Simulizi:The President and I(Mimi Na Rais)

Simulizi:The President and I(Mimi Na Rais)

The President And I(Mimi Na Rais) - Sehemu Ya Ishirini

Simanzi

Usiku ule haukuwa mzuri kwa Rais Costa, alilala usingizi wa mang’amung’amu. Mawazo yalijaa akili yake na kila alipopata usingizi kidogo basi aliota kuwa anapinduliwa. Hofu ilizizima moyoni, hakuwa akijua amwamini nani, na nani ni adui yake. Akiwaza maneno aliyoambiwa na Sabinas anaona yana mantiki lakini pia alichoambiwa na Macha aliona kina mantiki vilevile.

Hakupata suluhu au kuelewa afanye nini kuzuia hali ile ambayo alianza kuona ipo nje ya uwezo wake. Mtu pekee wa karibu yake ambaye angeweza kumshauri na aliyemuamini ni Gideon na sasa anahusishwa na mpango huo muovu dhidi yake na serikali ya Stanza.

Mke wake, Bi Sara alikuwa ni mfariji mkuu kwa miaka mingi, lakini uwepo wa Ketina na mkewe kuhusishwa na mpango wa mapinduzi uliwaweka mbali kwa kiasi fulani. Walipofika chumbani, kila mtu hakumsemesha mwenzake ingawa wakitoka nje mbele za watu wanaonekana kutabasamu na kucheka pamoja. Ndoa zina siri nyingi.

Rais Costa alijilaza kitandani usiku kucha akisubiri kesho yake atakapouona uso wa Gideon, angemuangalia kwa namna gani. Lakini je, ataweza kustahimili kuficha hisia zake Gideon asijue kama anamshuku kwa lolote kama alivyoambiwa na Macha?

Wakati huo huo alifikiri angemrudiaje Macha kumkatalia mapendekezo aliyotoa wakati alishayakubali na, ni vipi ikiwa Sabinas anampotosha na akapinduliwa, atajutia kutosikiliza ushauri aliopewa na Macha? Hakika Rais Costa alipoteza uwezo wake wa kufikiri na kuchanganua masuala baada ya wiki chache tu za misukosuko ya mapinduzi.
*********************************

Kama Sabinasi alivyoelekezwa na Rais Costa kuwa asimuwezeshe Macha kufikia taarifa na vifaa vyovyote hadi hapo atakapoongea nae tena kesho yake, alifanya hivyo. Hata hivyo Macha hakuomba kupewa ushirikiano wa suala lolote zaidi ya kuomba simu yake ya mkononi ili awasiliane na mkewe.

Macha hakutaka kurudi nyumbani kusalimia familia japo aliikumbuka sana maana likuwa bado na uvimbe usoni kutokana na mateso. Hakutaka kuishtua familia yake kwa kumuona katika hali ile hivyo alitaka tu awasiliane na watoto na mkewe na kuwataarifu kuwa yupo salama na ana kazi itakayomchukua muda kidogo hivyo wamvumilie.

Familia za watu wa usalama huelewa mambo kama haya. Mzazi aweza kutoweka nyumbani hata kwa miezi mitatu kwa kazi maalumu hivyo kwa Macha alitaka asirudi mpaka ahakikishe amepona vidonda na uvimbe wake wote. Aliwasiliana na mkewe kwa njia ya simu ya kawaida. Alifanya hivyo kusudi akijua fika simu zake zitakuwa zikifuatiliwa na alitaka atengeneze mazingira ya yeye kuonekana kile wazungu wanakiita ‘free soul’.

Baada ya hapo alipakua ‘game’ ya clash royale haraka na kuingiza nywila (passwords) zake ili kuweza kujiunga na Gideon na Joe.

“Che, Saddam, Tiger hapa najua tuna mengi ya ku ‘catchup’, lakini la muhimu nijue yafuatayo. Che upo wapi na kama upo salama. Sadam uliweza kuwasiliana na Meja?” Macha aliandika na kusubiria jibu.

Macha akiwa kwenye nyumba moja wapo ya Usalama wa Taifa Stanza alikuwa amepelekwa huko kupumzika. Alisubiri kama dakika kumi na tano na hakuna aliemjibu.

“Tiger, nilifikisha ujumbe na kanihakikishia anaufanyia kazi. Mambo yaliyotokea ni mengi. Kijana alizidiwa nguvu na mpaka sasa yamkini ameshafariki. Umeongea nini na Eagle?”. Alikuwa ni Gideon akijibu kwa shauku ujumbe ule kutoka kwa Macha huku akiwa nyumbani kwake.

“Nimesikia taarifa za kijana nitazifanyia kazi. Nimeumizwa sana. Che ni lazima aseme kama yupo salama kwasababu jamaa wakishafika China na wakifahamu Che alipo, tutampoteza tusipokuwa makini. Kuhusu nilichoongea na Eagle, Saddam uwe na moyo mgumu na lazima ujionyeshe kuwa hujui kinachoendelea.

Nimemwambia mpango huu ni hakika na kweli na kuwa wewe unahusika kwa namna moja ama nyingine. Ni ukweli kuwa atakuwa anakuchukia sana na ni lazima uwe katika hali ambayo hutamfanya ajue kama nimekwambia haya. Nimemwambia akuache nitadili na wewe ila akupange nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama”, Macha aliandika.

