HADITHI: THE DARKNESS OF AN ANGEL
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WhatsApp: +255621567672
Email:
thomasibabuya@gmail.com
UMRI: 18+
SEHEMU YA TISA
“Taarifa za mwanzo uliniambia kwamba ni watu ambao walikuwa wanapora tu kwa ajili ya njaa, sasa inakuaje kwamba watu hao wasababishe hali kama hiyo kwenye taifa hili?”
“Kwa sababu tangu mwanzo sikuwa sahihi kuamini hilo, wale watu walikuwa ni zaidi ya hilo ambalo nililifikiria”
“Unamaanisha kwamba wale watu hawakuja kwa bahati mbaya?”
“Hilo ndilo jibu lake sahihi”
“Hawa watu ni akina nani, kwanini waje kwenye nyakati kama hizi na wao wanahusika vipi na hawa watu mpaka yeye ndiye ahusike kuweza kuwaua? Na taarifa mahali ambako wanatoka hawa watu yeye alizipatia wapi?”
“Hayo ndiyo maswali ambayo hata mimi najiuliza japo ninahisi baadhi ya vitu kadhaa kwenye hili”
“Nakusikiliza”
“Hii familia tunajua namna inavyofanya mambo yake, hawa watu walipotea kwa miaka zaidi ya ishirini kiasi kwamba walitafutwa mpaka serikali ikakata tamaa ya kuweza kuwatafuta na baadae wakaja kujitokeza wenyewe. Kurudi kwao hakukuwa kwema kwa sababu kulikuja na matatizo mengi ya kutisha ambayo hayakuwa na mwisho mzuri kwa taifa letu lakini baadae tena wakaja kupotea kwa makubaliano ikiwa na maana kwamba kwa wakati huu hawakuwa kwenye rada za kutafutwa na serikali.
Silaha kubwa ya hawa watu juu ya usalama wao ni usiri wa kuto tambulika kwamba wako wapi kwa wakati huo na wanafanya nini. Kama ingekuwa ni mauaji ya kawaida tu na wao hawahusiki basi wasingejisumbua kabisa kujiingiza kwenye hili hivyo wao kuingilia maana yake ni kwamba huenda kuna taarifa ambazo wanazo zinawahusu moja kwa moja na ndiyo maana wameamua kuja hadharani kwa mara nyingine tena jambo ambalo ni la hatari kuweza kutokea’’
‘Subiri kwanza, umesema kwamba wameamua kuja hadharani?”
“Ndiyo kiongozi”
“Kuua watu sio kuja hadharani Kai na wote tunalijua hilo, hizi habari za uwepo wao unazo wewe tu na vijana wako pamoja na mimi ambaye unanipatia muda huu”
“Hapana mheshimiwa haipo hivyo”
“Unamaanisha nini?”
“Othman alifanya mauaji ndani ya kasino ambayo alijua kabisa ina kamera kila kona na baada ya kukamilisha hilo akaondoka bila hata kuhangaika nayo, unahisi ni kwa bahati mbaya?”
“Kwamba alihitaji mamlaka ziitambue sura yake kuweza kuwepo pale?”
“Ndiyo”
“Oooooh shiiiit! Ni kweli wameamua kurudi kwa namna hii?”
“Iko hivyo na kama sio kijana wangu kuwahi pale pale ingekuwa ni tatizo kubwa”
“Kwanini anataka kutambulika hadharani namna hii?”
“Hii ni njia ambayo huwa wanatumia pale ambapo wanamtafuta mtu ambaye hawamjui”
“Unamaanisha kwamba huenda kuna mtu ambaye alisahaulika wakati ule ndo amerudi tena kwa sasa?”
“Sina uhakika na hilo, inawezekana ikawa hivyo lakini pia inawezekana ni mtu mpya amekuja kwa njia yake mwenyewe na huenda naye alikuwa anarusha karata zake gizani ili familia hiyo isije kutambua uwepo wake ili azipige hatua zake kimya kimya”
“Maana yake kama wakijuana kwamba wote wanawindana itatokea vita ya hadharani!”
“Ndiyo mheshimiwa”
“Unahisi ni nani anaweza kuwa anawatafuta na kwa sababu zipi?”
“Hili ndilo jambo ambalo limenifanya mimi kuja hapa usiku huu kuongea na wewe”
“Ukiwa una maana ya kwamba?”
“Inatakiwa hawa watu tuwapate mapema”
“Watu gani hao?”
“Familia ya Gavin Luca”
“Vipi Kai umechanganyikiwa au?”
“Nipo timamu na akili zangu zote hapa”
“Bila shaka ulikuwepo kule Morogoro na ulishuhudia yote ambayo yalitokea si ndiyo?”
“Ndiyo mheshimiwa”
“Unakumbuka kwamba ni wewe ambaye vijana wako wote walikufa ndani ya mitaa ya zamani ya Peenuga siku ile wakati lile eneo linalipuka si ndiyo?”
