpango mzima. Mfano mimi nilikuwa namjua Macha tu na nimekujua na wewe kwa sababu umeniletea lile neno la siri. Hivi ndivyo hutakiwa mambo kuwa tunakwenda kwa alama, ishara na maneno ya siri”
“Sasa kwa mtindo huu nitashindwa kukuuliza nilichotaka kukuuliza Meja”
“Jambo gani Gidi? Niulize”
“Yule kijana aliekuwa akimlinda ‘Eagle’ inasemakana ameuawa, sasa natafuta wa kunihakikishia taarifa hizo nakosa”
“Vijana wengi wanamlinda ‘Eagle’, nawajua baadhi maana sipo sana huko kwenye mambo ya Idara ya Usalama sasa sijajua unamwongelea nani”
“Kuna yule alikuwa mrefu hivi kama wewe mweusi karibu mfanane weusi. Ha ha ha”
“Unamaanisha Meshack?” Meja Byabato alihoji.
“Huyo huyo. Nimesikia ameuawa sasa sijaelewa kwenye mazingira gani na sijui nimuulize nani, mimi na Sabinasi hatuelewani kabisa hivyo siwezi kumuuliza suala lolote”, Gidieon alimwambia Meja Byabato.
“Ameuawa? Kauawaje tena…ngoja nimuulize huyu…” Meja Byabato alihoji kwa kushangaa huku akitoa simu yake ya mkononi na kuanza kumpigia mtu ambae Gideon hakumfahamu.
Eagle ni neno wanalotumia watu wa usalama kumuita Rais Costa. Meja Byabato japo hakuwa akijua mengi ama kujuana na wengi katika idara ya usalama wa Taifa Stanza lakini kutokana na urafiki wake na Stanley Macha aliweza kujuana na wachache, Meshack akiwa mmojawapo.
“Kwa hiyo unasema mwili wake haukuonekana pale Casino? Sasa hapakuwa na Camera kule vyooni?..........Aisee basi sasa endelea kufatilia, utanijuza kamanda huyu kijana wetu bwana si unajua tena sisi watu wa mazoezi vijana kama hawa ndio wetu hawa” Meja Byabato alimaliza kuongea na ile simu.
“Ni kuwa ninasikia Meshack alipambana na kijana anaitwa Sylvanus huko Casino sasa inavyoonekana alishindwa nguvu na Sylvanus alitoa taarifa kuwa amemuaa lakini sasa wao walipofika pale hawakuukuta mwili wa Meshack hivi wanafatilia upo wapi na wameshikilia uongozi wa ile Casino”, Meja Byabato alikuwa akimpa mrejesho Gideon.
Gideon alianza kupatwa mashaka sana juu ya nini kimempata Meshack. Je yupo hai, amekufa ama nani aliuwahi mwili wake na kuupeleka wapi. Hakutaka kuuliza mengi waliongea na Meja kwa muda mchache kisha waliagana.
****************************************
Rais Costa aliingia Ikulu ya Peron akiwa na mawazo mengi sana. Alikuwa kwa hakika haelewi nini kinaendelea kwenye utawala wake, alikuwa hana hakika amuamini nani. Alikuwa akitembea kwenye korido za Ikulu akielekea kwenye makazi yake huku akisindikizwa na walinzi wawili.
Akiwa anapiga hatua simu yake ya mkononi iliita na alikuwa ni Sabinas Paulo akipiga.
“Mh. Rais nimejikaza lakini nimeshindwa nimeona nami niwahi kukupa tahadhari kabla hujatekeleza jambo lolote”, Sabinas alianza maongezi.
“Unasema nini Sabinas?”, Rais Costa aliuliza kwa wasiwasi.
“Kwanza unisamehe kwa kukiuka utaratibu na kuwa nasikiliza maongezi yako na Macha ya faragha. Ila nimeona uongo mkubwa wa Macha ulioniachia mashaka makubwa juu ya alichokuambia. Macha anakuchezea akili Mh. Rais”, Sabinas alikazia.