“Tiger unaongea nini? Umenitaja kuwa Nashiri katika jaribio hili? This is insane! Nitawezaje kufanya asinitambue? Tunapambana kumnasua Che wakati huku unafanya mambo ya ajabu? What is in your mind Tiger?”, Gideon alionekana kushindwa kuvumilia, aliandika mfululizo.

Alisahau kabisa kama sehemu ile haitakiwi uandike kwa uwazi namna ile. Alitamani Macha atokee mbele yake ampige hata ngumi. Suala la Macha kumtaja Gideon kwa Rais Costa kuwa anahusika katika mpango wa kumpindua ulimvuruga akili kabisa. Ni jambo aliloshindwa kufikiria na kung’amua ni nini matokeo yake.

“Come down kid. Kwa hali ilivyo Eagle hawezi kukufanya chochote, ananisikiliza mimi. Utapelekwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama na ukifika kule Che atakuelekeza cha kufanya lakini kikubwa ni kuandaa namna ya kumpokea Habibu huko. Ikumbukwe misheni hii ni kufanya mapinduzi yasiyotoa mlio hata kwa Raia. Eagle tunamtoa katika hali ambayo tutaingia kwenye vitabu vya historia, yeye atakuja kugundua tulimtoa labda baada ya miaka mitatu. Itakuwa imebaki historia.

Mpango huu umewekwa kwa namna ambayo raia hawatoshiriki na wala hakutakuwa na umwagaji damu kama ukienda kama ulivyopangwa. Dunia na wanastanza wanapaswa kuamini na kuona kuwa utaratibu huu ni wa kawaida tu kwani hakutakuwa na fujo wala matumizi ya silaha yasiyo na ulazima. Mchakato huu unahitaji umakini na kujitoa. Usihofu”, Kwa mara ya kwanza Macha aliandika kwa urefu sana ndani ya game ile.

“Ninakuheshimu, lakini niseme katika hili mmenikosea sana. Hauwezi kufanya mambo ya hatari kama haya bila kumshirikisha mlengwa kabla ya utekelezaji” Aliandika Gideon.

“Tiger pole sana. Umetenda yote kwa umaridadi mkubwa lakini niseme jamaa wameshafika hapa Beijing na wametuona kwenye mgahawa. Tumeondoka kwa haraka maeneo ya nje na sasa tumekuja ndani kuwapoteza. Ukweli ni kuwa tupo katika hali ya hatari lakini tutajua cha kufanya tu, hatuwezi kukata tamaa. Alikuwa ni Joe amejibu kiufupi.

“Che, naelewa hali mliyo nayo hapo, lakini kuna machaguo mawili tu. Moja muwasiliane na Korea au usubiri na kukabiliana na jamaa wakifika kukudhuru. Chaguo la kwanza litaokoa maisha yako lakini litasimamisha hii misheni kwa muda mrefu kwasababu nyingi ambazo sitaweza kuzitaja hapa. Chaguo la pili litaweka Maisha yenu hatarini na mnaweza kupoteza maisha, kwani nimefanya kazi na jamaa na ninafahamu uwezo wao katika mauaji ya siri. Njia zote zina hasara na faida zake. Uchaguzi ni wako katika hali hii”, Macha aliandika.

Gideon alibaki kimya akitafakari kitendo cha Macha kumtaja kuhusika na jaribio la mapinduzi ya Rais Costa, akili yake ilisimama kufikiri kitu chochote isipokuwa aliwaza ataangaliana vipi na Rais kesho yake asubuhi.

Joe aliwaza sana kisha, “Tiger, nipo tayari kwa lolote ili misheni iendelee. Nitajaribu kupambana, aidha wao ama mimi. Mashushushu wa Korea walinipa silaha baada ya tukio la uwanja wa ndege ingawa uwezo wangu wa kutumia silaha kitaalamu ni mdogo. Najua wanaamini nimemshikilia Habibu na hatakuwa na mengi ya kujibu wala hataguswa na hawa jamaa waliotumwa huku. Nipo tayari kufa”, Joe aliandika.

Kulitokea ukimya wa muda. Hakuna aliyekuwa akiandika chochote. Ilikuwa ni simanzi kubwa kwani kumkosa Joe kwenye misheni hii ingewaweka katika wakati mgumu. Joe alikuwa ni mtu muhimu katika kupanga na kutekeleza misheni ya mabadiliko ya uongozi wa Stanza.

Kitendo cha Joe kukubali kuwa Maisha yake hayana thamani Zaidi ya misheni na kukubali lolote litokee kwake ili misheni iendelee kilimfanya kila mmoja asikitike kwa namna yake. Japo walikuwa hawaonani lakini hakika Gideon na Macha waliiona dhamira ya dhati ya Joe kutaka Rais Costa ang’oke na kuleta pumzi mpya katika kusogeza maendeleo ya Stanza mbele.

“Che, if you will not survive, we shall always honor your commitment in this great mission, forever and for always.” Aliandika Macha na alitoka hewani.