“Ndiyo mheshimiwa”
“Bila shaka uliona makubaliano ambayo mimi niliingia na ile familia si ndiyo?”
“Ndiyo mheshimiwa”
“Nadhani unaijua vizuri historia ya hii familia kwenye taifa hili si ndiyo?”
“Ndiyo mheshimiwa”
“Kwa hayo yote basi ni mtu asiye na akili pekee ndiye ambaye anaweza kuja kuniambia mimi nifanye jambo kama hilo. Siwezi kuruhusu ufanye jambo la namna hii kwenye taifa langu tena kwenye nyakati kama hizi ambazo wakati wangu unaelekea tamati, hili taifa limepitia mambo mengi ya kutisha mno sitaki kuwa sehemu ya kuliharibu kwa mara nyingine tena, yale ambayo yalitokea kipindi kile sitaki yaje kujirudia tena” raisi hakuwa tayari kabisa kuweza kufanya jambo kama hilo.
“Unaogopa kwamba hawa watu watakuua mheshimiwa?”
“Unahisi kwamba unaweza ukanilinda Kai?”
“Naweza kujaribu”
“Hahahaha hahaha, hivi unahisi kwamba mimi naogopa kufa?”
“Nisamehe kama nimeongea vibaya mheshimiwa”
“Nisikilize vizuri bwana Kai, ni jambo la hatari kuweza kuvunja ahadi ambayo ipo mezani na umeingia na watu wa namna ile, hili taifa wanaweza kulifanya wanavyotaka wao unajua kwanini?”
“Nakusikiliza mheshimiwa”
“Kwa sababu wale wana nguvu ya pesa na nguvu ya kummudu mtu yeyote yule. Wale wana pesa nyingi kumzidi mtu yeyote yule ndani ya hili bara na wanaweza kumfikia yeyote na kwa wakati wowote ambao wanataka wao hivyo kama kuna utofauti ukifanyika na yale makubaliano basi kuna vifo vingi vitatokea. Halafu kuna jambo ambalo nahisi haulifahamu ngoja nikwambie leo” mheshimiwa alivuta pumzi na kuhema kwa nguvu.
“Kwenye yale makubaliano tulikubaliana kwamba hatuji kuyavunja kwa namna yoyote ile na ndiyo maana yalifanyika kwa maandishi na ahadi ya Lionela ya mwisho kwangu ilikuwa ni kwamba kama ikija kutokea nikayavunja yale maandishi basi atakuja kufanya mambo ya kutisha zaidi ya yale ndani ya hili taifa, je huko ndiko ambako wewe unataka tulipeleke taifa?”
“Sina maana hiyo mheshimiwa”
“Sasa maana yako ni ipi hasa kama unataka kulazimisha familia hiyo ipatikane?”
“Bila hao maana yake itakuwa ni ngumu sisi kujua tunaanzia wapi, watu pekee ambao walikuwa wana uwezo wa kutupatia hizo taarifa ndio hao ambao wao wenyewe wamewaua, maana yake ni kwamba Othman hakutaka hizo taarifa zifike kwa mtu mwingine. Huoni kama ni hatari kubwa kwa taifa na tunajua kabisa kuna janga baya linakuja na hakuna kitu tunaenda kufanya mpaka kusubiri maamuzi kutoka kwenye familia moja kwa sababu tu imefanya mambo makubwa ndani ya hili taifa?” raisi alionyesha masikitiko makubwa akiwa anamwangalia bwana huyo ambaye ni kama alikuwa anajisahaulisha yale ambayo yalikuwa yametokea huko nyuma.
“Una uhakika kabisa upo kwenye akili yako?”
“Mpaka nakuja hapa maana yake sijaona jambo lingine la kuweza kufanya zaidi ya hili, tunapaswa kumpata Othman na kufanya hivyo maana yake ni kwamba tutajua hii familia nzima ilipo. Tukimpata huyu tutampa machaguo ya kushirikiana na sisi kwa lazima au tutumie nguvu kama inawezekana”
“Nenda kapumzike Kai nadhani siku ya leo umechoka sana” Raisi alimtaka kiongozi huyo aondoke huku naye akiwa anamshangaa raisi wake, sio kwamba hakuwa akiwatambua watu hao bali kwa nyakati ambazo walikuwepo hakukuwa na namna nyingine ya kuweza kufanya ili kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa. Raisi alitembea hatua kadhaa lakini alisimama na kugeuka.
“Kai kama ikitokea ukapuuza amri yangu basi amini kwamba nitakufanyia jambo baya sana kwenye maisha yako” aliongea kwa msisitizo kuonyesha kwamba alikuwa akimaanisha yale ambayo aliyaongea na kutoweka akimuacha mkurugenzi akishangaana na anga.
Hawa watu wameanza kupishana wenyewe, ngoja tuone wanataka kutupeleka kwenye dunia gani.
Sehemu ya 9 sina la ziada tena.
Febiani Babuya.