“Kwanini unasema hivyo? Wakati mpaka sasa hujajua ni nani alimtuma Meshack kumvamia Sylvanus na alijuaje. Kwanini nisimuamini Macha?”, Rais Costa alihoji mfululizo.
“Mh. Rais sijakataa kuwa labda Gideon hayupo kwenye mpango huu lakini nashawishika kabisa kuwa hata Macha yupo na wote wanakuchezea akili. Inakuwaje Gideon alikuwa akikubembeleza sana uonane na Macha? Huoni kama ni mpango huu Rais wangu?”
“Na kama wote wapo kwenye mpango, kwa nini Macha amtaje mwenzake?” Rais Costa alihoji.
“Kwanini akuzuie kumuwajibisha? Kwanini akusihi umpange utendaji mkuu wa Chama? Mh. Rais think deeply”, Sabinas alimsihi Rais Costa.
Rais Costa alibaki kimya kwa dakika kadhaa akitafakari sentensi zote za Sabinas. Alijitahidi kuchekesha akili ikae sawa.
“You are probably right Sabi, Macha is fooling around, bastard! Do not provide him with any access till tomorrow”, Rais Costa alimpa maelekezo Sabinas na kukata simu.
Rais Costa aliendelea kuchanganyikiwa kwa mawazo mgongano kila baada ya muda mchache.
**************************************
Wakati Stanza ikiwa ni jioni ya saa mbili usiku katika jiji la Beijing China ilikuwa ni alasiri ya saa tisa. Joe na Habibu wakiwa amekaa kwenye moja ya baa umbali mchache tu kutoka kwenye nyumba wanayoishi aliwaona watu wenye asili ya Afrika wengi wakiwa nao wanapata kinywaji maeneo yale.
Habibu akiwa hana lile wala hili mwenzake Joe alikuwa akipepesa macho sana kama mlinzi. Ilikuwa ni kawaida yake pindi anapokuwa nje ya nyumba kukaa kwa tahadhari kubwa. Akiwa anapepesa macho ghafla alimwona kijana kwa mbali akikatiza huku akimtupia jicho.
Joe, alikazana kumwangalia vizuri lakini kijana yule alijichanganya na watu wengine hivyo hakuweza kumwona vizuri. Akili ya Joe ilianza kwenda kwa kasi sana katika eneo lake la ubongo kitengo cha kumbukumbu ili kung’amua mtu yule amewahi kukutana nae wapi, kwa kingereza tungesema ni ‘memory searching’.
Haraka Joe alishtuka baada ya kukumbuka kuwa amefanana na picha moja wapo aliyowahi kutumiwa na Gideon. Haraka alichukua simu yake na kuanza kupekua kwenye picha alizokuwa nazo. Hakuamini alipokuta sura ile inafanana na sura ya picha aliyotumwa na Gideon na kuambiwa huyo ndiyo Sylvanus.
“Habibu be prepared. Tunaondoka”, Joe alimwambia Habibu kwa haraka.
“Kuna nini?”, Habibu alihoji kwa hofu akijua labda wanakuja kukamatwa.
“Ni kama nimemuona Sylvanus”, Joe alimwambia Habibu huku akimpa ile simu ili aangalie ile picha.
“Haiwezekani, amejuaje kama tupo hapa Joe. Ngoja na mimi apite nimuone”. Habibu alimjibu Joe baada ya kuangalia ile picha na kuanza kupepesa macho taratibu kuzunguka lile eneo.
Wakati akizungusha kichwa huku na kule kwa kasi ya ajabu yule kijana alikatiza tena kurudi eneo alilotokea huku akiwakata jicho kina Joe.
“Holy shit, he is the one. Sylvanus is here. Tunafanyaje Joe?”, Habibu alishtuka na kuongea kwa kutetemeka.
“I honestly do not know. Tayari tumeshaingia kwenye ‘target’ yake na nina hakika tumezungukwa na wenzake. My God!” Joe kwa mara ya kwanza alionyesha woga wa Dhahiri.
*************************************
Je Huu Ndio Mwisho Wa Misheni?.Tukutane Kwenye Sehemu Ijayo.
the Legend☆