Hakutoka hewani kwasababu aliamua bali betri ya simu yake ilizima chaji na ilimbidi kutafuta chaji aweze kumalizia maongezi yake. Alikumbuka kuwa aliporudishiwa simu hakurudishiwa na chaja. Aliomba muhudumu mmoja wa nyumba ile amtafutie chaja lakini badala yake muhudumu yule alimwambia anaihitaji simu yake.

Wahudumu wote katika nyumba ile ni vijana wa Idara ya Usalama wa Taifa Stanza. Macha alipitiwa na kushindwa kutambua kuwa ule ulikuwa ni mtego aliotegewa na Sabinasi. Alifanya kusudi kumrudishia simu iliyo na chaji kidogo ili aanze kufanya ayafanyayo kwa simu izime na kisha kijana mmoja aichukue hata ikibidi kwa kutumia nguvu na kwenda kunyonya data kujua alikuwa akifanya nini au kuwasiliana na nani.

Kwasababu Macha mara ya kwanza alipokamatwa alifuta taarifa zote kwenye simu yake na walishindwa kupata taarifa hata moja, wakati huu walikuwa na hakika hatakuwa na wazo hilo wala muda wa kufanya hivyo.

Walijua kwa vyovyote vile angekuwa ameweka nywila kwenye simu yake hivyo kwa kutumia utaalam waliouita ‘Phone excavation’ waliamini kuwa watakuwa na uwezo wa kuona kila alichokuwa ukifanya kwenye simu yake kwa kuchukua ‘operating system’ ya simu yake na kuiweka kwenye kadi ndogo na kuiunganisha na mfumo wao ya ‘Phone excavation’. Kwa sababu hajafuta kitu chochote wakati huu wangeweza kupata taarifa zote.

“Abdul, kwa nini unaninyang’anya simu yangu badala ya kunipa chaja?”. Macha alimuuliza yule kijana aliyekuja kuichukua ile simu yake kwa sauti ya upole. Hakuwa anaamini kinachotokea.

“Nimepewa maagizo tu mkuu”, alijibu kwa ufupi.

“Maagizo kutoka kwa nani? Nimepewa kazi na Rais, ni nani mkubwa kuliko Rais?”, Macha alihoji tena.

“Sijui Chief, ila Mkurugenzi ameniambia niichukue. Samahani sana Mkuu”, yule kijana alimjibu Macha na kutoka.

Macha alipata mshtuko mkubwa kwa kujua kuwa kulikuwa na lengo la kufuatilia mawasiliano yake. Alijilaumu sana ni kwa nini amekuwa mjinga namna ile kwa kutong’amua mapema. Alikuwa amekwepa mishale mingi kwa umahiri aliwaza imekuwaje huu umemchoma. Aliumia sana. Alikuwa akijihisi apige kelele kwa nguvu lakini aligundua haitosaidia, macho yalianza kubadili rangi kwa kasi na kuwa mekundu.

“My God, my God, My God….”. Macha kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi aliita jina la Mungu na kuvuta pumzi ya kina.

Ni mara chache hofu ya kifo ilimwingia na uchungu wa dhahiri ulimfika, hii ikiwa mojawapo, Uchungu ulizidi kwa kufikiria ikiwa simu yake ingeweza kudukuliwa na Usalama wa Taifa basi angeiachaje familia yake kwasababu ni Dhahiri kuwa Costa angehakikisha anauawa kwa kosa la uhaini. Alijilaumu sana kwa uzembe huo.
********************************************

Kitendo cha Macha kutoka kwenye maongezi bila kuaga kiliwaacha na maswali mengi Gideon na Joe. Hawakujua nini kimemkuta japo walihisi atakuwa yupo na mtu maana ni kawaida mtu kutoka hewani ghafla kama ameona hali isiyomruhusu kuwa hewani kwenye mawasiliano yale.

“Che, stay safe my brother it was an honor working together and you have been my good friend all long”, Gideon aliandika ili na yeye atoke hewani. Hakuwa na msaada kwa wakati huo.

“You too, kama jamaa wakifika hapa nitakuageni kwa mara ya mwisho. Nikifa, utamwambia Eliza na Derick kuwa nawapenda sana”, Joe aliandika kwa huzuni. Walitoka hewani.
**********************************

Fredrick Nyari alikuwa ni mwenzake na Sylvanus, wote walikuwa Idara ya usalama wa Taifa Stanza kitengo cha Mauaji na Uhujumu. Siku ile mara baada ya Sylvanus kumpigia simu Nyari kumweleza uwepo wa Meshack pale Casino, Nyari alihisi hali ya hatari baina ya watu wawili.

Nyari na Meshack ni watu walioingia pamoja katika Idara ya Usalama wa Taifa. Japo waligawanywa wakati Meshack akipangwa kitengo cha ‘Executive Protection Section’ yaani ulinzi wa watu muhimu Nyari alipangwa ‘Assasination and Sabotage Section’, yaani kitengo cha Mauaji na Uhujumu.

Kugawanywa huku hakukuzuia urafiki wao ulioshibana kuendelea. Ukweli ni kuwa aliewaingiza kwenye Idara ya Usalama wa Taifa alikuwa ni babaye Meshack. Meshack alipopata nafasi alimuombea sana Nyari nae apate nafasi kwani hakuwa amefanya vizuri kwenye matokeo yake ya kidato cha nne wakati ule.

Nyari akiwa mtoto wa kwanza na pekee wa kiume kutoka kwa baba yake ndiye aliyekuwa akitegemewa kuikomboa familia yake kutoka kwenye dimbwi kubwa la umaskini waliokuwa nao.

Meshack ndiye aliekuwa akimsaidia Nyari baadhi ya fedha ili aiwezeshe familia yake pindi ilipokuwa ikimuomba msaada, hivyo deni alilokuwa nalo Nyari kwa Meshack lilikuwa halilipiki.

Simu ya Sylvanus ya kuulizia uwepo wa Meshack pale Casino na jinsi Sylvanus alivyokuwa anaongea vilimtia mashaka Nyari. Alipomaliza tu kuongea na Sylvanus haraka sana aliwasha gari lake na kuelekea Casino muda ule ule. Aliingia na hakuwaona lakini pia alipojitahidi kupiga simu hakuna aliyepokea kati ya Meshack wala Sylvanus. Alipata hofu kuwa suala linaweza kuwa limeshatokea.

Kama zilivyo hulka za wanausalama wengi, hufanya uchunguzi wa haraka katika eneo husika ili kutambua hali ya kiusalama. Nyari hisia zake zilimwelekeza akawaangalie kule vyooni. Aliamini kuna jambo halipo sawa. Nyari akiwa anatembea kuelekea vyooni alimwona Sylvanus akitoka. Nyari alijibanza nyuma ya mtu na kujaribu kumpigia Sylvanus simu aone kama angeipokea.

Huku akiwa anamwangalia akiwa anakatiza kati kati ya watu akielekea nje Sylvanus hakupokea ile simu. Hapo alijua fika kuwa Sylvanus atakuwa amekabiliana na Meshack. Alikimbia haraka vyooni na kuanza kufungua mlango mmoja mmoja kuangalia kama atamuona Meshack. Hakumuona.

Haraka alielekea sehemu maalumu ya kuvutia na sigara na baada ya kuangaza macho huku na kule alimuona Meshack amelala chini akionekana kutokujitambua au kufanya mjongeo wa aina yoyote wa kimwili. Moyo wa Nyari ulilipuka kwa majonzi makubwa. Alimsogelea haraka na kumgusa sehemu muhimu za mwili ili kumkagua dalili yoyote ya uhai. Huu ni utaratibu wa wanausalama na au hata madaktari na watoa huduma ya kwanza sehemu zote duniani.

Kabla ya kuchukua hatua yoyote hupaswa kukagua mazingira ikiwa yanaruhusu kutoa msaada kwa kuangalia pande zote, kisha husogea kwa uangalifu kuelekea alipo muathirika na kufuata taratibu fulanifulani ili kuangalia ikiwa kuna dalili zozote za uhai ili kufahamu ni aina gani ya huduma ya kuifanya kwa haraka ili kuokoa uhai wa muhusika.

Alimgusa kila mahali walipofundishwa kugusa kuangalia kama mtu ana uhai au amepoteza Maisha. Alipogusa eneo la shingo alishtuka baada ya kusikia kwa mbali mapigo ya moyo, lakini Meshack hakuwa akijigusa wala kujibu komandi yoyote aliyofanyiwa ikiwemo kufinywa na kutikiswa.

Nyari alianza kumpulizia mdomoni kuona kama ataweza kushtuka. Alikuwa akifanya yote hayo huku machozi yakimlenga kwani ana historia ndefu na Meshack tangu katika ngazi ya familia zao. Hakuamini anachokishuhudia.

“Aaanghh”, Meshack alishtuka lakini akiwa ameishiwa nguvu.

“It’s fine Shack, mimi Nyari. Twende”. Nyari alimwambia Meshack kwa kumuita jina lake kwa kifupi, jina alilozoea kumuita tangu walipokuwa wadogo.

Meshack hakuwa anajitambua hivyo Nyari alimvua ile kofia ya kininja aliyokuwa amevaa pamoja na ‘gloves’ kisha alimnyanyua na kumsimamisha na kumuegamisha kwenye mabega yake na kuanza kutoka nae nje. Alitembea nae akimkokota kama vile mtu anaemsaidia mwenzake aliyelewa chakari. Walitoka na kuelekea nae anapoishi Nyari.

Kutokea siku ile hakuna aliyejua Meshack yupo wapi. Taarifa za Sylvanus kwa Sabinas juu ya kifo cha Meshack hakuna aliekuwa amezithibitisha kwasababu hakuna aliyeona mwili wake. Meshack alipozinduka alimsihi Nyari asiseme lolote.
**************************************

Gideon alikuwa amelala lakini mwenye mawazo mengi. Alifumba tu macho lakini hakika hakuwa na usingizi. Akiwa amelala alisikia mlio wa ujumbe wa WhatsApp kutoka kwenye simu yake. Aliichukua na kufungua, alikuta ni namba mpya imemtumia ujumbe kwa kuandika jina lake yaani “Gideon”

“We ni nani?”, Gideon aliandika.

“Tafadhali naomba ukae mahali ambapo nitaweza kukupigia simu ya video’’

Gideon alitoka chumbani kwake na kuelekea chumba wanachokitumia watoto wake kama maktaba na alipofika yeye ndiye alipiga ile simu ya video.

“Naitwa Fredrick Nyari”, Kijana yule alijitambulisha huku macho yake yakionekana kulengwa na machozi na akiongea kwa sauti yenye masikitiko makubwa.

“Sikufahamu, na kuna nini basi mbona unanipigia siku usiku wote huu? Na kwanini unalia?” Gideon aliuliza maswali mfululizo kwa hofu.

“Ni Rafiki yake na Meshack na nipo Idara ya Usalama wa Taifa. Kaka Meshack amefariki muda huu” Nyari alimwambia Gideon na kuielekezea kamera kwenye mwili wa Meshack aliokuwa ameulaza kitandani.

“Nyari, please….pl….pleas…Oh God” Gideon alishindwa kuuangalia mwili wa Meshack.

Nyari alimwelezea kila kitu Gideon kuanzia historia ya udugu wao hadi mwisho Meshack alipofariki. Alimwelezea jinsi alivyojitahidi kuokoa maisha ya Meshack lakini ameshindwa kwani anahisi mapafu yalishindwa kufanya kazi na alikuwa akipumua kwa shida huku akikohoa damu mfululizo toka siku ya tukio.

Alishindwa kumpeleka hospitali kubwa kwasababu ya ombi la Meshack na alichokuwa akifanya ni kumpa matibabu yeye kwa kuuliza madaktari. Nyari alimwambia Gideon uhusiano wake na Meshack na kuwa ni Meshack aliempa maagizo yale kuwa siku akifa basi amtafute Gideon na kumpa taarifa hizo. Wote walihuzunika sana.

“Nyari, naomba unipigie picha mwili wa Meshack. Na utauhifadhi vipi? Gideon alihoji.

“Ninajua cha kufanya, mimi ni mwanausalama. Nitauharibu mwili kwa namna ambayo hata vipimo havitoonesha kuwa alishawahi kukutana na mtu mwingine yeyote zaidi ya Sylvanus. Kisha nitakwenda kuutupa kandokando ya barabara ili upatikane na familia yake iweze kumpa heshima za mwisho. Inaniuma sana lakini lazima nifanye hivi ili familia yake ipate mwili huu na wauzike na kubaki na kumbukumbu”, Nyari aliongea kwa huzuni kuu.

“I can’t say a lot. Utakuwa ukinipa taarifa watakapouokota ili niangalie namna ya kushiriki kwenye mazishi yake. Thank you Nyari” Gideon alimalizia na kuagana na Nyari.

Baada ya hapo, Gideon nae alianza kutokwa machozi. Meshack alikuwa na kumbukumbu kubwa kwa kila mmoja na waliumia kumpoteza kwa namna ile. Hakuna aliyeamini kama Meshack amefariki na ule ndio ulikuwa mwisho wake. Meshack aliondoka duniani kwa kuuawa katika kutelekeza majukumu yake ya kimisheni.

Haraka Gideon alichukua simu na kumpigia Joe simu kwa njia ya WhatsApp. Alimweleza kila kitu kama alivyoelezwa na Nyari na alimtumia picha ya mwili wa Meshack.

Ilikuwa ni siku ambayo simanzi ilitawala miongoni mwa wanamisheni. Gideon alishindwa kujizuia na kuanza kulia kwa sauti hali iliyosababisha mkewe Lucia kuamka na kuja kwa haraka kumuuliza mumewe kulikoni. Alimweleza mmoja wa wafanyakazi wa ikulu aliyekuwa rafiki yake mkubwa amefariki.

Lucia mkewe na Gideon alimbembeleza na kumtia moyo lakini haikusaidia sana kwa wakati ule. Ulihitajika muda ili huzuni ile ipungue na hatimaye kwisha. Siku moja haikutosha. Lucia aliondoka na kumwacha Gideon aendelee kuongea na Joe.

“I wasn’t trained to handle the pain for loosing someone close to me. I am breaking. I may as well loose you anytime. Be sure to be safe mate’’, Gideon alilalamika.

“Stop crying Gidi. Some sacrifices must happen in the process. I am as well very low for his ultimate demise”, Joe alimjibu Gideon kwa kujikaza sana. Joe alishakubali kuwa lolote linaweza kutokea na alipunguza hofu ya masuala yaliyo nje ya uwezo wake kuyatawala.

Wote walisikitika kwa namna yao. Habibu alikuwa kimya ila mishipa ya kichwa ikiwa imevimba huku akihuzunika na kutafakari kwa kina. Hakumfahamu marehemu moja kwa moja lakini alijua wazi kuwa alikuwa ni mtu muhimu katika misheni ile.
********************************************

Usiku ulikuwa mrefu, lakini kila liwialo ni lazima lichwee, na kila lichwalo lazima liwie. Hatimaye asubuhi ilifika. Ingawa wakati Stanza kukiwa kunapambazuka, nchini China alipo Joe na Habibu bado ilikuwa usiku wa manane.

Gideon akiwa amejikaza kana kwamba hakuna ajuacho japo alikuwa akijua mengi na akiwa amegubikwa na uchungu mkubwa aliwasili Ikulu za Peron zilipo ofisi zake.

Alipofika tu lango kuu alikutana na Katibu Mkuu Kiongozi Bwana Jabir Salehe.

“Rais anakuulizia sana toka alfajiri. Yaani leo amewahi sana kufika ofisini kunani mdogo wangu?”, Jabir alimuuliza Gideon.

“Sijui kaka mbona hajanipigia simu? Lakini leo ndio aliniambia nirudi na yale marekebisho ya ile barua yake labda ndo hayo anayasubiri”, Gideon alijibu lakini akiwa amejawa hofu. Sauti yake ilitoka kwa kutetemeka.

“Mbona sauti yako inatetemeka leo Gidi. Unaumwa?”. Jabiri aligundua Gideon hayupo sawa. Gideon alikuwa anaona anaongea kawaida kumbe mtu wa pili alimwona kabisa hayupo sawa.

“Najihisi Malaria kaka”, Gideon alijibu kwa kudanganya.

“Sasa mdogo wangu wewe wa Ikulu ukiumwa Malaria yule wa kijijini aumwe nini? Ha ha ha. Haya kaonane na Mkuu”, Jabir alimalizia na kuacha na Gideon.

Gideon aliingia ndani na kuanza kushika korido iliyoelekea ofisini kwake. Alifika ofisini na kujiangalia kwenye kioo. Alijiongelesha mwenyewe kuwa ajikaze. Aliichukua ile karatasi iliyokuwa na marekebisho ya majibu ya Costa kwa Rais wa Marekani na kuanza kutembea kuelekea chumba cha ofisi ya Rais.

Alifika na kufunguliwa mlango na walinzi na kuingia. Alikutana uso kwa uso na Rais. Costa alimwangalia Gideon machoni kama dakika mbili hivi mfululizo bila kumsemesha. Hata Gideon alipojaribu kumsalimia hakumjibu. Kadiri Gideon alivyotazamwa na Rais Costa ndivyo alivyozidi kutetemeka na kupata hofu ya suala aliloambiwa na Macha. Alitetemeka mpaka viliota vile vipele vya mtu anaesikia baridi kali.

“Gideon, nataka nikupangie kazi kubwa kidogo. Nimekuamini sana na sasa nataka ukaninyooshee Chama. Nataka nikupe Ukatibu Mkuu wa Chama Chetu Cha Ukombozi Stanza, kama kumbukumbu zangu zipo sawa nadhani hata shahada yako ya Uzamili ulisomea Sayansi ya Siasa sasa umepata pa kuifanyia kazi. Niambie unataka nini chochote nitakupatia ili ukafanye kazi kwa uhuru na ufanisi”, Rais Costa alimwambia Gideon kwa sauti kubwa baada ya kimya kirefu.

“Mh. Rais hapana. Nashukuru kwa uaminifu wako lakini sitaweza. Najua ni heshima kubwa na ninajua ni nafasi kubwa kuliko hii niliyo nayo sasa lakini kwa nidhamu kubwa naomba umpe nafasi hiyo mtu mwingine mwenye uzoefu na siasa zetu za Stanza”, Gideon alijibu kwa nidhamu kubwa.

“Gidi, unanishangaza. Wewe ndiye umekuwa ukinishauri yote ninayokwenda kuyaelekeza kwenye chama sasa inakuwaje useme huwezi? Lazima uende kule bwana”, Rais Costa alionekana kusisitiza.

“Mh. Rais, unajua sijawahi kuweka pingamizi ya jambo ulilowahi kushauri na unajua utii wangu kwako. Ninakuomba sana kama sikufai hapa, basi Mtukufu Rais naomba unipe ruhusa nikapumzike na kufanya majukumu mengine kwa amani kabisa. Kazi yangu hapa ninaifurahia na inanipa nafasi ya kujifunza mengi zaidi.

Pia ninakusudia kufanya Shahada ya Uzamivu ya Mahusiano ya Kimataifa na ninaamini katika nafasi yangu ya sasa ninajifunza mengi zaidi hasa kupitia wewe unavyoendesha mahusiano na mataifa mengine”, Gideon alijibu kwa heshima kubwa.

Rais Costa alimtazama tena usoni Gideon kwa sekunde kadhaa bila kumwambia neno. Kisha alimruhusu aketi.

Ule ulikuwa ni mtego. Rais Costa aliamua kumpa zile taarifa Gideon ali amuone angezipokea kwa namna gani. Nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Chama ilikuwa na maslahi makubwa kuliko nafasi aliyokuwa nayo Gideon kwa wakati huo. Isingewezekana mtu yeyote akatae nafasi ile.

Lakini jambo la pili kabla ya kwenda kuonana na Macha alitaka ajaribu kuona kama Gideon angekubali. Kwa kufanya hivyo basi ingeleta kiashirio kuwa ni mpango wamepanga Macha na Gideon kama alivyoambiwa na Sabinasi. Kitendo cha Gideon kukataa na kuwa tayari kuacha hata kazi na kurudi nyumbani kilimpa uhakika kuwa Gideon hana ajualo na kuwa Sabinas ana wasiwasi wa bure.

Rais Costa alianza kuona pengine utendaji wa Sabinasi unasukumwa na hisia za wivu kuwa ikiwa angeruhusu yeye Rais amuamini Macha tena, basi angeweza kurudishiwa Ukurugenzi wa Usalama wa taifa na yeye kuondolewa

“Nipe hiyo barua. Halafu unaumwa? mbona umenyong’onyea namna hiyo Gidi?”, Rais Costa alimuuliza Gideon huku akichukua ile barua na kuisoma.

“Ndiyo mkuu, nahisi nina malaria”, Gideon alijibu.

Rais Costa alikaa kimya akiwa anasoma na kuhakikisha kama yale marekebisho aliyoagiza yamewekwa sawa na Gideon.

“This is now perfect. Mpe Jabir aitengeneze kwenye muundo maalum kisha nipatiwe niweke sahihi aitume. Pole sana Gidi. You need to consult a doctor if the situation persists. Ukiona umezidiwa ukapumzike”, Rais Costa alimwambia Gideon.

“Asante Mheshimiwa”, Gideon alijibu huku akiichukua ile barua.

Akiwa anajikusanya pale ili atoke simu ya Rais Costa iliita na Rais aliipokea.

“Mh. Rais you need to come and see this”, Alimsikia Sabinas kwa mbali akimwambia Rais Costa.

“Nini Sabinas, nije wapi? Huwezi kuniita mimi kiholela hivyo unajua sitembei tu kiholela kama wewe there is a process comeon” Rais Costa alionekana kufoka.

“Msafara nimeshauweka tayari unakusubiri nje mkuu, nakuomba sana hapa kwenye nyumba yetu anayoishi Macha”. Sabinas alisikika.

“Gideon twende”, Rais Costa alikata simu kwa hasira na kumuamuru Gideon aongozane nae.

Baada ya dakika kama kumi na tano walifika kwenye nyumba aliyokuwa amelala Macha na walipokelewa na Sabinas pamoja na maafisa wengine waandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa Stanza na kutembea moja kwa moja kuelekea kwenye chumba alichokuwa amelala Stanley Macha.

Sabinasi alifika na kuusukuma mlango.

“Holy shit” Rais Costa alipata mshtuko mkubwa mara baada ya kuuona mwili Stanley Macha ukiwa umelala pale sakafuni huku povu jingi likiwa limemtoka mdomoni.

Gideon alisogea kwa kupiga hatua kama mtu anaenyata asitake kushuhudia anachotaka kukitazama. Alijihisi kama anaota lakini ulikuwa ni ukweli Stanley Macha, aliyekuwa amelala pale chini alikuwa AMEFARIKI.

Chumba kizima kilizizima kwa ukimya. Rais Costa alipiga magoti chini na kumshika shavu Macha huku akitokwa na machozi pasi kusema neno lolote. Aligugumia kwa uchungu lakini hakutaka kuachia kilio.

Gideon alipatwa na huzuni kuu na alitaka kuuliza sababu za kifo cha Macha lakini akasita. Alitoa simu yake akapiga picha mwili wa Macha kwa siri kisha akamtumia Joe bila kumwambia neno lolote. Aliogopa sana. Kifo cha Meshack na sasa Macha kilizidi uwezo wa Gideon wa kuhimili huzuni.

Mwili ulishindwa kuhimili simanzi iliyojaa moyo wake. Aliifanyia simu yake ‘Hard reset’ ili kufuta kila taarifa kwenye simu yake maana alijiona anaanza kupoteza nguvu, na haikuchukua dakika hata tatu Gideon alidondoka na kupoteza fahamu.
************************************

Huko Beijing China ilikuwa ni usiku wa manane. Joe hakuwa amelala, alijawa huzuni kwa kifo cha Meshack lakini pia hofu ya uwepo wa Sylvanus ilimtanda pasi kawaida. Akiwa amekaa anatazama luninga alisikia mlio wa simu wa WhatsApp. Aliinyanyua simu yake haraka na kufungua kuangalia ni taarifa gani imeingia.

“Jesus Christ”, Joe aling’aka kwa nguvu kitendo kilichomfanya Habibu aliyekuwa amejilaza kwenye kochi pembeni ya Joe kushtuka.

Joe alikuwa ameipokea ile picha ya mwili wa Macha aliyotumiwa na Gideon.

“Nini?”, Habibu alishtuka kwa hofu.

Joe bila kusema neno huku akitoa machozi mengi kabisa alimpa Habibu ile simu ili aitazame.

“Ya Allah!” Kwa mara ya kwanza Habibu alianza kutokwa na machozi.

Joe aliinamisha kichwa juu ya meza huku akiwa ameuficha uso wake kwa viganja vya mikono lakini machozi yalipenya kwenye vidole vyake kwa jinsi yalivyokuwa mengi. Kila mmoja alikuwa kimya.

Baada ya dakika kama tatu hivi Joe aliichukua simu yake na kuanza kumpigia Gideon kwa kutumia WhatsApp lakini siku haikuweza kuunganishwa. Alijaribu mara nyingi bila mafanikio. Wakati akiendelea kujaribu mlango wao uligongwa.

“Habibu nasikia mlango umegongwa”, Joe alishtuka na kumwambia Habibu kwa sauti ya chini kabisa.

“Hata mimi nimesikia”, Habibu nae alikata kilio na kumjibu Joe.

Waliangalia saa ya ukutani na waliona ilikuwa ni saa tisa usiku kwa saa za China.

“Nenda kwenye dirisha lile utaweza kuchungulia nani amesimama mlangoni. Hakikisha unachungulia kwa kujificha. Tumia upande ule ambao hatujawasha taa” Joe alimwelekeza Habibu.

Haraka Habibu alinyanyuka na kufuata maelekezo ya Joe. Joe alibaki amekaa pale chini asijue afanye nini.

Habibu alifika na kuchungulia kisha akiwa pale dirishani alimgeukia Joe na kumtazama kwa jicho la kukata tamaa. Alirudi na kumsogelea Joe karibu.

“Joe, ni Sylvanus anagonga. Na kwa mbali nimewaona watu kama watatu hivi, nadhani wapo pamoja. Tunafanyaje”. Habibu alionekana kumwambia Joe kwa sauti ya chini sana na ya mtu aliekosa Tumaini.

Joe, hakumjibu neno lolote Habibu. Alinyanyuka na kumkumbatia kwa nguvu na kwa ufupi na kuchukua bastola yake aliyopewa na mashushushu wa Korea kwa ajili ya ulinzi wake binafsi. Alisogea na kukaa kwenye moja kati ya kona za chumba kile na kumuelekeza Habibu akae kwenye moja ya kona akiwa amenyoosha mikono yake juu ili wakiingia basi wasimpige risasi kwa kuona kuwa hakuwa na madhara kwao. Yeye aliamua kuwa ni bora afe kuliko arudi Stanza na kuangukia mikononi mwa Rais Costa.

“I pray that you stand your ground and you shall become a great leader one day. Do not forget us in your story. Joe alikuwa akimwambia Habibu kutokea kwenye kona aliyokuwepo.

Mlango ulizidi kugongwa. “Nenda kamfungulie”, Joe alimwachia Habibu na kumwagiza.

“Joe siwezi. Siwezi kuhalalisha kifo chako. Tuombe msaada Ubalozi wa Korea tafadhali.” Habibu alishindwa kustahimili.

“Hapana. Hata hivyo tumechelewa sasa natamani tufanye hivyo baada ya kuona kifo kimenifikia na kifo cha Macha na sintofahamu ya Gideon lakini hapana. Kafungue mlango”, Joe alisisitiza huku mlango ukigongwa tena kwa fujo.

“Hapana sitafungua Joe. Hapana” Habibu aligoma.

Joe alimtazama Habibu machoni kwa sekunde kadhaa na kuuelekea mlango ili akaufungue mwenyewe.

Wakati akielekea kwenye mlango, alisikia milio isiyo ya kawaida masikioni mwake ingawa alifahamu ni nini hasa. Alisikia risasi zikifyatuliwa lakini mlio wake haukwenda mbali kwasababu silaha zilizotumika zilifungwa kiwambo maalumu cha kuondoa sauti au kwa Kingereza wangeita ‘bullet silencer’. Joe aliondoka kwa haraka eneo la mlango na kurudi kwenye kona aliyokuwapo huku akiishikilia bastola yake kwa makini. Mikono ilikuwa ikimtetemeka.

Habibu aliendelea kuwa na hofu kuwa huu ndiyo mwisho wa Maisha yao. Aliamini kuwa wahudumu wa eneo lile walipigwa risasi na kina Sylvanus ili waweze kuingia kwa uhuru zaidi kutekeleza majukumu yao.

Wakiwa bado hawajui wafanye nini mlango ulizidi kugongwa Zaidi na wakati huu uligongwa kwa fujo. Kwa sababu walisikia ile milio ya risasi wakati huu hata ujasiri mdogo aliokuwa nao Joe wa kutaka kupambana na Sylvanus uliondoka. Alikiona kifo hiki hapa kunamwita hadharani. Alishindwa hata kuishikilia vizuri bastola aliyokuwa nayo.

Wakiwa kila mmoja amesimama kwenye kona yake wakitazamana kwa macho ya kupeana buriani Joe alisikia mlango ukifunguliwa kwa nguvu kwa kitu kuingizwa kwenye kitasa cha mlango na loki ikafyatuka.
****************************************
Taarifa.

Nini Kimeendelea Katika Kisa Hiki?Joe Amepona?Misheni Itafanikiwa?Usikose Mwendelezo Kwa Kusoma Nusu iliyobaki Ya Simulizi Hii Kwa kununua Kitabu Kitakachokuwa Mtaani Muda Mfupi Ujao.

Kisa Hiki Kimeboreshwa Tena Tangu Mwanzo Na Kitakupa Ladha Tamu Zaidi Kuliko Iliyokuwa Mwanzo. Tumalizie Nusu Iliyobaki Ya Kisa Hiki Kwenye Kitabu.

Asanteni.

the Legend☆
Mtunzi tuelekeze msiba wa macha ulipo [emoji22][emoji22]

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Aaaahggggr mnaanzisha stori halafu haziishi
 
Back
Top Bottom